Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Fahamu wachezaji 10 wanaoweza kuhama katika siku ya mwisho ya usajili Ulaya leo
Na Yusuph Mazimu, BBC Swahili
Dirisha la usajili la msimu wa majira ya joto kwa ligi tano kubwa Ulaya limebakiza masaa machache tu kabla ya kufungwa.
Kwa ligi kuu ya England (EPL), La Liga (Hispania) na Ligue 1 (Ufaransa), dirisha litafungwa saa 7 usiku wa kuamkia Septemba 2 huku Bundesliga (Ujerumani) na Serie A (Italia), likifungwa mapema kidogo kabla ya kuanza siku mpya ya September 2.
Kwa ujumla ni masaa tu yaliyosalia kabla ya heka heka za usajili zilizoanza Juni 10, 2022 kumalizika kwa baadhi ya mshabiki kufurahisha usajili wa timu zao na wengine kunung'unika.
Timu kubwa zimeingia sokoni kwelikweli zikitapakanya fedha za kutosha kusajili nyota kutoka vilabu mbalimbali.
Dirisha hili kwa upande wa England mpaka wakati huu tayari limeshuhudia timu zikitumia zaidi ya £1.5billion ambayo ni zaidi ya £1.43bn iliyoweka rekodi mwaka 2017 kwa fedha zilizotumika katika dirisha kubwa la usajili la kiangazi.
Lakini pia ni zaidi ya £1.44bn zilizotumika msimu wote uliopita wa mkwa jana.
Ingawa rekodi ya wakati wote ya fedha zilizotumika za usajili ni £1.86bn, kwa masaa haya machache yaliyosalia haitashangaza rekodi hiyo ikivunjwa. Miongoni mwa wanaoweza kusababisha hilo ni wachezaji hawa ambao wanaweza kuhama timu zao leo.
1. Pierre-Emerick Aubameyang
Alikuwa nahodha wa Arsenal, akatibuana na kocha wa timu hiyo Mikael Arteta kabla ya kutimikia Barcelona katika dirisha la mwezi Januari mwaka huu.
Licha ya kuanza vyema na Barca akifunga mabao 13 na kutoa pasi moja ya bao katika mechi 23 alizoichezea timu hiyo, ujuo wa Robert Lewandowski kutoka Bayern Munich katika dirisha hili, umemfanya kutokuwa na uhakika wa namba na sasa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Gabon yuko katika hatua za mwisho kutua Chelsea.
Mazungumzo yalianza kuhusu kutua kwa £25mil ikashuka mpaka £10mil lakini kuumizwa na vibaka nyumbani kwakwe wiki hii kunabadilisha uelekeo wa mazungumzo na huenda akatua kwa mkopo.
2: Marcos Alonso
Mlinzi huyu wa Chelsea anatarajiwa kutua Barcelona kabla ya jua kuzama na kufungwa kwa dirisha la usajili. Mazungumzo yanayoendelea kati ya Barcelona na Chelsea ni kumjumuisha kwenye mpango wa uhamisho wa Pierre Aubameyang. Kwamba Chelsea itoe £10m na Marcos Alonso kwenda Barça, ili Barca imuachie Aubameyang kutua Chelsea.
3. Cristiano Ronaldo
Ingawa kuna ugumu kutokea, waswahili wanasema kila kitu kinawezekana. Mchezaji huyu bora mara tano wa dunia, tangu msimu kuanza hana uhakika wa namba, na hakucheza katika michezo miwili mfululizo ya ligi dhidi ya Liverpool na Southampton.
Kocha wake, Erik Ten Hag anasema yuko katika mipango yake lakini masaa machache yaliobakia yanaweza kubadilisha hali ya mambo kwa kuwa Mreno huyo anasaka timu ya kucheza ligi ya mabingwa Ulaya, United inacheza Europa ligi msimu huu.
Sporting CP, klabu yake ya utotoni ndiyo inayooonekana kuwa klabu pekee inayovutiwa na mpango wa kumrejesha Ureno nyota huyo.
4: Martin Dubravka
Martin Dubravka atakamilisha usajili wake leo na kuwa mlinda mlango mpya wa Manchester Utd akitokea Newcastle. Yeye anatua kwa mkopo kwenda kumsaidia David de Gea
5: Manuel Akanji
Mlinzi huyu wa Borrusia Dortmund amekaribia kabisa kutua Manchester City kwa ada ya £17m . Hata usiku wa jana baada ya City kuilaza Nottingham Forest6-0 kocha wa timu hiyo Pep Guardiola aligusia usajili wa mlinzi huyo.
Tangu ligi kuanza msimu huu City imekuwa na ukuta wa karatasi ikiruhusu mabao 5 mpaka sasa katika mechi tano, ikiruhusu mabao 3 dhidi ya Newcastle na mawili dhidi ya Crystal Palace. Akanji analetwa kuongeza nguvu.
6. Cody Gakpo
Miongoni mwa wachezaji wanaosakwa sana sasa Ulaya ni winga huyu Cody Gakpo wa PSV. Alihusishwa na Manchaster United, Arsenal na Juventus, lakini Leeds United na Southampton wanaonekana wako mstari wa mbele wakiwasilisha maombi yao kwa PSV Eindhoven. Mazungumzo kuhusu ada ya uhamisho bado yanaendelea.
7: Douglas Luiz
Nyota huyu wa Ason Villa amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake, na leo huenda akahama klabu hiyo iliyoanza kwa suasua ligi ya msimu huu, ikitoka kulambwa 2-1 usiku wa leo na Arsenal.
Kocha wa Villa Steve Gerrard alipozungumzia kuhusu Douglas Luiz: “Liko nje ya uwezo wangu suala la Douglas Luiz. Hatuko katika nafasi ya kupoteza wachezaji wetu nyota, lakini wakati huo huo amesalia na mkataba wa mwaka mmoja…”.
Kwa kauli hii lolote linaweza kutokea kwa Luiz, ambapo anasakwa na vilabu vinne Atletico Madrid, Chelsea, Arsenal na Liverpool, huku klabu moja ikitajwa leo kwamba itapeleka ofa ya £20m.
8: Sergino Dest
Hakuwa na tatizo la namba alipojiunga Barcelona mwaka 2020 chini ya kocha Ronald Koeman lakini sasa chini ya Xavi, Mlinzi huyu wapembeni amekuwa na wakati mgumu wa kupata namba, akiwa hajaanza mchezo hata mmoja msimu huu. Na ujio wa mlinzi Jules Kounde ndo unampoteza kabisa.
Inaelezwa Man United inavutiwa naye na itapeleka ofa kwa Mmarekani huyo ikiwa Aaron Wan-Bissaka ataondoka kwa mkopo. Lakini uwezekano mkubwa ni kutua Villarreal ya Laliga.
9: Ainsley Maitland-Niles
Muingereza anayecheza kama beki wa kulia na kiungo wakati, Ainsley Maitland-Niles wa Arsenal na yeye anatarajiwa kukamilisha uhamisho wake wa mkopo kwenda Southampton leo siku ya mwisho ya usajili.
Ataongeza kwanza mkataba Arsenal kufikia 2024 halafu atasaini mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja Saint ambao unakipengelea cha kumnunua moja kwa moja atakapomaliza mkopo wake.
10: Abdou Diallo
Abdou Diallo anasafiri kwenda Ujerumani kwa ndege asubuhi ya leo kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kutua RB Leipzig.
Beki huyu wa kati wa PSG anakwenda kwa mkopo kukiwa na kipangele cha kumnunua moja kwa moja kwa dau la €25m.
Mario Balotelli nae yumo
Mshambuliaji huyu muitalia aliyewahi kuchezea Machester City na Liverpool huenda na leo akakamilisha uhamisho wake kuelekea klabu ya Uswisi, FC Scion. Hii itakuwa klabu ya 11 kuchezea nyota huyo mtata katika maisha yake ya soka.