Upi msimamo wa nchi za Afrika Mashariki kuhusu vita vya Israel-Hamas?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Michael Bishku
- Nafasi, The conversation
Majibu ya baadhi ya nchi za Afrika Mashariki kuhusu mzozo unaoendelea huko Gaza yamekuwa madogo ukilinganisha na majibu ya nchi kama Afrika Kusini. Bunge la Afrika Kusini limepitisha azimio la kutaka kufungwa kwa ubalozi wake mjini Tel Aviv.
Algeria na Afrika Kusini zimekuwa zikiunga mkono zaidi Wapalestina. Hadi sasa ni Afrika Kusini na Chad pekee ndizo zimewaondoa wawakilishi wao kutoka Tel Aviv.
Mwanzoni mwa mzozo wa sasa wa Gaza, Rais wa Kenya William Ruto alionyesha mshikamano wake na Israel na kulaani mashambulizi ya kigaidi dhidi ya raia wasio na hatia wa Israel.
Kwa upande wa Uganda na Tanzania - zililaani aina zote za vurugu na kutaka zisitishwe ili kuzuia vifo zaidi.
Miitikio ya mataifa ya Afrika Mashariki kwa mzozo wa Mashariki ya Kati yanachangiwa na mambo mawili; tishio la ugaidi kutoka makundi ya Kiislamu na maoni ya ndani ya umma.
Nchi hizi tatu haziwezi kubadilisha msimamo wao labda mzozo uliopo uongezeke. Kwa upande mmoja wataendelea kupiga kura katika Umoja wa Mataifa kwa maazimio ya kuwaunga mkono Wapalestina. Na upande mwingine wataendelea kuomba msaada wa kiufundi - hasa katika kilimo na usalama kutoka Israel.
Kenya na Israel

Chanzo cha picha, PSC
Uhusiano kati ya nchi za Afrika na Israel umeingia katika changamoto hapo awali. Mwaka 1973, nchi 25 huru za Afrika zilikata uhusiano wa kidiplomasia na Israel baada ya kuikalia kwa mabavu ardhi ya Misri.
Miongoni mwa mataifa hayo ni mataifa ya Afrika Mashariki; ikiwemo Kenya, ambayo ilikuwa na uhusiano mzuri na wa karibu na Israel tangu uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1963.
Nchi za Afrika Mashariki zilizotawaliwa na Uingereza zilitafuta usaidizi wa kiufundi baada ya uhuru katika sekta ya kilimo. Waliiona Israel kama nchi mbadala ya kupata usaidizi badala ya mataifa makubwa.
Wakati mataifa ya Afrika yalipokataa uhusiano wa kidiplomasia na Israel mwaka 1973, Kenya ilikuwa na kigugumizi lakini hatimaye ilibidi kuungana na mataifa mengine huru ya Afrika.
Hata hivyo, iliendelea na ushirikiano wake na Israel hata kabla ya uhusiano rasmi kurejeshwa mwaka 1988. Iliiwezesha Israel katika operesheni ya uokoaji ya 1974 katika uwanja wa ndege wa Entebbe wa Uganda.
Operesheni hiyo ilikusudiwa kuwaokoa abiria wa ndege wa shirika la ndege la Ufaransa iliyotekwa nyara ilipokuwa ikitoka Israel kuelekea Ufaransa, na kusafirishwa hadi Entebbe.
Tanzania na Israel

Chanzo cha picha, FOREIGN TANZANIA
Tanzania, kwa upande mwingine, ilifuata njia ya kutoegemea upande wowote baada ya uhuru. Ilivutiwa na serikali za chama cha Labour huko Israel - lakini ukaliaji wa maeneo ya Palestina kufuatia Vita vya Siku mwaka 1967 - ulivuruga uhusiano wa nchi hizo mbili.
Tanzania ilikuwa mojawapo ya mataifa ya mwisho Afrika kuanzisha upya uhusiano na Israel mwaka 1994. Ilikuwa ni mwaka mmoja baada ya makubaliano ya Oslo kati ya Israel na Shirika la Ukombozi wa Palestina.
Mwaka 1973 Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza Afrika kulitambua shirika hilo na kukaribisha kuweka ofisi yake katika jiji la Dar es Salaam.
Uganda na Israel

Chanzo cha picha, AP
Uganda imekuwa na uhusiano wenye mvutano zaidi na Israel. Chini ya Idi Amin nchi hiyo ilivunja uhusiano na Israel na kuikumbatia Libya. Israel na Uganda zimekuwa na uhusiano mzuri chini ya Rais Yoweri Museveni.
Kampuni za Israel kwa sasa zinafanya kazi katika sekta ya ujenzi, miundombinu, kilimo na maji, mawasiliano na teknolojia nchini Uganda.
Uganda ilijiunga na nchi nyingine nyingi za Afrika kuanzisha upya uhusiano na Israel baada tu ya kumalizika kwa Vita Baridi.
Israel imekuwa ikifanya kazi kubwa kujenga uhusiano wa kidiplomasia na nchi mbalimbali za Afrika. Kufikia 2023 ina uhusiano na nchi 46 kati ya 55 wanachama wa Umoja wa Afrika.
Usalama na Maoni ya Umma

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kenya imeathiriwa na ukosefu wa utulivu kutokana na kundi la Al-shabab kutoka nchi jirani ya Somalia na imekuwa mwathirika wa mashambulizi ya kigaidi.
Kenya imekumbwa na mashambulizi mpakani na katika jiji kuu Nairobi kutoka al-Shabaab.
1998, al Qaeda ilishambulia ubalozi wa Marekani mjini Nairobi na Dar es Salaam. Shambulizi la Nairobi lilisababisha zaidi ya vifo 200 na maelfu ya watu kujeruhiwa.
Tangu wakati huo, Israel imekuwa mstari wa mbele miongoni mwa mataifa ya kigeni kuisaidia na kuishauri Kenya kiusalama.
Uganda ina matatizo yake ya usalama. Shambulio la kigaidi katika mji mkuu wa Uganda Kampala mwaka wa 2010 lilihusishwa na al-Shabaab. Lakini tishio kubwa zaidi kwa usalama wa Uganda limetoka kwa waasi wa Kiislamu wanaojulikana kama Allied Democratic Forces yenye makao yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kuna sababu nyingine inayoelezea uhusiano wa Afrika Mashariki na Israel; Imani za kidini za watu wa eneo hilo.
Israel ni maarufu kwa Wakristo wengi wacha Mungu wa Afrika Mashariki, kama ilivyo katika bara zima la Afrika. Iwapo Wakristo hawa wangepewa fursa - wangehiji katika ardhi takatifu. Sababu hii ni dhahiri kuwa inaathiri maoni ya umma.
Kinyume chake, Waislamu wa Afrika Mashariki wana wasi wasi kuhusu hali ya Wapalestina. Nchi zote tatu - Kenya, Uganda na Tanzania - zina watu ambao ni waumini wa dini hizi mbili.
Kenya ambapo maoni ya umma yana athari kwa wanasiasa. Hilo limeonekana kutokana na Rais Ruto kulegeza lugha yake baada ya awali kuikosoa vikali Hamas.
Tanzania imeendelea kukemea aina zote za vurugu. Nchi hiyo inataka suluhu ya mataifa mawili katika mzozo wa Israel na Palestina, wito huo hutolewa pia na mataifa mengine ya Afrika Mashariki.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Munira Hussein.












