Mpango wa nyuklia wa Iran unaotia tumbo joto Marekani

Muda wa kusoma: Dakika 6

Iran na Marekani wanafanya mazungumzo ya ngazi ya juu nchini Oman, yanayolenga kuanzisha mazungumzo mapya kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuchukua hatua za kijeshi iwapo makubaliano hayatafikiwa.

Vyombo vya habari vya Iran viliripoti kuwasili kwa wajumbe wa Iran na Marekani katika mji mkuu, Muscat.

Shirika la Habari la Jamhuri ya Kiislamu la Iran limeripoti kuwa Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araqchi, ambaye anaongoza ujumbe wa Iran, yuko Muscat.

Mjumbe wa Trump wa Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi wanatarajiwa kuongoza mikutano ya faragha huko Muscat.

Tehran iko kwenye mazungumzo kwa tahadhari, ikiwa na mashaka kuwa yataleta makubaliano, na ina wasiwasi na Trump, ambaye mara kadhaa amekuwa akitishia kuishambulia Iran ikiwa haitasitisha mpango wake wa nyuklia.

Wakati kila upande imezungumzia fursa ya kupiga hatua, pengo kati yao bado ni kubwa kutokana na mzozo ambao umedumu kwa zaidi ya miongo miwili, na hawajaafikiana iwapo mazungumzo hayo yatakuwa ya moja kwa moja, kama Trump anavyodai, au yasiyo ya moja kwa moja, kama Iran inavyotaka.

Dalili za hatua zozote zinaweza kusaidia kutuliza hali ya wasiwasi nchini Iran ambayo imekuwa ikikabiliana na changamoto kadhaa kama vile vita vya Gaza, uhasama kati ya Israeli na Hezbollah nchini Lebanon, kushambuliana kwa makombora kati ya Iran na Israeli, mashambulizi ya Houthi dhidi ya meli katika Bahari ya Shamu, na kuanguka kwa utawala wa Assad nchini Syria.

Kwa nini Iran hairuhusiwi kuwa na silaha za nyuklia?

Iran inasema mpango wake wa nyuklia ni kwa madhumuni ya kiraia pekee.

Inasisitiza kuwa haijaribu kutengeneza silaha za nyuklia, lakini nchi nyingi - pamoja na shirika la kimataifa la kudhibiti nyuklia, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) – haziamini hilo.

Mashaka juu ya nia ya Iran yaliibuka wakati nchi hiyo ilipogunduliwa kuwa na vifaa vya siri vya nyuklia mnamo mwaka 2002.

Hili lilivunja mkataba unaoitwa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia (NPT), ambao Iran na takriban nchi nyingine zote zimetia saini.

NPT inaruhusu nchi kutumia teknolojia ya nyuklia isiyo ya kijeshi - kama vile dawa, kilimo na nishati - lakini hairuhusu utengenezaji wa silaha za nyuklia.

Je, mpango wa nyuklia wa Iran umeendelea kiasi gani?

Tangu Marekani ilipojiondoa katika mapatano ya nyuklia yaliyopo - yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA) - mwaka 2018, Iran imekiuka ahadi kuu, kulipiza kisasi uamuzi wa kurejesha kwa vikwazo.

Imeweka maelfu ya vinu vya kisasa ili kurutubisha madini ya urani, jambo ambalo lilipigwa marufuku na JCPOA.

Silaha za nyuklia zinahitaji madini ya urani ambayo imerutubishwa hadi 90%. Chini ya JCPOA, Iran iliruhusiwa tu kumiliki hadi kilo 300 (lb 600) za madini ya uranium iliyorutubishwa hadi 3.67% - inayotosha kutengeneza nguvu za nyuklia za kiraia na kwa ajili ya utafiti lakini sio mabomu ya nyuklia.

Lakini kufikia Machi 2025, IAEA ilisema Iran ilikuwa na takriban kilo 275 za madini ya uranium ambayo ilikuwa imerutubishwa hadi 60%.

Hiyo inatosha kinadharia kutengeneza takriban nusu dazeni ya silaha, iwapo Iran itarutubisha zaidi madini ya uranium.

Maafisa wa Marekani wamesema wanaamini kuwa Iran inaweza kugeuza madini ya uranium kuwa nyenzo za kutengeneza bomu moja ndani ya wiki moja.

Hata hivyo, wamesema pia itachukua Iran kati ya mwaka hadi miezi 18 kutengeneza silaha za nyuklia. Wataalamu wengine wanasema silaha ya "kawaida" inaweza kutengenezwa ndani ya miezi sita au chini ya hapo.

Soma zaidi:

Kwanini Trump alijiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia?

Umoja wa Mataifa, Marekani na Umoja wa Ulaya ziliiwekea Iran vikwazo vikubwa vya kiuchumi kuanzia mwaka 2010, kutokana na tuhuma kwamba mpango wake wa nyuklia ulikuwa unatumiwa kutengeneza bomu.

Vikwazo hivyo viliizuia Iran kuuza mafuta katika masoko ya kimataifa na kuzuia $100bn (£77bn) ya mali ya nchi hiyo katika nchi za kigeni.

Uchumi wake ulidorora na thamani ya sarafu yake ilishuka hadi kufikia kiwango cha chini, jambo ambalo lilisababisha mfumuko wa bei kupanda.

Mnamo mwaka wa 2015, Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani - Marekani, China, Ufaransa, Urusi, Ujerumani na Uingereza - walikubaliana na JCPOA baada ya miaka mingi ya mazungumzo.

Pamoja na kuweka kikomo kile Iran iliruhusiwa kufanya na mpango wake wa nyuklia, iliruhusu IAEA kufikia vifaa vyote vya nyuklia vya Iran na kufanya ukaguzi wa maeneo yanayoshukiwa.

Kwa upande wake, mamlaka zilikubali kuondoa vikwazo.

Makubaliano ya JCPOA yalipangwa kudumu hadi miaka 15, na baada ya hapo vikwazo vingeisha.

Donald Trump alipoingia madarakani mwaka wa 2018, aliiondoa Marekani kwenye mazungumzo - ambayo ilikuwa nguzo muhimu ya makubaliano hayo.

Alisema ilikuwa "mpango mbaya" kwa sababu haukuwa wa kudumu na haikushughulikia mpango wa makombora wa balistiki wa Iran, miongoni mwa mambo mengine. Trump aliiwekea tena Iran vikwazo kama sehemu ya kampeni ya "shinikizo zaidi" ili kuishinikiza Iran kujadili makubaliano mapya na wigo mpana.

Uamuzi wa Trump ulishawishiwa na washirika wa kikanda wa Marekani ambao walikuwa wakipinga mpango huo, haswa Israeli.

Israeli ilidai kuwa Iran bado inachunguza mpango wa siri wa nyuklia, na kuonya kuwa Iran itatumia mabilioni ya dola kuondolewa vikwazo ili kuimarisha shughuli zake za kijeshi.

Marekani na Israeli wanataka nini sasa?

Tangazo la Trump kuhusu mazungumzo na Iran lilionekana kuishangaza Israeli. Kwa muda mrefu alisema atafanya makubaliano "bora" kuliko JCPOA, ingawa hadi sasa Iran imekataa kuyajadili tena makubaliano hayo.

Trump ameonya hapo awali kwamba Iwapo Iran haitafanya makubaliano mapya "kutakuwa na mashambulizi ya mabomu".

Mshauri wake wa usalama wa taifa Mike Waltz amesema kuwa Trump anataka "kuvunjwa kabisa" kwa mpango wa nyuklia wa Iran, na kuongeza: "Kilichofanyika, ni utumiaji silaha, na huo ndio mpango wake wa kimkakati wa makombora."

Ingawa Trump alisema kutakuwa na "mazungumzo ya moja kwa moja", Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alisema mazungumzo hayo nchini Oman hayatakuwa ya moja kwa moja.

Alisema Iran iko tayari kuzungumza na Marekani, lakini Trump lazima kwanza akubali kwamba hakutakuwa na "chaguo la kijeshi".

Baada ya tangazo la Trump Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alisema makubaliano pekee yanayokubalika yatahusisha Iran kukubali kuachana na mpango wake wa nyuklia.

Alisema hiyo ilimaanisha: "Tunaingia ndani, tunalipua vifaa, na kuharibu vifaa vyote, chini ya usimamizi na utekelezaji wa Marekani."

Hofu kubwa ya Israeli itakuwa kwamba Trump anaweza kukubali maelewano ya Iran kutii ambao anaweza kusema ni ushindi wa kidiplomasia.

Israeli, ambayo haijatia saini Mkataba wa NPT, inadhaniwa kuwa na silaha za nyuklia, jambo ambalo haithibitishi wala kukanusha.

Inaamini kuwa Iran yenye silaha za nyuklia, ambayo haikubali haki ya Israeli kuwepo, itakuwa tishio kubwa.

Je, Marekani na Israeli zinaweza kushambulia Iran?

Marekani na Israeli zina uwezo wa kijeshi kulipua miundombinu ya nyuklia ya Iran, lakini operesheni kama hiyo itakuwa ngumu na ya hatari, na matokeo yake hayana uhakika.

Maeneo muhimu ya nyuklia yako chini ya ardhi, ikimaanisha kuwa ni mabomu yenye nguvu zaidi ya kulipua yanayoweza kuyafikia.

Wakati Marekani inamiliki mabomu haya, Israeli haijulikani kama iko nayo au la.

Kushindwa kufanikiwa kwa mazungumzo hayo kutazidisha hofu ya vita vikubwa katika eneo ambalo linauza nje asilimia kubwa ya mafuta duniani.

Iran itajilinda yenyewe, ambayo inaweza kujumuisha kushambulia mali ya Marekani katika eneo hilo, na kurusha makombora kwa Israeli.

Iran ilizionya nchi jirani zinazohifadhi kambi za Marekani kwamba zitakabiliwa na "athari kubwa" ikiwa zitashiriki katika shambulio lolote la kijeshi la Marekani dhidi ya Iran.

"Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei, ambaye ndiye mwenye usemi wa mwisho kuhusu masuala muhimu ya serikali katika masuala tata wa mamlaka ya Iran, amempa Araghchi mamlaka kamili katika mazungumzo hayo," afisa wa Iran aliambia Reuters.

Pia, muda wa mazungumzo hayo ambayo yatahusu suala la nyuklia, itategemea uzito na nia njema ya upande wa Marekani," afisa huyo, ambaye aliomba kutotajwa jina kutokana na unyeti wa suala hilo, aliiambia Reuters.

Iran inakataa kujadili uwezo wake wa kujihami, kama vile mpango wake wa makombora.

Soma zaidi:

Imefasiriwa na Asha Juma