'Nasafiri kwa saa 50 kumuona mume wangu kwa dakika 50'

Wakati mwingine, baada ya safari ndefu, wake za wanajeshi hupata muda wadakika chache tu na wenzi wao

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wakati mwingine, baada ya safari ndefu, wake za wanajeshi hupata muda wa dakika chache tu na wenzi wao
    • Author, Ilona Hromliuk
    • Nafasi, BBC News, Ukraine
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Picha hii inakumbusha filamu za Vita vya Pili vya Dunia: mwanamke akiwa amevaa viatu virefu, akimkumbatia na kumbusu askari aliyevaa sare.

Huko mashariki mwa Ukraine, ni jambo limezoeleka kujitokeza hasa nyakati hizi vita kati ya Ukraine na Urusi zikichacha.

Wakati Urusi inakaribia kuadhimisha miaka mitatu tangu kushambulia Ukraine, madhara ya vita yanadhihirika sio tu kwa wanajeshi wa Ukraine wanaopigana mstari wa mbele, bali pia kwa wake zao wanaosubiri kurudi kwa waume zao.

Oksana na Artem walikuwa wameoana kwa miezi 18 wakati vita vilipoanza na Artem alijiunga na jeshi la Ukraine.

Walikuwa na ndoto ya kuwa na mtoto, lakini Artem aliweza kupata mapumziko mafupi tu.

Hivyo, kama Oksana alitaka kuwa naye faragha, alilazimika kufanya safari ndefu kutoka kijijini kwao, Bila Tservka, karibu na Kyiv hadi kanda ya Donetsk mashariki mwa Ukraine, alikokuwa akishika doria mumewe.

Pia unaweza kusoma:
Wanandoa Oksana na Artem.
Maelezo ya picha, Wanandoa Oksana na Artem.

Safari yao ya kwanza ilifanyika mwezi Aprili 2022, ya pili ikafuata mwezi Novemba mwaka huo.

Wakati huo Artem alikuwa akiuguza majeraha aliyoyapata vitani naye Oksana alikuwa anakabiliwa na msongo wa mawazo baada ya mimba kuharibika.

Safari ilikuwa ndefu na ilichosha.

Alikuwa akihitajika kusafiri hadi kanda ya Kharkiv, kisha kutoka huko hadi Donetsk, lakini Oksana alijua kuwa alikuwa na jukumu la kufanya safari hiyo mara kwa mara, kwa matumaini ya kupata mtoto aliyeamua kuwa naye alipoolewa,

Ingawa Artem alikuwa na wasiwasi kuhusu usalama wake kila alipopaswa kuvuka nchi inayoendelea na vita na kufika kwenye eneo la mgogoro.

"Siwezi kufikiria maisha bila kumwona," Oksana alisema katika mahojiano na BBC. "Hizo zilikuwa siku pekee nilizohisi kuwa hai."

Wapenzi hawa walikutana katika kijiji kilichokuwa karibu na eneo linalozozaniwa na walikaa katika jengo ambalo wamiliki wake waliruhusu waishi bila malipo.

Familia zilizokuwa hapo awali hazikuishi tena.

"Ulijisikia furaha kuwa na mumeo, lakini kwa wakati mmoja huzuni kuona picha za wageni waliokuzunguka."

Oksana alihisi uzito wa "maisha yote haya, yaliyoharibiwa na vita."

Talaka zimeongezeka Ukraine

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwezi Februari 2022, zaidi ya wanandoa wengi wamekuwa wakitengana nchini humo.

Shirika la Umoja wa Mataifa linasema watu milioni sita wamekimbia makwao, karibu asilimia 15 ya idadi ya watu wa Ukraine kabla ya vita.

Wanawake na watoto wengi walikimbia makazi yao, kwani sheria ya kijeshi inakataza wanaume kati ya miaka 18 na 60 kuondoka Ukraine.

Wanajeshi walioitwa kwa huduma za usalama wanaruhusiwa likizo ya siku 30 kwa mwaka, na siku 10 za ziada kwa mazingira ya familia ya kipekee.

Katika nchi ambapo wanandoa na familia wanakosa kuwa na muda mwingi pamoja, kiwango cha kuzaliwa kimepungua kwa kiasi kikubwa.

Mnamo mwaka 1991, wakati Umoja wa Kisovieti ulivunjika na Ukraine kuwa nchi huru, watoto 630,000 walizaliwa.

Idadi hiyo imeendelea kupungua, ikiwa 309,000 mwaka 2019. Mwaka mmoja baada ya uvamizi wa Urusi, idadi ya watoto waliozaliwa ilifikia kiwango cha kihistoria cha 187,000.

Kulingana na Wizara ya Haki za Binadamu ya Ukraine, talaka zimeongezeka kwa asilimia 50 katika miezi sita ya kwanza ya 2024.

Safari ni za kutimiza wajibu

Safari za kwenda eneo linalozozaniwa ni ndefu, ngumu na hatari.

Lakini wanawake hawa huamua kusafiri kuona waume zao ambao ni wanajeshi ikiwa njia pekee ya kuhifadhi ndoa zao na familia zao.

Wanawake mara nyingi huchagua kusafiri kwa treni hadi mji wa karibu na kisha kumalizia safari kwa basi au teksi.

Wakati mwingine wanatumia muda mrefu zaidi barabarani kuliko muda wa miadi yao halisi, kwani wanajeshi ambao si kwenye likizo rasmi wanaruhusiwa kuondoka huduma kwa muda mfupi tu.

Natalya na mumewe
Maelezo ya picha, Natalya na mumewe

Natalya alisafiri kutoka Lviv magharibi mwa Ukraine hadi Kramatorsk mashariki kuona mumewe.

Ilikuwa safari ndefu ya kilomita 1,230 na zaidi ya siku mbili (saa 50) barabarani, lakini alifanikiwa kumwona kwa muda mfupi tu, kwani miji mitano ya karibu ilikua ikilengwa na mashambulizi ya mara kwa mara.

"Tulikuwa kwenye jukwaa kwa dakika 50 tu, kisha alinipeleka kwenye treni niliyofika nayo," alisema Natalya kwa machozi. "Lakini dakika hizo 50 zilikuwa za thamani."

Ingawa safari ilimgharimu karibu dola 120, ambayo ni robo ya mshahara wa wastani nchini Ukraine, anasema alijitahidi kumtembelea mumewe kila baada ya miezi miwili au mitatu.

Wameoana kwa miaka 22 na wamelea watoto wawili.

"Safari hizi ni nafasi ya kuhisi tena kuwa familia," alisema Natalya.

Wanajeshi wanaongoja kwa stendi za magari wakiwa na mashada ya maua imekuwa jambo la kawaida nchini Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanajeshi wanaongoja kwa stendi za magari wakiwa na mashada ya maua imekuwa jambo la kawaida nchini Ukraine

Lakini si kila hadithi ya wanandoa waliokutana kwenye eneo linalozozaniwa huwa ina ufanisi na mwisho mzuri.

Baadhi ya wanaweke husafari mwendo ndefu lakini lakini wanaishia kugundua kwamba waume zao wana wapenzi wengine katika mji mmoja wa eneo linalokabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara.

Wakati Urusi ilipoanzisha vita vyake vya siri dhidi ya Ukraine mwaka 2014 na vikosi vya uvamizi vikachukua baadhi ya maeneo ya mashariki mwa nchi, Maria (sio jina lake halisi) alikuwa na mumewe aliyekuwa akihudumu katika eneo hilo muhimu kwa Ukraine.

Alikuwa akisafiri kutoka Kyiv, bila kujali safari ya siku tatu iliyowatenganisha, lakini mambo yalikwenda mrama na akaanza kuugua matatizo ya kisaikolojia baada ya vita.

Alipostaafu jeshini na kurudi nyumbani, alianza kuonyesha mienendo ya kikatili dhidi ya Maria na watoto wao.

Mahusiano ya nje ya ndoa pia yalijitokeza. Walitalakiana haraka.

Aliolewa tena na askari mwingine, lakini Maria hakujali kuhusu kusafiri kumtembelea.

"Kuchumbiana katika eneo linalokumbwa na mashambulizi kila mara hakuokoi familia," alisema.

"Unaweza kuokoa familia ikiwa nyinyi wawili mna maono ya pamoja, ikiwa mnaweza kuzungumza kuhusu malengo ya maisha."

Subira huvuta heri

Tukirejelea wanadoa Oksana na mumewe wanaoishi Bila Tserkva, Oksana amejifungua mtoto wa kiume.

Haya yanajiri baada ya mimba mbili kuharibika , huku mtoto huyu akiwa faraja kwa wanandoa hawa wachanga.

Alitamani sana mumewe kuwa karibu naye katikamazazi yake lakini Artem hakuruhusiwa likizo ya uzazi.

Kwa picha ni Artem na Oksana.
Maelezo ya picha, Kwa picha ni Artem na Oksana.

Dakika chache kabla ya kumzaa mtoto wao,Oksana aliniambia: ''Ni ndoto ya kila mwanamke kuandamana na mumewe wakati anajifungua lakini niko hapa pekeyangu nikiamini wakati sahihi utajiunga nasi,''

Mada zinazofanana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa Ambia Hirsi