Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ndani ya jimbo ambalo vita vya Mashariki ya Kati vinaweza kubadili matokeo ya uchaguzi wa Marekani
Siku ya kupiga kura inapokaribia katika uchaguzi wa rais wa Marekani, jumuiya ya Wamarekani wa Michigan inajikuta katika njia panda.
Huku kura za wajumbe15 za uchaguzi za jimbo hilo (ambazo ni ufunguo wa kuamua matokeo ya uchaguzi) zikining'inia kwenye mizani, Wamarekani wengi wa Kiarabu wanapambana na chaguo ambalo linaonekana kuwa gumu zaidi kuliko hapo awali.
Uamuzi kati ya kumchagua Kamala Harris na Donald Trump sio wa moja kwa moja, haswa kwa wapiga kura ambao vipaumbele vyao vinahusu masuala ya nyumbani na mizozo ya Mashariki ya Kati ambayo inakaribia nyumbani.
Kura za maoni zinaonyesha kinyang'anyiro kati ya wagombea hao wawili kinakaribiana zaidi katika historia, huku Kamala Harris, mgombeaji wa chama cha Democratic, akiongoza kwa sasa katika kura nyingi za kitaifa. Hata hivyo, kama ilivyo kawaida katika chaguzi za Marekani, mfumo wa chuo cha uchaguzi hatimaye utaamua mshindi; na Michigan, kama jimbo kuu la linaloweza kuegemea kokote inaweza kuwa mojawapo ya waamuzi muhimu.
Wamarekani Waarabu, hasa katika miji kama Dearborn yenye wakazi wake wengi Waarabu, wanaweza kushawishi kura katika jimbo ambalo mara nyingi uchaguzi umeamuliwa na kura chache.
Jamii kubwa, iliyogawanyika
Wamarekani waarabu wanaoishi Michigan sio wapiga kura wa kuunga upande mmoja. Huku mamia ya maelfu wakiishi katika jimbo lote, misimamo ya kisiasa na vipaumbele vinatofautiana sana, vikiakisi asili zao tofauti za kitamaduni na maoni yao kuhusu sera ya ndani na nje ya Marekani.
Rima Meroueh, ambaye anaongoza Mtandao wa Kitaifa wa Jumuiya za Wamarekani katika Kituo cha Jumuiya ya Waarabu cha Huduma za Kiuchumi na Kijamii huko Dearborn, aliambia BBC kwamba ni vigumu kukadiria ukubwa kamili wa kura za Waarabu.
Sensa ya Marekani haitambui rasmi Waarabu kama kundi tofauti la rangi, na hivyo kufanya kuwa vigumu kufuatilia idadi, lakini Bi Meroueh anakadiria kuwa kuna angalau wapiga kura Waarabu Wamarekani 300,000 huko Michigan.
Ili kuweka idadi hii katika muktadha, Trump alishinda Michigan mnamo 2016 kwa kura 10,000 pekee. Wakati Joe Biden alichukua jimbo hilo mnamo 2020, kwa kiwango cha 100,000. Kwa hivyo ingawa wapiga kura wa Kiarabu wanawakilisha kipande kidogo cha wapiga kura wa Michigan, wanaweza kuleta tofauti kubwa katika kinyang’anyiro cha karibu .
Bi Meroueh anabainisha kuwa kijadi, wapiga kura Waarabu hawakujitolea kuzungumzia suala moja. Lakini uchaguzi huu, anaongeza, ni tofauti. Tangu vita vya Gaza, kumekuwa na mabadiliko na Bi Meroueh anasema Mashariki ya Kati sasa ndio msingi wa kile ambacho Wamarekani wengi wanajali.
Hata hivyo licha ya mtazamo huu wa pamoja, wapiga kura wanasalia kugawanyika katika njia bora zaidi ya kusonga mbele. Wengine wanaegemea upande wa Trump, wakiamini msimamo wake wa "Marekani Kwanza" unaweza kumaliza vita katika eneo hilo. Wengine wanasema kuwa Harris ana uwezekano mkubwa wa kujihusisha kidiplomasia na kusukuma suluhu za muda mrefu. Na kisha, kuna kundi linalomuunga mkono mgombea wa Chama cha Kijani Jill Stein, ambaye ukosoaji wake wa Marekani kuunga mkono Israel unawahusu sana.
Vita dhidi ya sera ya Mashariki ya Kati
Kamala Harris amejisalimisha kwa jumuiya ya Waarabu, na kuahidi kufanyia kazi usitishaji mapigano katika eneo la Mashariki ya Kati huku akithibitisha kuiunga mkono Israeli.
Hata hivyo, pia amezungumza kuhusu haki za Wapalestina, akitoa wito wa usalama, utu na kujitawala kwa watu wote katika eneo hilo. Ni nafasi isiyoeleweka, lakini ambayo ni ngumu kuuza kwa wapiga kura kama Sam Abbas.
Akiwa ameketi katika mgahawa wake wenye shughuli nyingi wa Dearborn, Bw Abbas anatoa sauti ya kuchanganyikiwa kwa Waamerika wengi wa Kiarabu: anawawajibisha Biden na Harris moja kwa moja kwa umwagaji damu katika Mashariki ya Kati, akiongeza kwamba kila mtu anayemjua anasema hatampigia kura Harris.
Kwa Bw Abbas, uchaguzi huu unaleta utata, kwani anauelezea kama kuchagua kati ya "mtu mwenye maovu madogo kati ya wawili hao ", akiongeza kuwa bado hana uhakika kuhusu ni nani atampigia kura na kuna uwezekano wa kufanya uamuzi wake siku ya uchaguzi.
Trump, kwa upande mwingine - licha ya sera yake ya uhamiaji ambayo imekuwa ikizingatiwa na watu wengi kama chuki dhidi ya Waislamu na Waarabu, na licha ya msimamo wake wa kuunga mkono Israeli na uhusiano wa karibu na Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu - amefanikiwa kushinda idadi ndogo ya wapiga kura wa Kiarabu.
Madai yake kwamba hakuna vita vilivyozuka wakati wa urais wake - na madai yake kwamba vita vya Ukraine na Mashariki ya Kati vingeepukika kama angesalia madarakani - yamegusa hisia kwa wale waliochoshwa na migogoro.
Trump pia ameegemea sana upande wa baba mkwe wa bintiye Mwarabu Massad Boulos, ambaye mtoto wake wa kiume ameolewa na Tiffany Trump. Rais huyo wa zamani hata alisema, kwa kiburi, kwamba mjukuu wake atakayezaliwa hivi karibuni atakuwa nusu Mwarabu.
Kubadili uaminifu
Hisia ya kuchanganyikiwa katika Chama cha Democrats imesababisha upinzani zaidi ndani ya jumuiya ya Waarabu wa Marekani. Kampeni iliyoanzishwa mwaka jana, chini ya jina Abandon Biden na sasa Abandon Harris, imeshika kasi.
Waanzilishi wake wanakishutumu Chama cha Democrats kwa kutoa huduma chache kwa masuala ya Waarabu na Waislamu huku kikishiriki katika kuendeleza ghasia katika eneo la Mashariki ya Kati.
Mmoja wa waanzilishi wa kampeni hiyo, Hassan Abdel Salam, anasema upinzani wao haumpingi mgombea fulani, bali ni jibu la msimamo wa chama hicho unaoiunga mkono Israel.
"Tumefikia hitimisho kwamba vyama vyote vya kisiasa vinadharauliwa," anasema, akisisitiza kwamba Wamarekani Waislamu wanahitaji kuhamasishwa kupiga kura, lakini kwamba "lazima wakatae vyama vyote viwili vya kisiasa".
Kundi hilo limemuidhinisha mgombeaji wa Chama cha Kijani Jill Stein, hata kama kumpigia kura Stein kunahatarisha kuongeza kiwango kwa kumpendelea Trump. Bw Abdel Salam anasema chama cha Democrats kinahitaji kuwajibika kwa kupuuza sauti za Waarabu na Waislamu.
Licha ya kuongezeka kwa mvuto wa Trump huko Michigan, Chama cha Democrats hakikati tamaa. Kimekuwa na uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa Wamarekani wengi wa Kiarabu, hasa tangu mashambulizi ya Septemba 11 na upinzani dhidi ya jumuiya iliyofuata.
Sami Khalidi, ambaye anaongoza Klabu ya Democrats huko Michigan, ana imani kwamba Harris bado anaweza kushinda wapiga kura wa Kiarabu.
Harris amekuwa akitoa wito wa "kuijenga upya Gaza na kuleta misaada zaidi ya kibinadamu kwa Wapalestina", anaiambia BBC, akiongeza kuwa haamini katika "kuikalia tena Gaza" na hilo linawavutia wapiga kura Waarabu Wamarekani.
Bw Khalidi anasema Chama cha Democrats ndicho chombo pekee cha kisiasa kinachowapa Wamarekani utambulisho wanaohitaji na kustahili. Pia anaamini mtazamo wa Kamala Harris kwa Mashariki ya Kati unatofautiana na ule wa Rais Biden na unawapendelea zaidi Wamarekani Waarabu.
Hata hivyo, anadokeza kuwa wengi katika jamii bado hawajafahamu maoni na misimamo yake, akisisitiza haja ya Chama cha Democrats kuendelea na juhudi zake za kuimarisha ushirikiano na mawasiliano na jumuiya hii.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla