Uchaguzi wa Marekani 2024: Je, kwanini watafuta hifadhi wa Afrika wana wasiwasi?

Muda wa kusoma: Dakika 7

Daktari wa Congo, Yves Kaduli, anasema aliikimbia nchi yake baada ya kutekwa nyara na kuteswa.

Kutokana na ongezeko la idadi ya Waafrika wanaotafuta hifadhi na wahamiaji wa kiuchumi nchini Marekani, uchaguzi ujao wa rais unaweza kuunda upya mustakabali wao wote.

"Tunastahili usalama," anasema Dk Yves Kaduli, mtafuta hifadhi mwenye umri wa miaka 38 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo anayeishi Marekani.

"Nina ndoto kwamba nitatetea wale wanaonyanyaswa," anaongeza katika mahojiano ya BBC.

Dk Kaduli anasema mwaka wa 2014, alitoroka mashariki mwa Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo- ambayo imekumbwa na zaidi ya miongo mitatu ya vita - baada ya kutekwa nyara na kuteswa.

Alikuwa akifanya kazi kama daktari katika Hospitali ya Cifunzi iliyopo katika mji wa Kalonge na aliona athari za mzozo huo kwa karibu.

“Wanawake walibakwa. Niliona. Nilihisi mwilini mwangu," aliiambia BBC.

Dk Kaduli anasema kutokana na kushtushwa na vifo vya raia, yeye na wenzake wengi akiwemo mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Dk Denis Mukwege, walishiriki katika maandamano ya kupinga mauaji na ubakaji unaofanywa na makundi yenye silaha, na kuikosoa serikali ya rais wa wakati huo Joseph Kabila kwa kushindwa kwake kuwahakikishia watu usalama.

Daktari huyo anasema hili lilipelekea yeye kulengwa na watu wasiojulikana.

"Walikuja, wakanichukua mimi na mwenzangu mwingine kwa nguvu wakati wa zamu ya usiku," Dk Kaduli anakumbuka, akiongeza kwamba walipelekwa kwenye kambi ya muda katika msitu wa karibu ambapo walipigwa, kuteswa na kutishiwa kuuawa.

Dk Kaduli anasema baada ya kushikiliwa kwa siku moja alifanikiwa kutoroka na kuamua kutoka nje ya nchi.

Akimuacha mama yake na mwanaye mdogo, Dk Kaduli anasema alianza safari ya miaka mitano, akipitia kwanza nchi jirani ya Rwanda, kisha akasafiri kwa ndege hadi Cuba, Ecuador, Nicaragua na hatimaye kufika mpaka wa Marekani na Mexico mwaka 2019.

Unaweza pia kusoma:

"Nilikaa mpakani kwa angalau mwezi mmoja, tulikuwa tukiishi katika mahema madogo katika mazingira ya kinyama."

Dk Kaduli anasema kisha alifaulu kuvuka hadi Marekani na alizuiliwa kwa miezi 15, kabla ya kuachiliwa.

Sasa anaishi Virginia akifanya kazi kama fundi wa kimatibabu, akisubiri uamuzi kuhusu kesi yake ya kuomba hifadhi.

Dk Kaduli ni mmoja wa maelfu ya wahamiaji wa Kiafrika ambao bila shaka wanamaliza safari ndefu na ya hatari ya kuufikia mpaka wa Marekani na Mexico kila mwaka. Idadi ya wale wanaofika kwenye mpaka huo inaongezeka.

Lakini huku Wamarekani wengi wakisema uhamiaji ni jambo muhimu zaidi katika uchaguzi huu, na wagombea wote wawili wakiahidi kuwadhibiti wahamiaji kwenye mpaka huo, watafuta hifadhi wa Kiafrika wana wasiwasi kuwa huenda umma ukawageuka.

"Tunaona wanasiasa wetu wakiigeuza hadhi yetu kuwa uhalifu, kuchafua jamii yetu na wakiwa rais, wanaweza kuamua mustakabali wetu," Dkt Kaduli aliiambia BBC.

Unaweza pia kusoma:

Mnamo 2022, karibu wahamiaji 13,000 wa Kiafrika walisajiriwa kwenye mpaka wa Marekani na Mexico, kulingana na data ya forodha ya Marekani na ulinzi wa Mipaka. Kufikia 2023, idadi hii ilikuwa imeongezeka mara nne hadi 58,000.

Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa wa shirika la huduma kwa wakimbizi (UNHCR) ameripoti ongezeko kubwa la maombi ya hifadhi kutoka nchi za Afrika Magharibi kama vile Senegal, Mauritania na Guinea tangu 2022 katika mpaka huo huo.

Maombi mapya ya hifadhi kutoka kwa raia wa Senegal pekee yalipanda kutoka 773 mwaka wa 2022, hadi 13,224 mwaka wa 2024.

Ingawa Senegal ni tulivu, zaidi ya theluthi moja ya watu nchini humo wanaishi katika umaskini, kulingana na Benki ya Dunia.

Idadi inayoongezeka ya vijana wa Senegal wanachagua kuhamia Marekani badala ya kukabili njia hatari ya kuelekea Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania.

Wanachagua njia inayozidi kuwa maarufu kupitia Nicaragua ambayo ni rafiki kwa visa, ambayo inashirikiwa kupitia mitandao ya kijamii, pamoja na TikTok.

Mnamo Septemba 2023, zaidi ya watu 140 wa Senegal walirejeshwa katika nchi yao baada ya kuvuka mpaka wa Mexico na Amerika.

Watu wanakuja Marekani kwa sababu tofauti, anasema Kathleen Bush-Joseph kutoka Taasisi ya Sera ya Uhamiaji, taasisi isiyoegemea upande wowote inayofadhiliwa na ruzuku za utafiti na taasisi.

"Watu wanaweza kuwa wanakimbia mateso na kutoroka hali ya kiuchumi ambayo inawafanya watoto wao kuwa mgumu, kuna vishawishi vya kuomba hifadhi kwasababu wanaweza kupata kibali cha kufanya kazi wakiwa wanasubiri na hiyo inaweza kuleta mvuto kwa watu wanaotaka kuboresha maisha yao. ," anasema.

Kufanikiwa kudai hifadhi nchini Marekani ni changamoto kwa wahamiaji wa Kiafrika.

Vikwazo vya lugha, ukosefu wa jumuiya unapowasili na ukosefu wa ufahamu wa migogoro ya Kiafrika hufanya mchakato huo kuwa mgumu zaidi kwa Waafrika, anasema Bi Bush-Joseph.

"Majaji na mawakili mara nyingi hawajui hali katika baadhi ya nchi za Kiafrika ambazo watu wanazikimbia," anaiambia BBC.

Pia kuna hatari kwa wale ambao wanashindwa kuingia Marekani.

Mnamo 2022, Human Rights Watch (HRW) ilitoa ripoti inayodai kwamba makumi ya waomba hifadhi kutoka Cameroon walifungwa, kuteswa na kubakwa baada ya kurudishwa kutoka mpaka wa Marekani.

"Watu walifukuzwa moja kwa moja na kurejeshwa kwenye hali ya madhara na mateso na katika mazingira ya migogoro inayoendelea na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu," mtafiti wa HRW Lauren Seigbert anaiambia BBC.

"Ni hatari kubwa tu kurudisha watu nyuma," anaongeza.

Nils Kinuani, ambaye ni meneja wa sera za shirikisho katika African Communities Together, shirika linalounga mkono watafuta hifadhi wa Kiafrika na wakimbizi nchini Marekani, anasema matamshi kuhusu uhamiaji katika kampeni za uchaguzi yamesababisha "hofu kubwa" miongoni mwa jamii yake.

"Watu wana hofu, kuna wasiwasi kwamba mipango ya wakimbizi inaweza kushambuliwa," Bw Kinuani asema.

Shirika lake na mashirika mengine yanatoa wito wa kuwepo kwa njia zaidi za kisheria kusaidia wahamiaji wa Kiafrika ambao wanaogopa kufukuzwa.

Chaguo moja ni hali ya msamaha wa kibinadamu, ulinzi wa kisheria kwa raia wa kigeni kutoka nchi zinazokabiliwa na migogoro kama vile migogoro au majanga ya asili.

Ulinzi huu uweza kutolewa na serikali ya Marekani kuruhusu watu walio katika hatari kuishi na kufanya kazi nchini Marekani kwa muda - mipango ya sasa ni pamoja na Ukraine, Cuba, Nicaragua, Haiti, Venezuela na Afghanistan.

Hakuna programu rasmi za msamaha wa kibinadamu zilizopo kati ya Marekani na nchi yoyote ya Kiafrika.

Bw Kinuani anaongeza kuwa kuna chuki fulani kuhusu jinsi wakimbizi kutoka Ukraine wamekuwa wakitendewa, ikilinganishwa na mataifa mengine.

Wiki chache tu baada ya vita kuzuka nchini Ukraine, raia waliokimbia mzozo walistahili kuomba msamaha wa kibinadamu, anasema.

"Jumuiya za watu kutoka Ukraine hazikuhitaji hata kuuliza au kutetea msamaha wa kibinadamu. Kwa nchi kama Sudan, lazima tuweke msukumo.”

Vita vinavyoendelea nchini Sudan tangu Aprili 2023 vimewalazimu watu milioni tisa kuhama makwao.

Vyama vya Democratic na Republican vimeweka udhibiti wa uhamiaji na utatuzi wa mgogoro wa mpaka wa Marekani na Mexico juu kwenye orodha yao ya ahadi za kampeni.

Iwapo atachaguliwa, mgombea wa chama cha Republican na Rais wa zamani Donald Trump atafanya "operesheni kubwa zaidi ya kuwafukuza katika historia ya Marekani" na kurejesha sera za mpaka zinazokumbusha muhula wake wa kwanza madarakani, kulingana na Jukwaa rasmi la 2024 la Kamati ya Kitaifa ya Republican.

Wakati huo huo, mgombea wa chama cha Democratic na Makamu wa Rais Kamala Harris ameahidi kufufua mswada wa usalama wa mpaka wa pande mbili ambao haukufaulu katika Congress mapema mwaka huu.

Mswada huo "utaongeza wafanyakazi wa hifadhi" na kuhakikisha kunakuwa na mchakato wa "haraka na wa haki" wa kupata hifadhi, kulingana na Ikulu ya White House.

Lakini umepokea ukosoaji kutoka kwa mashirika ya haki za binadamu na UN.

Utawala unaomaliza muda wake wa Rais Joe Biden, ambaye Harris ni sehemu yake, tayari una kabiliana na wahamiaji kwenye mpaka.

Chini ya agizo kuu lililotolewa mwezi Juni, maafisa wanaweza kuwaondoa haraka wahamiaji wanaoingia Marekani kinyume cha sheria bila kushughulikia maombi yao ya hifadhi mara tu kiwango cha kila siku kitakapofikiwa na mpaka "kuzidiwa".

Hii imesababisha kupungua kwa kasi kwa idadi ya watu wanaojaribu kuingia Marekani kupitia mpaka, kulingana na maafisa wa Marekani.

Kwa mara ya kwanza katika takriban miongo miwili, zaidi ya nusu ya Wamarekani wanataka viwango vya uhamiaji vipunguzwe Marekani, badala ya kuwekwa katika kiwango chao cha sasa au kuongezeka, kura ya maoni ya hivi majuzi kutoka kwa uchanganuzi wa kimataifa na kampuni ya ushauri ya Gallup inaonyesha.

"Nchini Marekani kuna ufahamu unaoongezeka kwamba mfumo wa hifadhi ya wahamiani umezidiwa na watu wanadai ni kwasababu hakuna njia nyingine za kuja Marekani," anasema Bi Bush-Joseph.

"Kuchanganyikiwa kwa watu kuhusu kutofanya kazi kwa mfumo wa uhamiaji wa Marekani kunamaanisha kuwa kuna wasiwasi kuhusu idadi ya watu wanaodai hifadhi."

Kwa sasa, Dk Kaduli amekwama na anaweza kuachwa akisubiri miaka minne hadi 10 hadi uamuzi wa ombi lake la hifadhi uchukuliwe.

Anasema kuwa miaka kadhaa iliyopita, baba yake alifariki dunia, lakini hali yake ya sasa haimruhusu kuondoka nchini kwenda kuiona familia yake.

"Ninajisikia vibaya wakati kesi yangu bado inasubiri kuamriwa na ninaona kwenye televisheni hotuba za wanasiasa, lakini najua kama niko hapa ni kwasababu," anasema.

Matumaini yake ya mwisho ni kwamba siku moja mwanaye na mama yake wataungana naye Marekani.

"Ninaamini kuwa Amerika itanipa maadili sawa, kujifanyia kazi, kusaidia familia yangu, na kushiriki katika uchumi wa nchi hii, kwa hivyo niko kati ya shaka na matumaini."

Unaweza pia kusoma:

imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Seif Abdalla