'Je, ni Mwafrika au Mhindi?': Trump ahoji utambulisho wa rangi wa Harris

    • Author, Rachel Looker
    • Nafasi, BBC News, Washington
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Donald Trump ametilia shaka utambulisho wa rangi wa Kamala Harris wakati wa mahojiano makali kwenye kongamano la waandishi wa habari weusi.

Trump alidai kwa uongo kuwa makamu wa rais na mgombea mtarajiwa chama cha Democratic alikuwa ameshikilia utambulisho wake wa Mmarekani mwenye asili ya Kihindi hadi hivi majuzi ambapo, alidai, "kuwa mtu mweusi".

"Sikujua kuwa alikuwa mweusi hadi miaka kadhaa iliyopita alipobadilika kuwa mweusi na sasa anataka kujulikana kama mtu mweusi," alisema katika kongamano la Chama cha Kitaifa cha Wanahabari Weusi huko Chicago Jumatano.

"Kwa hiyo sijui - ni Mhindi? Au ni mweusi?"

Bi Harris alisema matamshi ya Trump ni "mtazamo ule ule wa zamani" wa "kugawanya watu ... na kutowaheshimu".

"Watu wa Marekani wanastahili kiongozi bora zaidi," alisema hilo katika mkutano wa Sigma Gamma Rho huko Houston. "Tunastahili kiongozi ambaye anaelewa kuwa tofauti zetu hazitugawanyi - ni chanzo muhimu cha umoja wetu."

Bi Harris ndiye makamu wa rais wa kwanza mweusi na mwenye asili ya Kihindi, akiwa na wazazi wazaliwa wa India na Jamaica. Alihudhuria Chuo Kikuu cha Howard, chuo kikuu cha watu weusi kihistoria, na kujiunga umoja wa wanawake weusi wa vyuo vikuu uitwao Alpha Kappa Alpha .

Alikuwa mwanachama wa muungano wa wabunge weusi (Congress Black Caucus) baada ya kuingia katika Seneti mnamo 2017.

Kauli hiyo ya Trump ilizua mabishano makali kati yake na mwandishi wa ABC News Rachel Scott, mmoja wa wasimamizi wa hafla hiyo ya Chicago.

"Ninaheshimu upande wowote," Mrepublican huyo alisema akimaanisha utambulisho wa rangi ya Harris. "Lakini yeye hafanyi hivyo kwa sababu alikuwa Mhindi wakati wote na ghafla akageuka na kuwa mtu mweusi."

Katibu wa waandishi wa habari wa Ikulu ya White House, Karine Jean-Pierre alisema hakuna mtu "aliye na haki yoyote ya kumwambia mtu yeye ni nani, jinsi anavyojitambulisha. Hiyo sio haki ya mtu yeyote."

"Nani alimteua Donald Trump kuamua yupi ni mtu mweusi na asiyekuwa mweusi?" aliuliza Mwakilishi Ritchie Torres wa New York. Alimtaja Trump kama "Kumbusho la zamani la taasubi za kibaguzi".

Soma pia:

Mgombea huyo wa chama cha Republican na rais wa zamani ana historia ya kuwashambulia wapinzani wake kwa misingi ya rangi.

Alidai bila ya kuwa na ushahidi kwamba Barack Obama, rais wa kwanza mweusi wa nchi hiyo, hakuzaliwa Marekani.

Trump alimshambulia balozi wa zamani wa Umoja wa Mataifa na mpinzani wake mkuu wa chama cha Republican Nikki Haley kwa kudanganya kuwa hawezi kuwa rais kwa sababu wazazi wake hawakuwa raia wa Marekani alipozaliwa.

Bi Harris amekabiliwa na msururu wa mashambulizi tangu apendekezwe kuwa mgombea wa chama cha Democratic. Warepublican wamekosoa uamuzi huo, wakisema alichaguliwa tu kwa sababu ya rangi yake.

Tim Burchett, mbunge wa chama cha Republican kutoka Tennessee, alimwita "makamu wa rais wa DEI" - akiashiria programu za kuleta,usawa na ujumuishi.

Siku ya Jumatano, Scott alimtaka Trump kufafanua ikiwa anaamini Bi Harris alikuwa "mwandani wa DEI". Alijibu: "Kwa kweli sijui, huenda akawa."

Bi Harris ameelezea jinsi alivyojivunia asili yake ya Kihindi na kwamba mara nyingi alitembelea nchi hiyo.

Mama yake pia aliwakuza binti zake wawili katika utamaduni wa watu weusi wa Oakland, California - ambako alilelewa, alisema.

Trump alishambulia pia sifa za kufuzu za Bi Harris wakati wa majadiliano, akisema alifeli mtihani wake wa uanasheria mwanzoni katika taaluma yake ya uwakili. Kauli ambayo ilipokelewa na manung'uniko kutoka kwa umati uliohudhuria .

"Nawaambia ukweli tu. Hakufaulu mtihani wake wa uwakili na hakufikiria kuwa angefaulu na hakufikiria kuwa angeweza kufaulu na sijui nini kilitokea. Labda alipitishwa, "alisema.

Bi Harris alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha California Hastings,Chuo cha Sheria mwaka 1989. The New York Times liliripoti kwamba alishindwa jaribio lake la kwanza na akafaulu katika la pili.

Mamlaka ya mahakama ya serikali ya jimbo la California inasema chini ya nusu ya wale wanaofanya mtihani huo hufaulu katika jaribio la kwanza.

Majadiliano ya Chicago yalianza na mabishano kati ya Scott na rais huyo wa zamani. Trump alimshutumu mwanahabari huyo kwa kutoa "kutambuliusha vibaya sana" alipoanza mazungumzo akiuliza juu ya ukosoaji wake wa zamani wa watu weusi.

Alimnukuu Trump akiyaita maswali ya waandishi wa habari weusi kuwa ''ya kijinga na ya kibaguzi'' na kwamba ''alikula chakula cha jioni na mzungu mwenye ubabe katika makazi yake ya Mar a Lago''.

"Ninawapenda watu weusi wa nchi hii, nimefanya mengi kwa watu weusi wa nchi hii," alijibu.

Rais huyo wa zamani alikosoa mazungumzo hayo saa chache baadaye kwenye mtandao wake wa kijamii. "Maswali yalikuwa ya kijeuri na mabaya, mara nyingi katika mfumo wa taarifa, lakini tuliiponda!" alisema.

Maelezo zaidi:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Yusuf Jumah