Nani anaweza kuwa mgombea mwenza wa Kamala Harris?

Muda wa kusoma: Dakika 5

Rais wa Marekani Joe Biden siku ya Jumapili alitangaza kujiondoa kwenye kampeni ya kugombea mhuhula wa pili, na kumpendekeza makamu wake Kamala Harris, kuchukua nafasi yake.

"Nataka kumuunga mkono Kamala kuwa mgombea wa chama chetu mwaka huu," aliandika kwenye X. "Wanademocrats - ni wakati wa kujumuika pamoja na kumshinda Trump."

Kuna uwezekano wa Bi Harris kuchukua nafasi hiyo, ingawa sio mchakato wa moja kwa moja.

Viongozi wengine wametajwa kama wanaoweza kuchukua nafasi ya Bw Biden lakini wamemuunga mkono Bi Harris.

Uidhinishaji ukiwa rasmi, mgombea mwenza atahitajika.

Wajumbe watapiga kura mwezi ujao katika Kongamano la Kitaifa la Kidemokrasia kuthibitisha rasmi ni nani atajaza nafasi ya Bw Biden, na mgombea wa makamu wa rais.

Majina yafuatayo yanaweza kuwa kwenye orodha

Soma pia:

Gavana wa Michigan Gretchen Whitmer

Gretchen Whitmer, gavana aliyeongoza kwa mihula miwili katika jimbo la Michigan anazidi kuwa mwanademokrasia maarufu wa Midwest ambaye wadadisi wengi wa kisiasa wanakisia kuwa huenda atagombea urais mwaka 2028.

Amemfanyia kampeni Bw Biden hapo awali na haoni haya kuhusu matarajio yake ya kisiasa.

Aliiambia New York Times kwamba anataka kuona rais wa Kizazi cha X mnamo 2028, lakini aliacha kupendekeza kwamba anaweza kuchukua jukumu hilo.

Mwaka 2022, aliongoza kampeni iliyowaacha Wanademokrasia wa Michigan kudhibiti bunge la jimbo na jumba la gavana.

Hilo lilimruhusu kutunga sera kadhaa endelezi, ikiwa ni pamoja na kulinda uavyaji mimba Michigan na kupitisha hatua za usalama wa kumiliki bunduki.

Bi Whitmer alisema muda mfupi baada ya Bw Biden kujiondoa kuwa kazi yake "itasalia ileile ....nikifanya kila niwezalo kuwachagua Wanademokrasia na kumzuia Donald Trump".

Govana wa California Gavin Newsom

Gavana wa California ni mmoja wa wasimamizi wenye msimamo mkali wa utawala wa Biden.

Mara nyingi ameorodheshwa kama mgombea anayeweza kuwania 2028, lakini wadadisi wengi wa Democratic walikuwa wamependekeza kuwa anaweza kuwa katika kinyang'anyiro cha kuchukua nafasi ya Bw Biden.

Bw Newsom aliinua hadhi yake ya kitaifa katika miaka ya hivi majuzi kwa kuwa mjumbe mkuu wa chama kwenye vyombo vya habari vya kihafidhina, na kupitia mjadala dhidi ya Gavana wa Florida Ron DeSantis mwaka jana.

Alimuunga mkono rais kabla ya tangazo lake.

Alisafiri hadi Washington kuhudhuria mikutano mnamo Julai na Bw Biden na magavana wengine wakuu wa Democrats, na akaongoza hafla ya kampeni ya Biden huko Michigan mnamo tarehe 4 Julai.

Bw Newsom alimsifu Bw Biden kama rais "aliyejitolea" baada ya kujiondoa, na akasema anaunga mkono "mwanamke asiyeogopa" Bi Harris kukabiliana na Trump.

Waziri wa Uchukuzi Pete Buttigieg

Sio siri kuwa Pete Buttigieg ana matarajio ya urais.

Aligombea mnamo 2020 na mara nyingi anatajwa kama mmoja wa wazungumzaji bora wa utawala wa Biden.

Bwana Buttigieg amesimamia mizozo kadhaa ya umma wakati wake kama waziri wa uchukuzi.

Alisaidia kusimamia mwitikio wa serikali kuhusu kudorora kwa treni ya Palestina Mashariki huko Ohio, kuporomoka kwa Daraja la Baltimore na shida ya kupanga ya Shirika la Ndege la Kusini Magharibi mwaka 2022.

Bw Buttigieg alisema kwenye Twitter/X kwamba Bw Biden "amejumlishwa miongoni mwa marais bora na wenye matokeo makubwa katika historia ya Marekani".

Alisema atafanya "yote niwezayo kusaidia kumchagua Kamala Harris Rais ajaye".

Josh Shapiro, Gavana wa Pennsylvania

Viwango vya umaarufu wa Josh Shapiro vimepanda tangu alipoidhinishwa mwaka wa 2022 katika jimbo ambalo nusra linyakuliwe na Trump mwaka wa 2016.

Gavana huyo, ambaye awali aliwahi kuwa mwanasheria mkuu wa serikali, amefanya kazi katika safu za chama wakati wa uongozi wake.

Aligonga vichwa vya habari mwaka jana baada ya kujenga upya kwa haraka daraja lililoporomoka kwenye barabara kuu ya Philadelphia – ikiwa ni ushindi mkubwa wa kisiasa kwa gavana wa awamu ya kwanza.

Ukarabati huo wa haraka ulisifiwa na wengi kama njia bora ya mazungumzo ya miundombinu kwa mgombeaji wa urais wa 2028.

Bw Shapiro alisema Bw Biden ni mmoja wa "marais wenye matokeo makubwa katika historia ya kisasa" na "nitafanya kila niwezalo kusaidia kumchagua Kamala Harris kama Rais wa 47 wa Marekani".

Gavana wa Illinois JB Pritzker

JB Pritzker, gavana wa Illinois, ameinua hadhi yake katika miaka ya hivi majuzi kwa kumkabili Trump kisiasa na kumtetea Bw Biden.

Akiwa Mfanyabiashara bilionea na Mrithi wa msururu wa hoteli za Hyatt - ni mwepesi wa kuchapisha ukosoaji wa Trump kwenye mitandao ya kijamii.

Baada ya mjadala huo alimuita Trump "mwongo" na kusema yeye ni "mtuhumiwa wa makosa 34 ambaye anajijali yeye pekee".

Kama Bi Whitmer, Bw Pritzker ana rekodi ya vipengee vya ajenda kwenye orodha ya Wanademokrats kuhusu masuala kama vile haki za uavyaji mimba na umiliki wa bunduki.

Alisema Bw Biden alikuwa amegombea "mojawapo ya urais uliokamilika na mzuri zaidi katika maisha yetu". Hajazungumzia nani anafaa kumrithi.

Wagombea wengine wanaopigiwa upatu

Orodha ya wanaotarajiwa kuteuliwa kwenye tikiti ya urais inavuka zaidi ya Wanademokrats hawa, kwa kuwa chama kimekuza kiwango kikubwa cha vipaji.

Gavana wa Kentucky Andy Beshear, aliyeongoza kwa mihula miwili katika jimbo la kihafidhina, amepata usikivu wa kitaifa tangu kuchaguliwa tena mwaka jana.

Gavana wa Maryland Wes Moore alijikuta katika uangalizi katika miezi ya hivi majuzi kufuatia kuporomoka kwa Daraja kuu la Francis Scott huko Baltimore.

Maseneta Amy Klobuchar na Cory Booker wamewania urais siku za nyuma na wana sifa fulani miongoni mwa Wanademokrats.

Seneta wa Georgia Raphael Warnock, ambaye alishinda mbio za Seneti zilizokuwa zikishindaniwa kwa karibu katika jimbo la bembea.

Maelezo zaidi:

Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi