Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mafao ya talaka: Jinsi makampuni yanavyosaidia wafanyakazi kukabiliana na talaka
Kuvunja kwa ndoa kunaweza kuwa na mfadhaiko mkubwa.
Kampuni zingine zimetengeneza mifumo ya kusaidia wafanyikazi katika kipindi cha talaka.
Huduma za afya ya akili, matibabu ya uwezo wa kuzaa, likizo ya hedhi yenye malipo, hata kufiwa na mnyama kipenzi - katika miaka michache iliyopita, mafao ya mahali pa kazi yamebadilika ili kuendana na ongezeko la hamu ya wafanyikazi ya kusawazisha maisha ya kazini.
Na kutokana na hilo, baadhi ya makampuni yanatoa usaidizi kwa wafanyakazi kukabiliana na talaka ambayo inaweza kuchukua muda mwingi wa mtu.
"Talaka bila shaka ni mojawapo ya matukio ya maisha yenye uwezo wa kusababisha mfadhaiko mkubwa, na athari ya haraka ya kihisia ya kuvunjika kwa uhusiano inaweza kuumiza sana.
"Afya ya akili inaweza kuathiri uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi," anasema Rebecca Pierce, wakili wa zamani wa familia na mwanzilishi mwenza wa shirika la ushauri la talaka la Pierce & Groves lenye makao yake London.
Anasema mwisho wa ndoa unaweza kuwa "mshtuko mbaya" kwa baadhi ya watu ambao hawakutarajia, na pia inaweza kuwa kazi kubwa kwa kila mtu anayehusika.
"Mchakato wa talaka, hasa masuala ya kifedha yanayohusiana nayo, unaweza pia kuchukuwa muda mwingi na umakini kutoka kwa wahusika wenyewe katika kushughulikia maombi ya wanasheria ya utoaji taarifa na nyaraka fulani."
Mbali na mfadhaiko, hii inaweza kusababisha utoro kwani wafanyikazi huchukua likizo kushughulikia maswala haya, na kuwarejesha wafanyikazi nyuma.
Idadi inayoongezeka ya makampuni yanafahamu matatizo haya - na yana nia ya kuwapa wafanyakazi wao mafao ambayo waajiri hawajatoa tangu jadi.
Baadhi ya makampuni yanatoa likizo ya kulipwa au mipango ya kufanya kazi inayoweza kubadilika ili kuruhusu wafanyakazi wao kushughulikia masuala ya kibinafsi yanayohusiana na kuvunjika kwa ndoa, kama vile mikutano na vikao vya mahakama.
Baadhi yao pia hutoa msaada wa ushauri wa kihisia na kiakili.
Hata hivyo, mafao hayo bado hayajaenea sana, lakini wataalam wanasema yanaweza kuwa muhimu kusaidia wafanyikazi wenye mfadhaiko.
Kusaidia wafanyakazi
Nchini Marekani, kampuni ya uchapishaji ya Hearst ilianzisha mpango wa mafao ya talaka kwa wafanyakazi wake 12,000 kupitia ushirikiano na SupportPay, mfumo wa usimamizi wa usaidizi wa watoto na jukwaa la malipo kwa wazazi wenza, mnamo Septemba 2022.
Mafao kwa wafanyakazi wanaopitia talaka ni pamoja na matibabu ya bure na usaidizi wa kisheria, kulingana na kampuni.
Mpango huu unalenga kushughulikia athari mbaya za talaka zinazoathiri "jinsi [wafanyakazi] wanahisi, vile wanavyofanya kazi zao na ustawi wao kwa ujumla", anasema Maria Walsh, mkuu wa kitengo kinachosimamia mafao hayo.
Na huko Uingereza, mwanzoni mwa 2023, Positive Parenting Alliance (PPA), kikundi cha mashirika nchini Uingereza kinachoangazia watoto wakati wazazi wametengana na kipindi cha talaka, lilitangaza mpango wa kukuza sera zaidi za kifamilia kwa wafanyikazi wanaopitia talaka.
Wametoa wito wa talaka kutambuliwa kama tukio la maisha katika sera za kitengo cha huduma za raslimali watu.
Pia wameomba makampuni kuwapa wazazi kazi rahisi, kuwezesha ufikiaji wa ushauri nasaha na huduma za usaidizi wakati wa talaka kwa wafanyakazi (kwa mfano, mashirika yanayosaidia wazazi wasio na wenzi wa ndoa).
Muuzaji wa mboga kimataifa Tesco ni mojawapo ya makampuni ambayo yamezindua mpango wa mafao ya talaka kulingana na mapendekezo ya PPA nchini Uingereza.
"Tunafikiri kwamba mabadiliko haya yatasaidia wafanyakazi katika kusimamia kile ambacho kinaweza kuwa mojawapo ya matukio magumu zaidi ya maisha ambayo wanaweza kukumbana nayo, ama kupitia rasilimali ambazo tumewezesha upatikanaji wake au kupata majibu kwa urahisi na uelewa kutoka kwa wasimamizi na timu zao," anasema Mustafa Faruqi, mkuu wa kampuni ya malipo na mahusiano mahali pa kazi.
Faida hizi zimewezekana kufikiwa - na zimewekwa kwa wakati mzuri – kwani ilibainika kuwa wafanyikazi wengi wanapitia matatizo ya afya ya akili, na, kwa njia nyingi, kufanya kuwa kawaida mazungumzo ya mfadhaiko mahali pa kazi katika jamii, anasema Peter Cappelli, profesa wa usimamizi katika Shule ya Wharton, na mwandishi wa kitabu, ‘Our Least Important Asset: Why the Relentless Focus on Finance and Accounting is Bad for Business and Employees’.
“Dhana ya zamani ya wafanyakazi ‘kuwa wataalamu na kuacha matatizo yao mlangoni’ imepitwa na wakati,” asema Craig Jackson, profesa wa Saikolojia ya afya ya kazini katika Chuo Kikuu cha Jiji la Birmingham, Uingereza.
Mabadiliko haya ya mafao yanaweza kuwakilisha kiini cha vuguvugu ambalo limekuwa likifanya kazi tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000 - kuongeza ufahamu kuwa afya kamilifu ya wafanyakazi ni muhimu mahali pa kazi.
Kwa hakika, waajiri wanazidi kufahamu athari za kisaikolojia za talaka, anaongeza Jackson, ambaye amefanya utafiti kuhusu athari za talaka.
Anaamini mfadhaiko huu unaozidi kuongezeka, pamoja na kuongezeka kwa viwango vya talaka baada ya janga la corona katika baadhi ya nchi, kumemaanisha kuwa kampuni zina nia ya kuweka hatua za usaidizi.
Ni 'Biashara ya busara'
Kuanzisha mafao haya pia ni jambo zuri kwa biashara, anasema Capelli.
Katika soko dogo la wafanyikazi, anasema, waajiri "wana ufahamu zaidi wa kufanya mambo ambayo yanaweza kuwafanya wafanyikazi kendelea kuwa nao.".
Mara nyingi kwa biashara au shirika, inaweza kuwa na maana ya kifedha, pia.
"Faida kama hizi zinaweza zisigharimu kiasi kikubwa – kwa sababu hazitumiwi mara kwa mara - na ni rahisi zaidi kutekelezwa kuliko kushughulikia sababu za msongo wa mawazo mahali pa kazi," anaongeza.
"Kuchukua hatua sasa kusaidia kupatanisha athari za talaka kwa wafanyakazi na waajiri wao ni jambo la busara," anakubali Jackson.
"Inachukulia watu kama rasilimali muhimu ambao watajibu vyema kwa usaidizi wa haraka wakati wa dhiki.
Mahali pa kazi penye kutoa usaidizi kama huu, wafanyikazi watarejea kazini na kufanya kazi kikamilifu baada ya talaka haraka kuliko sehemu za kazi zisizo na msaada huu.”
Vile vile, anaamini kujumuisha mafao haya ni ufunguo wa kuridhika kwa mfanyakazi - zana nyingine ambayo inaweza kupunguza ushupavu.
“[Sera hizi] hazitaongeza viwango vya talaka … lakini zitawaruhusu wafanyakazi kuendelea na kazi zao huku wakipitia mojawapo ya uzoefu mgumu zaidi wa maisha yao. Hii inaongeza uaminifu wa wafanyakazi na mafao yote yanayoambatana nayo,” anasema.
Hata kama kampuni zingine zinatoa mafao haya, hata hivyo, Jackson anaonya wafanyikazi wasitarajie hatua hii kuchukuliwa na kampuni zote.
"Baadhi ya makampuni ambayo hayaendelei sana yanaweza kuwa na wasiwasi kwamba mafao kama haya yanaweza kutumiwa vibaya na baadhi - kwa mfano, kuchukua muda mwingi wa kupumzika - na matatizo yanaweza kutokea wakati wa kujaribu kutumia mafao kama hayo kuwa haki," anasema.
Kwa mfano, anasema Jackson, inaweza kuwa haijulikani vizuri ni nani anahitimu kupata mafao haya - kama ni kwa wanandoa waliooana kihalali pekee , au inajumuisha hata wafanyakazi wanaoishi pamoja lakini bado hawajafunga ndoa.
Hatimaye, hata kama yatatolewa polepole, mafao ya talaka yanaweza kusaidia sehemu kubwa ya wafanyakazi kimataifa, kwani ni wafanyakazi wengi hupitia talaka.