Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini talaka za uzeeni zinaongezeka?
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 76 hajihusishi na dansi wala kuimba kama ilivyo kwa wengi kwenye mtandao wa Tik Tok, lakini video zake - ambazo anasimulia, kwa mfano, namna alivyokua akienda kufanya manunuzi bila mume wake zimepata maoni zaidi ya milioni 3.5.
Mama wa mabinti watatu na nyanya wa wajukuu sita, Sedano alitengana na mume wake Mmarekani miaka tisa iliyopita, baada ya miongo minne ya ndoa.
"Wakati uhusiano haupo tena, unachukua muda wako utulize akili na uanze kuishi maisha yako", aliiambia BBC News Mundo.
Maneno yake yanaangazia mawazo ya watu wengi wakati ambapo, kwa ujumla, watu wanaishi kwa muda mrefu na kufikia uzee wakiwa katika hali bora ya afya ya kimwili na kiakili ikionekana kuwa maendeleo ya sasa hivi.
Mwenendo huo ni maarufu sana hivi kwamba umesababisha watafiti wa Marekani kama vile Susan L. Brown kubuni neno kuhusu hili: "talaka ya uzeeni."
Neno hilo kwa kawaida hurejelea talaka ya watu wenye umri wa miaka 50 na zaidi wanaoamua kuwaacha wapenzi wao baada ya miaka mingi ya ndoa.
"Talaka haionekani tena kama kitu cha unyanyapaa kama ilivyokuwa hapo mwanzoni, inaonekana kuwa ya kawaida zaidi", anaelezea mwanasaikolojia na mwandishi Silvia Congost.
"Wakati talaka inaendelea kuwa jambo la kawaida, pia imeongezeka sana enzi hizi."
"Aidha, umri wa kuishi unaongezeka, tunapofikisha miaka 65, tuna wastani wa miongo miwili ya maisha mbele yetu, na ikiwa mtu hana furaha, hataki tena kuishi na mtu aliye naye. Anajua fika kwamba ana chaguzi zaidi."
Kulingana na utafiti wa Susan L. Brown, ambaye anaongoza kituo cha utafiti wa ndoa na familia katika Chuo Kikuu cha Bowling Green State nchini Marekani, idadi ya talaka za uzeeni iliongezeka mara mbili kati ya 1990 na 2010 nchini humo.
Katika kizazi kilichopita, talaka na wenzi wa ndoa wenye umri wa miaka 50 na zaidi ilikuwa chini ya 10% .
Leo, zaidi ya 25% ya waliotalikiana wana zaidi ya umri wa miaka 50.
Nchini Brazili, mwaka wa 2021, 25.9% ya waliokuwa wametalakiana waolithibitishwa katika tukio la kwanza la utafutaji Haki walikuwa na umri wa zaidi ya miaka 50, kulingana na uchunguzi wa BBC na data kutoka Taasisi ya Jiografia na Takwimu ya Brazil (IBGE).
Mnamo 2019, asilimia ilikuwa chini kidogo, 25.2%. Ripoti hiyo haikuweza kupata data ya miaka iliyopita kwa kutumia mbinu sawa.
Bado kulingana na ripoti ya IBGE, mnamo 2021, wakati wa kutalakiana, wanaume walikuwa na wastani wa miaka 43.6 na wanawake, miaka 40.6.
Wakati huo huo, mwaka wa 2010, muda wa wastani kati ya tarehe ya ndoa na tarehe ya kutolewa kwa uamuzi wa talaka au kuanza kutekelezwa kwa kitendo hicho ilikuwa karibu miaka 16.
Mnamo 2021, muda huu ulipungua hadi miaka 13.6.
Nchini Mexico, idadi ya watu zaidi ya umri wa miaka 50 waliotalikiana imeongezeka katika kipindi cha miaka kumi, kutoka talaka 10,531 zilizosajiliwa mwaka 2011 hadi 28,272 mwaka 2021, kulingana na data kutoka Taasisi ya Kitaifa ya Takwimu na Jiografia (INEGI).
Uhispania, ni mfano mwingine wa mwelekeo huu, watu 34,449 wenye zaidi ya miaka 50 walitalikiana mnamo 2021, ikilinganishwa na 24,894 waliosajiliwa mnamo mwaka 2013, kulingana na data rasmi.
'Kwa siku nilizosalia nazo maishani mwangu, sitaki matatizo yoyote'
"Wakati wa kustaafu unapowadia, wanandoa wengi zaidi na zaidi hawataki tena kuwa pamoja", anachambua Sacramento Barbas, mpatanishi na mwanasaikolojia katika taasisi ya ATYME, mwanzilishi katika utekelezaji wa mbinu za upatanishi nchini Uhispania.
Baadhi ya misemo ambayo yeye na wenzake huisikia mara kwa mara ni pamoja na: "'Kwa siku nilizosalia nazo maishani mwangu, sitaki matatizo yoyote' " na "Simtambui mpenzi wangu, ni kama mtu mwingine yeyote yule".
Lakini, kulingana na mwanasaikolojia, "wakati mwingine ni watoto wakubwa ambao huwa vikwazo, kwa sababu hawataki wazazi wao watengane".
Beatriz Goldberg, mwanasaikolojia wa Argentina ambaye ni mtaalamu wa migogoro ya mtu binafsi, anasema kwamba watu wanaopitia talaka za uzeeni mara nyingi huingia katika mahusiano mapya na matarajio tofauti.
"Kuna watu ambao wanahisi kwamba mwenzi mpya ni kwa ajili ya kufurahia maisha zaidi, na mwingine alikuwa kwa ajili ya kujenga familia", asema Goldberg, mwandishi wa vitabu.
Maisha yanapofika katikati, yanaashiriwa na mabadiliko muhimu maishani.
Watoto hukua na kuondoka nyumbani kila mmoja akashika shughuli zake, wakati taaluma zinaweza kurudi nyuma na pia wazazi wakastaafu.
Bila utaratibu wa kila siku wa malezi ya watoto na saa nyingi kazini, wenzi wa ndoa wanaweza kuona kuwa wanaendana kwa mambo kidogo sana.
Talaka ya uzeeni kawaida haitokei kwa sababu ya tukio fulani, lakini mara nyingi ni matokeo ya watu kuishi mbali mbali, wataalam wanaelezea.
Mbali na kufanya talaka kuwa kitu cha kawaida, leo hii pia tunathamini uhuru wa wanawake.
"Sisi wanawake tunatambua kwamba hatupaswi kuvumilia mambo fulani ambayo bibi zetu walivumilia.
Mfano ni familia ambayo mtu kumuunga mkono mwingine sio lazima tena", anaeleza Silvia Congost.
"Ikiwa huna furaha, unajua huna haja ya kukubali hilo tena. Kiwango cha uvumilivu katika baadhi ya matukio ni cha chini."
Kutalakiana ukiwa na umri wa miaka 65
Aída Sedano aliolewa akiwa na umri wa miaka 24, lakini punde akagundua kuwa ndoa haikuwa vile alivyofikiria.
Akiwa amejifungia nyumbani kwake Tijuana siku nzima na binti zake na kulazimishwa kuacha kufanya kazi ya ualimu kijijini, taaluma aliyoipenda, alitazama kwa macho miaka ikipita.
"Nilizungumza na shangazi zangu na kusema kwamba sipendi uhusiano huo, kwamba hakuja nyumbani, alikuwa anakunywa pombe, alitumia pesa nyingi. Na kila mtu aliniambia: Una nyumba nzuri, una samani nzuri, unavaa vizuri. Hakuna kinachokosekana," aliambia BBC News Mundo.
Hatimaye Sedano alipohamia San Diego pamoja na mume wake, alifanikiwa kurejea chuoni kusomea ualimu akiwa na umri wa miaka 45.
"Niliporudi chuo kikuu ndipo nilianza kujifunza kwamba sisi wanawake tuna haki, kwamba ulimwengu ulikuwa umebadilika." Hatimaye, akiwa na umri wa miaka 65, aliamua kumwacha mumewe – jambo analokubali lilikuwa "ngumu sana".
"Maumivu hufika mwisho."
"Mimi ni mwanamke wa kawaida ambaye niliteseka na nilipata namna ya kuungana na wengine kupitia video na kuwa na marafiki," anasema kuhusu akaunti yake ya TikTok.