Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Hage Geingob: Rais wa Namibia afariki dunia
Rais wa Namibia Hage Geingob amefariki dunia wakati akipokea matibabu hospitalini katika mji mkuu, Windhoek.
Makamu wa rais Nangolo Mbumba ametangaza kuwa Geingob alifariki Jumapili alfajiri.
"Mkewe Monica Geingos na wanawe walikuwa karibu naye," Mbumba alisema katika taarifa yake.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 aligunduliwa kuugua saratani na alitangaza hali yake mbele ya umma mwezi uliopita.
Ofisi yake ilitangaza kwamba angesafiri kuelekea Marekani kupata matibabu, lakini kwamba angerudi Namibia Februari 2.
Geingob aliapishwa kuwa rais mnamo 2015 na alikuwa anatumikia awamu yake ya pili na ya mwisho uongozini.
Alifanyiwa upasuaji wa moyo mwaka jana, na mnamo 2014 alifichua kuwa amepona saratani ya tezi dume.
Namibia inatarajiwa kuandaa uchaguzi mkuu mwezi Novemba.
Chama tawala cha Swapo ambacho kimekuwa madarakani tangu 1990, kimemteua Bi Nandi-Ndaitwah kama mgombea urais.
Yeye ndiye Waziri mkuu wa sasa na iwapo atashinda, atakuwa rais wa kwanza mwanamke nchini humo.
Viongozi watuma risala za rambirambi
Tayari baadhi wa viongozi barani Afrika wakiwemo marais wa mataifa mbali mbali wameanza kutuma risala za rambirambi kwa taifa la Namibia na familia ya marehemu.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika ujumbe wa rambirambi uliochapishwa katika mtandao wa x zamani Twitter amemuomba mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.
Wakati huohuo Rais wa Kenya William Ruto amesema Rais Geingob alikuwa kiongozi mashuhuri aliyetumikia watu wa Namibia kwa umakini na kujitolea.
Katika ujumbe wake kwa mtandao wa x , Rais Ruto amesema kwamba kiongozi huyo alikuwa muumini wa Afrika iliyounganishwa na alikuza sana sauti na mwonekano wa bara hili katika nyanja ya kimataifa.
Amemuomba Mungu awape nguvu na ujasiri wananchi wa Namibia katika kipindi hiki kigumu.
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alisema Dk. Hage G. Geingob alikuwa kiongozi mashuhuri aliyejitolea maisha yake kuwatumikia watu wake na alikuwa sauti ya kuheshimiwa katika bara la Afrika.
Alisema: Katika kipindi hiki kigumu, tunasimama kwa mshikamano na familia yake na watu wa Namibia wanapoomboleza kuondokewa na kiongozi mkuu.
Kiongozi wa Upinzani nchini Kenya Raila Odinga alisema bara la Afrika limepoteza mwana-Pan-Africanist wa kweli.
Raila Odinga: Urithi wake kama kinara wa mapambano ya ukombozi na mbunifu wa katiba ya Namibia utarejea milele katika mioyo ya watu wake na kote barani Afrika.
Rais Everiste Ndayishimiye wa Burundi alisema tumesikitishwa sana na msiba mkubwa wa kiongozi mwenye maono, Mheshimiwa Dkt @hagegeingob,Rais wa Namibia.
Kwa niaba ya Serikali na watu wa Burundi, natoa rambirambi na rambirambi zetu za dhati kwa watu wa Namibia na familia inayoomboleza katika kipindi hiki kigumu.