Lifahamu taifa la Afrika lenye mpango mkubwa wakuongeza nguvu ya haidrojeni

"Kwa hivyo, hatimaye sasa tuko kwenye ramani," anasema Philip Balhoa kuhusu Lüderitz, mji wa kusini mwa Namibia, ambapo jangwa hukutana na bahari isiyo na rangi.

Mji huo wa bandari hapo awali ulinufaika kutokana na almasi na ongezeko la uvuvi, lakini sasa unapambana na viwango vya juu vya ukosefu wa ajira na miundo mbinu iliyozeeka.

Mradi unaopendekezwa wa hidrojeni ya kijani umewekwa kuwa "mapinduzi ya tatu ya Lüderitz," anasema Bw Balhoa, mwanachama wa baraza la mji.

Ana matumaini kuwa mradi huo utatoa mafunzo na kuajiri watu wa ndani, au "Buchters" kama wanavyojiita kwa upendo - na kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira cha 55%.

"Kwa mji ambao kwa kweli umekuwa ukijitahidi kiuchumi katika kipindi cha miaka 10 au 15, labda zaidi, hili ni jambo ambalo watu wanalifurahia sana," anasema.

Mradi huo utakuwa karibu na mji katika Mbuga ya Kitaifa ya Tsau //Khaeb, na hatimaye kuzalisha takriban tani 300,000 za hidrojeni ya kijani kwa mwaka.

Kwa maneno rahisi, nishati mbadala kutoka kwenye jua na upepo itatumika kutenganisha molekuli za hidrojeni kutoka kwenye maji.

Molekuli hizo za hidrojeni katika umbo safi au katika amonia ya kijani kibichi inaweza kutengeneza bidhaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na nishati endelevu.

Mzabuni anayependekezwa, Hyphen Hydrogen Energy, anatazamiwa kuanza uzalishaji mwaka wa 2026 na atakuwa na haki za mradi kwa miaka 40, mara tu michakato muhimu ya upembuzi itakapokamilika.

Kampuni hiyo inasema miaka minne ya ujenzi huenda ikatengeneza nafasi za kazi 15,000 za moja kwa moja na 3,000 zaidi wakati wa operesheni kamili - na kwamba 90% yao itajazwa na wenyeji.

Bw James Mnyupe ni mshauri wa rais upande wa uchumi wa serikali ya Namibia na kamishna wa hidrojeni.

Anafafanua kuwa eneo la Lüderitz ni bora, kwa sababu ya rasilimali nyingi za jua na upepo na ukaribu wa bahari, kama chanzo cha maji na bandari.

Bw Mnyupe anasema hii yote ni sehemu ya mpango wa mabadiliko nchini Namibia na Rais Hage Geingob.

"Rais alikuwa na nia ya kuandaa mpango wa kufufua uchumi ambao ni msikivu, unaofaa kimataifa, na wa utaratibu."

Hii ni sehemu ya maendeleo makubwa zaidi yanayochochewa na hidrojeni ya kijani ambayo serikali inatarajia kupata ufadhili, kupanua katika kilimo, uendeshaji wa kazi na nishati.

Bw Mnyupe anazungumzia treni za kijani za hidrojeni na mabomba ya kufanya biashara na nchi jirani.

Kuna matumaini ya kuunda umeme mbadala, kwa ajili ya kuuza nje na kama mbadala wa nishati ya makaa ya mawe kutoka kutoka Afrika Kusini.

"Wazo ni kugeuza Namibia kuwa sio tu kitovu cha kijani kibichi cha hidrojeni, lakini kuwa chanzo cha nishati ya viwandani," anasema.

Athari hiyo inatazamiwa kuwa ya kimataifa, huku mikataba ikiwa tayari imesainiwa na Ujerumani, Ubelgiji na Rotterdam nchini Uholanzi.

Hii inakuja na baadhi ya mikataba ya ufadhili, lakini Namibia inaangalia namna nyingine kama kuweka uhusiano wa nishati kijani kuwa endelevu, na kufika takriban $9.4bn (£7.1bn) zinazohitajika kwa mradi wa awali.

Kuweka ukubwa wa uwekezaji katika mtazamo - wa Pato la Taifa la Namibia mwaka 2020 lilikuwa $10.7bn tu.

"Watu wanaweza kuanza kutuchukulia kwa uzito kama washirika wa kibiashara, na sio wapokeaji wa jumla wa usaidizi wa maendeleo," anasema Bw Mnyupe.

"Kwa Namibia wa kawaida, hii ina maananisha matumaini."

Bwana Balhoa anatarajia kwamba mpango huo wa biashara utaimarisha miundombinu huko Lüderitz, kama barabara na hospitali, na kwamba mradi huo utavutia uwekezaji zaidi kutoka kwa serikali kuu katika eneo hilo.

Lakini matumaini huja na wasiwasi unaolingana.

Bwana Balhoa anasema miradi mikubwa ya awali haijawekeza katika jamii kama ilivyotarajiwa.

Wasiwasi ni kwamba mji mdogo hautaweza kukidhi mahitaji ya miundombinu yaliyoongezeka - na nyumba zinazopatikana tayari kuwa changamoto kubwa.

"Ninaamini kuwa mradi huu utaleta mabadiliko, sio tu kwa Namibia, lakini kwa bara la Afrika," anasema Kennedy Chege, mtafiti na mwenyekiti wa utafiti wa Sheria ya Madini Afrika, Chuo Kikuu cha Cape Town.

Lakini ameonya kuwa changamoto kuu ni ufadhili:

"Kujaribu kuandaa mipango ya nishati mbadala kwa kawaida kunahitaji fedha nyingi sana, na serikali yenyewe haina uwezo wa kutoa fedha hizo kupitia bajeti yake.

Hivyo unahitaji ufadhili kutoka kwa sekta ya umma na sekta binafsi."Bw Chege anasema ushirikiano wa kimataifa wa Namibia ni ishara chanya.

Changamoto nyingine ni kiwango cha maji kinachohitajika kuzalisha hidrojeni.

Kufanya hivi kwa kuondoa chumvi, kama Namibia inavyopanga, kunaweza kuwa ghali - kama vile michakato ya kielektroniki inayotumika baadaye katika mchakato wa kutengeneza hidrojeni.

Bw Chege anasema wasiwasi kuhusu uwezekano wa mradi huo na kuunda aina ya miundombinu inayohitajika ni halali, lakini ana matumaini akilinganisha faida ambazo Namibia itazipata.

Wakati nchi kadhaa barani Afrika, kama Afrika Kusini, Kenya na Nigeria zinatengeneza mipango ya hidrojeni ya kijani, Namibia ndiyo iliyoendelea zaidi.

"Lakini katika suala la utekelezaji, hakujawa na maendeleo mengi katika suala hilo, kote barani Afrika."

Wakati kuna mengi ya kufanywa, Namibia inasonga mbele - kiasi kwamba serikali inaweza kutangaza wito wa mapendekezo ya mradi wa pili wa hidrojeni ya kijani kibichi mapema Januari 2022.