Vita vya Ukraine: Zelensky aamuru raia kuhama mkoa wa Donetsk

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameamuru raia wote ambao bado wanaishi katika maeneo ya mashariki mwa mkoa wa Donetsk chini ya udhibiti wa Ukraine kuhama.
Akizungumza wakati wa hotuba ya usiku wa manane kutoka Kyiv, Bw Zelensky alionya kuhusu kuongezeka kwa mapigano.
Eneo hilo limeshuhudia mapigano makali huku kukiwa na mwendo wa polepole wa vikosi vya Urusi kusonga mbele, ambavyo tayari vinadhibiti sehemu yake kubwa.
‘’Jinsi watu wengi watakavyoondoka katika mkoa wa Donetsk sasa, ndivyo jeshi la Urusi litakavyokuwa na watu wachache kuwaua, kiongozi huyo wa Ukraine alisema.
‘’Tutatumia fursa zote zinazopatikana kuokoa maisha ya watu wengi iwezekanavyo na kupunguza ugaidi unaotekelezwa na Urusi kadiri iwezekanavyo.’’
Kuingilia kati kwa Bw Zelensky kunakuja wakati Urusi imewaalika maafisa wa Umoja wa Mataifa na Msalaba Mwekundu kuchunguza vifo vya wafungwa 50 wa vita wa Ukraine katika sehemu nyingine ya mkoa wa Donetsk inayoshikiliwa na watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi.
Wanajeshi hao waliuawa katika hali isiyoeleweka wakati wa shambulio dhidi ya gereza moja huko Olenivka, na pande zote mbili za kulaumiana.
Wakizungumza Jumamosi jioni, maafisa wa ulinzi wa Urusi walisema Moscow itakaribisha uchunguzi wenye ‘’malengo’’kuhusu tukio hilo.

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Shirika la Msalaba Mwekundu lilisema siku ya Ijumaa lilikuwa linaomba ufikiaji wa kituo cha kizuizini kinachoendeshwa na Urusi na wafungwa walionusurika - lakini haikupewa ruhusamoja kwa moja.
Naibu mkuu wa ujumbe wake nchini Ukraine, Daniel Bunnskog, alisema kutoa fursa kwa wafungwa wa kivita ni wajibu chini ya Mikataba ya Geneva.
Kambi ya gereza ya Olenivka inadhibitiwa na eneo la Donetsk lililojitangazia uhuru wake linaloungwa mkono na Urusi.
Kilichotokea hapo Ijumaa bado hakijafahamika.
Picha za video za Urusi ambazo hazijathibitishwa za matokeo zinaonyesha msongamano wa vitanda vilivyoharibika na miili iliyoungua vibaya.
Siku ya Jumamosi, Urusi ilichapisha orodha ya kile ilichosema ni wafungwa wa kivita 50 waliouawa katika shambulio hilo.
Moscow inasema shambulio hilo lilitekelezwa na Ukraine kwa kutumia mfumo wa mizinga wa HIMARS uliotengenezwa Marekani.
Kyiv inakanusha kutekeleza shambulizi hilo na inadai kuwa Urusi ilifyatua risasi kwenye kituo hicho ili kuficha ushahidi wa uhalifu wa kivita.

Chanzo cha picha, EPA
Kwingineko, maafisa wa Ukraine waliitaja Urusi kama ‘’nchi ya kigaidi’’ baada ya ubalozi wa Moscow nchini Uingereza kutuma ujumbe kwenye Twitter kwamba wanajeshi wa Kikosi cha Azov cha Ukraine walistahili ‘’kifo cha kufedhehesha’’ kwa kunyongwa.
Twitter ilikubali kwamba chapisho hilo kutoka kwa ubalozi wa Urusi lilikiuka ‘’sheria za kampuni ya mitandao ya kijamii kuhusu mienendo ya chuki’’ - lakini ikaongeza kuwa inaweza kuwa kwa manufaa ya umma kuiweka wazi ili waweze kuufikia.
Ujumbe huo uliyotumwa Ijumaa usiku ulisema kwamba Azov ‘’wanamgambo wanastahili kunyongwa, lakini kifo sio kwa kupigwa risasi bali kwa kunyongwa, kwa sababu sio wanajeshi wa kweli. Wanastahili kifo cha fedheha’’.
Tweet hiyo ilijumuisha klipu ya video inayowaonyesha wanandoa katika jengo lililoharibika, wakiwatuhumu wanajeshi wa Azov kwa kushambulia nyumba yao.
Wito wa ubalozi wa kunyongwa unarudia kile mtu aliye kwenye video anasema.
Wanajeshi wa Azov walilazimika kuweka silaha chini mwezi Mei baada ya kulinda vikali kwa wiki nzima kiwanda cha chuma cha Azovstal, kikubwa zaidi katika bandari ya kusini-mashariki ya Mariupol ambacho hatimaye kilitekwa na Urusi.
Kikosi cha Azov ni kikundi cha wazalendo chenye uhusiano na mrengo mkali wa kulia kilipoanzishwa mwaka wa 2014. Baadaye kilijumuishwa katika Walinzi wa Kitaifa wa Ukraine.
Kwa muda mrefu Urusi imekuwa ikishutumu kikosi hicho kwa kuwa Wanazi mamboleo na wahalifu wa vita, kama sehemu ya kampeni ya propaganda ya Kremlin kuhalalisha uvamizi wake dhidi ya Ukraine wa tarehe 24 Februari 2022.












