Jinsi umoja wa familia ulivyomsaidia Kylian Mbappe kupata umaarufu

Chanzo cha picha, BBC Sport
Macho yote leo yako kwa mchezaji wa soka wa Ufaransa Kylian Mbappe.
Je atasaidia mabigwa hao wateteziwa Kombe la Dunia kuhifadhi taji hilo ndio swali lililo midomoni mwa watu wanasubiri mechi ya fainali itakayochezwa saa chache zijazo.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 ataongoza Ufaransa dhidi ya Argentina jioni hii katika uwanja wa Lusail akiwa na nafasi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kushinda Kombe la Dunia la pili tangu Pele alipofanya hivyo akiwa na umri wa miaka 21 mwaka 1962.
Ni mmoja wa wafungaji bora katika dimba hilo - akiwa sawa na mpinzani wa wake Lionel Messi - na tayari amefunga mabao tisa katika mechi za Kombe la Dunia, na kumfanya kuwa mfungaji bora wa 15 katika historia ya michuano hiyo.
Kwa hakika, ni mchezaji mmoja tu wa kiume katika historia ya Ufaransa aliyefunga mabao zaidi ya Kombe la Dunia - Just Fontaine, akiwa na mabao 13, yote mwaka 1958 - huku mshambuliaji huyu mwenye kasi wa Paris St-Germain akitishia kuvunja rekodi zote mbele yake.
Mfaransa namba 10 alizaliwa katika vitongoji kidogo cha Bondy, kaskazini mwa Paris.
Familia ya Mbappe - Kylian, baba Wilfried, mama Fayza na kaka yake Jires Kembo-Ekoko - waliishi katika shamba la baraza lililo karibu na uwanja wa nyumbani wa Bondy FC.
Kaka yake mdogo Ethan, ambaye sasa ana umri wa miaka 15, alizaliwa baadaye.
Kulikuwa na barabara moja tu ya kuvuka na uwanja ulikuwa wa Kylian kucheza kwa saa nyingi na marafiki zake.
Baba yake alihusika sana katika kilabu cha mashinani, ambapo alifundisha timu tofauti na alikuwa na sauti na sifa inayoheshimiwa katika ulingo wa soka ya Paris.

Chanzo cha picha, REUTERS AND DYLAN MARTINEZ
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwanawe hakupendezwa na kitu kingine chochote isipokuwa mpira wa miguu. Alichotaka ni kupiga mpira na kuwa karibu na timu za baba yake.
Kandanda ikawa kitu kinachofuatiliwa mara kwa mara katika nyumba yao, iwe kutazama mechi kwenye televisheni, kucheza kwa ushindani au na marafiki, shuleni, Bondy au popote pengine.
Mbappe alifanya kila kitu kwa kuzingatia mpira wa miguu. Juu ya kuta za chumba chake cha kulala, unaweza kupata picha ya Cristiano Ronaldo.
Ilikuwa wazi tangu utotoni mwake kwamba kijana Kylian alikuwa na kipaji. Kuanzia umri wa miaka 10, pande zote za Paris, watu wangezungumza juu ya mwanasoka huyu kutoka Bondy.
Haikuchukua muda sifa hizo zilienda zaidi ya mji mkuu wa Ufaransa. Pamoja na kila klabu ya Ligue 1, timu zote kubwa za Ulaya zilitahadharishwa na wasaka talanta wao.
Waliafikiana kwamba Kylian miaka michache ijayo itaiwakilisha Ufaransa kimataifa na walitaka kumuona akiwa katika ubora wa hali ya juu.
Kwa hiyo familia yake ilikubali ofa kutoka kwa Chelsea, ambao walimchukua Kylian kwa wiki moja ya mazoezi akiwa na umri wa miaka 11, baadaye Real Madrid, nao walifanya vivyo hivyo alipokuwa na umri wa miaka 12.
Wakubwa wote wa Ulaya walijaribu kumshawishi yeye na wazazi wake kuhamia London au Uhispania, tayari kutoa chochote.
Lakini familia yakeilichokuwa ikitaka ni kumjaribu mtoto wao. Na kila mahali alipoenda, alikuwa bora zaidi, hata katika chuo cha mafunzo ya soka ya Clairefontaine - mjini Paris.
Baada ya kuchaguliwa miongoni mwa mamia ya vijana wenye umri wa miaka 13, unaishi katika kituo hicho kwa miaka miwili na, mwishoni mwa juma, unachezea klabu yako ya mashinani, kama Kylian, au klabu ya kitaaluma inayokuajiri.
Vilabu vilipanga foleni kumpata Mbappe lakini, tofauti na kila mchezaji mwenzake, alisubiri hadi mwisho wa miaka yake miwili katika Clairefontaine kuchagua uhamisho wake mwingine.
Caen waliamini kwamba atajiunga nao kabla ya kinda huyi kuamua kuchagua Monaco baada ya kuahidiwa kwamba atakuwa na nafasi ya kujiunga na kikosi cha kwanza cha klabu hiyo.
Mbappe alikuwa na umri wa miaka 15 na alichotaka ni kucheza soka tu; mapenzi yake kwa ajili ya mchezo huo yalikuwa ya ajabu.
Katika chuo cha Monaco, alipokuwa akichezea timu za vijana, alikuwa na ndoto ya kucheza kwa mara ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa, akifuata nyayo za shujaa wake Ronaldo.
Lakini ili kuelewa mafanikio yake, ni muhimu kuelewa umuhimu wa familia yake. Wanafanya kila kitu pamoja. Hivi karibuni, waliishi pamoja huko Monaco.
Walipohisi hakupewa nafasi katika kikosi cha kwanza licha ya kufanya vyema katika mazoezi, waliwasiliasha malalamiko yao.
Na hatimaye Leonardo Jardim alimpatia nafasi kwa mara ya kwanza Desemba 2015. Mbappe, mwenye umri wa miaka 16 na siku 347, alivuka rekodi ya Thierry Henry kama mchezaji mwenye umri mdogo zaidi katika kikosi cha kwanza cha Monaco.
Haikuchukua muda mrefu kabla ya Mbappe kuvunja rekodi ya Henry kama mfungaji mabao mdogo zaidi katika klabu hiyo.
Kuanzia hapo na kuendelea, hakuna kitu kingeweza kumzuia kufikia ndoto zake. Mechi yake ya kwanza ya mechi ya Ufaransa ilikuwa tarehe 25 Machi 2017 dhidi ya Uhispania, alipokuwa na umri wa miaka 18 na siku 95, bao lake la kwanza lilifuatiwa katika mapumziko yaliyofuata ya kimataifa.
Katika miaka yake yote ya ujana, vilabu vyote vya juu viliendelea kujaribu kumsajili. Real Madrid walifanya kila wawezalo.
Walipanga majaribio mengi, mechi za kirafiki, kukutana na kusalimiana na Zinedine Zidane na Ronaldo mwenyewe. Walitoa kila walichoweza lakini hawajafanikiwa. Juhudi zao hazijakoma mpaka sasa.
Mbappe alichagua PSG, mwanzoni alijiunga nao kwa mkopo wa msimu mzima mnamo Agosti 2017 kabla ya kukamilisha uhamisho wa pauni milioni 130, na amewasaidia kushinda mataji manne ya Ligue 1 katika misimu mitano tangu hapo.
Mengine ni historia. Mbappe anatinga fainali ya leo kama mchezaji mkuu wa Ufaransa.
Akiwa na umri wa miaka 24 pekee siku mbili baada ya fainali ya Kombe la Dunia, tayari amefunga mabao 33 akiwa na Ufaransa - 20 tu nyuma ya mchezaji mwenzake Olivier Giroud, ambaye anashikilia rekodi ya ufungaji mabao ya kwa taifa lake.
Lakini jambo muhimu zaidi kwa mshindi wa Kombe la Dunia 2018, kinachomsukuma, ni upendo wake wa mchezo wa soka.
Tangu alipokuwa mtoto, alikuwa na mpira miguuni mwake - na sasa miguu yake inazungumza.












