Vitu 7 vinavyomfanya Mbappe kuwa nyota wa Dunia

Chanzo cha picha, Reuters and Dylan martinez
England itakutana na Ufaransa katika robo-fainali ya Kombe la Dunia siku ya Jumamosi (saa 19:00 GMT kuanza) - na mchezaji mmoja haswa yuko akilini mwa kila mtu.
Mshambuliaji wa Paris St-Germain Kylian Mbappe bila shaka ndiye mchezaji bora zaidi duniani kwa sasa, na mengi yamezungumzwa kuhusu jinsi anaweza kuzuiwa na Three Lions ya Gareth Southgate.
BBC Sport imechagua mambo saba unayohitaji kujua kuhusu Mbappe na sifa zinazomfanya kuwa juu ya wote..
1. Ni mchezaji wa pili ghali zaidi katika historia
Mnamo 2017, Mbappe alijiunga na PSG, mwanzoni kwa mkopo, kutoka Monaco, kabla ya kufanya uhamisho wa kudumu mwaka mmoja baadaye kwa euro 180m (£ 166m).
Bado ni uhamisho wa pili ghali zaidi kuwahi kutokea. Dili pekee lililogharimu zaidi lilikuwa ni euro 222m (£200m) la fowadi wa Brazil Neymar kwenda PSG kutoka Barcelona 2017.
Mbappe amefunga mabao 190 katika michezo 237 akiwa na mabingwa hao wa Ufaransa, ambapo anacheza pamoja na Neymar na nguli wa Argentina Lionel Messi.
2. Yeye ameshinda mfululizo
- Katika miaka saba kama mtaalamu, Mbappe ameshinda:
- Kombe la Dunia 2018
- Ligi ya Mataifa ya Uefa 2020-21
- Mataji matano ya Ligue 1 (manne PSG, moja huko Monaco)
- Vikombe vitatu vya Ufaransa
- Vikombe viwili vya Ligi ya Ufaransa
Yeye binafsi , ameshinda tuzo ya Golden Boy - iliyotolewa kwa mchezaji bora wa chini ya umri wa miaka 21 katika ligi kuu za Ulaya - mwaka wa 2017, ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Ufaransa mara mbili, na mchezaji bora wa mwaka wa Ligue 1 na mchezaji mdogo wa mwaka mara tatu. Pia alikuwa mchezaji bora chipukizi katika Kombe la Dunia la 2018 na kuwa mfungaji bora wa Ligue 1 katika misimu minne.
Na aliisaidia PSG kufika fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2020, ingawa walifungwa na Bayern Munich.
3. Amezoea kulichangamsha Kombe la Dunia
Mbappe alikuwa na umri wa miaka 19 pekee alikuwa na jukumu muhimu katika harakati za Ufaransa kutwaa ubingwa wa Urusi 2018, akifunga mabao manne ugenini.
Bao lake katika ushindi wa 4-2 dhidi ya Croatia lilimfanya kuwa kijana wa pili kufunga katika fainali ya Kombe la Dunia, baada ya gwiji wa Brazil Pele mwaka 1958.
Mbappe ndiye kinara wa mabao nchini Qatar hadi sasa akiwa amefunga mabao matano, na jumla yake ya mabao tisa katika Kombe la Dunia ina maana tayari amewapita Diego Maradona, aliyeifungia Argentina mabao nane, na Mreno Cristiano Ronaldo.
Hakika, ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga mabao tisa Kombe la Dunia, akivunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Eusebio, ambaye aliifungia Ureno magoli nane akiwa na umri wa miaka 24 na siku 182.
4. Alivunja rekodi akiwa na umri mdogo
Mbappe, ambaye alizaliwa nje kidogo ya jiji la Paris na akaanzia kucheza katika timu yake ya AS Bondy, alicheza kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Monaco mnamo Desemba 2015.
Akiwa na umri wa miaka 16 na siku 347, alikua mchezaji mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya klabu hiyo - akiipiku rekodi iliyowekwa na nguli wa Ufaransa na Arsenal Thierry Henry mwaka 1994 - alipotokea kama mchezaji wa akiba dakika ya 88 dhidi ya Caen.
Miezi mitatu baadaye, alikua mfungaji mdogo zaidi wa kilabu kwa bao lake la kwanza la kikosi cha kwanza dhidi ya Troyes. Nani aliweka rekodi ya awali? Henry.
5. Ana kasi ya juu
Wakati Ufaransa iliposhinda 3-1 hatua ya 16 bora dhidi ya Poland, kasi yake ya juu ilirekodiwa kwa kilomita 35.3 kwa saa na kabla ya mechi ya Jumapili, ni wachezaji sita pekee waliokuwa wameandikisha mbio za kasi zaidi katika Kombe la Dunia mwaka huu.
Mnamo Septemba, Ligue 1 ilisema ndiye mchezaji mwenye kasi zaidi kwenye ligi msimu huu akiwa na kasi ya 36km/h.
Ili kuweka hilo katika muktadha, nguli wa mbio za Olimpiki wa Jamaika Usain Bolt aliweka rekodi yake ya dunia ya mita 100 ya sekunde 9.58 mwaka wa 2009 akiwa na kasi ya wastani ya 37.58km/h (ingawa kasi yake ya juu ilikuwa 44.72km/h katika sehemu ya 60-80m).
6. Alikataa uhamisho wa pesa nyingi kwenda Real Madrid msimu uliopita
Baada ya uchumba wa muda mrefu kutoka kwa rais wa Real Florentino Perez na kuafikiana kuhusu kifurushi cha fedha na wababe hao wa La Liga, Mbappe aliamua kusalia Paris na kusaini mkataba mpya wa miaka mitatu.
Kulingana na mtaalam wa soka wa Uhispania Guillem Balague, vilabu vyote viwili vilikuwa tayari kulipa euro 150m (£127m) kama ada ya kusaini.
Hata hivyo, hajakataa kuhamia kwa mabingwa hao wa Uhispania na Ulaya katika siku zijazo, akiambia BBC mnamo Mei ndoto yake ya Real Madrid "haijatimia".
7. Nyota mnyenyekevu wa kimataifa
Mbappe pia ni maarufu kwenye mitandao ya kijamii, akiwa na wafuasi takriban milioni 100 kwenye Facebook, Instagram na Twitter.
Pia alitajwa pamoja na Ronaldo, Messi na Neymar kama wanasoka wenye ushawishi mkubwa zaidi kwenye Instagram kutokana na kucheza Kombe la Dunia la 2022.
Mikono yake ya ajabu iliyokunjwa na kusherehekea kwa goti imeonyeshwa kwenye mchezo wa Fifa 21 na inasemekana ndiye mwanariadha mwenye umri mdogo zaidi kuonekana peke yake kwenye jalada, kabla ya kurejea kwa toleo la 2022.
Baada ya kushinda Kombe la Dunia miaka minne iliyopita, Mbappe alitangaza kuwa ametoa mshahara wake wote wa pauni 380,000 kwa ajili ya mashindano hayo kwa shirika la hisani la watoto.












