Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Inamaanisha nini kuwa mwanaume bora?
Wanaume wanapaswa kuonekanaje? Wafanye nini? Wasifanye nini? Jawabu zinaweza kutofautiana kutokana na maeneo, tamaduni na dini.
Sote tumekuwa tukisikia mambo fulani kuhusu wanaume katika nyumba zetu au kutoka kwa watu wanaotuzunguka ama katika jamii zetu.
Utasikia mwanaume halii au mtazamo kwamba jukumu la kuendesha nyumba ni la mwanaume, wanaume wanaweza kufanya kazi ngumu, wanaume hufanya uamuzi wa mwisho juu ya jambo lolote ndani ya nyumba. Haya yote yamekuwa sehemu ya fikra zetu katika kijamii.
Profesa wa Idara ya Mafunzo ya Wanawake, Chuo Kikuu cha Punjab, Ameer Sultana anasema, "mtazamo wa aina hii kuhusu wanaume hutengenezwa na jamii na hauhusiani na maumbile."
“Na ndio sababu tunaona katika jamii kuna tafsIri tofauti za uanaume. Lakini kuna kitu kimoja kinafanana katika jamii zote - wanaume wana nguvu na hufanya maamuzi ya mwisho."
Uanaume ni Nini?
Katika jitihada za kupata jibu la swali hili, neno jipya limeanza kutumika - uanaume chanya.
Gary Barker, Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa Kituo cha Masculinities and Social Justice. Barker ni mwanzilishi mwenza wa Utafiti wa Kimataifa wa Wanaume na Usawa wa Jinsia.
Ni utafiti mkubwa zaidi kuwahi kutokea kuhusu mada juu ya tabia za wanaume, ubaba, unyanyasaji na usawa wa kijinsia.
Akizungumza na BBC, anasema wanaume wenyewe wamechanganyikiwa kuhusu maana ya kuwa mwanaume mwema.
Barker aligundua katika utafiti wake wanaume wanapotunza familia, familia nzima inafaidika. Anaamini uanaume chanya ni tiba kwa fikra zenye sumu dhidi ya mwanamke.
Anaamini njia rahisi ya kuwafahamisha wanaume kuhusu unyanyasaji wa kijinsia ni kuwaeleza kuwa wanapaswa kupaza sauti zao kuupinga unyanyasaji.
Mwanaume anapojua mwanaume mwingine amefanya ukatili wa kijinsia ofisini kwake au miongoni mwa marafiki au jamaa zake, anapaswa kupaza sauti kukemea.
Sultana anaamini ikiwa kuna kitu kibaya katika jamii dhidi ya wanawake na wasichana, wanaume wanapaswa kupaza sauti zao. Anaamini hiyo ndio maana ya uanaume chanya.
Jukumu la Wanaume
Barker anasema wanaume wana jukumu muhimu la kutekeleza katika uwezeshaji wa wanawake na usawa kamili wa kijinsia kati ya wanaume na wanawake.
Harish Iyer kutoka Mumbai, anayepigania haki za wapenzi wa jinsi moja nchini India kwa miaka mingi, anasema uanaume mzuri unamaanisha mtu kuwa na mawazo kwamba watu wa jinsia zote wako sawa na kupewa fursa sawa.
Harish Iyer anasema ufimenia ndio mzizi wa itikadi ya uanaume mzuri. Ufimenia unaona kuwa jamii inamkandamiza mwanamke na kumtendea isivyo haki katika jamii ya mfumo dume.
Harish anaeleza - sio wanaume tu wenye nguvu ya uanaume hasi, pia kuna wanawake wanakuza uanaume mbaya.
Ameer Sultana pia anasema, “wanawake ni sehemu ya jamii na wanatoa umuhimu zaidi kwa uanaume."
Gary Barker anaon fikra za wanaume pia zimeanza kubadilika,'' wanaume wanapaswa pia kuelewa mawazo (uanaume mbaya) yanafanya iwe vigumu kwao pia.''
Ikiwa ulimwengu utaelekea kwenye usawa wa kijinsia, itawanufaisha wanaume pia. Katika mapambano haya ya usawa wa kijinsia, ikiwa mwanaume atakuwa na rafiki wa kike, anakuwa mwanaume bora zaidi.
Haja ya kubadili fikra
Barker anasema, “watu wameanza kuzungumza kuhusu uanaume nchini India lakini mazungumzo yanahitaji kuenea zaidi.''
Sultana yeye anasema, "aina hii ya fikra inaweza kubadilishwa tunapoweza kuwafundisha watoto wa kike na wa kiume - wote ni sawa tangu wakiwa wadogo. Mwanaume anaweza kuwa mtu mwema anapoanza kuwa mwanaume mwema.”
Sultana anamaliza kwa kusema, ''si tu kuhusu wanawake na wanaume, lakini pia kuhusu LGBTIQ. Jamii inaweza kubadilika ikiwa jamii nzima itabadilika.''
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi