Sponji za baharini zilivyoboresha maisha ya wanawake Zanzibar

    • Author, Kizito Makoye
    • Nafasi, BBC

Huku upepo mwanana wa asubuhi ukivuma katika ufuo wa Zanzibar, Hindu Simai Rajabu anatembea kwenye maji ya kina cha magoti hadi kufikia shamba lake la sponji katika pwani ya Jambiani, Zanzibar, Tanzania,.

Hapa ni katika Bahari ya Hindi. Akiwa amevaa miwani na kitambaa cha pua juu kafunga kilemba. Kicheko chake kutokana na tajriba ya kurekodiwa kinachanganyika na sauti ya mawimbi ya bahari.

Mawimbi yakiongezeka, Rajabu mwenye umri wa miaka 31 na mama wa watoto wawili huogelea na kuzamia kwenye maboya ambayo hushikilia shamba lake sponji.

Kutafuta kipato kumepelekea Rajabu na wanawake wengine 12 waliopewa talaka na akina mama wasiokuwa na waume kutoka kijiji cha Jambiani visiwani Zanzibar kuingia katika Bahari ya Hindi kupanda sponji zinazostahimili mabadiliko ya tabia nchi.

Kulima sponji baharini ni biashara yenye faida kwa wanawake hao katika miaka ya hivi karibuni. Wanawake wengi huko Jambiani wanalima mwani, lakini hupata mavuno kidogo kutokana na kuongezeka kwa joto la bahari.

Mwaka 2009, baadhi ya wanawake walihama kwenye ukulima wa mwani na kuanza kulima sponji laini za baharini –zinapovunwa hutumiwa kwa kuogea na usafi. Sponji za baharini hustahimili joto na huchuja vichafuzi kama vile maji taka na dawa za kuua wadudu.

Wanaharakati wa haki za wanawake wa eneo hilo wanasema ufugaji wa sponji baharini unasaidia kuboresha usawa wa kijinsia Zanzibar na umewaondoa wanawake hao kutoka kwenye umaskini. Wakulima wenyewe wanasema maisha yao yameboreka.

Rajabu anapoyafikia maboya, anajisogeza mbele ili kukagua sponji kwenye kamba. Kisha hukwangua kamba kwa kisu ili kuwaondoa bakteria wanaonyemelea sponji zinazokuwa sasa.

"Sponji ni wanyama dhaifu, nisipowasafisha vizuri watakufa," anasema Rajabu, huku akizishughulikia kwa uangalifu, akijihadhari asije kuziharibu.

Ili kuzuia sponji zisipate joto kupita kiasi na jua au kuharibiwa na boti zenye injini, Rajabu huhakikisha kwamba daima zinabaki chini ya maji. Hutumia saa nne kila siku baharini, akihudumia shamba lake. Alasiri, huenda ofisini ili kuchambua na kuweka lebo sponji zilizokaushwa kwa ajili ya kuuza.

Rajabu aliacha shule akiwa na umri wa miaka 17 kwa sababu mama yake hakuwa na uwezo tena wa kulipia masomo yake, na kukatisha ndoto yake ya kuwa daktari. Mume wake alipomuacha baada ya miaka tisa, alianza kilimo cha mwani ili kusaidia watoto wake wawili.

Lakini hakupata mapato ya kutosha - shilingi 70,000 tu za Kitanzania (£22/$28) kila mwezi.

2020, aliwasiliana na Marine Cultures kuelezea hali yake ngumu na kutafuta kazi. Alichukuliwa na kuanza kupata mapato mazuri. "Ni kazi ngumu, lakini ninafurahia kuifanya na inalipa vizuri," anasema. Sasa anapokea mshahara wa kila mwezi wa shilingi 250,000 za Kitanzania (£80/$100).

"Ninapata mapato mazuri ya kila mwezi, ya kutosha kukidhi mahitaji ya familia yangu," anasema.

Sponji za baharini, ambazo kitaalamu ni wanyama lakini hukua, kuzaliana na kuishi kama mimea, zina matundu madogo ambayo huruhusu maji kuingia na kutoka. Viumbe hawa wa baharini wanadhaniwa kuwepo kwa zaidi ya miaka milioni 600. Wanasayansi wamegundua zaidi ya aina 15,000 duniani kote za sponji.

Shirika lisilo la kiserikali la Marine Cultures la Sweden lilianzisha kilimo cha sponji visiwani Zanzibar mwaka 2009 ili kuwawezesha wanawake maskini kupata kipato bora na kusaidia kulinda maliasili za eneo hilo.

‘’Hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000, kilimo cha mwani kilikuwa uti wa mgongo wa uchumi wa ndani wa Zanzibar, ikiajiri wakulima wanawake 20,000, na kuinua kiwango chao cha maisha na hadhi ya kijamii. Lakini sekta ya mwani imeathiriwa na ongezeko la joto,’’ anasema Vaterlaus, mwanzilishi wa kampuni ya Marine Cultures.

Utafiti wa 2021 uliofanywa na watafiti katika Chuo Kikuu cha York nchini Uingereza uligundua mavuno na ubora wa mwani umeshuka sana katika eneo hilo kutokana na kupanda kwa joto, upepo mkali na mvua zisizokuwa za kawaida.

Uzalishaji wa mwani pia ulipungua kwa 47% kati ya 2002 na 2012 kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, magonjwa na kupungua kwa idadi ya wakulima kutokana na bei ya chini, watafiti walihitimisha.

Biashara ya Sponji na mafanikio

Sponji huboresha bahari kwa kutema mafuta na asidi ya amino kwa viumbe vingine kunyonya. Mifupa yao huvunjika vipande vipande na husaidia kudhibiti mzunguko wa kaboni katika bahari na kupunguza athari ya chafu , wataalamu wanasema.

Tangu mwaka 2009, wanawake 13 wamepewa mafunzo, kulingana na Ali Mahmudi Ali, ambaye anasimamia shamba hilo. "Tunawafundisha wakulima kwa mwaka mmoja ili kuhakikisha wana ujuzi na maarifa," anasema.

Mafunzo hayo yanahusisha kuwafundisha kuogelea, kupiga mbizi, kutumia vifaa na zana, jinsi ya kusafisha na kutunza sponji, utunzaji wa hesabu, masoko na kupanga madaraja ya sponji kwa ajili ya kuuza.

Kila sponji huuzwa kwa shilingi 37,000-74,900 za Kitanzania (£12-£24/$15-$30), kulingana na ukubwa na ubora wake. Zinauzwa katika maduka, kwa watalii na hoteli za Zanzibar na nje ya nchi.

Mkulima hupata asilimia 70, huku 29% ikienda dukani na 1% kwa Ushirika wa Wakulima wa Sponji Zanzibar, Jumuiya inayoongozwa na wanawake inayosimamia uajiri wa wakulima na shughuli za uzalishaji.

"Imeboresha mapato ya wakulima kwa kiasi kikubwa. Tunajivunia sana mpango huu," anasema Haji, mama wa watoto wanne mwenye umri wa miaka 48.

Anasema ufugaji wa sponji umewasaidia wanawake hao kuondokana na utegemezi wa kifedha kwa wanaume, jambo ambalo liliwafanya wanyonywe na kunyanyaswa. "Kama wanawake, tunapaswa kuyasimamia maisha yetu. Tusingojee tu mume wetu alete chakula mezani," Haji anasema.

Kwa kuwa sasa wanapata mapato ya kutosha, ushawishi wao katika kufanya maamuzi ya familia umeongezeka, anaongeza.

Kazi ngumu ya Rajabu kama mkulima wa sponji imezaa matunda. Katika miaka miwili tu, amepata pesa za kutosha kununua shamba ambalo anajenga nyumba ya vyumba vitatu.

"Nataka kukaa na watoto wangu katika nyumba yangu mwenyewe," anasema.

Rajabu anasema kupanda kwake kwa kasi kiuchumi kumezua udadisi miongoni mwa majirani zake. “Nilipoanza nilikuwa kicheko, lakini sasa waliokuwa wanacheka wananiuliza niliwezaje kujenga nyumba,” anasema.

Kama Rajabu, Haji anaona kilimo cha sponji kinafaa zaidi kuliko kilimo cha mwani alichokuwa akifanya. Kwa miaka 15 alikokota mwani mzito kutoka baharini, akikabiliana na hali mbaya ya hali.

Hata hivyo, kilimo cha sponji kimeleta pesa na kumfanya atabasamu. Anasema "siri pekee ni kufanya kazi kwa bidii. Kazi ngumu inalipa."

Zulfa Abdalla anasema alikuwa akihangaika kutafuta riziki. Aliachwa atunze watoto wawili baada ya mumewe kumtaliki alipokuwa na umri wa miaka 23. Mume wa zamani wa Abdalla alioa tena na hakuwahi kusaidia watoto wake, akimuacha akiwalea peke yake.

Aligeukia kusuka kofia ili kupata pesa. Hata hivyo, mapato ya kila mwezi ya shilingi 40,000 za Kitanzania (£13/$16) hayakuwa ya kutosha kukidhi mahitaji ya familia yake. Abdala alipopata kazi ya ufugaji wa sponji, ilimbidi ajifunze kuogelea.

Ndani ya miezi mitatu ya kuanza kama mkulima wa sponji baharini, Abdalla alizalisha mavuno mengi, ambayo yalimletea shilingi 1,600,000 za Kitanzania (£513/$639). Mafanikio haya yalimwezesha kununua kitanda, meza na kabati la nguo. Mapato yake pia yalimruhusu kukarabati nyumba ya mama yake.

Licha ya faida hizo. ‘’Kukua sponji za baharini pia ni mchakato mrefu. Wakulima lazima wasubiri mwaka mzima kwa sponji kukua hadi kukomaa. Jitihada za utafiti zinapaswa kuzingatia kuendeleza aina za sponji zinazokua kwa kasi na zenye ubora wa hali ya juu,‘’ anasema mtaalamu katika taasisi ya Sayansi ya Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nchini Tanzania, Leonard Chauka,

Licha ya changamoto hizo, soko la sponji la Zanzibar ni zuri, Vaterlaus anasema. Anasema kuwa taasisi ya Marine Cultures ina mpango wa kuanzisha kilimo cha sponji katika kisiwa cha Pemba na jiji la Tanga mwishoni mwa mwaka huu.

Huku mwito wa swala kutoka msikiti ulio karibu ukisikika angani, Mkasi Abdalla anasema: "Ninashukuru sana kwa fursa hii. Mapato ninayopata yananisaidia kutatua matatizo yangu."

Hadithi ya Abdalla na wanawake wengine inaonyesha nguvu ya kilimo cha sponji, kutoa uhuru wa kiuchumi na usawa wa kijinsia, wakati wa kuhifadhi mazingira ya baharini.

“Nafanya kazi bila kuchoka kutafuta pesa ili watoto wangu wapate elimu bora na kufaulu maishani,” anasema Rajabu. "Nataka kuvunja mzunguko wa ujinga katika familia yangu."