'Sijala nyama kwa miezi kadhaa lakini sitajiuza'

Tulane, mama wa watoto sita, asiye na mwenzi amedhamiria kutorejea Syria, licha ya kudhulumiwa kingono na kiuchumi.

Alikuwa mwalimu nyumbani lakini sasa anafanya kazi Uturuki kama mpishi, akipata lira 6,000 za Kituruki ($220) kwa mwezi. Ni zaidi ya nusu ya kima cha chini cha mshahara, ambacho ni dola 420 kwa mwezi.

Tulane (42), si jina lake halisi, anasema mumewe hakuweza kukabiliana na mazingira magumu ya kazi kwa wakimbizi. Alirudi Syria miaka miwili iliyopita, akimuacha yeye na watoto wao.

Hapo ndipo maisha yake yalipozidi kuwa magumu, ananiambia.

Wanaume wangemkaribia wakimpa msaada au kazi, lakini baada ya kujua kwamba alikuwa mama asiye na mwenzi, "wangemtogoza" yeye au binti zake wadogo.

"Bosi aliwahi kunishika mkono, nikamsukuma na kukimbia, wanadhani tutajiuza kwa chakula kidogo au pesa. Sijala nyama kwa miezi kadhaa, lakini sitajiuza," anasema.

Mume wa Tulane alioa tena nchini Syria na anaishi maisha tofauti.

"Nikirejea Syria, elimu ya watoto wangu itaathirika. Sina budi kupambana na njaa, unyanyasaji na chuki dhidi ya wageni hapa lakini siwezi kurudi nyuma," anasema.

Uturuki imepokea rasmi zaidi ya wakimbizi milioni 3.3 wa Syria, na kuifanya kuwa nchi yenye wakimbizi wengi zaidi duniani.

Wasyria kwa ujumla hufanya kazi katika sekta ya nguo, kilimo, upishi au ujenzi ambapo ajira ambazo hazijasajiliwa ni za kawaida.

Takriban wakimbizi milioni moja wa Syria wanakadiriwa kufanya kazi bila kibali. Hii ina maana kwamba hawana uwezo wa kupata hifadhi ya jamii na mara nyingi hulipwa chini ya kima cha chini cha mshahara.

Kulingana na sheria ya kazi ya Uturuki, ikiwa mwajiri anataka kumwajiri mgeni, anahitaji kulipa mara tatu ya mshahara wa chini.

Hii ndiyo sababu waajiri wengi huchagua kutotoa vibali vya kufanya kazi - ili waweze kuwalipa wakimbizi kiasi kidogo sana cha pesa.

Takwimu rasmi za serikali zinaonyesha kuwa ni wanawake 5,000 tu wa Syria nchini Uturuki walio na vibali vya kufanya kazi.

Na huku mfumuko wa bei ukiwa 56% na nchi ikistahimili gharama kubwa ya maisha, wanawake wa Syria wanasema lazima wavumilie unyanyasaji wa kijinsia ili kushikilia kazi zao.

Lamya ananipandisha ngazi hadi kwenye jengo bovu analoishi. Tunakaribishwa na harufu kali ya maji taka.

Mama huyu wa watoto watano ambaye pia hana mwenzi, ananiambia hakuwa na lingine ila kuhamia hapa kwani aliibiwa mara kwa mara katika orofa yake ya awali, na inayojulikana kienyeji kama "nyumba bila wanaume".

"Sikuweza kulala usiku kwa sababu nilikuwa nikiangalia watoto wangu. Niliogopa na ikabidi niondoke," mama huyo mwenye umri wa miaka 38 anasema.

Lamya - pia sio jina lake halisi - anasema amekumbana na unyanyasaji wa mara kwa mara wa kijinsia kazini pia.

"Unapokuwa mke aliyeachika, macho yote yanaelekezwa kwako. Wanakufuata kila mara.

"Kuwa mjane kazini ni sawa na sumaku kwa wanaume. Wanaume wengi hunijia kwanza kwa nia ya kutaka kunisaidia au kazi, lakini huniambia ni nini hasa wanataka kutoka kwangu.

“Nimejifunza kutomwambia mtu kazini kwamba sina mume, hapo awali bosi wangu aligundua kuwa mume wangu hayupo, akaanza kunifuata na kunipigia simu mara kwa mara, ikabidi niache kazi hiyo. "

Katika nyumba nyingine iliyo karibu, mama wawili Wasyria wasio na waume wanaishi pamoja ili kusaidiana kujikimu kimaisha.

Rana anafanya kazi katika kiwanda cha nguo bila kibali na anapata chini ya kima cha chini cha mshahara. Yousra anakaa nyumbani na kuwatunza watoto wao wanne na mama yake mkubwa.

Wanasema wamekuwa wakikabiliwa na manyanyaso na chuki dhidi ya wageni katika maeneo ya kazi na katika jamii pana, pamoja na unyanyapaa wa kijamii wa kuwa mama wasio na waume.

Angawa alifika Uturuki akiwa na matumaini makubwa, Rana sasa anasema haoni tena mustakabali wa watoto wake.

"Kila senti tunayopata inakwenda kwenye kodi na bili. Tuna njaa kila wakati na juu ya hayo, kila mtu mitaani anatuchukia," anasema.

Lamya pia analalamika kuhusu kutengwa na jamii ingawa tayari ameishi kwa zaidi ya miaka 10 nchini Uturuki.

"Wakati mmoja tulikuwa tumekaa kwenye benchi, na ghafla wanawake wawili wa Kituruki walikuja na kuanza kutufokea. 'Mtarudi lini Syria,' walikuwa wakifoka. Nilihisi kama mwili wangu wote umekufa ganzi," anasema.

"Ndoto yetu kubwa kwenda Ulaya. Nimekuwa nikiwaza kuhusu hili usiku na mchana."