Mfungwa wa zamani, bunduki haramu na hofu ya polisi wa Kenya

    • Author, Elijah Kanyi & Tamasin Ford
    • Nafasi, BBC Africa Eye, Nairobi & London

Kenya ikikabiliana na ongezeko la uhalifu, BBC Africa Eye inamfuatilia mhalifu mmoja wa zamani anapojaribu kuwashawishi wanaume kusalimisha silaha zao haramu, bunduki moja baada ya nyingine.

"Jambo baya zaidi nililowahi kufanya ni kuua. Niliua mtu,” kijana huyo anasema baada ya kukubali kurekodiwa kwa sharti la kutotajwa jina.

"Sikuhisi chochote, kwa sababu nilikuwa natumia dawa za kulevya. Nilihisi kama nimeua nzi.”

Samuel, sio jina lake halisi, yuko Kisumu kwenye ukingo wa Ziwa Victoria magharibi mwa Kenya, kukutana na Mfalme Kafu, mfungwa wa zamani ambaye sasa anawasaidia watu kujiepusha na uhalifu.

Anaonekana kuwa na wasiwasi. Ana bunduki aina ya AK47 katika eneo lililofichwa ambalo sasa anataka kuwasilisha kwa polisi.

Alipoulizwa kwa nini, anasema: “Siku itakuja ambapo familia yangu haitakuwa na chakula chochote. Wataumia hatimaye.

"Nikifanya fujo kisha nipigwe risasi, hakuna mtu atakayekuwepo kutunza familia yangu. Kwa hiyo niliamua, kutoka moyoni mwangu, kurudisha kitu hiki.”

Soma pia:

Takwimu kutoka Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya zinaonyesha wizi wa mabavu uliongezeka kwa karibu 20% mwaka jana.

Silaha haramu huingizwa nchini kwa njia ya magendo kupitia mipaka yake iliyo wazi, na kufanya Kenya kuwa inchi ambayo ina idadi kubwa ya raia wanaomiliki silaha kwa njia haramu katika Afrika Mashariki, kulingana na Taasisi ya Mafunzo ya Usalama.

Takwimu za hivi punde kutoka katika Utafiti wa Silaha Ndogo Ndogo, ambao unafuatilia mienendo ya silaha duniani, zinaonyesha kuwa kuna takriban bunduki 750,000 mikononi mwa raia nchini Kenya. Hiyo ni zaidi ya jeshi na polisi kwa pamoja.

Kafu anafanya kazi ya kuwaunganisha watu wanaotaka kukabithi bunduki zao kwa polisi.

Alikuwa na umri wa miaka 15 alijunga na uhalifu kwa mara ya kwanza. Ilianza kwa kunyakua mifuko ya watu, lakini alipopata uzoefu zaidi akahamia kwenye wizi wa kutumia silaha.

Mnamo 2003, alihukumiwa kifungo cha miaka minne jela kwa wizi.

Samuel alikuwa amewasiliana naye kwenye Instagram akiomba msaada. King Kafu alizungumza na polisi wa eneo la Kisumu na wakakubali kupokea bunduki ya Samuel, na kuahidi kuwa hatachunguzwa kulingana na mpango uliowekwa vizuri wa msamaha.

Lakini muda wa kukutana tena akiwa na bunduki ya AK47 ulipofika, Samuel hakutokea.

Kafu, ambaye sasa ana umri wa miaka 40, ni mtangazaji wa Ghetto Radio, kituo maarufu miongoni mwa vijana katika maeneo ya vitongoji duni katika mji mkuu, Nairobi, na anatumia jukwaa lake kuzungumzia ghasia za kutumia bunduki.

“Baada ya kuachiliwa, niligundua marafiki zangu wengi waliohusika katika uhalifu walikuwawameathirika vibaya, wengi wao wakifariki kutokana na maisha yao ya uhalifu,” asema.

Hili ndilo lililomfanya abadilishe maisha yake.

"Hakuna mtu anayezaliwa mwizi. Lakini hata kama vijana hawana kazi, tunawaambia kwamba uhalifu sio mzuri. Watu wanapaswa kurejesha bunduki zao haramu kwa serikali,” asema.

Katika miaka 20 iliyopita serikali ya Kenya imetumia msamaha kama njia ya kudhibiti uhalifu wa kutumia bunduki, na kuahidi kinga kwa wale wanaosalimisha silaha zao.

Maelfu ya bunduki zimekabidhiwa kwa mamlaka. Lakini hii ni sehemu ndogo ya silaha haramu zinazosambazwa.

Mhalifu mmoja aliambia BBC Africa Eye kwamba kupata bunduki nchini Kenya ni rahisi. Alisema angeweza kununua moja kwa shilingi 40,000 za Kenya ($300).

Kafu anasema watu walio tayari kusalimisha silaha zao haramu kwa mamlaka wanahofia wanaweza kuwa walengwa wao wenyewe.

Polisi wameshutumiwa kwa kuhusika na mauaji ya nje ya mahakama. Shirika la misaada la Kenya Missing Voices linasema zaidi ya watu 800 walikufa mikononi mwa maafisa wa polisi katika miaka mitano iliyopita. Wengi wao walikuwa vijana maskini.

Jijini Nairobi, BBC Africa Eye inaandamana na Kafu kukutana na mwanamume mwingine, ambaye tunamwita John, aliye tayari kusalimisha bunduki yake.

“Niko tayari kuirejesha. Unaenda kuua mtu. Utatumia pesa utakayopata ndani ya miezi mitatu, lakini umemwaga damu ya mtu. Umemuumiza mtu na kubaki na hatia. Hayo ni maisha ya shida."

Hofu kubwa ya John ya kwenda polisi ni kwamba kuna jambo lingemtokea.

Anaeleza kilichompata rafiki yake aliyemweleza mzee mmoja katika jamii kwamba alitaka kusalimisha bunduki mbili. Alichukuliwa na polisi na kisha kupatikana katika chumba cha kuhifadhi maiti wiki moja baadaye.

"Tatizo ni kuamini nani wa kumwambia, jinsi ya kuikabidhi," anasema.

Kumekuwa na madai mengi ya polisi wa Kenya kukodi na kuuza bunduki na risasi kwa wahalifu. BBC Africa Eye ilielekeza madai haya kwa polisi, lakini hawakujibu.

Kafu alimpigia simu mkuu wa polisi wa eneo hilo ili kumhakikishia mtu huyo usalama wake na siku chache baadaye walikwenda kituo cha polisi pamoja na kusalimisha bunduki yake.

Afisa huyo aliangalia nambari ya usajili ya silaha hiyo na ilikuwa na alama ya KP ambayo ni kifupi cha Polisi wa Kenya.

Katika mkutano wa polisi na waandishi wa habari kutangaza kurejeshwa kwa silaha hiyo, Kafu alitoa taarifa kwa umma kuhakikisha polisi wanazingatia ahadi yao ya kuwahakikishia usalam watu hao.

“Nataka serikali iwe wazi na vijana. Je, watakaporudisha silaha hizi, watatoweka au kuungwa mkono? Naiomba serikali itoe ushirikiano. Vijana hawa wanataka kuonyeshwa upendo.”

Hii pekee haitakomesha uhalifu wa kutumia bunduki nchini Kenya, lakini Kafu anasema ni mwanzo. Wahalifu wanamwamini, anasema, na anatumai kuwa anaweza kuhimiza watu zaidi kusalimisha silaha zao bila hofu ya kuadhibiwa.

“Tunajaribu kuwapigania vijana hawa,” anasema Kafu.

Maelezo zaidi:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi