Kupigwa hadi kukosa fahamu kwa kuchukua chakula cha ziada shuleni

    • Author, By Tom Odula Nairobi & Tamasin Ford iLondon
    • Nafasi, BBC Africa Eye

Caleb Mwangi alipigwa vibaya sana katika shule yake nchini Kenya baada ya kula chakula cha ziada wakati wa kifungua kinywa hadi akapoteza fahamu na kulazwa hospitali kwa siku 11 katika chumba cha wagonjwa mahututi.

"Nilipofika huko, hakuweza kuondoka kwenye kitanda chake. Hakuweza kuzungumza," babake Fred Mwangi aliambia BBC.

Hili lilitokea karibu miaka miwili iliyopita wakati Calebu alipokuwa na umri wa miaka 13. Sasa akiwa ameketi kati ya mama yake na baba yake kwenye sofa nyumbani kwao Mombasa, pwani ya Kenya, anasema huwa anajitenga mara kwa mara.

Kijana huyo amejawa na hasira ambayo nyakati fulani humfanya apige ngumi ukuta. Madhara, anasema, ya kiwewe kilichosababishwa na tukio hilo lililomtishia kifo.

Bw Mwangi anamfanya mwanawe asimame na kuvuta fulana yake nyeupe ili kunionyesha kovu kubwa kwenye mgongo wake.

Anasema majeraha yalikuwa mabaya hivyo daktari wa upasuaji alilazimika kutoa vipande vikubwa vya ngozi kwenye mapaja yake ili avitumie kama vipandikizi vya ngozi.

"Hapa yuko hospitalini," mamake Agnes Mutiri anasema, akionyesha picha za Caleb kwenye simu yake, ambazo haziwezi kuchapishwa. Amelala kifudifudi kitandani, michubuko imefunika miguu yake, mgongo na mikono, na hata uso wake. Ilikuwa na karibu mia kwa jumla.

"Mwili wake wote ulikuwa hivi."

Adhabu ya viboko shuleni ina historia ndefu nchini Kenya, tangu enzi ambapo wamisionari na wakoloni waliitegemea kudhihirisha mamlaka yao.

Mwaka wa 2001, serikali ya Kenya ilipiga marufuku adhabu hiyo shuleni, lakini imekuwa vigumu kubadili mitazamo ya watu.

Takwimu kutoka kwa ripoti ya hivi punde ya Ukatili Dhidi ya Watoto, utafiti wa kitaifa wa mwaka wa 2019, ulifichua kuwa zaidi ya nusu ya watoto wenye umri wa miaka 18 hadi 24 nchini Kenya walikubali kuwa ni muhimu kwa walimu kutumia adhabu ya viboko.

BBC Africa Eye imefichua ongezeko la kutia wasiwasi katika idadi ya visa hatari vinavyoripotiwa.

Caleb anasema Nancy Gachewa, mkurugenzi wa Gremon Education Centre - shule iliyopo Bamburi karibu na Mombasa - kwanza alimpiga na kisha akawaamuru wanafunzi wengine kuendelea na adhabu. Bi Gachewa anakanusha hili, na anasema hakuwepo shuleni lilipotokea.

"Nilikuwa na njaa sana, nilichukua chapati tano na kula pamoja na chai," Caleb anasema.

Bi Gachewa na mwanafunzi mkuu, Idd Salim, walikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya shambulio na kusababisha madhara makubwa mwilini. Salim alihukumiwa kifungo cha miaka minne jela mwaka jana na, katika makubaliano ya kusihi, ametoa ushahidi dhidi ya Bi Gachewa mahakamani. Kesi dhidi yake inaendelea.

Ingawa kisa cha Calebu ni cha kutisha, sio cha kipekee. Mfanyakazi katika Tume ya Kuajiri Walimu (TSC), shirika huru linalosimamia masuala yote ya taaluma ya ualimu nchini Kenya, alizungumza na BBC Africa Eye kwa sharti la kutotajwa jina.

Walisema kuwa katika miaka mitatu iliyopita, ripoti za vipigo vikali zaidi shuleni zimeongezeka zaidi ya mara nne kutoka saba hadi 29. Matukio mengi hayaripotiwi.

"Inazidi kuwa mgogoro na…tunahisi inaelekea kubaya. Visa vya watoto kujeruhiwa na kulemazwa. Baadhi ya visa vimesababisha madhara makubwa sana, hata kifo," walisema.

Chanzo hicho kilisema kuwa visa vya vipigo shuleni vinavyoripotiwa kwa TSC katika ngazi ya kaunti mara nyingi haviendi mbali zaidi, na kuongeza kuwa matukio "yalizimwa" na "hayawafikii wakuu wa elimu".

"Mara nyingi, hadi kesi inapotufikia, ushahidi mwingi umeharibika. Wakati mwingine hatuwezi hata kupata mashahidi."

BBC Africa Eye iliwasiliana na TSC kujibu madai haya, lakini haikujibu ombi hilo.

Mawazo ya kwamba mwanafunzi anaweza kufia mikononi mwa wataalamu wa elimu wanaopaswa kuwalinda ni jambo lisilofikirika kwa watu wengi, lakini katika miaka mitano iliyopita, zaidi ya vifo 20 vinavyohusishwa na vipigo shuleni vimeripotiwa kwenye vyombo vya habari.

Ebbie Noelle Samuels mwenye umri wa miaka kumi na tano anaaminika kuwa mmoja wao.

Ebbie alikuwa mwanafunzi wa shule ya malazi katika shule ya Sekondari ya Gatanga CCM katika kaunti ya Murang'a, karibu kilomita 60 (maili 37) kaskazini-mashariki mwa mji mkuu, Nairobi.

Mnamo tarehe 9 Machi 2019 mamake, Martha Wanjiro Samuels, alipigiwa simu na shule kusema binti yake alikuwa mgonjwa na kwamba yuko hospitalini.

Alipofika huko, Ebbie alikuwa tayari amekufa.

Shule hiyo ilisema kuwa alifariki akiwa usingizini, lakini walioshuhudia wanasema alipigwa na naibu mkuu wa shule kwa jinsi alivyosuka nywele zake.

"Ripoti ya uchunguzi wa maiti ilifichua kwamba alikuwa na jeraha kubwa la kichwa, kiwewe cha nguvu. Kwa hivyo, mtu alimpiga na kumsababishia jeraha la aina hiyo, na kusababisha kifo chake," alisema Bi Samuels.

Alifanya kampeni kwa miaka minne kutaka kifo cha bintiye kichunguzwe.

Januari iliyopita, Elizabeth Wairimu Gatimu, aliyekuwa naibu mkuu wa shule ya Ebbie, alikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji. Anakanusha mashtaka dhidi yake.

“Nitafanya kila ninaloweza kufanya maadamu niko hai ili kuhakikisha mtoto wangu anatendewa haki,” alisema Bi Samuels, ambaye bado anasubiri kusikiliza matokeo ya kesi hiyo.

"Nilijiambia: 'Sitanyamazishwa. Sitakaa kimya. Sitaacha kupigana.' Labda siku nitakayokata tamaa ndiyo siku nitalala kama binti yangu. Lakini muda wote nitakaoishi, sitakata tamaa."

BBC Africa Eye iliomba mahojiano na Wizara ya Elimu ya Kenya, lakini hakuna aliyekuwa tayari kuzungumza.

Shirika moja ambalo linashinikiza mabadiliko ni Beacon Teachers Africa, Iliyozinduliwa nchini Kenya miaka minne iliyopita na shirika lisilo la kiserikali la Plan International, pamoja na TSC, lengo lake ni kuwapa walimu fursa ya kuwalinda watoto shuleni na jamii zao.

Sasa ina mtandao wa walimu 50,000 katika nchi 47 barani Afrika.

Robert Omwa ni mmoja wa walimu 3,000 wa Beacon nchini Kenya. Pamoja na kuwaelimisha watoto kuhusu haki zao, pia hufanya warsha za kuwafundisha walimu jinsi ya kutoa nidhamu bila kutumia adhabu ya viboko.

"Hapo awali nilikuwa na mashaka juu yake. Nilidhani hii ni itikadi ya Kimagharibi, mtoto wa Kiafrika lazima apigwe. Lakini nilipojaribu, nilihisi faraja kama mwalimu. Nilihisi mwepesi zaidi. Nilihisi watoto wakinivutia zaidi." alisema.

Huko Mombasa, Caleb na familia yake wanasubiri kusikia hatima ya mkurugenzi wa shule yake. Bi Gachewa amekana mashtaka.

Kijana huyo wa miaka 15 bado anapata ugumu kukabiliana na hali iliyomsibu.

"Ili nipate haki, nataka mwanamke huyu afungwe jela."