Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Urusi inanufaika vipi na vita vya Iran?
- Author, Steve Rosenberg
- Nafasi, Editor de BBC News Ruso
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Rais wa Iran na Urusi wamezungumza kwa njia ya simu mara mbili kwa muda wa wiki moja.
Isreal na Marekani ikiendeleza mashambulizi yake dhidi ya Iran, rais wa Urusi Vladimir Putin, amejitokeza kama kiongozi anayetaka kuwapatanisha Iran na maadui wake.
Ingawa hili halina ushawishi. Kwani kiongozi huyo wa Urusi ndiye aliyevamia taifa huru la Ukraine mwaka wa 2022.
Wakati huo, Umoja wa Mataifa ulilaani uvamizi wa Ukraine kwa kusema ni ukiukwaji wa sheria za umoja wa mataifa.
Na huku ikitaka "suluhisho la haraka na la kisiasa kupatikana"
katika mgogoro wa Iran, Moscow inaendelea na vita vyake dhidi ya Ukraine.
Putin amejitolea kuwa mpatanishi
Moscow ina makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati na Iran.
Wiki hii Putin alisema kuwa anaiunga Tehran mkono.
Hata hivyo, ushirikiano huu wa kimkakati haijumuishi mkataba wa ulinzi wa pamoja. Badala yake, Moscow imejitolea kuwa mpatanishi wa mgogoro huo.
Katika mazungumzo ya simu siku ya Jumatatu na Rais wa Marekani Donald Trump, kwa mujibu wa Kremlin, Putin "alieleza mawazo yake ya kupata suluhisho la haraka la kidiplomasia la vita na Iran, kwa kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi za Ghuba, rais wa Iran na viongozi wa nchi nyingine."
Kwa Urusi, hii ni njia ya kuimarisha taswira yake katika mataifa ya Ghuba na Mashariki ya Kati, na kujionesha kama taifa lenye ushawishi. Pia fursa ya kuimarisha uhusiano wake na Washington.
Kremlin inataka kudumisha uhusiano mzuri wa kikazi na Trump. Inaamini kuwa uhusiano wake na utawala wa Trump unafaidi malengo ya kijeshi ya Moscow nchini Ukraine.
Hii inaelezea kwa nini Rais wa Urusi amekuwa akiepuka kumshutumu mwenzake wa Marekani, akisalia kimya hadharani kuhusu vita vya Iran.
"Anataka kusaidia," Trump alitangaza Jumatatu baada ya mazungumzo yake ya simu na Putin.
"Nikamwambia, 'Unaweza kuwa na msaada zaidi ikiwa utaisha vita kati ya Ukraine na Urusi. Hilo lingekuwa msaada zaidi,'" aliongeza.
Vikwazo vya mafuta
Huku Kremlin ikitoa wito wa "kusitishwa kwa vita" nchini Iran, mzozo huo unatoa fursa nyingine ya kuifaidi Moscow.
Hizi ni pamoja na fursa za kiuchumi.
Kuongezeka hivi karibuni kwa bei ya mafuta duniani kunaongeza mapato ya serikali ya Urusi, na kama bei ya mafuta itabaki juu kwa kipindi kirefu, itaisaidia Urusi kuendelea kufadhili vita vyake dhidi ya Ukraine.
Bajeti ya Urusi imejikita kwenye mauzo ya mafuta kwa bei ya dola za Marekani 59 kwa kila pipa.
Wiki hii, bei ya mafuta ghafi ilipanda na kufikia dola 120 kwa kila pipa. Ingawa bei hiyo imepungua bado iko juu ya dola 59.
Zaidi ya hayo, Trump ameashiria kwamba Marekani itafuta vikwazo vinavyohusiana na mafuta kwa baadhi ya mataifa ili kupunguza upungufu uliosababishwa na vita na Iran.
Iwapo vikwazo vya mafuta dhidi ya Urusi vitapunguzwa, Moscow inaweza kupata faida kubwa zaidi kifedha. Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, alisema kwamba hii itakuwa "pigo kubwa" kwa Kyiv na aliomba Trump asifanye hivyo.
Ingawa Kremlini haikukosoa rais wa Marekani, baadhi ya magazeti ya Urusi yamemkosoa vikali Trump na vita vya Iran.