Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mashambulizi ya anga yasababisha 'mvua nyeusi' ambayo haijawahi kushuhudiwa Tehran, wanasayansi wanasema
Picha za setilaiti zinaonesha moshi mwingi uliosababishwa na mashambulizi ya ghala la mafuta na mitambo ya kusafishia mafuta ukienea kote Tehran Jumatatu, huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likionya kwamba mashambulizi dhidi ya vituo vya mafuta yanaweza kusababisha hatari kubwa za kiafya kwa wakazi.
Tangu mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yaanze tarehe 28 Februari, tumethibitisha mashambulizi dhidi ya vituo vinne vya mafuta karibu na mji mkuu.
Wakazi walisema moshi na uchafuzi wa mazingira vimezuia Jua na kuacha harufu kali ya kuungua katika sehemu za jiji, huku wataalamu wakionya kuwa kiwango cha uchafu kinaweza kuwa ambacho hakijawahi kutokea.
Kuongezeka kwa uchafuzi wa hewa kunaonekana kujikita karibu na maeneo ya mafuta yaliyoharibika yaliyo karibu na mji mkuu, mji wenye takribani wakazi milioni 10, huku mamilioni zaidi wakiishi katika maeneo yanayozunguka.
Picha za hivi karibuni za setilaiti, zilizopigwa tarehe 9 Machi na kuchunguzwa na kitengo cha BBC Verify, zinaonesha kuwa vituo viwili vikubwa vya mafuta Tehran bado vinaungua moto, kufuatia mashambulizi ya anga yaliyoripotiwa kufanyika usiku wa kuamkia Jumamosi.
Picha hizo pia zinaonesha moshi ukitoka katika bohari la mafuta la Shahran depot lililoko kaskazini-magharibi mwa mji mkuu wa Iran, pamoja na kiwanda cha kusafisha mafuta cha Tehran oil refinery kilichoko kusini-mashariki mwa jiji hilo.
Video zilizothibitishwa za muda mfupi baada ya shambulio la Jumamosi zilionesha milipuko mikubwa ya moto ikimulika anga la usiku katika kiwanda hicho cha kusafisha mafuta.
Mchanganyiko wa mawingu na moshi unaotokana na moto unaoendelea unamaanisha kuwa bado hatuwezi kutathimini kiwango cha uharibifu katika vituo hivyo viwili vya mafuta vilivyoshambuliwa mwishoni mwa wiki.
Hata hivyo, picha zilizopigwa katika Shahran depot Jumapili asubuhi zilionesha wahudumu wa dharura wakikagua malori ya mafuta yaliyoteketea, majengo yaliyo na weusi na moto unaoendelea kuwaka.
Jeshi la Israel lilisema lilishambulia "bohari za mafuta" karibu na Tehran katika chapisho kwenye X tarehe 7 Machi, likiwa na picha inayoonesha uharibifu katika kinu cha kusafisha mafuta.
Kitengo cha BBC Verify kilitoa eneo la kituo hiki pamoja na maeneo mengine matatu tuliyotambua kwa jeshi la Israel na Wizara ya Ulinzi ya Marekani ili kutoa maoni.
Wizara ya Ulinzi haikutoa majibu, huku jeshi la Israel ikisema kuwa "hakukuwa na mashambulizi ya IDF katika maeneo hayo."
Tumeomba ufafanuzi zaidi kuhusu suala hilo.
Mashambulizi dhidi ya vinu vya kusafisha mafuta yanaweza kusababisha uchafuzi mkubwa wa hewa, kwa sababu maeneo hayo huwa na aina nyingi za kemikali.
Wakati mafuta yanapochomwa bila kukamilika, yaani kunapokuwa na oksijeni kidogo,huweza kutolewa gesi ya monoksidi ya kaboni (carbon monoxide) na chembechembe za masizi badala ya dioksidi ya kaboni na maji.
Moto wa mafuta pia unaweza kutoa oksidi za sulfuri na nitrojeni, ambazo zinaweza kuunda asidi zinapochanganyika na maji ya mvua. Aidha, moto huo unaweza kutoa hidrokaboni hatari, mchanganyiko wa metali, na matone ya mafuta yanayoweza kudhuru mazingira na afya ya binadamu.
Uchafuzi wa hewa ni mbaya kiasi gani?
Mwanamke mmoja wa Tehran mwenye umri wa miaka ya ishirini alisema kuwa anaweza "kunusa harufu ya kitu kinachoungua" kutokana na mashambulizi dhidi ya vituo vya mafuta.
"Siwezi kuona jua. Kuna moshi mbaya sana. Bado upo. Nimechoka sana," aliiambia BBC Persian siku ya Jumamosi.
Kutathmini kwa usahihi kiwango cha uchafuzi wa hewa ni jambo gumu kwa sababu hakuna vipimo vinavyofanywa ardhini, na data ya setilaiti ni vigumu kuitafsiri kutokana na upepo, mawingu na mambo mengine.
Hata hivyo, kutokana na mchanganyiko wa kemikali zinazoweza kuwa zimetolewa kutoka kwenye maeneo ya mafuta yaliyoharibiwa, wanasayansi wanaamini kuwa uchafuzi huo ni hatari sana na mkali, na ni tofauti kabisa na moshi wa kawaida unaoonekana katika miji kama Beijing au Delhi.
"Kilichotokea nchini Iran ni jambo ambalo halijawahi kutokea, kwa sababu uchafuzi huu unatokana na makombora na mashambulizi ya anga dhidi ya vinu vya kusafisha mafuta," alisema Akshay Deoras, mwanasayansi wa utafiti katika Chuo cha Reading.
Aliongeza kuwa migogoro mingi husababisha vumbi na chembechembe nyingi hewani, lakini mchanganyiko wa kemikali tofauti katika tukio hili ni wa kipekee sana.
Eloise Marais, profesa wa kemia ya anga na ubora wa hewa katika Chuo kikuu cha London, alikubaliana na maoni hayo.
Alisema kwamba katika hali nyingi, aina hii ya uchafuzi ingeonekana tu baada ya ajali kubwa sana ya viwandani, kama pale kiwanda kizima cha kusafisha mafuta kinapolipuka.
'Mvua nyeusi' ni nini na inasababishwa na nini?
Siku ya Jumapili, wakazi wa Tehran waliripoti mvua kubwa "mvua nyeusi."
Mvua nyeusi ni neno lisilo rasmi linalotumiwa kuelezea mvua iliyochanganyika na uchafuzi wa hewa, ambayo huifanya ionekane ya rangi nyeusi au nyeusi-kijivu.
Kwa kawaida, uchafuzi wa hewa huoshwa na mvua na kuondolewa kutoka angani, lakini mvua nyeusi ni tukio nadra na mara nyingi hutokea pale kunapokuwa na viwango vya juu vya masizi na uchafuzi mwingine wa hewa, wanasayansi waliiambia BBC Verify.
"Matone ya mvua yalifanya kazi kama sponji, ndogo au sumaku, yakikusanya vitu vyote vilivyokuwa angani wakati yalipokuwa yakishuka.
Ndiyo sababu wakazi waliona kile kinachoelezwa kama 'mvua nyeusi'," alieleza Akshay Deoras.
Pia inawezekana kwamba baadhi ya chembechembe kubwa za uchafu zilianguka kutoka hewani hata bila mvua kunyesha.
Athari zinaweza kuwa zipi?
Mkuu wa Shirika la Afya Duniani tayari ameonesha "wasiwasi mkubwa" kuhusu athari za mgogoro huo kwa afya ya watu.
Uharibifu wa vituo vya mafuta "unaweza kuchafua chakula, maji na hewa, hatari ambazo zinaweza kuwa na athari kubwa kiafya, hasa kwa watoto, wazee, na watu wenye magonjwa yaliyokuwepo tayari," alisema Tedros Adhanom Ghebreyesus.
"Kuathiriwa sana na chembechembe hizi ndogo hewani kuna athari za haraka kwenye mapafu," aliongeza Anna Hansell, profesa wa epidemiolojia ya mazingira katika Chuo Kikuu cha Leicester.
"Lakini pia kunaweza kuwa na athari za muda mrefu kwa miaka mingi, zikiathiri mfumo wa kupumua na kuongeza hatari ya saratani."
Doug Weir, mkurugenzi wa Conflict and Environment Observatory, shirika ambalo hufuatilia na kuongeza uelewa kuhusu athari za mazingira zinazotokana na migogoro ya kijeshi na shughuli za kijeshi,alisema jambo lisilo la kawaida kuhusu Tehran ni kwamba mashambulizi kama haya hayajawahi kuonekana katika eneo lenye watu wengi kiasi hiki.
"Mara nyingi maeneo ya visima au maeneo ya mafuta huwa mbali vijijini. Lakini watu wa Tehran sasa wanakabiliwa na kemikali nyingi tofauti katika mvua hii nyeusi, sio mafuta tu," alisema.
Utabiri wa hali ya hewa wa BBC Weather unaonesha vipindi vya mvua Jumanne na tena kuanzia Alhamisi, pamoja na upepo mkali zaidi. Hali hiyo inaweza kusaidia kusambaza na kuondoa baadhi ya uchafuzi wa hewa.
Hata hivyo, hiyo haimaanishi hatari za uchafuzi zitaisha kabisa. Uchafu huo unaweza:
kuingia katika mito na njia nyingine za maji au kukaa ardhini, na baadaye ardhi ikikauka upepo unaweza kuuchukua tena na kuurudisha hewani.