Je, ni kisiwa gani muhimu cha Iran ambacho Marekani inataka kukiteka?

Muda wa kusoma: Dakika 3

Kisiwa cha Kharg nchini Iran, ni eneo ambalo limekuwa likilengwa siku za hivi karibuni, baada ya Israel na Marekani kuishambulia Iran, huku Iran ikijibu mashambulizi hayo.

Kisiwa hicho kidogo kaskazini mwa ghuba ya uajemi, kilomita 25 hadi 30 kutoka pwani ya Iran, ni eneo muhimu katika sekta ya mafuta nchini humo. 90% ya mafuta kutoka Iran, husafirishwa kutoka eneo hili.

Kutokana na kuwa katika eneo la kimkakati, kisiwa hiki kinaweza kushambuliwa, ila bado hakijashambuliwa moja kwa moja katika vita vinavyoendelea.

Mtandao wa Marekani wa Axios, umesema kuwa, Marekani bado inajadili jinsi ya kukabiliana na vita eneo la Mashariki ya Kati, ikiwemo kuichukua kisiwa cha Kharg.

Umuhimu wa kisiwa hicho, imewafanya wachambuzi na maafisa wa Washington kuhoji athari za kuilenga na kukiteka kisiwa hicho.

Kisiwa cha Kharg kinalengwa kijeshi

Eneo la kimkakati la kiuchumi la kisiwa cha Kharg linaiweka katika hatari ya kulengwa kijeshi.

Baadhi ya wachambuzi wanaamini kwamba kulenga au kuchukua kisiwa hicho kunaweza kuathiri mapatao ya mafuta ya Iran.

Jarrod Agen, mshauri wa Bunge, alisema mjini Washington kwamba "Marekani inajaribu kuondoa akiba za mafuta ya Iran mkononi mwa magaidi," akiashiria uwezekano wa kudhibiti rasilimali za nishati za Iran ili kushinikiza serikali ya Tehran kujisalimisha.

Wazo la kudhibiti Kisiwa cha Kharg, ambacho ndicho kitovu kikuu cha usafirishaji wa mafuta nchini humo, limeibuliwa tena.

Mchambuzi Michael Rubin alielezea hatua hiyo kama njia moja ya kuathiri mapato ya mafuta ya serikali ya Iran.

Lakini kwa upande mwingine, afisa wa zamani wa Marekani, Richard Nephew, alionya kwamba kulenga kisiwa hicho "kunaweza kusababisha kuongezeka kwa mashambulio na kuhatarisha utulivu wa masoko ya nishati duniani."

Wataalamu wengine wanasema kwamba kukichukua kisiwa hicho kunahitaji operesheni za kijeshi za ardhini, wala si mashambulio ya angani pekee.

Kitovu cha usafirishaji Mafuta nchini Iran

Kisiwa cha Kharg ndicho bandari kubwa zaidi cha usafirishaji mafuta ya Iran, na ni nguzo muhimu ya miundombinu ya nishati ya nchi hiyo.

Takriban asilimia 90 ya mauzo ya mafuta ghafi ya Iran hupitia kisiwa hiki kabla ya kusafirishwa kwenda masoko ya kimataifa, mara nyingi kupitia eneo la bahari la mlango wa Hormuz, mojawapo ya njia muhimu za nishati duniani.

Vituo vya mafuta vya kisiwa hiki vina uwezo wa kusafirisha mamilioni ya mapipa ya mafuta kila siku, na kufanya kisiwa hiki kuwa kiungo muhimu katika usafirishaji wa mafuta ya Iran hadi masoko ya kimataifa.

Kisiwa hiki kimeunganishwa na mabomba ya mafuta ya chini ya bahari, ambayo yanaunganisha baadhi ya visima vikubwa zaidi vya mafuta vya Iran.

Mafuta huchimbwa kutoka visima hivyo, kisha kusafirishwa hadi kwa kisiwa hicho ambapo huhifadhiwa kwenye tanki kubwa, kabla ya kupakiwa kwenye meli kubwa za kusafirisha mafuta. Eneo hili la bahari lina kina ndefu za kustahimili meli kubwa za kubeba mafuta.

Hii ni muhimu kwa sababu sehemu nyingi za bahari pwani ya Iran zina kina kidogo, na hivyo haziwezi kuhimili meli kubwa za mafuta.

Hii inaifanya Kisiwa cha Kharg kuwa mojawapo ya maeneo machache yanayoweza kutekeleza operesheni ya kiwango kikubwa.

Kwa kuwa miundombinu muhimu ya mafuta ya Iran ipo katika eneo hili, wataalamu wanasema kisiwa hiki ni "udhaifu" mkubwa wa uchumi wa Iran.

Maafisa wa Marekani wanasema umuhimu wake ni mkubwa kiasi kwamba uchumi wa Iran unaweza kuathirika sana ikiwa operesheni za kisiwa hicho zitavurugika.

Hadi leo, kisiwa hiki kina vituo vikubwa vya kuhifadhi mafuta, bandari za usafirishaji wa mafuta, makazi ya wafanyakazi, na uwanja mdogo wa ndege unaouunganisha kisiwa hicho na bara la Iran.