Mahsa Amini: Gharama ya kutangaza habari ya kifo iliyotikisa Iran

Niloufar Hamedi and Elaheh Mohammadi

Chanzo cha picha, Twitter

Maelezo ya picha, Niloufar Hamedi na Elaheh Mohammadi wamezuiliwa nchini Iran kwa zaidi ya siku 200

Jina la Mahsa Amini liligonga vichwa vya habari kote ulimwenguni, wakati mauaji yake mnamo Septemba 2022 yalisababisha mawimbi ya maandamano nchini Iran.

Lakini si watu wengi wamesikia kuhusu Niloufar Hamedi na Elaheh Mohammadi.

Hao ni waandishi wa habari wawili waliosaidia kutangaza kisa cha kifo cha Mahsa na wamezuiliwa katika jela moja maarufu nchini Iran tangu wakati huo.

Iran ni moja ya nchi mbaya zaidi linapokuja suala la uhuru wa vyombo vya habari.

Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani tarehe 3 Mei inalenga kuangazia Iran na maeneo mengine, ambapo waandishi wa habari wanaweza kuteswa, kufungwa jela na hata kuuawa kwa kazi yao.

A man and a woman hugging in a hospital corridor

Chanzo cha picha, Twitter

Maelezo ya picha, Picha hii ya baba na bibi wa Mahsa ilisambaa kwa kasi

Mahsa alifariki akiwa chini ya ulinzi wa polisi baada ya kuzuiliwa kwa kushindwa kuvaa kilemba chake "vizuri".

Wakiwa hospitalini, walipopata habari za kifo cha kijana huyo mwenye umri wa miaka 22, babake Mahsa na nyanyake walikutana pamoja kwa kukumbatiana.

Niloufar Hamedi, mwandishi wa habari wa gazeti la Shargh, alipiga picha ya wakati huo wa huzuni, na kuiweka kwenye akaunti yake ya Twitter. Kando ya picha hiyo, Hamedi aliandika: "Vazi jeusi la maombolezo limekuwa bendera yetu ya taifa."

Siku mbili baadaye, Elaha Mohammadi, mwandishi wa gazeti la Hammihan, alichapisha ripoti kuhusu mazishi ya Mahsa katika mji aliozaliwa wa Saqez, katika jimbo la Kurdistan.

'Nchi ya majonzi'

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mohammadi alianza makala yake - yenye kichwa cha habari "Nchi ya majonzi" - akimnukuu baba yake Mahsa: "Mahsa hakuwa tatizo lolote la kiafya. Yeyote anayesema hivyo, anadanganya."

Mashahidi walisema kuwa Mahsa alipigwa akiwa chini ya ulinzi wa polisi lakini mamlaka ya Iran imekanusha hilo, na kulaumu "kushindwa kwa moyo kwa ghafla" kwa kifo chake.

Makala ya Mohammadi yaliendelea kuelezea jinsi karibu wanaume na wanawake 1,000 walikusanyika katika makaburi kwa ajili ya mazishi.

Waombolezaji walipiga kelele, "Mwanamke, maisha, uhuru," aliripoti. Maneno haya yangesikika baadaye kwenye maandamano kote nchini.

Juu ya kaburi la Mahsa iliandikwa: "Hutakufa. Jina lako litakuwa ishara."

Ulikuwa ni unabii wa matukio ambayo yangetikisa nchi katika siku na miezi ijayo.

Siku chache tu baada ya kutweet picha ya familia ya Mahsa ikiwa na huzuni, Hamedi alikamatwa.

Wakati huo huo, vikosi vya usalama pia vilivamia nyumba ya Mohammadi, na kukamata vifaa vyake vya kielektroniki. Wiki moja baadaye, yeye pia alikamatwa.

Mahsa Amini

Chanzo cha picha, Mahsa Amini family

Maelezo ya picha, Mahsa Amini alikaa kwa siku tatu akiwa katika hali ya kukosa fahamu kabla ya kufariki dunia hospitalini

Hamedi na Mohammadi walijulikana kwa ripoti ngumu za habari na uandishi wa masuala ya haki za binadamu.

"Mara nyingi alikuwa mwandishi wa habari wa kwanza kutoa taarifa," anasema Sina Ghanbarpour, mwandishi wa habari wa Irani.

"Kwa hivyo Mahsa Amini alipokamatwa na maafisa wa polisi wa maadili, haikushangaza kwamba nilisoma juu yake mara ya kwanza kwenye ripoti ya Nilofar Hamedi."

Wawili hao hivi majuzi walitunukiwa tuzo ya Louis M Lyons kutoka Chuo Kikuu cha Harvard, ambayo inatambua dhamiri na uadilifu katika uandishi wa habari.

"Hamedi na Mohammadi waliweka riziki na maisha yao kwenye mstari, na kupoteza uhuru wao katika mchakato huo," wenzake waliopigia kura tuzo hiyo walisema.

"Walijua hatari kubwa wanayoweza kukabiliana nayo lakini walibaki wamejitolea kusimulia hadithi ya Amini.

"Waandishi wa habari nchini Iran wanahatarisha maisha yao kila siku ili kuripoti hali na dhuluma huko."

Protesters hold up picutres of Mahsa Amnini in Berlin, Germany

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Kifo cha Mahsa Aminiled kilisababisha maandamano makubwa Iran na maeneo mengine Duniani

Utawala wa Kiislamu unadhibiti sehemu kubwa ya vyombo vya habari nchini humo na waandishi wa habari na vyombo huru vya habari viko chini ya shinikizo kubwa. Upatikanaji wa mtandao mara nyingi hukatwa.

Kulingana na shirika la Reporters Without Borders, waandishi wa habari nchini Iran "hudhulumiwa mara kwa mara kwa kukamatwa kiholela na hukumu nzito zinazotolewa baada ya kesi zisizo za haki mbele ya mahakama za mapinduzi".

"Ni jinamizi lisiloisha," mwandishi mmoja wa habari anayeishi Tehran hivi majuzi aliwaambia Waandishi Wasio na Mipaka. "Ninaogopa kuandika chochote, hata kwenye daftari langu. Ninahisi ninatazamwa kila wakati."

Ingawa Hamedi na Mohammadi waliungwa mkono na magazeti yao, bado ni waandishi wa habari ambao walipaswa kukabiliana na matokeo.

Waandamanaji kuzuiliwa na waandishi kukamatwa

Makumi ya waandishi wa habari walikamatwa nchini Iran tangu kifo cha Mahsa na mamlaka zinajulikana kuwanyanyasa wanafamilia wa waandishi wa habari pia.

Waandamanaji pia wamezuiliwa kwa maelfu yao, na mamia wameuawa.

Miezi sita baadaye, maandamano hayaonekani lakini wengi bado wanapigania kukomeshwa kwa mfumo ambao umedhibiti maisha yao ya kibinafsi na ya umma.

Wanawake wengi kote Irani wanachagua kutotii sheria za hijab zinazolazimishwa na wanahatarisha sana kila wanapotoka nje bila hijabu.

A woman stands on top of a car bonnet and sets her headscarf on fire on 19 September 2022 in central Tehran during protests for Mahsa Amini

Chanzo cha picha, Twitter

Maelezo ya picha, Wanawake wameonekana wakichoma hijabu zao wakati wa maandamano

Wanahabari hao wawili wamezuiliwa katika mazingira magumu katika mfumo wa magereza wa Iran. Ripoti kutoka ndani zinaonyesha kuwa vituo hivyo havina ubinadamu, na ukosefu wa dawa, chakula, na hata maji salama ya kunywa au hewa safi.

Mohammadi alipoteza kilo 10 katika miezi mitatu ya kwanza ya kizuizini, mumewe aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Wakati huo huo, Hamedi na Mohammadi wametatizika kupata usaidizi wa kisheria.

Mwanasheria kukamatwa

Wakili wa kwanza aliyeteuliwa kuwawakilisha wawili hao alisema mnamo Oktoba 2022 kwamba hakuweza kuwasiliana nao au kupata hati za kisheria zinazohusu kukamatwa kwao.

Chini ya mwezi mmoja baadaye, alikamatwa.

Familia za Hamedi na Mohammadi zinakabiliwa na uchungu wa kutojua kitakachowapata.

"Ninaulizwa, 'Wenye mamlaka wanakuambia nini?' Sina uhakika hata na taasisi gani au mtu gani wa kuwasiliana naye," mume wa Hamedi, Mohammad Hossein Ajorlo, alisema katika mahojiano na Sharq.

Yeye pia ametatizika kupata taarifa kuhusu kile ambacho mkewe anatuhumiwa nacho na kile kinachoweza kumtokea.

Siku chache kabla ya Mwaka Mpya wa Iran, mkuu wa mahakama ya Iran alitangaza msamaha kwa maelfu ya wafungwa, ikiwa ni pamoja na waandamanaji 22,000.

Lakini si Hamedi wala Mohammadi aliyepokea msamaha.

Man looks at newspaper with drawing of arrested journalists Elaheh Mohammadi and Niloufar Hamedi on 30 November 2022

Chanzo cha picha, EPA-EFE

Maelezo ya picha, Wanahabari Elaheh Mohammadi na Niloufar Hamedi, miongoni mwa waliokamatwa, wameshikiliwa tangu Septemba.

Baada ya zaidi ya siku 200 rumande, wiki hii Hamedi na Mohammadi waliambiwa mashtaka yanayowakabili.

Masoud Satayshi, msemaji wa Idara ya Mahakama ya Iran, alisema wawili hao wanashutumiwa kwa "ushirikiano na serikali hasimu ya Marekani, kula njama na njama dhidi ya usalama wa taifa, na shughuli za propaganda dhidi ya utawala huo".

Hakimu mashuhuri Abolqasem Salavati, anayejulikana kwa kutoa hukumu kali sana, anaongoza kesi za Hamedi na Mohammadi.

Anaitwa "jaji wa kifo" kwa sababu ya hukumu nyingi za kifo ambazo ametoa.

Mwezi uliopita, mume wa Hamedi alishiriki picha kwenye Twitter ya bangili mbili za urafiki, zikiwa zimefungwa kwenye mkono wake.

Katika maelezo, alielezea ilikuwa zawadi ambayo alikuwa amempa kuashiria Nowrooz, mwaka mpya wa Irani. Hamedi alikuwa amezisuka kwa uzi uliotolewa kwenye taulo za jela.

Alimaliza chapisho hilo kwa maneno, "Mwanamke, maisha, uhuru."