Jangwa lisilokalika la California ambako Marekani huwatelekeza wahamiaji wanaovuka mpaka

Chanzo cha picha, Getty Images
Na Leire Sales
BBC News, California
"Thursday," ni neno lililoandikwa kwenye bangili ya rangi ya bluu ambayo Marta ameivaa kwenye mkono wake. Ni neno linalomaanisha siku ya Alhamisi lililoandikwa kwa lugha ya Kiingereza.
Ni kwa ajili ya kumbukumbu ya siku gani alifika; kwa sababu tarehe yake ya kuondoka haijulikani.
Wiki mbili zilizopita, raia huyu wa Colombia alisafiri kwa ndege kama mtalii kwenda Cancun na kisha akaelekea katika mpaka wa kaskazini mwa Mexico, hadi eneo la Baja California ambako ukuta uliamriwa kujengwa na Donald Trump. Akavuka mpaka na kuingia Marekani na kujisalimisha kwa mamlaka na kuomba hifadhi.
Na leo itambidi alale nje katika eneo lenye upepo kwenye kipande hiki cha jangwa la California, katikati ya San Diego na Calexico, kilomita kadhaa kutoka mji wa karibu wa Jacumba.
Wastani wa wahamiaji 500 hufika kila siku tangu mwezi Mei, wakisubiri kuchukuliwa ili kesi zao ziweze kushughulikiwa.

Chanzo cha picha, LEIRE VENTAS
Sio kituo rasmi cha kizuizini, lakini ni aina kituo kisicho rasmi cha kusubiri foleni uliyojaa, kulingana na maelezo kutoka Forodha na Ulinzi wa Mpaka (CBP) yenyewe. Lakini kuondoka katika eneo hilo huchukuliwa kuwa ni uhalifu na serikali ya shirikisho.
"Walituacha eneo ambalo hatulijui, bila ya chochote," anaeleza kwa majonzi muuguzi kijana, huku akisugua mikono yake kupambana na baridi. "Hakuna anayejua atakaa hapa hadi lini. Kuna watu wamekaa mpaka siku tano hapa."

Chanzo cha picha, Getty images
Kambi zisizo na miundombinu
Wanaiita Camp Willow. Ni moja ya hizo kambi tatu katika eneo hilo.
Kitu pekee kinachopatikana ni vichaka, ardhi, miamba, vyoo viwili vinavyoweza kuhamishwa vilivyotolewa na mamlaka za Marekani ambavyo hutolewa mara moja baada ya wiki na nusu.
Mahema ya rangi ya waridi yaliyotolewa na mashirika yanayotetea haki za wahamiaji.

Chanzo cha picha, Getty Images
Theresa Chang, ni daktari ambaye pia ni mwanasheria, amekuja kutoka San Francisco kuwasaidia wahamiaji katika mpango wa kujitolea ambapo hutoa maji na chakula mara mbili kwa siku.
Kazi yake ni kutathmini afya ya wale wanaosubiri hapa na kuwasaidia ikiwa mtu ana tatizo la afya.
"Ana dalili za msongo wa mawazo," ananiambia Chang kuhusu Yenis Leydi Arias, msichana mwenye macho meusi anayejieleza kwa shida.
"Tuliondoka Cuba na ndoto ya kuja Marekani lakini angalia namna tulivyowasili, inasikitisha," aliniambia huku akizungumza kwa kigugumizi.
Wakati huo huo, Armando Cárdenas ambaye ni muathiriwa wa kimbunga cha Carribean alikuwa akimsaidia msichana huyo kuvaa viatu na kufunika miguu yake.

Chanzo cha picha, LEIRE VENTAS
Walipata ajali ya barabarani huko Chiapas, kusini mwa Mexico, nchi ya tatu kwenye njia yao ya kaskazini tangu walipoondoka katika kitongoji chao cha Havana mwezi Septemba kupitia Nicaragua.
"Nililazwa siku 25 bila fahamu katika hospitali ya Huixtla. Nilipoamka waliniambia sitaweza tena kutumia mkono wangu," anaeleza.
''Ninashangaa jinsi walivyoweza kusafiri kilomita 4,000 zinazotenganisha mipaka ya kusini na kaskazini mwa nchi hiyo katika hali hii,'' anasema Cheng huku akijaribu kuwasiliana na walinzi wa doria wa mpaka ili kuwahamisha.
"Kazi ya Mamlaka"
Wahudumu wengine wa kujitolea wanajiandaa kutoa chupa za maji, mchuzi wa maharagwe, mchuzi wa karanga, sandwichi na chai ya moto.
''Wanawake watatu wenye watoto watano waliondoka Ecuador wiki nane zilizopita,'' anasema María, mama wa watoto wawili. Walikuwa na duka dogo la vyakula, lakini walilazimika kulifunga kwa sababu ya unyang'anyi.

Chanzo cha picha, LEIRE VENTAS
Ni "majambazi," alijibu alipoulizwa anazungumzia watu gani. "Nchi imekuwa mbaya sana," anasema, huku akiwakaripia watoto kwamba wasipoharakisha watakosa mgao wao wa chakula.
Chakula kilicholetwa na watu wa kujitolea ndio pekee utakachoona katika kambi wiki nzima.
Katika eneo hili lenye wahamiaji 550, inaelezwa kuwa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita wahamiaji 16,000 waliweza kulishwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Tunafanya kazi ambayo Shirika la Msalaba Mwekundu kwa kawaida hufanya katika hali kama hii; kazi ambayo mamlaka inapaswa kufanya," anasema Samuel Schultz.
Mhandisi huyo alifanya kazi kwa miaka kama mkandarasi wa mashirika ya misaada ya majanga ya kimataifa huko Asia ya Kusini.
Takwimu
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, zaidi ya wahamiaji milioni mbili wamezuiliwa katika mpaka wa Mexico na Marekani, idadi ambayo ni kubwa kulingana na rekodi za wahamiaji, kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka (CBP).
Kanuni ya 42, ambayo tangu Machi 2020 iliruhusu mamlaka za Marekani kuwafukuza wahamiaji ambao wanajaribu kuingia nchini humo bila utaratibu, ilimalizika Mei mwaka huu.
Kabla ya sera hiyo kumalizika, utawala wa Biden ulibuni njia za kisheria za kuingia kwa wahamiaji huku ukiweka adhabu kali kwa kuvuka mpaka kinyume cha sheria.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Wizara ya Usalama wa Ndani inaendelea kutekeleza sheria za uhamiaji za Marekani, kupanua njia za kisheria huku ikiwachukulia hatu wale wanaovuka mpaka kinyume cha sheria," alisema msemaji wa shirika hilo, alipoulizwa kwa nini mamia ya watu wanahifadhiwa kwa masaa, hata siku katika kambi kama Willow.
Katika taarifa iliyotumwa kwa BBC, inaeleza wale ambao wameingia kinyume na utaratibu huenda wakafukuzwa nchini Marekani na watazuiwa kuingia Marekani kwa angalau miaka mitano. Vilevile kuna uwezekano wa kukabiliwa na kesi za jinai ikiwa watajaribu tena kuingia Marekani bila idhini.
"CBP inatumia rasilimali zote zilizopo na ushirikiano kuwachunguza wahamiaji kwa ufanisi na kwa mujibu wa sheria," inasema ripoti hiyo.
Katika mazungumzo yasiyo rasmi, wakala wa doria ya mpakani anasema lengo ni kuwasafirisha haraka iwezekanavyo hadi kwenye vituo rasmi ambapo kesi zao zitachunguzwa, na wale walio katika mazingira magumu zaidi wanapewa kipaumbele.
Hata hivyo kumekuwa na ukosoaji kwa kile kinachofanyika tangu mwezi Mei.
Mashirika saba yanayotetea haki za wahamiaji yaliwasilisha malalamiko katika Ofisi ya Haki za Kiraia na Uhuru wa Kiraia (CRCL), dhidi ya Wizara ya Usalama wa Ndani na Ofisi yake ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka (CBP), kwa kukiuka haki za ulinzi kwa wanaotafuta hifadhi katika kambi hizi.
"Ni jambo la kusikitisha kwamba Wizara ya Usalama wa Ndani inadai kuna 'ukosefu wao wa rasilimali' na kuwaweka wakimbizi katika mazingira magumu katika magereza ya wazi bila chakula, maji, makazi, vifaa vya kutosha vya usafi au huduma za matibabu," alisema mtetezi wa wahamiaji, Erika Pinheiro.
Maafisa wawili waliovaa sare huwaamrisha wahamiaji kupanga mistari sita mirefu ili kupanda katika mabasi madogo. Wengi huachwa nyuma, wahamiaji kutoka nchi mbalimbali kama China, Uzbekistan, Cameroon, Brazil na Uturuki.
Hali ni hiyo hiyo katika kambi nyingine mbili za wazi zilizoko katika jangwa linalozunguka Jacumba zinazoitwa Valley of the Moon na Camp 177.

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika upande mwingine wa ukuta, mamlaka ya uhamiaji ya Mexico pia inaangazia ongezeko la wahamiaji wanaowasili na asili ya wahamiaji.
Watu kutoka nchi 126 wanawasili katika viwanja vya ndege vya Mexico na Tijuana kila mwezi. Idadi hiyo inaongezeka. Na wengine hufika kwa magari na kuomba hifadhi nchini Marekani.
Wakati huo huo, Schultz anaendelea kuratibu watu wa kujitolea na kuwahudumia wahamiaji waliopo jangwani.
"Walinzi wa mpaka walituambia - njia pekee ya kubadilisha hali hii ni sisi kuacha kufanya kile tunachowafanyia wahamiaji na kuwaacha wawe na njaa, wapate magonjwa, labda hata wafie hapa," anasema Schultz.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Rashid Abdallah












