Wanaume Uingereza wapewa pauni milioni 10 kujifanya baba katika ulaghai wa visa, uchunguzi wa BBC umegundua

.

Wanaume wa Uingereza wanachukua malipo ya maelfu ya pauni ili kujifanya baba kwa wanawake wahamiaji, uchunguzi wa BBC umegundua.

Wanapewa hadi £10,000 ili kuongeza majina yao kwenye vyeti vya kuzaliwa - kuwezesha mtoto kupata uraia wa Uingereza na kuwapa akina mama njia ya kuishi.

Walaghai wanatumia Facebook kupigia debe biashara hiyo na wanadai kuwa wamesaidia maelfu ya wanawake kwa njia hii.

Facebook inasema maudhui kama hayo yamepigwa marufuku kulingana na sheria zake.

Uchunguzi uliofanywa na BBC Newsnight, uligundua kuwa ulaghai huo unafanyika katika jamii tofauti nchini Uingereza.

Iligundua mawakala wanaofanya kazi kote Uingereza ambao wanatafuta wanaume wa Uingereza kuwa baba bandia.

Mtafiti alifanya uchunguzi wake kichini chini, akijifanya kama mwanamke mjamzito ambaye alikuwa nchini Uingereza kinyume cha sheria, na alizungumza na watu wanaotoa huduma hizi.

Wakala mmoja, aliyefahamika kwa jina la Thai, alimwambia kuwa ana wanaume wengi wa Uingereza ambao wangeweza kuwa baba bandia na akatoa "kifurushi kamili" kwa £11,000.

Thi Kim, one of the agents who spoke to BBC Newsnight
Maelezo ya picha, Thi Kim, wakala aliyejitolea kuanzisha mpango na kumtafuta Muingereza

Alielezea mchakato huo kuwa "rahisi sana" na akasema "atafanya kila kitu" kumpatia mtoto huyo pasipoti ya Uingereza.

Thai, ambaye hakutangaza kwenye Facebook, alisema angetunga simulizi ya kushawishi ili kufanikiwa kudanganya mamlaka.

Alimtambulisha mtafiti huyo wa siri kwa mwanaume Muingereza anayeitwa Andrew, ambaye alisema angejifanya kama baba.

Andrew angelipwa £8,000 kutoka kwa ada ya jumla.

Wakati wa mkutano wao, Andrew alionyesha pasipoti yake ili kuthibitisha kuwa alikuwa raia wa Uingereza. Pia alijipiga picha na mtafiti huyo.

.
Maelezo ya picha, Mtafiti wa Newsnight (uso ukiwa umefunikwa) akiwa na Andrew
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

BBC haikulipa pesa zozote kwa ajenti yeyote anayetoa huduma hiyo ya kudanganya kuwa baba.

Wakati Thai alipokabiliwa baadaye kuhusu kuhusika kwake katika sakata hiyo, alikanusha makosa yoyote na kusema "hakujua chochote kuhusu hilo".

Andrew bado hajajibu ombi letu la kutoa maoni yake.

Wakala mwingine, anayejiita Thi Kim, alidai kuwa amesaidia maelfu ya wanawake wajawazito wahamiaji.

Alisema anaweza kumtafuta mwanaume wa Uingereza na ingegharimu "elfu kumi kwa baba", na ada yake kuwa £300.

"Wanaume wote ninaowatumia walizaliwa hapa na hawajawahi kujiandikisha kupata watoto wowote," Thi Kim alimwambia mtafiti.

"Najua jinsi ya kushughulikia kila kitu. Huna haja yakuwa na wasiwasi kuhusu kutokuwa na pasipoti. Hakika hatimae utaipata."

Thi Kim hajajibu ombi la BBC la kutoa maoni yake.

Ulaghai huo wa kujifanya kuwa baba bandia unaelezewa kuwa "uliofafanuliwa sana" na wakili wa uhamiaji Ana González.

"Ni wa kisasa sana, na ni vigumu sana kugundulika na polisi," anasema.

"Kwa namna fulani ni uthibitisho wa jinsi wanawake hawa walivyo na tamaa na bila kujali watapitia nini ili kupata haki ya kubaki Uingereza."

Ikiwa mwanamke mhamiaji yuko nchini Uingereza kinyume cha sheria na amejifungua mtoto aliyezaa na raia wa Uingereza au mwanamume aliye na hati ya kuwa Uingereza milele, mtoto huyo moja kwa moja ni Mwingereza kwa kuzaliwa.

Kisha mama anaweza kutuma maombi ya visa ya familia, ambayo itampa haki ya kubaki Uingereza - na kuomba uraia kwa wakati ufaao.

"Sheria hii ni ya kuwalinda watoto, sio kuwapa viza wanawake ambao hawana stakabadhi halali nchini Uingereza," anasema Bi González. "Sio mwanya. Haifai kuchukuliwa hivyo."

BBC haikuweza kukadiria ukubwa wa ulaghai huo, kwani Ofisi ya Mambo ya Ndani haikuweza kutoa data kuhusu idadi ya kesi ilizochunguza.

Pia haichapishi data kuhusu idadi ya visa zilizotolewa kwa wazazi wasio Waingereza wa watoto wa Uingereza.

"Sio mara moja tu, ni uwezekano wa maelfu" ya visa

Thai, who offered to act as a broker
Maelezo ya picha, "Thai" ilijitolea kufanya kazi kama wakala wa mtafiti wa siri wa Newsnight

Hata hivyo, mwaka jana visa 4,860 za familia zilitolewa kwa "wategemezi wengine" - kitengo ambacho kinajumuisha wale wanaoomba kukaa Uingereza kama wazazi wa watoto wa Uingereza.

Kutoa maelezo ya uwongo kwa makusudi kwenye cheti cha kuzaliwa ni kosa la jinai.

Ofisi ya Mambo ya Ndani imeambia BBC kwamba ina hatua za kuzuia na kugundua ulaghai wa uhamiaji kwa kutumia vyeti vya uongo vya kuzaliwa.

Inasema kwamba "cheti cha kuzaliwa pekee kinaweza kisiwe ushahidi wa kutosha wa uthibitisho wa baba" na katika hali ambapo hii inahitaji kuthibitishwa, "ushahidi wa ziada unaweza kuombwa ili kuwezesha ukaguzi wetu kukamilika kwa kujiridhisha".

Hata hivyo, wakili wa uhamiaji Harjap Bhangal hakubaliana na hayo kwamba hatua za kutosha zinachukuliwa: "Sio mara moja tu, ni uwezekano wa maelfu... Ofisi ya Mambo ya Ndani haijachukua hatua kuhusiana na hili."

Anasema kuwa tabia hiyo hutokea katika jamii nyingi tofauti za wahamiaji zikiwemo zile za India, Pakistan, Bangladesh, Nigeria na Sri Lanka, na kwamba imekuwa ikitokea kwa miaka mingi.

Uchunguzi wa programu ya Newsnight uligundua kuwa kitendo hicho haramu kinatangazwa sana kwenye baadhi ya vikundi vya Facebook vya Vietnam kwa wanaotafuta kazi.

"Ikiwa una mimba na huna baba zungumza na mimi."

Tulipata machapisho kadhaa kutoka kwa akaunti zinazojivunia sifa kama baba bandia wanaofaa na vile vile wanawake wanaotafuta wanaume wa Uingereza wa kujifanya baba.

Akaunti moja ilichapisha ujumbe huu: "Nina ujauzito wa miezi 4. Nahitaji sana baba wa uraia mwenye umri wa kati ya miaka 25-45."

Mwingine aliandikwa: "Mimi ni baba mwenye kitabu chekundu [msemo wa Kivietinamu unaomaanisha pasipoti ya Uingereza]. Ikiwa una mimba na huna baba zungumza na mimi."

Meta, kampuni inayomiliki Facebook, inasema hairuhusu "kuomba watoto wa kuasili au udanganyifu wa cheti cha kuzaliwa kwenye Facebook". Inasema itaendelea kuondoa maudhui ambayo yanakiuka sera zake.