Nini maana ya vikosi vya SADC kujitosa DRC?

Bendera

Chanzo cha picha, SADC

    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi Tanzania

Hatua ya viongozi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuamua kupeleka vikosi vya kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imefungua ukurasa mpya katika mojawapo ya migogoro ya muda mrefu barani Afrika.

Pasi na shaka yoyote, huu hautakuwa ukurasa wa mwisho katika kitabu cha amani ya DRC – hasa ikizingatiwa kwamba SADC iliwahi kupeleka vikosi vyake katika taifa hilo; lakini kwa sababu ya mazingira ambayo yapo hadi sasa, vikosi hivyo viliondoka.

Uamuzi wa kupeleka vikosi DRC ulifikiwa kutokana na ushauri uliotolewa na Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (Troika) ambayo kwa mujibu wa taratibu huundwa na Mwenyekiti wa sasa wa SADC, Mwenyekiti aliyepita na yule ajaye.

Mkutano wa Troika ulifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita nchini Namibia chini ya Uenyekiti wa Rais Hage Geinghob wa Namibia na kuhudhuriwa pia na nchi zinazounda Kikosi cha Dharura cha SADC (FIB) kinachoundwa na nchi za Tanzania, Afrika Kusini na Malawi.

Swali pekee la kujiuliza ni kwamba; nini tofauti ya hatua ya sasa ya SADC kupeleka vikosi DRC kulinganisha na mara ya mwisho ilipofanya hivyo miaka 10 iliyopita? Kwa nchi ambayo imekuwa na vikosi vya kulinda amani kwa majina tofauti kwa zaidi ya miaka 20 sasa, nini vikosi vya SADC vitaenda kufanya tofauti na vingine vilivyopo?

Majirani wasioaminiana

R

Chanzo cha picha, Reuters

Katika masuala ya Uhusiano wa Kimataifa (International Relations), jambo moja muhimu linalohusu uhusiano baina ya nchi na nchi au na mataifa mengine ni kuaminiana miongoni mwao.

Hii ni kwa sababu nguzo kuu inayoongoza uhusiano wa kimataifa ni kwamba hakuna ajuaye yaliyo moyoni mwa jirani yake au wenzake.

Ndiyo sababu nchi zinanunua silaha hata wakati wa amani na pasipo na ugomvi wowote na jirani.

Lakini kwa sababu mfumo mzima umejengwa kwenye dhana ya “hujui jirani yako anawaza nini”, hili ni jambo la kawaida. Majirani wanapokuwa hawaaminiani, dhana hii inakuwa na mashiko zaidi.

Nilikuwa ofisi za BBC London Oktoba mwaka jana wakati Rais wa DRC, Felix Tshisekedi, alipofanya mahojiano na chombo hicho na kueleza wazi kwamba miongoni mwa jirani wanaomzunguka, hana imani na jirani zake wa Rwanda na Uganda.

Zaidi ya mara moja, Tshisekedi ametamka bayana kwamba Rwanda ndiyo wanasaidia kundi la waasi la M23 kufanya mashambulizi ndani ya DRC.

Kwa sababu hiyo, Rwanda si sehemu ya vikosi vya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) vilivyokwenda DRC kulinda amani tangu mwaka jana. Lakini Uganda, ambayo tayari DRC imeeleza haina imani nayo, imepeleka vikosi na viko nchini humo pamoja na vile vya Kenya na Burundi.

Kagame
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kama mfumo wa uhusiano wa kimataifa umejengwa kwenye dhana ya kutojua anachowaza mwenzako, kama uhusiano na jirani ni mbaya – maana yake imani yako kwake ni kuwa anakuwazia mabaya na kwa maana ya nchi na nchi, huenda anapanga kukuondoa madarakani.

Akiwa nchini Botswana mwanzoni mwa wiki hii, Tshisekedi pia alilalama kuhusu vikosi vya EAC vilivyoko DRC, akilaumu kwamba badala ya kupambana na vikundi kama M23 kama ilivyotakiwa, vyenyewe vinashirikiana na kikundi hicho.

Lawama hizo zilielekezwa moja kwa moja kwa Kenya ambayo ndiyo iliyochangia idadi kubwa zaidi ya vikosi vya EAC vilivyoko DRC.

Maneno ya Rais Tshisekedi wiki hii yanathibitisha madai ya aliyekuwa Kamanda wa Vikosi vya EAC nchini DRC, Jenerali Jeff Nyagah, aliyetangaza kujiuzulu wadhifa huo mwezi uliopita – akidai kwamba serikali ya nchi mwenyeji inafanya vitendo vya hujuma dhidi yake binafsi na vikosi vyake.

Maelezo ya Tshisekedi na Nyagah yanatoa picha kwamba serikali ya DRC haina imani na vikosi vya EAC kwa sababu imepoteza imani na Kenya ambayo ndiyo nchi ya Afrika iliyojitoa zaidi kwenye suala la kutoa vikosi vya kulinda amani Mashariki mwa DRC.

Kwa nini uamuzi wa SADC una mantiki kwa sasa?

Kwenye siasa za kulinda amani, masuala mawili huwa ni ya kuzingatia – mosi jambo kuungwa mkono na serikali ya nchi mwenyeji na pili imani ya serikali dhidi ya wale wanaokuja kulinda amani.

Kama serikali haitaki vikosi, vikosi haviwezi kupelekwa na kama serikali haitaki vikosi fulani, itavikataa au kufanya hujuma dhidi yake visifanikiwe.

Inaonekana Tshisekedi anataka vikosi vya amani DRC. Rais Tshisekedi amewahi kuzungumza huko nyuma kwamba miongoni mwa jirani zake – anawaamini marais watatu; Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Evariste Ndayishimiye wa Burundi na William Ruto wa Kenya.

Rais huyo wa DRC amewahi pia kusafiri hadi Angola – moja ya nchi wanachama wa SADC, kuzungumza na Rais Joao Lourenco, kuzungumzia suala hili la amani. Hii inamaanisha kwamba Tshisekedi anataka amani na anaamini viongozi wa SADC. Hali hii ni tofauti na ilivyo kwa baadhi ya viongozi wa EAC – kwa kunukuu maneno yake ya siku za nyuma, ambao sasa vikosi vyao ndiyo vinalinda amani nchini humo.

Katika historia ya miaka ya karibuni, ni SADC pekee kupitia vikosi vilivyoongozwa na Mtanzania Luteni Jenerali, James Aloizi Mwakibolwa – kwa ufadhili wa Umoja wa Mataifa, ndivyo vilivyowahi kuingia DRC na kufanikiwa kuwasukuma nyuma wapiganaji wa M23 mwaka 2013 na kurejesha amani Mashariki mwa taifa hilo – amani ambayo imevurugika tena kufuatia kurejea kwa M23.

Wafuatiliaji wa masuala ya kidiplomasia wanaamini kwamba matukio ya DRC mwaka 2013, ndiyo yalikuwa chanzo cha kuvurugika kwa uhusiano baina ya Tanzania na Rwanda mnamo mwaka 2014 – kiasi cha kufikia hatua ya kurushiana maneno baina ya marais Jakaya Kikwete na Paul Kagame.

Uamuzi wa sasa wa SADC una mantiki kwa sababu yenyewe ndiyo yenye rekodi ya kuingia DRC na kuleta amani – ingawa haikudumu baada ya vikosi kuondoka, inaaminika na utawala wa Kinshasa na inaungwa mkono na Afrika Kusini ambalo ni taifa lenye msuli wa kiuchumi na kijeshi kukabiliana na changamoto za sasa za taifa hilo mwanachama wa EAC.

Kidonda cha muda mrefu

Haitarajiwi kwamba vikosi vya SADC pekee vinaweza kuleta amani ya kudumu DRC. Vikosi vya Umoja wa Mataifa vya MONUSCO viko nchini humo kwa zaidi ya miongo miwili na amani bado imekuwa jambo adimu hadi sasa.

Rwanda imekuwa ikijitenga na tuhuma za kusaidia M23 na imedai kwamba Tshisekedi anatumia mgogoro huu kujijenga kisiasa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa DRC uliopangwa kufanyika mwakani na kwamba limekuwa jambo la kawaida kwa wanasiasa wa taifa hilo kutumia ukabila na tuhuma dhidi ya Rwanda kujijenga.

Mwandishi mashuhuri wa Uganda, Andrew Mwenda, ambaye amekuwa akifuatilia mgogoro wa DRC kwa karibu katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, anaamini kwamba suluhisho la kudumu la mgogoro huo halitaletwa na mtutu wa bunduki bali kwa majadiliano baina ya viongozi wa DRC na M23.

“Serikali ya Tshisekedi inatakiwa kukubali kwamba M23 ina madai yake ya muda mrefu kuhusu wao kutotendewa kama raia wa DRC badala yake kuonekana kama wavamizi. Suala hili halitaweza kumalizwa kwa vikosi vya amani au mtutu wa bunduki bali kwa majadiliano yatakayojali maslahi ya taifa hilo kwa pande zote zinazokinzana, aliandika Mwenda kwenye gazeti analohariri la The Independent.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amepewa jukumu na Umoja wa Afrika (AU) kuwa msuluhishi wa mgogoro huo lakini kikwazo kikubwa mpaka sasa ni msimamo wa Serikali ya Tshisekedi kutokubali kukaa mezani na M23 hadi pale watakapokuwa wako nje ya mipaka ya taifa lake. M23, kwa upande wao, wanaamini kwamba nyumbani kwao ni ndani ya mipaka ya DRC na si nje.

Tofauti kubwa iliyopo kati ya sasa na miaka 10 iliyopita ni kubadilika kwa hali ya dunia. Nchi za Magharibi zilizokuwa zikifadhili juhudi za kutafuta amani nchini DRC sasa zimetingwa na matatizo mengi ya kiuchumi yaliyosababishwa kwanza na ugonjwa wa Uviko 19 na Vita ya Ukraine ambayo sasa inatajwa kuelekea kubaya zaidi.

Hadi sasa haijajulikana ni nani atafadhili vikosi vya SADC vitakavyokwenda DRC na vitachukua muda gani kubaki huko. Afrika Kusini ambayo ilikuwa msaada mkubwa mwaka 2013, sasa inakabiliwa na hali mbaya ya uchumi na Rais Cyril Ramaphosa anapitia wakati mgumu kwenye utawala wake.

Na hata kama SADC itafanikiwa tena kufukuza waasi wa M23 kutoka ndani ya DRC, kuna nafasi kubwa kwamba tutarejea tena katika tatizo hilihili huko baadaye kwa sababu wanaounga mkono kundi hilo wanaamini kwamba wanapigania uhai wao na mustakabali wa vizazi vyao vijavyo.

Mgogoro huu utamalizwa mezani na pale ambapo Jumuiya ya Kimataifa – hasa mataifa makubwa ya Magharibi kama Marekani, Uingereza na Ufaransa, yataamua DRC iwe na amani ya kudumu.

Lakini kwa sasa, mpira uko mezani kwa Tshisekedi na walinda amani kutoka SADC.