Zelensky:Putin atafariki hivi karibuni - ni kweli na kila kitu kitakwisha

Muda wa kusoma: Dakika 4

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, alipozuru Ufaransa, alifanya mahojiano na kundi la vyombo vya habari la Eurovision.

Katika mahojiano hayo, alithibitisha kuwa kusitishwa kwa mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati kumeanza kutekelezwa.

Alishangaza waandishi wa habari alipojibu maswali kuhusu wasiwasi alionao kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin na kusema kuwa kifo chake kiko karibu.

Zelensky pia alieleza kuwa uongozi wa Marekani hivi sasa unashawishiwa na simulizi za Urusi.

Zelensky alieleza kwa uwazi kuwa Putin anahofia kupoteza madaraka aliyonayo.

Alisema, "Kinachomwogopesha Putin ni kupoteza mamlaka yake. Hili linategemea ustawi wa jamii, lakini pia linategemea umri wake. Putin atakufa hivi karibuni, hiyo ni kweli, na yote haya yataisha," alisisitiza.

"Anaweza kufa kabla ya kumaliza maisha yake ya kihistoria ambayo ni ya kutofaulu. Hicho ndicho anachohofia. Na pia kuachwa pweke," Volodymyr Zelensky alijibu wanahabari hao alipoulizwa kuhusu Putin.

Rais Zelensky hakutoa maelezo zaidi kuhusu msimamo wake, isipokuwa kusema kuwa Putin anataka kurejesha Umoja wa Kisovieti (USSR) na hata zaidi ya hapo.

Akizungumzia kuhusu mapumziko ya mashambulizi ya nishati, Zelensky alithibitisha kuwa hakukuwa na mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundombinu ya nishati usiku uliopita.

"Hii ni hali ngumu kuhusu ufuatiliaji wa mashambulizi. Hadi sasa, timu za kiufundi bado hazijajua itakavyokuwa. Lakini sitaki kusema uongo, hakukuwa na mashambulizi dhidi ya nishati usiku huu. Kulikuwa na mashambulizi kwenye miundombinu mingine ya kiraia, zaidi ya ndege zisizo na rubani mia moja, lakini hakukuwa na mashambulizi dhidi ya nishati usiku," alifafanua.

Pia upande wetu wa Ukraine hatukujibu kwa kushambulia miundombinu ya nishati, Zelensky aliendelea kusema.

Kuhusu mapumziko ya mapigano katika Bahari Nyeusi, Zelensky alisisitiza kuwa Warusi wanahitaji mapumziko hayo kwa sababu hawadhibiti tena ushoroba wa Bahari Nyeusi.

"Tunapigania kudhibiti eneo hili kwa sababu ni hatua muhimu kuelekea kumaliza vita. Lakini tunadhibiti hali hiyo. Meli zao huenda ziko chini ya maji au zimejificha," alisisitiza.

Aliongeza kuwa Warusi wanataka mapumziko ya mapigano ya nishati kama sehemu ya mapatano kuhusu Bahari Nyeusi.

"Wanataka kutawala biashara ya vyakula, lakini hawatafaulu," alisema Zelensky.

Rais Zelensky alijitokeza pia kupinga baadhi ya matamshi ya mjumbe wa Rais Donald Trump, Steve Witkoff, ambaye alidaiwa kutumia mara kwa mara simulizi za Kremlin.

Zelensky alieleza kuwa matamshi hayo hayasaidii juhudi za amani na badala yake yanadhoofisha shinikizo la Marekani dhidi ya Urusi.

"Tunapigana na Putin na hatutaki msaada wa watu ambao wanamsaidia. Tunataka Wamarekani wawe upande wetu. Hata kama tunachagua mbinu za kati, tunataka ziwe katikati, sio karibu na Kremlin," alisema.

Zelensky aliongeza kuwa Marekani leo inashawishiwa sana na simulizi za Urusi, lakini wamesisitiza kuwa wataendelea kupigana na hizi propaganda kwani wanapigania uhuru wao.

Rais Zelensky alifika Paris mnamo Machi 26, ambapo alikutana na Rais Emmanuel Macron, kabla ya mkutano wa mataifa yanayojitolea kutoa dhamana za usalama kwa Ukraine.

Hii ilikuwa ni kabla ya mkutano wa "muungano wa walio na maono sawa" uliofanyika Paris Machi 27, ambapo Rais Zelensky alihudhuria.

Mapatano kuhusu bahari nyeusi na nishati

Siku moja kabla, Marekani na Ukraine zilitangaza makubaliano yaliyofikiwa baada ya mazungumzo yaliyofanyika Saudi Arabia, ikijumuisha makubaliano ya kutotumia nguvu za kijeshi katika Bahari Nyeusi na kutekeleza mapumziko ya mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati.

Ikulu ya White House ilitangaza kuwa Marekani na Ukraine zimekubaliana kudumisha usalama wa meli, kuzuia matumizi ya nguvu, na kuzuia matumizi ya meli za kibiashara kwa madhumuni ya kijeshi katika Bahari Nyeusi.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa makubaliano yalihusisha pia hatua za kutekeleza marufuku ya mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Urusi na Ukraine.

Hata hivyo, Urusi ilitoa taarifa ikisisitiza kuwa makubaliano yaliyotangazwa na White House hayakujumuisha baadhi ya masharti muhimu, ikiwa ni pamoja na ombi la kuondolewa kwa vikwazo katika sekta ya kilimo ya Urusi, ambayo itahusika katika usafirishaji wa bidhaa kupitia Bahari Nyeusi.

Pia, Urusi ilitaja masharti ya marufuku ya mashambulizi ya nishati, ambayo yanapaswa kuanza tarehe Machi 18, 2025, kwa kipindi cha siku 30, na kuna uwezekano wa kupanuliwa au kuvunjwa endapo moja ya pande zitavunja makubaliano hayo.

Upande wa Ukraine unadai kuwa hakukuwa na mashambulizi ya Urusi dhidi ya nishati tangu mwezi Machi 25, 2025.

Hata hivyo, Moscow imerekodi mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati tangu Machi 18, na inadai kuwa Ukraine imeshavunja makubaliano.

Marekani bado haijatoa tamko kuhusu lini usitishwaji wa nishati ulipaswa kuanza.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid