Madini gani adimu nchini Ukraine yanayoitoa 'roho' Marekani?

Muda wa kusoma: Dakika 3

Kyiv na Washington zinakaribia kutia saini mkataba utakatoa nafasi kwa Marekani kunufaika na madini ya Ukraine, kwa mujibu wa waziri wa Ukraine.

Olga Stefanishyna, Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine anayehusika na masuala ya ushirikiano wa Ulaya na Euro-Atlantic, alisema kupitia mtandao wa kijamii wa X kwamba "majadiliano yamekuwa yenye tija, huku karibu maelezo yote muhimu yakiwa yamekamilika."

Aliongeza kuwa "tumedhamiria kuhitimisha hili haraka ili kuendelea na utiaji saini wa mkataba huo."

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliingiza pendekezo la makubaliano ya madini katika mpango wake wa ushindi aliouwasilishwa kwa Donald Trump mnamo Septemba mwaka jana.

Lengo lilikuwa kumpa mgombea huyo wa urais wa wakati huo sababu ya wazi kwa Marekani kuendelea kuiunga mkono Ukraine.

Jumatatu, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Boris Johnson, aliambia BBC Kyiv kwamba "mkataba huu ni zawadi kubwa" kwa sababu utahakikisha Marekani inatoa ahadi ya kuilinda Ukraine ikiwa Trump atakuwa madarakani.

Ukraine ina madini gani adimu?

Ukraine inakadiria kuwa inamiliki karibu 5% ya malighafi muhimu duniani. Hii ni pamoja na madini haya:

  • Grafaiti

Ukraine ina tani milioni 19 za grafaiti, ambayo huifanya kuwa miongoni mwa nchi tano zinazoongoza duniani katika usambazaji wa madini hayo. Grafaiti hutumika kutengeneza betri za magari ya umeme.

  • Lithium

Ukraine inamiliki theluthi moja ya akiba ya lithiamu barani Ulaya, ambayo ni kiungo muhimu katika betri za kisasa.

  • Titanium

Kabla ya uvamizi wa Urusi, Ukraine ilikuwa ikichangia 7% ya uzalishaji wa titanium duniani. Titanium ni chuma chepesi kinachotumika katika ujenzi wa ndege, vituo vya nguvu, na bidhaa nyingine nyingi.

Madini adimu ya dunia (Rare Earth Metals)

Ukraine pia ina hifadhi kubwa ya madini adimu ya dunia, kundi la vipengele 17 vinavyotumika kutengeneza silaha, mitambo ya upepo, vifaa vya kielektroniki na bidhaa nyingine muhimu za kisasa.

Hata hivyo, baadhi ya akiba ya madini haya imeshikiliwa na Urusi.

Kwa mujibu wa Waziri wa Uchumi wa Ukraine Yulia Svyrydenko, madini yenye thamani ya dola bilioni 350 za Kimarekani kwa sasa yako chini ya maeneo yanayokaliwa na Urusi.

Mnamo 2022, kampuni ya ushauri wa hatari za kijiografia SecDev kutoka Canada ilifanya tathmini iliyoonyesha kuwa Urusi ilikalia 63% ya migodi ya makaa ya mawe ya Ukraine, na nusu ya hifadhi ya madini yake ya manganese, cesium, tantalum, na madini adimu duniani.

Dr. Robert Muggah, Mkuu wa SecDev, anasema kuwa madini haya yanaongeza "mwelekeo wa kimkakati na kiuchumi" katika vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.

Kwa kuyanyakua, Moscow inaizuia Ukraine kupata mapato, inapanua hifadhi yake ya malighafi, na inaathiri minyororo ya usambazaji duniani.

Kwa nini Marekani Inayahitaji?

Madini haya ni msingi wa uchumi wa karne ya 21, anasema Dr. Muggah.

Ni muhimu kwa nishati mbadala, matumizi ya kijeshi na miundombinu ya viwanda.

Yana jukumu kubwa la kimkakati katika siasa na uchumi wa dunia.

Marekani pia inataka kupunguza utegemezi wake kwa China, ambayo inadhibiti 75% ya uzalishaji wa madini adimu ya dunia, kwa mujibu wa Geological Investment Group.

Mwezi Desemba, China ilipiga marufuku usafirishaji wa baadhi ya madini adimu kwenda Marekani, ikiwa ni mwendelezo wa hatua iliyochukua mwaka uliopita wa kupunguza usafirishaji wa madini yake kwenda Marekani.

Makubaliano yamefikia wapi?

Kabla ya kauli ya Stefanishyna kwamba makubaliano yako karibu, kulikuwa na masuala kadhaa tata.

Jumatano iliyopita, Zelensky alikataa ombi la Marekani la kutaka 50% ya madini adimu ya Ukraine, ombi ambalo Trump alisema linalingana na kiasi cha msaada ambao Marekani imeipa Ukraine wakati wa vita vyake na Urusi.

"Siwezi kuiuza nchi yangu," alisema Zelensky.

Muswada wa pili wa mkataba uliotolewa Jumapili ulikuwa na masharti magumu zaidi.

Badala ya mgawanyo wa mapato wa 50/50, rasimu mpya ilipendekeza kuwa Marekani ipate udhibiti kamili, Zelensky aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano wa vyombo vya habari Jumapili.

Zelensky pia anataka mkataba wowote uwe na dhamana za kiusalama.

Jumatatu, Boris Johnson alitaja mkataba huu kuwa "zawadi kubwa" na alikataa madai kwamba ni unyonyaji kwa Ukraine.

"Wanachopata Waukraine kutoka kwa hii ni ahadi ya Marekani chini ya Donald Trump ya kuihakikishia Ukraine huru, yenye mamlaka na salama," alisema Johnson.

Baadhi ya wachambuzi wameelezea pendekezo la Marekani kama "ukoloni mpya", lakini Kyiv inaonyesha nia ya ushirikiano wa pamoja katika uchimbaji wa rasilimali hizi.

Kwa mujibu wa Iryna Suprun, Mkurugenzi Mtendaji wa Geological Investment Group, kampuni ya ushauri wa madini iliyo Ukraine, kuendeleza sekta ya madini ni gharama kubwa na inahitaji teknolojia za kisasa.

Anasema kwamba ikiwa Ukraine itaweza kuvutia wawekezaji wa Marekani, itaongeza ajira, mapato ya kodi, na kipato kutokana na madini.

"Tutapata teknolojia ambazo sekta yetu ya uchimbaji madini inakosa kwa kiasi kikubwa," anasema Bi. Suprun. "Tutapata mtaji. Hii inamaanisha ajira zaidi, mapato ya kodi, na faida kutokana na maendeleo ya migodi yetu."

Imetafsiriwa na Yusuph Mazimu na kuhaririwa na Ambia Hirsi