Kwanini Kenya imefuta usajili wa makanisa haya maarufu?
Na Dinah Gahamanyi
BBC Swahili

Chanzo cha picha, PASTOR EZEKIEL ODERO/FACEBOOK
Msajili wa serikali wa vyama nchini Kenya amefuta usajili wa Makanisa maarufu nchini Kenya mkiwemo Kanisa la Mchungaji mwenye utata anayemiliki kituo cha Newlife Prayer Centre Ezekiel Odero cha Newlife.
Taarifa hii inafuatia kuundwa kwa Kikosi Kazi kilichoundwa na Rais William Ruto kwa lengo la kusaidia kurahisisha usajili na rekodi za makundi ya kidini.
Rais Ruto alisema ‘’Kuna watu wanaotumia Biblia kwa biashara na kuendeleza uhalifu na kuongeza kuwa ''serikali itayamaliza’’
Kauli hizi za Rais Ruto zilitolewa kufuatia mauaji ya Shakahola ambapo wafuasi wa Kanisa la Mchungaji tata Paul Nthenge Mackenzie wa Kanisa la Good News International Church, anadaiwa kuwaagiza wafuati kufunga hadi kufa.
Mchungaji Ezekiel alihusishwa pia na madai ya vifo vya Shakahola ambapo hadi sasa miili zaidi ya 400 ya watu wanaodaiwa kufunga hadi kufa iligundulika.
Katika waraka uliowasilishwa mahakamani, Mamlaka ya upelelezi wa makosa ya jinai nchini Kenya (DCI), ilidai Mchungaji Ezekiel wa Kanisa la New Life Prayer Centre anashukiwa kwa utakatishaji wa pesa kutokana na uhusiano na Mchungaji Paul Mackenzie wa Kanisa la Good News International , ambaye anachunguzwa kwa madai ya kuwalaghai wafuasi wa kanisa lake kufunga hadi kufa ili ‘’kukutana na Yesu’’.

Wito wa kudhibiti makanisa nchini Kenya , ambayo baadhi yake yamekuwa yakishutumiwa kwa kuwalaghai raia na kwa kutoa kile kinachoitwa ‘’Kupanda Mbegu’’ au kutoa kiasi fulani cha pesa ili wapate miujiza umekuwa ukiongezeka nchini Kenya.
Kufuatia kisa cha mauaji ya Shakahola, Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua alitoa wito kwa viongozi wa dini kuunga mkono mpango wa serikali wa kupitia upya kanuni zinazosimamia mashirika ya kidini.
Hatahivyo Bw Gachagua alionya dhidi ya shutuma za makanisa na makasisi kwasababu ya vifo vya Shakahola .
Makanisa mengine manne yamefutwa.
"Katika kutekeleza mamlaka yaliyotolewa na kifungu cha 12 (1) cha Sheria ya Vyama vya Ushirika, Msajili wa Vyama anafuta usajili wa jamii zilizoainishwa katika safu ya kwanza ya Ratiba, na kuanzia tarehe husika zilizoainishwa katika safu ya tatu ya ratiba," Msajili wa Vyama Maria Nyariki alisema.
Makanisa mengine ni Goodnews International Ministries ambalo ilifutwa , Helikopta ya Christ Church , Kanisa la Theophilus pamoja na Kanisa la Kings Outreach , ambayo kulingana na tangazo la Msajiri wa vyama nchini Kenya yote usajiri wake ulifutwa tarehe 19 Mei, 2023.
Aidha Kanisa la The Royal Park Home Owners Estate Association Langata ambalo lilisajiriwa kama shirika usajiri wake ulifutwa pia tarehe 19 Juni, 2023.
Je Kenya inafuata nyayo za Rwanda?
Mwaka 2018, Serikali ya Rwanda iliyafunga makanisa zaidi ya 714 katika mji mkuu wa nchi hiyo Kigali kwa kukosa kutimiza masharti yaliyowekwa ya usafi na usalama
Afisa wa serikali Justus Kangwagye alisema kuwa makanisa hayo yalikiuka sharia za usalama.
"Shughuli ya kuabudu inafaa kufanywa kwa utaratibu na kwa kutimiza masharti ya viwango vya ubora na usalama vilivyowekwa. Kutumia uhuru wako wa kuabudu hakufai kuingilia haki za watu wengine. Wametakiwa kusitisha shughuli zote hadi watimize masharti yaliyowekwa," amesema.
Alisema baadhi ya makanisa hayo yalikuwa yakifanya kazi bila kuwasilisha upya maombi ya leseni na kwamba maafisa wa serikali hawataruhusu makanisa hayo yafunguliwe.
Je dini inaweza kudhibitiwa?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Masuala ya imani ama dini mara nyingi yanachukuliwa kuwa ya kiroho- Hivyo basi kila mtu ana uhuru wa kuchagua njia ya kuabudu, sehemu ya kuabudu na kupitia dini gani.
Lakini swali ni je uhuru uliyopo wa kuabudu umepita kiasi?
Swali hili limeibuka kutokana na visa kadhaa ambapo waumini wamedaiwa kutapeliwa ama kutumiwa vibaya katika maeneo ya ibada.
''Ni vyema kufahamu dini ilikujaje, kwani bila ya kujua historia ya dini tutakuwa tunajichanganya'' alisema mchungaji Osward Mlay ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano nchini Tanzania, alipozungumza na BBC awali.
Watu waliyokuwa wanafuata dini walikuwa wanafanya hivyo kiasi cha kuwa utadhani wanamuona Mungu isipokuwa ile sura yake.
Serikali ya kidunia haiwezi kudhibiti uhuru wa kuabudu ambao umetolewa na Mungu.
''Sisi ndio tunajenga serikali ya kidunia kwa hivyo haina uwezo wa kutudhibiti'' anasema Dr. Hassan Kinywa Omary, mwanazuoni kutoka Kenya.
Akipinga kauli ya mchungaji Osward, Dr. Hassan anasema Kenya kwa mfano kuna mamilioni ya watu wa dini tofauti na kwamba maeneo mengi watu wanafuata kanuni zilizopo.
Anasema maeneo ya ibada ambayo watu wanakera wengine au kuwahadaa wenzao ni machache sana.
''Maeneo mengi ni yale watu wanafuata mambo ambayo ni ya haki, lakini sasa tunasema kuwa serikali iko na uwezo wa kuwachukulia hatua wale ambao hawafuati utaratibu uliyowekwa na sheria.''
Ndio maana watu walikuwa wanaishi kulingana na mafundisho ambayo mtu anahisi ni kama anamuona Mungu japokuwa hajamuona.
Mchungaji- Osward Mlay anasema kuwa siku hizi mambo yamebadilika.
''Yamekuwepo mafundisho ambayo hata ukiangalia unaona siyo ya Mungu'' anasema mchungaji Osward.
Anaongeza kuwa siku hizi baadhi ya viongozi wa kidini wanauza maji ambayo wanasema yana ''upako,hakuna mahali ambayo imeandikwa Yesu aliuza maji yakawa na upako.
Katika kila jamii kuna watu wa dini tofauti na wote wanaishi pamoja bila shida yoyote,lakini baadhi ya viongozi wanatumia uhuru wa kuabudu vibaya.
''Kama utatumia ibada kuwa kero kwa wengine utakuwa unamkosea Mungu manake hakusema tumtukuze kwa kuwaadhibu wengine''
Akizingatia hilo mchungaji Osward anasema serikali ina wajibu wa kuhakikisha watu wanaishi pamoja kwa amani bila kukwazana.
Suala la kufutaa usajili wa baadhi ya Makanisa yanayoonekana kuwalaghai wafuasi si geni nchini Kenya, lakini baadhi wanaona kuwa serikali imechukua muda kudhibiti utendaji wa Makanisa.
Hii inatokana na imani waliyonayo waumini hususan katika viongozi wa Makanisa hayo wenye mvuto kwa wafuasi wao.
Hata hivyo bila shaka baadhi ya Wakenya watauona uamuzi wa sasa wa serikali kuwa ni hatua chanya lakini ndefu kuelekea udhibiti wa Makanisa yanayochipuka kila uchao na kujiendesha bila udhibiti imara wa serikali.















