Mzambia ashinda tuzo ya BBC Komla Dumor 2022

Mtangazaji wa runinga na redio wa Zambia Dingindaba Jonah Buyoya ameshinda Tuzo ya BBC News Komla Dumor ya mwaka wa 2022.
Akiwa na umri wa miaka 25, Buyoya ndiye mshindi mdogo zaidi wa tuzo hiyo, iliyozinduliwa mwaka wa 2015, na wa kwanza kati ya washindi saba hadi sasa kutoka kusini mwa Afrika.
Kwa sasa ni mtangazaji wa TV na ripota wa Televisheni ya Diamond nchini Zambia, ambapo alianza kazi miaka mitano iliyopita.
Tuzo hiyo ilianzishwa kwa heshima ya Komla Dumor, mtangazaji wa BBC World News, ambaye aliaga dunia ghafla akiwa na umri wa miaka 41 mnamo 2014.
Buyoya anafuata nyayo za Victoria Rubadiri, Solomon Serwanjja, Waihiga Mwaura, Amina Yuguda, Didi Akinyelure na Nancy Kacungira.
Mshindi wa pili wa tuzo ya mwaka huu ni Lindsay Aida Guei wa Ivory Coast, ambaye anawasilisha kipindi chake cha mazungumzo kwenye Canal+ Elles, chaneli ya TV inayolenga Afrika.
Mwanahabari huyo wa Zambia atatumia muda wa miezi mitatu kufanya kazi na timu za BBC News mjini London katika televisheni, redio na mtandaoni. Pia atapata mafunzo na kuongozwa na wanahabari wakuu wa BBC.
Kama sehemu ya mpango huo wa mafunzo , atasafiri hadi nchi moja barani Afrika kuripoti habari ambayo itatangazwa kwa hadhira ya kimataifa ya BBC.

"Kugundua kuwa nimeshinda Tuzo ya BBC News Komla Dumor ni mojawapo ya mambo bora kuwahi kutokea katika maisha yangu," Buyoya anasema.
"Ninavutiwa sana na kazi nzuri ya Komla. Nimekuwa nikitamani kuwa mwandishi wa habari na ningetazama ripoti za habari za Komla, nikichochewa na hadithi zake zenye nguvu na ari yake ya kuandika habari za Afrika kiuhalisi.
"Kwa kweli ninashukuru kuwa sehemu ya urithi wa Komla."
Majaji walimsifu Buyoya kwa uandishi wake wa habari, haiba yake na ari yake ya kuandika habari kuhusu bara kupitia majukwaa ya kidijitali.
"Tunatazamia kumkaribisha Buyoya kwa BBC News. Tumefurahishwa na talanta yake ya uandishi wa habari, na kumuona akisitawi wakati wa kuwekwa kwake BBC," mkuu wa BBC Africa Juliet Njeri alisema
"Kujitolea kwake katika kuhakikisha habari muhimu kutoka Afrika zinasimuliwa kwa njia ya kuvutia, inamfanya kuwa bora kusaidia kuendeleza urithi wa Komla - kushiriki hadithi za kina kuhusu bara.














