kwanini mataifa ya Afrika mashariki yanatofautiana kuhusu vita vya Ukraine?

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania
- Author, Munira Hussein
- Nafasi, BBC
Baraza kuu la usalama la umoja wa mataifa liliandaa azimio la kupinga kura za maoni zenye utata za Moscow katika mikoa minne ya Ukraine ambayo ilitangaza kuwa ni sehemu ya Urusi.
Mataifa wanachama 143 walipiga kura ya kuunga mkono, mataifa 5 yalipinga na 35 walipiga kura ya kutofungamana na upande wowote.
Kura hii ilikua na lengo la kukemea kitendo cha Urusi kunyakua mikoa minne ya Ukraine -Luhansk, Donetsk, Zaporizhzhia na Kherson.
Miongoni mwa mataifa yaliyopiga kura ya kuunga mkono ama kutofungamana na upande wowote ni nchi za Afrika, yakiwemo mataifa ya Afrika Mashariki.

Uhusiano wa Urusi na Ukraine kwa Afrika Mashariki
Urusi inatoa nafasi zaidi ya 500 za mafunzo ya kijeshi kwa nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Afrika mashariki, Nafasi hizo zinaweza kuonekana ni chache lakini zina ushawishi, angalau, fursa hizi za elimu ya kitaaluma ya kijeshi huipatia Urusi ufikiaji unaoendelea kwa maafisa wa kijeshi wa ngazi ya kati na ya juu katika kipindi cha kazi zao.
Urusi ndiyo inayoongoza kwa mauzo ya silaha barani Afrika, Moscow ilitoa 44% ya uagizaji wa silaha zote za Kiafrika kutoka 2017-2021, kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm.
Silaha za Kirusi zinaonekana kuwa za bei nafuu, rahisi kudumisha, na za kuaminika.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wateja wa Kiafrika wanazidi kuwa tayari kununua silaha za hali ya juu zaidi kutoka Urusi, zikiwemo ndege za kivita, helikopta, vifaru na mifumo ya ulinzi wa anga.
Urusi inadumisha mfululizo wa mabadilishano ya kielimu na kitamaduni na Afrika. Inakadiriwa kuwa Waafrika 15,000 wanasoma katika vyuo vikuu vya Urusi miongoni mwao ni wanafunzi kutoka Afrika mashariki.
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, alifanya ziara barani Afrika mwezi Julai, akitembelea nchi kama vile Uganda, Ethiopia na DRC
Uganda, Ethiopia na Congo hazijaegemea upande wowote katika vita vya Urusi nchini Ukraine, huku zote tatu zikijizuia au kutohudhuria wakati wa kura ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Machi kulaani mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine.
Kwa Upande mwingine uhusiano wa Ukraine na Afrika kwa ujumla hauna nguvu kubwa, na vivyo hivyo kwa Afrika mashariki.
Ukraine ina balozi 10 barani Afrika, kwa ukanda wa Afrika mashariki, ina ubalozi nchini Kenya na Ethiopia tu.
Lakini kama ilivyo kwa Urusi, Ukraine imekua ikitoa nafasi za elimu kwa wanafunzi kutoka Afrika mashariki wakisomea fani mbalimbali ikiwemo sekta ya Afya.
Ukraine pia imekua ikiingiza bidhaa za chakula kama ngano na mahindi katika Nchi za Afrika mashariki.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kupiga kura za Turufu na misimamo ya nchi za Afrika Mashariki.
Nchi za jumuiya ya Afrika mashariki katika kura iliyopigwa kukemea Urusi kunyakua sehemu ya Ukraine katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa zilipishana.
Nchi hizi zina masuala ya jumuiya ambayo kwa wakati fulani sera zao hufanana, lakini katika masuala ambayo ni nje ya jumuiya basi kila nchi huwa na msimamo wake.
Tanzania kwa muda mrefu imekua na sera ya kutofungamana na upande wowote katika masuala ya kimataifa.
Sera ambayo iliasisiwa na baba wa taifa hilo, Julius K. Nyerere.
‘Tunata kuwa na uhusiano na nchi ambazo si za magharibi, pia vile vile tunataka kuwa na uhusiano na nchi za Magharibi na kwa sharti la sisi kutowaangilia na wao pia kutoingilia hususani masuala ya ndani ya nchi yetu, na hatuwezi kukubali kuchaguliwa rafiki au adui wa nchi yetu’’ Alisema Nyerere katika mkutano mkuu wa TANU mwaka 1967.
Sera hiyo pia imejidhihirisha katika kura hii ambapo Tanzania ilipiga kura ya kutokufungamana na upande wowote.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa upande wa Kenya, iliunga mkono kulaani unyakuaji wa maeneo ya Ukraine uliofanywa na Urusi.
Kura hii ya kuunga mkono kutoka kwa Kenya inahusishwa moja kwa na uhusiano mzuri baina ya Taifa la Kenya na nchi za Magharibi hususani Marekani.
Lakini pia uhusiano wa Kenya na Ukraine, uhusiano kati ya Kenya na Ukraine ulianza Machi 1993 wakati Kenya ilipoitambua Ukraine kama taifa huru. Nchi hizo mbili zimeanzisha uhusiano mzuri na kuanzishwa kwa Ubalozi wa Ukraine nchini Kenya mnamo 2004, na Ubalozi wa Kenya huko Kyiv, Ukraine. Kumekuwa na ushirikiano katika maeneo yanayoanzia biashara, kijeshi kiuchumi, na utamaduni kati ya Kenya na Ukraine. Uagizaji wa Kenya kutoka Ukraine ulithaminiwa kuwa Ksh 7.47 bilioni mwaka wa 2020 na kuongezeka maradufu hadi Ksh 19.29 bilioni mwaka wa 2021 kutokana na kuongezeka kwa uagizaji wa ngano na bidhaa za chuma na chuma.
Kuongezeka maradufu kwa uagizaji kutoka Ukraine hadi Kenya kunaweza kuhusishwa kwa kiasi fulani na mabadiliko ya sheria ya 2021 nchini Ukraine kuruhusu uuzaji wa mashamba kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20.
Marufuku yalikuwa yamewekwa ili kuzuia oligarchs kuchukua nafasi. Kwa Ukraine, hii iliunda fursa kubwa ya kujaza pengo katika msururu wa chakula duniani unaosababishwa na janga la COVID-19.
Mwanzoni mwa 2022, Ukraine ilikuwa muuzaji mkubwa wa mafuta ya alizeti na msafirishaji wa nne kwa ukubwa wa mahindi. Mauzo ya Kenya kwa Ukraine hasa yanajumuisha chai, kahawa, maua yaliyokatwa na mboga.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni nchini Kenya ilitangaza kuwa kuna Wakenya 201 nchini Ukraine, ikijumuisha wafanyikazi 18 wa Ubalozi na wanafunzi 183 wa Kenya kufikia Februari 2022 wakati vita vya Ukraine na Urusi vilipoanza.
‘’Nchi hizi kila moja inaangalia maslahi yake katika kupiga kura hizi, kuna nchi zilizounga mkono na zile ambazo hazikua na mfungamano na upande wowote, kwa Afrika mashariki kila nchi ina msimamo wake kwasababu ni masuala ya nje ya Jumuiya’’ anasema Godwin Gonde, mchambuzi wa masuala ya diplomasia.
Anaongeza pia katika kura za umoja wa mataifa, hususan katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, kuna nchi huwa zinanunua kura hizo kwa mataifa yanayopiga kura.
'’ Kuna nchi ambazo hutumia pesa nyingi kununua kura ili kusukuma agenda zao, ili kuwa salama zaidi ni kutochukua msimamo wa upande wowote, anasema Gonde.

Chanzo cha picha, Kagame/Twitter
Kenya, Rwanda na DRC zimeunga mkono kura ya kuishutumu na kuikemea Urusi, Tanzania, Burundi na Uganda zilipiga kura ya kutofungamana na upande wowote.
Kila taifa katika haya lina maslahi ya kura zao.
Rwanda na DRC wamonesha wazi kuwa uhusiano wake na mataifa ya Magharibi hauwezi kutafsiriwa vibaya kwani wameunga mkono kukemea vitendo vya Urusi, hivyo wanapata pongezi nyingi kutoka mataifa ya Magharibi, ikiwemo Marekani na Ufaransa.
Lakini kwa upande wa Uganda na Burundi , kama ilivyo kwa Tanzania, wao hawataki kujifunga na kutafsiriwa kuwa wameegemea upande mmoja.
Uhusiano wa Urusi na bara la Afrika
Uhusiano baina ya Urusi na Afrika ulianza mbali tangu kipindi cha muungano wa Usovieti, lakini katika miaka ya hivi karibuni uhusiano huo umechukua sura mpya ya urafiki kwa upande mmoja na utata kwa upande mwingine.
Mataifa ya Afrika mengi ni yenye serikali dhaifu, maliasili nyingi, historia ya ukoloni pamoja na ukaribu na Ulaya. Jambo muhimu Afrika ni kuwa ina kura 54 katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hii inaipatia Urusi fursa ya kuivutia na kuendeleza maslahi yake kwa gharama ndogo za kifedha au kisiasa.
Mwezi Juni Rais wa Senegal Macky Sall, ambaye ni mkuu wa sasa wa Umoja wa Afrika (AU), alisafiri hadi Sochi nchini Urusi kujadiliana na Bw Putin jinsi ya kuondoa vikwazo vinavyozuia uuzaji wa chakula unaohitajika sana kutoka Urusi na Ukraine.
Mwezi huo huo Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alimpigia simu Bw. Putin kujadili jinsi bidhaa za kilimo na mbolea kutoka Urusi zinaweza kusafirishwa Afrika.
Urusi inasimamia kiwango cha wastani cha biashara na Afrika, inayofikia takriban dola bilioni 20 kwa mwaka (karibu moja ya kumi ya ile ya China). Wala haitoi mwangwi wa kulazimisha kiitikadi, kijamii, au kitamaduni kwa wengi barani Afrika.
Licha ya hayo, Urusi imepata ushawishi mkubwa barani Afrika katika miaka ya hivi karibuni kwa kucheza karata ilizonazo vyema. Ambapo imepata ushawishi mkubwa zaidi - Libya, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Sudan, Madagascar, Msumbiji, na Mali.

Chanzo cha picha, Getty Images
Urusi imetumia kwa ustadi mchanganyiko wa uingiliaji wa mamluki na upotoshaji katika kuunga mkono viongozi au washirika waliotengwa
Mapinduzi ya hivi punde nchini Burkina Faso yalishuhudia vijana wakipeperusha bendera za Urusi katika mitaa ya mji mkuu, Ouagadougou - jambo ambalo lazima lilichangamsha mioyo huko Kremlin na kuonesha kuna uhusika fulani wa Urusi katika mapinduzi hayo.
Urusi pia inadumisha mfululizo wa mipango ya kawaida ya usalama, kiuchumi na kiutamaduni barani Afrika. Maarufu zaidi kati ya haya ni Mkutano wa Wakuu wa Urusi na Afrika wa Oktoba 2019 ambapo Vladimir Putin aliwakaribisha wakuu wa nchi arobaini na tatu wa Afrika huko Sochi. Katika Mkutano huo, Putin aliahidi kusamehewa madeni na kuongeza maradufu biashara na Afrika katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Urusi pia imefanikiwa kupata nguvu kidogo kwa kuahidi mamilioni ya dozi ya chanjo ya COVID-19 kwa nchi za Afrika. Licha ya matukio haya ya ufikiaji wa hali ya juu, ushirikiano wa kawaida hauonekani kuwa ambapo Moscow inapata manufaa makubwa zaidi ya kijiografia barani Afrika, angalau katika muda mfupi.















