Misaada yamiminika kwa mwanamke aliyetamani kufa kutokana na ugumu wa maisha

    • Author, Mansur Abubakar
    • Nafasi, BBC

Shamsiyya Abubakar alikuwa ameanza kupoteza matumaini - mdororo mkubwa wa uchumi nchini Nigeria ulimfanya ahangaike kila siku kulisha familia yake ya watu tisa.

Bi Shamsiyya , mama wa mtoto mchanga, aliiambia BBC kwamba matatizo yake yamepeleka akili yake kuwa na mawazo mabaya.

"Wakati mwingine najiambia; 'badala ya kuishi hivi, si ingekuwa bora kufa?' alisema katika mahojiano na BBC, ambayo yalisambaa sana katika mitandao nchini Nigeria.

Tangu mahojiano hayo yalipochapishwa siku ya Jumanne, watu asiowafahamu wamekuwa wakiingia na kutoka nyumbani kwake wakimletea chakula na pesa.

Matendo ya watu hao ambayo hakuyatarajia, "yamebadilisha maisha yake," alisema wakati BBC ilipomuhoji kwa mara ya pili.

"Sijawahi kuona kiasi kikubwa cha pesa maishani mwangu. Nashukuru sana. Nilipata pesa taslimu kutoka kwa watu kadhaa, huku wengine wakileta magunia ya mchele na mahindi, kwa sasa tuna chakula cha kutosha," aliongeza.

Mumewe Haruna Abubakar pia alionyesha kufurahishwa na bahati hiyo.

"Siku ambayo video ya BBC vilisambaa, hatukuwa na chakula, nilijitahidi kuwapa naira 500 (£0.25) familia yangu kununua vikombe vya mchele," alisema.

"Leo nina furaha kwani maisha yetu yamebadilika na tuna chakula cha kutosha."

Sani Isah, mmoja wa waliotoa msaada kwa familia hiyo, anasema mkasa wa Bi Shamsiyya ulinfanya alie. Bwana Isah aliongeza kuwa alihisi kulazimika kusaidia kwa kidogo alichokuwa nacho.

"Nadhani kesi yake ni aibu kwa viongozi wetu, kwa kweli nililia baada ya kutazama video yake. Iweje mtu atamani kifo kwa sababu ya chakula tu?" Aliuliza.

"Ninaomba wengine walio katika hali kama yake pia wapate usaidizi wanauohitaji ambao utabadilisha maisha yao."

Kwa sasa Nigeria inakabiliwa na mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi katika historia, ambao umesababisha ugumu wa maisha na hasira kuenea.

Siku ya Jumanne, maelfu ya watu waliingia barabarani katika maandamano ya nchi nzima kupinga jinsi serikali inavyoshughulikia uchumi.

Mchele, chakula kikuu nchini Nigeria, umeongezeka bei maradufu katika mwaka uliopita. Bi Shamsiyya hayuko peke yake katika hali ngumu ya maisha.

Bi Shamsiyya anahisi kwamba kutokana na wema wa watu, sasa anaweza kutazamia siku zijazo.

Aliambia BBC, ili kuihudumia familia yake kwa muda mrefu, anataka kuanzisha biashara ya chakula kwa baadhi ya chakula ambacho amepokea.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi