Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ugumu wa maisha watawala maandamano Chama kikuu cha upinzani Tanzania, Chadema
Ugumu wa maisha unaotokana na kupanda kwa gharama za maisha sambamba na mabadiliko cha sheria za uchaguzi umeteka maandamano ya chama kikuu cha Upinzani Tanzania, Chadema.
Moja kwa moja
Abdalla Seif Dzungu, Asha Juma and Dinah Gahamanyi
Ugumu wa maisha watawala maandamano Chama kikuu cha upinzani Tanzania, Chadema,
Ugumu wa maisha unaotokana na kupanda kwa gharama za maisha sambamba na mabadiliko cha sheria za uchaguzi umeteka maandamano ya chama kikuu cha Upinzani Tanzania, Chadema.
Maandamano hayo yalianza leo jijini Dar es Salaam, ambapo Chadema ilikuwa na hoja tatu kuu huku ikieleza kuwa itaendelea na maandamani katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Hoja hizo kuu ilikuwa ni kutaka katiba mpya, mabadiliko ya miswada ya Sheria za uchaguzi na kupanda kwa gharama za maisha.
Hata hivyo, maandamano hayo yaliyokuwa yameanzia kwenye maeneo mawili tofauti yaani Buguruni na Mbezi mwisho yalitamatia katika ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) zilizopo katika eneo la Ubungo ambapo chama hicho kiliwasilisha barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa zikieleza kuwa barua hiyo inabeba yote wanayopitia watanzania.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema yalikuwa ni maandamano ya amani na yataendelea katika mikoa mingine mapaka pale yatakapotokea mabadiliko.
Mbowe alisema, ”Tumefanya maandamano makubwa na marefu bila mtu kuumizwa, na hiyo ndio tabia Chadema. Pale polisi wanapoelewa hoja zetu hatuna ugomvi na mtu. Tutaendelea kuandamana katika taratibu na mikoa mbalimbali mpaka wenzetu watuelewe tunamaamisha nini.”
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Muliro alisema kuwa jeshi hilo halijaona kasoro isipokuwa watafanya tathmini ya kiusalam ya maandamano hayo.
”Sisi jeshi la polisi, ushiriki wetu ulikuwa ni kuhakikisha vitendo vya uvunjifu wa sheria havifanyiki. Lengo letu lilikuwa kuhakikisha kila kitu kiko salama. Tutafanya tathmini ya maandamano hayo.”
Gharama ya maisha
Licha ya baadhi ya wafuasi wa chama hicho kusisitiza kuhusu miswada ya uchaguzi wakitaka marekebisho, huku wengine wakitaka katika Katiba mpya. Wengi walilia gharama ya maisha kuwa juu.
Waandamani hao wanadai bidhaa muhimu zimekuwa zikipatikana kwa gharama kubwa ikiwemo sukari na mafuta. Pia wameeleza kutatizwa na upatikani usio wa uhakika wa umeme.
Miongoni mwa wafuasi wa chama hao, Hamed Msuya ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam alisema,”gharama za maisha ziko juu, sukari inapatikana kwa shida na kwa gharama kubwa, leo hii sukari ni shilingi 5500 wakati siku za karibuni ilikuwa shilingi 2800.
Ni wazi kuwa gharama ziko juu, umeme haupo wa uhakika lakini yote inayokana na usimamizi usiokuwa mzuri hivyo tunataka mabadiliko ya sheria za uchaguzi ili tuchague viongozi wenye kutatua changamoto hizo.
Unaweza pia kusoma:
- Kwanini Chadema inaingia barabarani?
Tazama: Muda wakati ndege ya Urusi ilipoanguka leo Belgorod na kuwauwa wafungwa 65
BBC imethibitisha video hii inayoonyesha wakati ndege ya Urusi- inayoripotiwa kuwa IL -76- ilipoanguka katika eneo la Belgorod
Takriban wafungwa 65 wa vita wa Ukraine wameuawa, kulingana na wizara ya ulinzi ya Urusi.
Shirika la habari la Ria Novosti lilisema watu wengine tisa walikuwa ndani ya ndege hiyo, wakiwemo wafanyakazi sita.
Katika picha: Maandamano ya chama cha upinzani cha Chadema Tanzania
Kama ambavyo tumekua tukikuarifu maandamano yanaendelea katika maeneo mawili jijini Dar es salaam Tanzania yakiongozwa viongozi wa Chadema Freeman Mbowe na Tundu Lissu.
Wamekuwa wakipinga baadhi ya miswada iliyowasilishwa bungeni huku pia wakidai wanataka Katiba mpya na wanataka serikali kuchukua hatua juu ya gharama ya maisha kupanda.
Tumekuwa tukipokea picha mbali mbali kutoka kwenye maandamano hayo na hizi ni ni picha kutoka kwa waandishi wetu wanaofuatilia maandamano hayo:
Vurugu za jimbo la Plateau: Makanisa na misikiti yachomwa nchini Nigeria huku amri ya kutotoka nje ikitangazwa Mangu
Misikiti na makanisa yameteketezwa katika jimbo la Plateau katikati mwa Nigeria baada ya mzozo wa ng'ombe kuwa mbaya.
Watu wanane walifariki katika mapigano hayo Mangu baada ya ng'ombe kutoroka kuelekea barabarani ambako walikuwa wakizuia magari.
Gavana wa jimbo hilo ameweka amri ya kutotoka nje kwa saa 24 ili kusitisha ghasia, ingawa mazishi yanaruhusiwa kwa waliofariki.
Eneo hili la kati linakabiliwa na mvutano kati ya jamii ambazo mara nyingi huingia kwenye vurugu za kidini na kikabila.
Plateau ni eneo la kaskazini lenye Waislamu wengi hlinalopakana na eneo la kusini lenye Wakristo wengi na jamii nyingi zimechanganyika.
Mapigano hayo ya Jumanne ya Mangu, eneo lililopo umbali wa kilomita 74 (maili 45) kusini-mashariki kutoka mji mkuu wa jimbo, Jos, yalihusisha watu kutoka makabila ya Fulani na Mwagaful.
Mwandishi Ado Musa, ambaye alitembelea eneo hilo wa gazeti la Daily Trust, aliambia BBC kuwa misikiti sita na makanisa mawili yaliteketezwa katika ghasia hizo.
Tatizo lilianza baada ya wezi wengine wenye silaha kujaribu kuiba ng'ombe wa Wafulani, alisema.
Jaribio hilo la wizi halikufanikiwa, lakini ng'ombe hao walipotoroka wakati wa vurugu hizo, risasi zilifyatuliwa, jambo hilo lilisababisha fujo barabarani na kuwatia wasiwasi wakazi wengine.
Vijana kutoka jumuiya ya Wakristo Mwagaful na Wafula wa Kiislamu walilenga maeneo ya ibada.
Mapigano makali yaendelea nchini Somalia huku wanajeshi wa wakipambana na shambulio la al-Shabab
Mapigano makali yanaendelea katikati mwa Somalia baada ya wanamgambo wa al-Shabab kushambulia kambi za kijeshi katika eneo la Mudug.
Walioshuhudia wameiambia BBC kuwa walisikia milio ya risasi na milipuko alfajiri siku ya Jumatano.
Inasemekana kuwa shambulizi hilo lilianza kwa shambulio la kujitoa mhanga, likilenga vikosi maalum vya serikali.
Waziri wa Usalama wa Galmudug Mohamed Abdi Aden ameiambia BBC kwamba wanajeshi bado wanapambana na wanamgambo hao katika kijiji cha Aad, ambako vituo vya kijeshi viko.
Shirika la Habari la Kitaifa la Somalia (Sonna) linaripoti kwamba jeshi, likisaidiwa na wenyeji, lilizuia shambulio hilo, "na kusababisha hasara kubwa kwa magaidi".
Lakini al-Shabab ilisema iliteka kambi hizo tano za kijeshi na kuua makumi ya wanajeshi.
Vikosi vya serikali ya Somalia tangu Agosti 2022 vimekuwa vikiendesha mashambulizi makubwa dhidi ya kundi lenye uhusiano na al-Qaeda.
Wasiwasi waibuka huku M23 ikiunda utawala mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Kundi la waasi la M23 limeteua utawala wake katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na hivyo kuzua wasiwasi
Katika taarifa ya kundi hilo, kiongozi wa kisiasa wa M23 Bertrand Bisimwa amesema kundi hilo limeteua watawala katika eneo la Rutshuru la Kivu Kaskazini.
Aliongeza kuwa viongozi wa miji ya Kiwanja, Rubare na Bunagana, katika Kivu Kaskazini, wameteuliwa pia.
Waasi wanadhibiti sehemu kubwa ya Rutshuru na Masisi, mbili kati ya wilaya tano zinazounda jimbo la Kivu Kaskazini, na ziko takriban kilomita 35 (maili 22) magharibi mwa mji mkuu wa mkoa huo, Goma.
Katika siku za hivi karibuni, jeshi la Congo limeanzisha mashambulizi makubwa ya ndege zisizo na rubani katika maeneo yanayodhibitiwa na M23.
Siku ya Jumatano msemaji wa kundi hilo alisema wapiganaji wake waliiangusha moja ya ndege zisizo na rubani tatu zilizokuwa zikitumiwa na jeshi.
BBC haijathibitisha dai hili kwa duru huru, wala jeshi halijatoa maoni kulihusu.
Mitandao ya kijamii ya Kongo imekuwa ikijibu kuhusu M23 kuteua utawala wake katika Kivu Kaskazini.
Baadhi wanaona huo ni mwanzo wa hatua ya kuunda jimbo tofauti mashariki mwa Kongo, huku wafuasi wa M23 wakisema ni haki ya kundi hilo kutawala maeneo yanayodhibiti.
Unaweza pia kusoma:
- Kuzinduliwa kwa muungano wa waasi wa DR Congo, Kenya kwaibua mzozo wa kidiplomasia
- Mzozo wa DRC: Je inawezekana kuyamaliza makundi ya wapiganaji Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo?
Maandamano ya Chadema Tanzania: Waandamanaji wapinga miswada mitatu ya uchaguzi iliyofikishwa bungeni mwaka jana.,
Maandamano yanaendelea katika maeneo mawili jijini Dar es salaam Tanzania ambapo katika eneo la Buguruni yanayoongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe, wakati yale yanayoanzia katika eneo la Mbezi Mwisho yanaongozwa na Makamu Mwenyekiti,Tundu Lissu.
Wafuasi wa chama hicho wanaeleza kuwa maandamano ni moja ya njia ya kufikisha salamu kwa mamlaka za Kitaifa ya kutoridhishwa na baadhi ya mambo yanayoendelea nchini.
Viongozi sambamba na wafuasi wa chama hicho wanabdamana kupinga misuada mitatu ya uchaguzi iliyofikishwa bungeni mwaka jana.
Sambamba wanataka Katiba mpya na wanataka serikali kuchukua hatua juu ya gharama ya maisha kupanda.
Haya ni maoni ya baadhi ya waandamanaji wa chama cha Chadema katika video iliyoandaliwa na mwandishi wa BBC Eagan Salla:
Video imeandaliwa na Eagan Salla
Habari za hivi punde, Ndege ya Urusi yaanguka na kuwaua wafungwa 65 wa kivita kutoka Ukraine - Moscow
Ndege ya kijeshi ya Urusi aina ya Ilyushin-76 imeanguka katika eneo la kusini mwa Belgorod linalopakana na Ukraine.
Takriban wafungwa 65 wa vita wa Ukraine wameuawa, kulingana na wizara ya ulinzi ya Urusi.
Shirika la habari la Ria Novosti lilisema watu wengine tisa walikuwa ndani ya ndege hiyo, wakiwemo wafanyakazi sita.
Gavana wa mkoa Vyacheslav Gladkov alisema anafahamu "tukio" lakini hakutoa maelezo zaidi.
Video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ilionyesha ndege ikianguka karibu na kijiji cha Yablonovo na kufuatiwa na mlipuko, mwendo wa saa 11:00 kwa saa za huko (08:00 GMT).
Msemaji wa rais wa Urusi Dmitry Peskov alisema Ikulu ya Kremlin inafahamu kuhusu ajali hiyo lakini ilikataa kutoa maelezo zaidi.
Tazama Video: Maandamano ya kuishinikiza serikali kufanya mabadiliko katika sheria ya uchaguzi yaanza Tanzania
Polisi wameruhusu chama cha chadema kufanya maandamano katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam lakini wakaonya dhidi ya ghasia na uchochezi, vyombo vya habari vya ndani viliripoti
Kagame aapa kuilinda Rwanda huku kukiwa na mvutano na Burundi, DRC,
Rais wa Rwanda Paul Kagame ameahidi kuilinda nchi yake dhidi ya uchokozi wa nje wakati mvutano ukiongezeka kati ya Kigali na nchi jirani za Burundi na DR Congo.
"Linapokuja suala la kuitetea nchi hii ambayo imeteseka kwa muda mrefu na hakuna aliyekuja kusaidia, hatuhitaji ruhusa kutoka kwa mtu yeyote kufanya kile tunachotakiwa kufanya ili kujilinda," alisema Kagame katika hotuba iliyorushwa na televisheni ya taifa ya Rwanda jana.
Akiwahutubia wajumbe katika mkutano wa majadiliano ya kitaifa, Kagame kwa mara nyingine alikanusha madai ya DRC kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi katika maeneo ya mashariki mwa Congo.
Akizungumzia mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi, rais alisema: "Kama kuna atakayetufanya tunafikirie kama tunarudi nyuma katika nyakati hizo, basi hatuna cha kupoteza. Tutapigana kama watu ambao hawana kitu cha kupoteza."
Rwanda imeingia katika mzozo wa kidiplomasia na Burundi, ambayo ilifunga mpaka wa pamoja tarehe 11 Januari baada ya kuihusisha Rwanda na shambulio la kigaidi lililofanywa na waasi wa RED-Tabara mwezi Disemba.
Jana, Burundi ilikanusha madai ya Rwanda kwamba Rais Evariste Ndayishimiye alitoa wito wa kuondolewa mamlakani kwa Kagame wakati wa hotuba yake aliyoitoa katika Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo Januari 21.
Kwa Picha: Maandamano ya upinzani nchini Tanzania yaanza
Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema, kimefanya maandamano kukemea mapendekezo ya miswada ya sheria ya uchaguzi, gharama kubwa ya maisha na kucheleweshwa kwa marekebisho ya katiba.
Polisi wameruhusu chama khicho ufanya maandamano katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam lakini wakaonya dhidi ya ghasia na uchochezi, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.
Sababu za Maandamano
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Januari 13, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema maandamano yanalenga kuishinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau mbalimbali kuhusu masuala ya uchaguzi.
Vilevile chama hicho kinaitaka serikali iondoe Bungeni miswaada inayohusu vyama vya siasa na uchaguzi, ambayo ni muswada wa Marekebisho ya Sheria za Vyama vya siasa na Sheria ya gharama za Uchaguzi.
Badala yake Serikali iwasilishe muswada wa kukwamua mchakato wa Katiba mpya kwa kuzingatia mwafaka wa kitaifa. Kwani Chadema inaamini, "serikali imepuuza maoni yaliyotolewa na Kikosi Kazi pamoja na wadau mbalimbali."
Kadhalika, Chadema imeitaka Serikali iwasilishe bungeni muswada wa kufanya marekebisho ya mpito ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ili uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024 na ule mkuu wa 2025 uwe huru na haki.
Suala la gharama za maisha pia limekuwa ajenda ya maandamano: "Tunataka serikali ipeleke mpango wa kuwakwamua wananchi na hali ngumu ya maisha Bungeni, ikiwa ni pamoja na kushusha bei ya bidhaa muhimu au kuweka ruzuku katika baadhi ya bidhaa," amesema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Tazama Video: Gari lagonga mkahawa na kuingia ndani
Kanda za video za kushangaza zinaonyesha gari lililogonga mkahawa na kuingia hadi ndani Picha za CCTV zinaonyesha wakati gari lilipogonga mkahawa huko Turin, Italia.
Kisa hicho kilitokea mwendo wa saa 9:30 asubuhi kwa saa za huko, wateja walipokuwa wakifurahia kifungua kinywa ndani ya mkahawa wa eneo hilo.
Watu saba walipelekwa hospitalini wakiwa na majeraha madogo, lakini hakuna ripoti za majeruhi.
Kipima mwendo kasi kwenye gari wakati wa ajali kilikwama kwa kasi ya 115km/h (karibu 71mph), kulingana na vyombo vya habari vya ndani.
"lingeweza kusababisha maafa makubwa kweli, angalau watu 10 wangekufa," Simona Carastro, binti wa mmiliki wa mkahawa aliiambia BBC.
"Sasa tunatumai tu kuwa tutaweza kufungua tena mkahawa haraka iwezekanavyo, kwa kuzingatia hasara ya kifedha tuliopata.
"Polisi bado wanachunguza sababu za ajali hiyo.
Habari za hivi punde, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam: 'Fanyeni maandamano yenu kwa amani bila kuathiri shughuli zingine'
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amekutana na baadhi ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika eneo la Mbezi Mwisho huku akiwataka wafanye maandamano bila kuathiri shughuli mbalimbali ndani ya jiji hilo.
Chalamila ameyasema hayo alipofika katika eneo la Mbezi Mwisho ambapo wafuasi wameanza kujitokeza kwa wingi wakisubiri kuanza maandamano hayo.
Alisema, “Mnafahamu kuwa Dar ndiyo jiji kubwa zaidi la kibiashara nchini Tanzania, pia lenye mzunguko mkubwa wa kifedha, lenye hospitali kubwa zaidi. Basi fanyeni maandamano yenu kwa amani bila kuathiri shughuli zingine.”
Maandamano hayo yanatarajiwa kuanzia eneo la Buguruni kwenda Ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) huku wafuasi wengine wakianza katika eneo la Mbezi Mwisho mpaka Ofisi za UN.
Haya ni maandamano ya kwanza ambayo chama kikuu cha upinzani imepewa kibali kufanyika baada ya uchaguzi mkuu wa 2020.
Upinzani Tanzania wafanya maandamano kushinikiza mabadiliko ya sheria za uchaguzi
Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema, kinapanga kufanya maandamano kukemea mapendekezo ya miswada ya sheria ya uchaguzi, gharama kubwa ya maisha na kucheleweshwa kwa marekebisho ya katiba.
Polisi wameruhusu chama kufanya maandamano katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam lakini wakaonya dhidi ya ghasia na uchochezi, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.
Chadema imesema kibali hicho kimetolewa kufuatia makubaliano na polisi kuruhusu maandamano ya amani.
Chama hicho kilisema kitaongoza maandamano hayo Jumatano ili kuishinikiza serikali kutekeleza mageuzi hayo kabla ya uchaguzi mkuu mwaka ujao.
Ni kinyume na miswada mitatu ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni Novemba mwaka jana.
Chama kinataka iondolewe kwa madai kuwa maoni ya wadau wengi hayakuzingatiwa.Uchaguzi wa serikali za mitaa umepangwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Haya yatakuwa maandamano ya kwanza kabisa kufanyika nchini baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua madaraka Machi 2021 kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Magufuli.
Magufuli alikuwa akishutumiwa kwa kukandamiza upinzani baada ya kupiga marufuku mikutano ya kisiasa.
Tanzania inafurahia utulivu katika eneo lenye hali tete.Rais Hassan amepata uungwaji mkono ndani na kimataifa baada ya kuingia uongozini na sauti ya kisiasa ya mageuzi.
Paul Mackenzie: Kiongozi wa kanisa la 'kufunga hadi kufa' Kenya ashtakiwa kwa kuua bila kukusudia
Kiongozi wa kanisa la ekufunga hadi kufa nchini Kenya Paul Mackenzie ameshtakiwa kwa makosa 238 ya kuua bila kukusudia, pamoja na mkewe na watu wengine 93 wanaodaiwa kuwa washirika wake.
Mashtaka hayo ya ziada yanakuja baada ya Bw Mackenzie na watu wanaoshukiwa kuwa washirika wake kushtakiwa kwa ugaidi wiki jana.
Anadaiwa kuwahimiza waumini wa Kanisa lake la Good News International kuhamia Shakahola, msitu wa mbali katika pwani ya Kenya, na kufunga hadi kufa ili "kukutana na Yesu".
Miili ya watu 429 wakiwemo watoto imefukuliwa kutoka maeneo ya makaburi katika msitu huo.
Wengi wao walionyesha dalili za njaa, lakini wengine - watoto kati yao - wanaweza kuwa walivamiwa.
Waathiriwa 238 waliuawa arehe zisizojulikana kati ya Januari 2021 na Septemba 2023 huko Shakahola, ripoti ya vyombo vya habari vya ndani, ikitoa hati za korti.
Bw Mackenzie na washukiwa wengine walikana mashtaka walipofikishwa katika mahakama moja katika mji wa pwani wa Mombasa siku ya Jumanne.
Bw Mackenzie amekuwa kizuizini tangu kukamatwa kwake Aprili mwaka jana.
Khan Younis: Israel inasema vikosi vyake vimeuzingira mji wa pili mkubwa wa Gaza
Jeshi la Israel linasema kuwa vikosi vyake vya ardhini vimezingira mji wa Khan Younis, ambao ndio mkubwa zaidi kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Wanajeshi pia wameripotiwa kuingia ndani zaidi katika maeneo yaliyosalia ya mji, ambapo wanaamini kuwa viongozi wa Hamas wamejificha kwenye mahandaki na mateka.
Wakaazi walisema kuwa vifaru vilifunga barabara ya mwisho kutoka nje ya jiji kuelekea pwani ya Mediterania, na kuwazuia kukimbilia kusini.
Pia kulikuwa na mapigano makali karibu na hospitali kuu mbili za jiji hilo.
Makabiliano haya yanajiri wakati mazishi yakifanyika kwa baadhi ya wanajeshi 24 wa Israel waliouawa siku ya Jumatatu katika siku mbaya zaidi kwa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) tangu kuanza kwa mashambulizi yake ya ardhini huko Gaza wiki 12 zilizopita.
Takriban Wapalestina 195 pia waliuawa huko Gaza katika muda wa saa 24 zilizopita, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.
Wizara hiyo inasema zaidi ya watu 25,400 wameuawa - wengi wao wakiwa watoto na wanawake - wakati wa vita kati ya Hamas na Israel.
Vita hivyo vilichochewa na shambulio la kuvuka mpaka ambalo halijawahi kufanywa na wapiganaji wa Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, ambapo takriban watu 1,300 waliuawa - wengi wao wakiwa raia - na wengine wapatao 250 walichukuliwa mateka.
Marekani yawashambulia wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran nchini Iraq
Marekani inasema vikosi vyake vimefanya mashambulizi nchini Iraq dhidi ya vituo vitatu vinavyotumiwa na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran.
Mashambulizi hayo "ya sawia" yalilenga "kundi la wanamgambo wa Kataib Hezbollah na makundi mengine yenye uhusiano na Iran", Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin alisema.
Alisema mashambulizi hayo ni ya kujibu moja kwa moja" mashambulizi ya Iran dhidi ya ngome za Marekani na washirika wake nchini Iraq na Syria.
Wanajeshi kadhaa wa Marekani walijeruhiwa katika shambulio la kombora kwenye kambi ya anga magharibi mwa Iraq wiki iliyopita.
Kituo kikuu cha Jeshi la Marekani (CentCom) kilisema wakati huo kwamba wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran walilenga kambi ya anga ya Al Asad, ambayo inawahifadhi wanajeshi wa Marekani, kwa makombora na maroketi.
Kundi linalojiita Islamic Resistance in Iraq lilidai kuhusika na shambulio hilo.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Marekani ya Washington Institute for Near East Policy, kundi hilo liliibuka mwishoni mwa 2023 na linajumuisha makundi kadhaa yenye silaha yenye uhusiano na Iran yanayofanya kazi nchini Iraq.
Imedai mashambulizi mengine dhidi ya vikosi vya Marekani katika wiki za hivi karibuni.K
atika taarifa, Bw Austin alisifu "utaalamu" wa wanajeshi wa Marekani katika kupanga na kufanya mashambulizi ya Jumatano nchini Iraq kama sehemu ya juhudi za "kusambaratisha na kuidhalilisha ISIS [kundi la Islamic State].
"Bw Austin alisisitiza kuwa yeye na Rais wa Marekani Joe Biden "hawatasita kuchukua hatua zinazohitajika" kutetea maslahi ya Marekani.
"Hatutaki kuzidisha mzozo katika eneo hili. Tumejiandaa kikamilifu kuchukua hatua zaidi za kulinda watu wetu na vifaa vyetu.
Tunatoa wito kwa vikundi hivi na wafadhili wao wa Irani kusitisha mara moja mashambulizi haya," alisema.Katika taarifa tofauti, CentCom ilisema mashambulizi ya Jumatano nchini Iraq yalifanywa saa 00:15 saa za ndani (21:15 GMT Jumanne) kujibu shambulio hilo - miongoni mwa mengine - kwenye kambi ya ndege ya Al Asad magharibi mwa Iraq tarehe 20 Januari.
"Mashambulizi haya yalilenga makao makuu ya [Kataib Hezbollah], kuhifadhi, na maeneo ya mafunzo kwa makombora, na uwezo wa mashambulizi ya njia moja ya UAV," CentCom ilisema.
Jeshi la Marekani halikutoa maelezo yoyote kuhusu mahali ambapo vituo vya wanamgambo vilivyolengwa vilikuwa nchini Iraq.