Tinubu apingwa vikali kuhusu matumizi ya nguvu nchini Niger

w

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, By Nduka Orjinmo
    • Nafasi, BBC News, Abuja

Rais wa Nigeria Bola Tinubu anakabiliwa na upinzani mkubwa nchini mwake kutokana na tishio lake la kutumia nguvu za kijeshi kutengua mapinduzi katika nchi jirani ya Niger.

Vyombo vya habari vya nchini vimeripoti kuwa kuna na upinzani mkali dhidi ya uingiliaji kati wa kijeshi katika kikao cha baraza la juu la bunge, Seneti, Jumamosi, licha ya kwamba linadhibitiwa na chama cha Bw Tinubu.

Upinzani huu ulikuwa hasa kutoka kwa wabunge wanaowakilisha majimbo yaliyoko kwenye mpaka wa kilomita 1,500 (maili 930) unaotenganisha nchi hiyo na Niger, lakini pia kumekuwa na shutuma nchini kote kuhusu uwezekano wa vita.

Jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi Ecowas ilikuwa imeweka makataa ya Jumapili kwa serikali ya kijeshi kujiondoa madarakani - au ikabiliwe na uwezekano wa kuchukuliwa hatua za kijeshi.

Uamuzi huo ulionekana sana kama wa Bw Tinubu kwa vile yeye ndiye mwenyekiti wa sasa wa Ecowas, na Nigeria ni mwanachama wake mwenye ushawishi mkubwa.

Ingawa jeshi limekaidi uamuzi huo, Ecowas haikujibu kwa kutuma wanajeshi mara moja. Hii ilikuja kama afueni kwa Wanigeria wengi ambao wanataka suluhu la kidiplomasia katika mzozo huo.

Baadhi wanahoji kama makataa ya siku saba yalikuwa ya kweli ikizingatiwa kuwa Nigeria na nchi nyingine zinapaswa kupata kibali cha bunge kabla ya kupeleka jeshi.

Watu wengi pia wanashangaa kwamba umeme nchini Niger ulikatwa kwa amri ya Rais Tinubu, na kusababisha ukosefu wa huduma hiyo muhimu katika mji mkuu wa Niger, Niamey, na miji mingine.

Wakosoaji wanadai kuwa huu ni ukiukaji wa mkataba ambao uliiwezesha Nigeria kujenga bwawa kwenye Mto Niger, ingawa wafuasi wa Bw Tinubu wanasema kukatwa kwa umeme kunalenga kuishinikiza jeshi kurudisha mamlaka kwa Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum, bila makabiliano ya kijeshi.

Nigeria na Niger zina uhusiano mkubwa wa kikabila, kiuchumi na kiutamaduni na uingiliaji wowote wa kijeshi dhidi ya Niger utakuwa na athari kwa maeno ya kaskazini mwa Nigeria, ambayo tayari yanakabiliwa na changamoto zake za usalama.

Kundi lenye ushawishi mkubwa la viongozi wa dini ya Kiislamu kaskazini mwa Nigeria lilisema Bw Tinubu lazima "asiharakishe katika mzozo unaoweza kuepukika na jirani kwa matakwa ya siasa za kimataifa".

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanajeshi nchini Niger wanasema watapinga "uchokozi" wowote wa Ecowas na mataifa yenye nguvu ya Magharibi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Bw Bazoum alikuwa mshirika mkuu wa nchi za Magharibi, ambaye aliiruhusu Ufaransa ambayo ilikuwa mkoloni wake na Marekani kuweka kambi za kijeshi nchini humo ili kusaidia katika vita dhidi ya wanamgambo wa kijihadi wanaoyumbisha usalama katika maeneo mengi ya Afrika Magharibi.

Wanajeshi nchini Mali na Burkina Faso wameapa kuwatetea viongozi wa mapinduzi ya Niger iwapo Ecowas itatumia nguvu, na hivyo kuongeza uwezekano wa kutokea kwa mzozo mkubwa wa kikanda.

Macho yote sasa yanaelekezwa kwa Bw Tinubu ambaye amekuwa na sauti kubwa zaidi kulaani mapinduzi katika Afrika Magharibi, na alisema mwezi uliopita kwamba Ecowas haiwezi kuundwa na "mbwa wasio na meno".

"Lazima tusimame kidete kuhusu demokrasia. Hakuna utawala, uhuru na utawala wa sheria bila demokrasia. Hatutakubali mapinduzi baada ya mapinduzi ya Afrika Magharibi tena," Bw Tinubu alisema, muda mfupi baada ya kuchukua uongozi wa chombo hicho cha kanda.

Katiba ya Nigeria inasema kuwa rais hawezi kupeleka wanajeshi bila idhini ya Bunge - linaloundwa na mabaraza ya juu na ya chini ya bunge.

Haijabainika iwapo Bw Tinubu atapata uungwaji mkono kutokana na upinzani anaokabiliana nao.

"Ecowas ilifanya makosa, rais wa Nigeria pia amekosea," alisema Profesa Khalifa Dikwa, msomi katika Chuo Kikuu cha Maiduguri na mwanachama wa kundi la wazee wenye ushawishi kaskazini mwa Nigeria.

Katika taarifa iliyooonekana baada ya kikao cha faragha cha Jumamosi, kiongozi wa Seneti Godswill Akpabio alisema bunge la Ecowas ndilo lenye jukumu la kutatua mzozo huo, akisema kuwa linapaswa kutoa "suluhu za kutatua mgogoro huu haraka iwezekanavyo".

Msimamo mkali wa Rais Tinubu dhidi ya mapinduzi unaweza kuwa umetokana na uzoefu wake mwenyewe. Alikuwa na mwaka mmoja tu ofisini kama mbunge mapema miaka ya 1990 kabla ya uchaguzi kubatilishwa, bunge lilivunjwa na Jenerali Sani Abacha kunyakua mamlaka.

Alijiunga na vuguvugu la kuunga mkono demokrasia lililofanya kampeni ya kurejea kwa utawala wa kiraia, na kumuweka katika njia panda za kijeshi ambazo zilimlazimu kwenda uhamishoni. Alirejea mwaka wa 1998 baada ya kifo cha Jenerali Abacha, mmoja wa watawala katili na mafisadi wa kijeshi wa Nigeria.

Lakini kuna hisia miongoni mwa Wanigeria wengi kwamba Ecowas ilikuwa na haraka sana katika kutoa uamuzi wa mwisho kwa junta, na Rais Tinubu alikuwa hajafikiria vya kutosha juu ya athari za ndani za kutumia nguvu.

"Niger ilikuwa ni sehemu ya kaskazini mwa Nigeria hadi Mkutano wa Berlin [wa 1884-1885, wakati mataifa yenye nguvu ya kigeni yalipounda mipaka ya sasa ya Afrika]. Unatarajia kaskazini kuingia kwenye vita dhidi yake yenyewe?" aliuliza Prof Dikwa.

h

Chanzo cha picha, Getty Images

Tofauti na mtangulizi wake Muhammadu Buhari, Rais Tinubu hana historia ya kijeshi na mshauri wake wa usalama wa taifa, Nuhu Ribadu, ambaye ni polisi wa zamani hana historia hiyo pia.

Wakuu wa jeshi la Ecowas walitoa taarifa yao wenyewe wiki iliyopita, wakisema waliuonana uingilia kat iwa kijeshi kama ndio "suluhisho la mwisho".

Wakosoaji wanasema Bw Tinubu ana historia ya kuharakisha kufanya maamuzi makubwa, akiashiria ukweli kwamba alitumia hotuba yake ya kwanza kama rais mnamo Mei kutangaza kuondoa ruzuku ya mafuta ya miongo kadhaa, kwa matamshi yasiyo ya maandishi ambayo yalisababisha machafuko.

Viongozi wa Ecowas sasa watafanya mkutano katika mji mkuu wa Nigeria Abuja siku ya Alhamisi ili kuamua juu ya hatua inayofuata kuihusu Niger.

Ingawa baadhi ya nchi nyingine za Afrika Magharibi zimeahidi kushiriki katika uingiliaji kati wowote wa kijeshi, ni vigumu kuziona zikifanya hivyo bila Nigeria, ikiwa Bunge la Kitaifa halitatoa uungaji mkono wake.

Bw Tinubu anavaa kofia mbili - ile ya mwenyekiti wa Ecowas na rais wa Nigeria. Moja inalazimu kutenda kwa maslahi ya kikanda na kulinda demokrasia, lakini inaweza kusababisha gharama kubwa kwa kofia nyingine.