Mapinduzi Niger: Muda unayoyoma kwa maamuzi ya mwisho Afrika magharibi

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Yusuf Akinpelu
- Nafasi, BBC News, Lagos
Wakati siku saba zilizotolewa na viongozi wa Afrika magharibi kwa jeshi la Niger kurudisha uongozi wa nchi hiyo kwa rais Mohamed Bazoum zinakaribia kumalizika, pande zote zina maamuzi mazito.
Jumapili 30 Julai , jumuiya ya Afrika magharibi Ecowas, inayoongozwa na rais wa nchi jirani Nigeria Bola Tinubu ilisema utawala wa kijeshi una wiki moja kurudisha utaratibu wa kikatiba au ukabiliwe na kinachowezekana kuwa ni hatua za nguvu.
Tayari vikwazo vimeidhinishwa dhidi ya viongozi hao na huduma ya kusambaza umeme kutoka Nigeria zimekatwa, pamoja na kufungwa kwa mipaka, hatua inayomaanisha kuwa bidhaa haziingi na nchi hiyo kavu haizifikii bandari.
Lakini wakati wasiwasi wa kisiasa, kidiplomasia na kijeshi ukiongezeka, je ni kitu gani kinachowezeka kutokea wakati muda wa mwisho ukiwadia?
1. Kuongezwa muda wa mwisho
Hatua moja ni jumuiya ya Ecowas kuongeza muda huo. Hatua hii inaweza kuonekana kama kurudi nyuma lakini viongozi wa jumuiya hiyo wanaweza kuepuka aibu kwa kusema kuwa jitihada za kidiplomasia zimepiga hatua na wanataka kutoa fursa zaidi.
Tatizo ni kwamba kwa sasa jitihada za Ecowas hazijazaa matunda. Ujumbe uliotumwa Niger Alhamisi ulirudi baada ya saa kadhaa bila ya kubwa. Wakati huo huo uongozi wa kijeshi ulishinikiza kauli yake dhidi ya mataifa ya magharibi na Ecowas.
Ulitangaza kukatiza uhusiano wa kidiplomasia na Nigeria, Togo, Marekani na Ufaransa na kusema inakatiza makubaliano ya kijeshi yalioidhinishwa na Ufaransa,yanayoruhusu taifa hilo ambalo ndio mkoloni wa zamani wa Niger kutuma wanajeshi wake 1,500 huko.
Na Rais Bazoum, anayezuiwa na jeshi, alitumia lugha kavu katika maoni alioyaandika katika gazeti la Washington Post. Rais Bazoum alisema alikuwa akiandika "kama mateka" na ameziomba Marekani na jumuiya ya kimataifa kusaidia kurudisha utulivu kikatiba.
2. Makubaliano ya kukabidhi madaraka
Katika kujaribu kutuliza mambo na kupata muafaka, utawala wa kijeshi na Ecowas huenda wakaafikiana ratiba ya kurudi katika utawala wa kidemokrasia.
Huenda hili likajumuisha kuachiliwa kwa rais Bazoum Pamoja na viongozi wengine wa kisiasa wanaozuia ili kuendeleza mazungumzo na pia kuvuta muda. Hili limekuwa suala kuu linaloshinikizwa na wanaoshutumu mapinduzi Afrika na kwengineko.
Jumuiya hiyo ya Afrika magharibi tayari imefikia ukabidhi wa mamlaka kieneo katika ukanda wa Sahel, Mali na Burkina Faso ambazo zilipinduliwa kijeshi katika miaka ya hivi karibuni.
Lakini makubaliano hayo yalikabiliwa na changamoto, tarahe za uchaguzi zikiahirishwa na bado hakuna hakikisho kwamba madaraka yatakabidhiwa.
Sudan ilioidhinisha utawala wa kijeshi na kiraia mnamo 2019, uliotarajiwa kutoa fursa kwa demokrasia baada ya mpinduzi, ni mfano mwingine. Lakini mzozo ulioanza kati ya viongozi wa kijeshi wapinzani inatoa tahadhari.
3. Jeshi kuingilia kati
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Viongozi wa Afrika magharibi hawakusema kwamba watatumia nguvu bila shaka iwapo rais Bazoum hatorudishwa madarakani, lakini wameliacha hilo kuwa ni uwezekano.
Maafisa wa Nigeria wameitaja hiyo kuwa hatua ya mwisho. Ecowas imewahi kutumia nguvu za kijeshi kurudisha utawala wa kikatiba katika siku za nyuma mfano nchini Gambia 2017 wakati Yahya Jammeh alipokataa kujiuzulu baada ya kushindwa katika uchaguzi. Lakini hesabu ya iwapo kuliidhinisha hili ni ngumu.
Kwanza, kijiografia Niger ni nchi kubwa katika Afrika magharibi, wakati Gambia ni ndogo iliozungukwa na Senegal na bahari ya Atlantiki kwa hivyo kutuma kikosi itakuwa ni taswira tofauti.
Pili, Nigeria inayoongoza jitihada za kurudishwa madarakani rais Bazoum, inakabiliwa na changamoto nyingi nchini za kiusalama, kwahivyo kutuma kikosi Niger ina athari kwake.
Na tatu, Mali na Burkina Faso zimetangza kuwa hatua zozote za kijeshi dhidi ya Niger ni sawa na kutangaza vita na wataingia kuwatetea viongozi wenzao wa mapinduzi.
Kwahivyo kuna hatari ya kuzuka vita vikubwa zaidi, hususan iwapo raia Niger watakataa vikosi vya nje kuingilia kati. Ijapokuwa haiwezekani kujua namna watakavyoitikia hali hiyo.
Nchi kama Algeria, jirani na Niger kwa upande wa kaskazini, China na Urusi zimeomba pande zote kujizuia na kuendelezwa mazungumzo kusitisha wasiwasi uliopo.
Hatahivyo baada ya mkutano wa siku tatu Abuja, wakuu wa ulinzi wa Ecowas wanasema wameratibu mpango wa kina wa kutathminiwa na viongozi unaohusu kuingilia kati kijeshi.
Nigeria, Ivory Coast, Senegal na Benin zote zimesema ziko tayari kutuma wanajeshi Niger iwapo Ecowas itapitisha uamuzi huo.
Nigeria peke yake ina wanajeshi 135,000 kwa mujibu wa orodha ya Global Fire Power, na Niger ina takriban wanajeshi takriban 10,000 lakini hilo bila shaka halimaanishi kwamba uvamizi wa kijeshi utakuwa rahisi. Suluhu ya amani bila shaka ndio inayopendelewa kwa pande zote lakini Ecowas ina hamu kujidhihirisha kutokana na kushindwa kuzuia mapinduzi kadhaa katika eneo hilo katika miaka mitatu iliopita.













