Mapinduzi ya Niger mtihani wa demokrasia Afrika Magharibi

- Author, Yusuf Akinpelu
- Nafasi, Mwandishi
- Akiripoti kutoka, BBC
Rais Bola Tinubu, ambaye anaongoza Nigeria yenye nguvu ya kikanda, anayachukulia mapinduzi ya kuvuka mpaka wa Niger kama jaribio la demokrasia katika Afrika Magharibi.
Baada ya kushika uenyekiti wa kambi ya kanda ya Ecowas wiki tatu tu zilizopita, alikabiliwa na changamoto kubwa ya sera ya kigeni wakati jeshi lilipotwaa mamlaka nchini Niger, mshirika wa kimkakati katika mapambano dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu wanaofanya uharibifu katika sehemu kubwa ya Afrika Magharibi.
Bw Tinubu alikuwa ameelezea wasiwasi wake kuhusu mapinduzi ya Burkina Faso, Mali na Guinea alipochukua kiti cha urais wa Nigeria mwezi Mei, akisema Ecowas inahitaji kuimarisha kikosi chake cha kikanda ili kuzuia mapinduzi zaidi, na kupambana na wanamgambo.
Hivyo wakati Rais wa Niger Mohamed Bazoum alipopinduliwa na walinzi wake wiki iliyopita, alijibu haraka kwa kuitisha mkutano wa kilele wa viongozi wa Afrika Magharibi katika jumba lake la rais siku ya Jumapili.
Umoja wa kanda ulitoa uamuzi wa mwisho kwa serikali ya Niger, kurudisha madaraka kwa rais aliyechaguliwa ndani ya wiki moja au Ecowas itachukua "hatua zote muhimu kurejesha utaratibu wa kikatiba".
"Hatua hizo zinaweza kujumuisha matumizi ya nguvu" na wakuu wa kijeshi walipaswa kukutana "mara moja", taarifa yao iliongeza.
Ingawa ushindi wa Bw Tinubu katika uchaguzi wa urais wa Februari unapingwa mahakamani na wagombea wa upinzani wanaodai kuwa matokeo yalichakachuliwa, anajifanya kuwa mwanademokrasia ambaye alishiriki katika kampeni dhidi ya utawala wa kijeshi nchini Nigeria katika miaka ya 1980.

"Nadhani anaona [mapinduzi] haya kama dharau kwa sifa zake za kidemokrasia, hasa wakati anashikilia uenyekiti wa Ecowas," alisema Wole Ojewale, mchambuzi wa Nigeria katika Taasisi ya Mafunzo ya Usalama (ISS).
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Muhimu zaidi, mapinduzi yana athari ya moja kwa moja kwa Nigeria. Nchi hizo mbili zina mpaka unaoenea kwa zaidi ya kilomita 1,500 (maili 930), na zina uhusiano mkubwa wa kitamaduni na kibiashara ambao ulianza enzi ya kabla ya ukoloni wakati sehemu ndogo ya zote mbili zilikuwa sehemu ya ukhalifa wa Sokoto.
Kundi la wapiganaji wa Kiislamu la Boko Haram limefanya mashambulizi katika nchi zote mbili, huku kikosi cha kijeshi kinachoundwa na wanajeshi kutoka Nigeria, Niger, Chad na Cameroon kikipigana nao. "Washirika wa kimkakati na kiufundi" wa kikosi hicho ni pamoja na Uingereza, Marekani na Ufaransa, huku wawili wa mwisho wakiwa na kambi za kijeshi nchini Niger.
Wakati Niger ilichangia takribani 4% ya pato la uranium duniani mwaka 2022, ni nchi ya saba duniani kwa uzalishaji wa uranium na ina madini ya uranium ya daraja la juu zaidi barani Afrika.
Si Ecowas wala washirika wake wa Magharibi ambao wangetaka nyenzo za mionzi zinazotumiwa katika mazingira ya kiraia na kijeshi kuanguka katika mikono isiyo sahihi katika eneo ambalo wanamgambo wa Kiislamu wanafanya kazi na Urusi na kundi la mamluki la Wagner wanapanua ushawishi wao.

Chanzo cha picha, Getty Images
Baada ya mapinduzi yao, Mali na Burkina Faso ziliielekea Urusi, huku jeshi la serikali nchini Niger likitoa hisia kwamba linaweza kuelekea upande mmoja.
Kiongozi wa Chad Mahamat Idriss Déby Itno ambaye aliwekwa madarakani na jeshi lake mwenyewe baada ya baba yake kuuawa na vikosi vya waasi mwaka 2021, alikwenda Niger siku ya Jumapili kuwataka watawala kutii kauli ya Ecowas.
Chad si mwanachama wa jumuiya ya kikanda, lakini Bw Déby alihudhuria mkutano wake mapema Jumapili. Kama mwanajeshi hodari, alionekana kama mtu anayefaa kufanya urafiki na viongozi wa mapinduzi na kuwataka waondoke madarakani.
Lakini junta hadi sasa imekataa.
Badala yake, imeongeza maneno yake dhidi ya nchi za Magharibi na Ecowas, na maelfu ya wafuasi wake waliingia katika mitaa ya mji mkuu wa Niger, Niamey, siku ya Jumapili kuunga mkono mapinduzi hayo.
Baadhi yao walishambulia ubalozi wa Ufaransa na kupeperusha bendera za Urusi.
Lakini haijulikani kama unyakuzi wa kijeshi unaungwa mkono na watu wengi nchini Niger, zaidi ya nusu ya raia wake waliridhishwa na jinsi demokrasia ilivyofanya kazi katika nchi yao, kulingana na utafiti wa mwaka 2022 wa kikundi cha utafiti kinachoheshimika cha Afrobarometer.
Ni Tanzania, Zambia, Sierra Leone na Mauritania pekee ndizo zilizopata idhini bora ya kidemokrasia kati ya nchi 36 za Afrika zilizofanyiwa utafiti.
Hata hivyo, thuluthi mbili ya waliohojiwa walisema kuwa wanajeshi wanaweza kuingilia kati viongozi waliochaguliwa wakitumia mamlaka vibaya. Hii ni hoja ambayo wale wanaofanya mapinduzi, pamoja na wafuasi wao, mara nyingi hutoa ili kuhalalisha matendo yao.
Wanajeshi nchini Mali na Burkina Faso wameionya Ecowas dhidi ya kuingilia kijeshi nchini Niger, wakisema itakuwa "tangazo la vita" na watakwenda kuwatetea viongozi wenzao wa mapinduzi. Kwa hivyo uingiliaji kati wa kijeshi unahatarisha uwepo wa mzozo kamili.
Hata hivyo, Ecowas hapo awali ilituma wanajeshi katika nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na Liberia, Sierra Leone, Guinea-Bissau na Gambia ama kusaidia kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe, kuwarejesha madarakani marais waliong'olewa madarakani au kuwafukuza nje viongozi waliokataa kukubali kushindwa katika uchaguzi.
Uingiliaji kati huu ulikuwa kwa mujibu wa mamlaka yake ya kudumisha "amani, utulivu na usalama ndani ya eneo", ingawa askari wake pia walishutumiwa katika baadhi ya matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Bw Ojewale hana uhakika kama jumuiya hiyo ina uwezo wa kijeshi kuingilia kati nchini Niger, nchi kame kwenye ukingo wa Jangwa la Sahara, hasa wakati nchi nyingi zinazounda jumuiya hiyo, ikiwa ni pamoja na Nigeria, zinakabiliwa na changamoto zao za usalama.
"Rasilimali kidogo walizonazo zinaweza kupunguzwa," alisema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mchambuzi huyo anaamini kuwa mzozo kati ya pande mbili "unaweza usipate suluhu", na kuzidisha mzozo wa kibinadamu katika eneo hilo.
"Kungekuwa na majeruhi kwani kungekuwa na watu walionaswa kwenye mapigano," alisema, akiongeza kuwa utatuzi wa kidiplomasia wa mgogoro huo ungekuwa bora zaidi.
Pia kuna maswali kuhusu usalama wa rais aliyepinduliwa, ambaye anashikiliwa na jeshi la serikali. Mchambuzi mwingine, Jaafar Abubakar, anahoji kuwa anaweza kuwa "mwenye mazungumzo" katika tukio la makabiliano ya kijeshi kati ya Ecowas na junta.
"Ni kwa manufaa [ya junta] kumuweka [Bw Bazoum] hai na mzima," alisema. "Ikiwa watamwua, wanakuwa waasi wasio na aina yoyote ya uhalali."















