Arteta anasema ubingwa bado 'unawezekana' - lakini Arsenal ina nafasi gani?

"Katika soka kila wakati kuna uwezekano."

Hayo yalikuwa maneno ya mkufunzi wa Arsenal Mikel Arteta baada ya ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya Manchester United kuwarudisha kileleni mwa jedwali la Ligi ya Premia na kuweka kimyang’anyiro cha kuwania taji hilo kuelekea wiki ya mwisho ya msimu.

The Gunners sasa wako pointi moja mbele ya Manchester City wanaoshika nafasi ya pili, ingawa vijana wa Pep Guardiola wana mchezo mmoja mkononi dhidi ya Tottenham siku ya Jumanne.

Kwa vyovyote vile matokeo ya mchezo huo kwenye Uwanja wa Tottenham Hotspur, ushindi wa Arsenal katika uwanja wa Old Trafford unahakikisha vita vya kuwania taji hilo vitafikia hadi siku ya mwisho.

"Leo tulitaka kufungua lango hilo," Arteta aliambia Sky Sports. "Mbele ya watu wetu tuishi moja ya siku nzuri zaidi ambazo tumeishi pamoja.

"Tutakuwa tumekaa tukitazama mechi hiyo [kati ya Tottenham na Manchester City] na ni kweli tunahitaji matokeo ili kafikia lengo letu.

Ikiwa timu zitakuwa sawa baada ya mechi 38, taji litaamuliwa kwa tofauti ya mabao na ikiwa bado ni sawa, litaamuliwa kupitia kupitia mabao yaliofungwa.

Je, takwimu zinasemaje kuhusu nafasi ya Arsenal?

Kulingana na Opta, nafasi ya Arsenal kushinda Ligi ya Premia sasa iko 41.3%, huku Manchester City ikisalia na 58.7%.

The Gunners walikuwa na nafasi ya chini ya 23.6% tu kabla ya mechi ya Jumapili - na baada ya City kushinda 4-0 dhidi ya Fulham - Walidhihirisha umuhimu wa ushindi wao dhidi ya United.

Arsenal watawakaribisha Everton siku ya mwisho ya msimu na City watakuwa nyumbani kumenyana na West Ham (wote Jumapili, 19 Mei saa kumi na mbili saa za Afrika Mashariki).

Hata hivyo, onyo ni kwamba - hakuna timu katika historia ya Ligi Kuu ambayo imewahi kuanza siku ya mwisho katika nafasi ya pili na kushinda taji.

Hilo linawaacha Arsenal katika hali ya kushangaza ya kushangilia wapinzani wao wakubwa Spurs watakapomenyana na mabingwa hao watetezi Jumanne.

Kama mshambulizi wa The Gunners, Kai Havertz alivyosema: "Nitakuwa shabiki mkubwa zaidi wa Tottenham ! Hebu tuwe na tumaini."

Wadadisi wanafikiria nini?

Kiungo wa kati wa zamani wa Manchester United Roy Keane anasema "haoni Manchester City ikizuiwa sasa" licha ya Arsenal kuwasukuma.

"Nilihoji Manchester City wiki nne au tano zilizopita, nikifikiri kwamba sina uhakika kabisa wanaweza kusinda taji," alisema kwenye Sky Sports.

"Lakini katika wiki chache zilizopita sijui kwa nini niliwatilia shaka.

"Hata jana ugenini kwa Fulham, ulikuwa mchezo rahisi na walishinda kwa mabao manne."

Mchambuzi mwenzake na mchezaji wa zamani wa Arsenal Paul Merson anaamini mengi yataambatana na matokeo ya Aston Villa dhidi ya Liverpool siku ya Jumatatu, huku Villa wakichuana na Tottenham kuwania nafasi ya nne.

Ikiwa Villa itashindwa kuilaza Liverpool, Spurs bado watakuwa na nafasi ya kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa - lakini tu iwapo wataifunga City.

"Ikiwa Liverpool wanaweza kuifunga Villa basi hiyo itaifanya Tottenham kuwa na njaa siku ya Jumanne," alisema. "Kila shabiki wa Tottenham atakuwa akiishangilia Liverpool."

Lakini ikiwa Villa itafanikiwa kushinda? "Wao [Tottenham] hawataki Arsenal kushinda ligi. Itafikia hatua ambayo mashabiki wa Tottenham watashangilia ikiwa Manchester City watafunga."

Je, yote yalianzaje mwaka jana?

Sare tatu mfululizo mnamo Aprili 2023 ziliigharimu Arsenal wakati Manchester City iliposhinda taji la msimu uliopita, huku uwezekano wa The Gunners kuwa mabingwa ukididimia.

Je, ikiwa timu zitamaliza kwa pointi sawa?

Iwapo kutakuwa na sare, ligi inaamuliwa kwa tofauti ya mabao, kisha mabao yaliofungwa, kisha pointi nyingi katika mechi za ana kwa ana, kisha mabao mengi ya ugenini katika rekodi ya ana kwa ana.

Chochote kile, usishangae ikiwa kutakuwa na misukosuko na mabadiliko kati ya sasa na siku ya mwisho ya msimu tarehe 19 Mei.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla