Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wachezaji sita wa Uingereza wanaoweza kuuzwa kwa faida kubwa
Wahasibu wa vilabu vya Premier League hufurahi kuwauza wachezaji – na kuzalisha faida nzuri - na kusaidia kufuata sheria kali za kifedha.
Everton, Nottingham Forest na Leicester zote zimekumbwa na ukiukaji wa kanuni za fedha huku vilabu kama Chelsea, Tottenham, Aston Villa, Newcastle na Wolves zikiwa zimepata hasara kubwa katika akaunti zao za hivi karibuni.
Baada ya mhitimu wa akademi ya Manchester City, Cole Palmer kuondoka kwenda Chelsea kwa dili la kushangaza la pauni milioni 42.5 msimu uliopita wa joto. Je, tunaweza kuona msururu wa uhamisho kama huu msimu huu wa joto?
Conor Gallagher
Conor Gallagher ana umri wa miaka 24, kiungo wa kati wa Chelsea. Mkataba wake wa mwaka mmoja unamaliza mwishoni mwa msimu. Sokoni anakadiriwa kuwa na thamani ya pauni milioni 68. Anahusishwa na Tottenham.
Kabla ya Cole Palmer kuchukua nafasi ya katikati, inaweza kusema alikuwa ni mchezaji bora wa Chelsea kwa msimu.
Gallagher amechukua nafasi ya nahodha na amekuwa akisifiwa mara kwa mara na meneja Mauricio Pochettino katika msimu huu.
Uchezaji wa Gallagher umewavutia viongozi waandamizi wa klabu hiyo, hasa ikizingatiwa uwekezaji ambao umefanywa katika nafasi anayocheza kwa kumsajili Enzo Fernandez kwa pauni milioni 106 na dili lenye thamani ya pauni milioni 115 kwa Moises Caicedo.
Mazungumzo kati ya klabu hiyo na wakala wa Gallagher yamekuwa yakiendelea na Gallagher ana furaha klabuni hapo, lakini inafahamika ikiwa ofa ya bei inayostahili itatolewa, Chelsea watakuwa tayari kumuuza.
Marcus Rashford
Marcus Rashford, 26, mshambuliaji wa Manchester United. Alisaini mkataba wa miaka mitano hadi 2028 msimu uliopita. Thamani yake sokoni ikakadiriwa kuwa pauni milioni 85. Anahusishwa kuhamia Paris St-Germain.
Manchester United wako tayari wako wazi kuuza takribani mchezaji yoyote katika msimu huu wa joto, akiwemo Marcus Rashford .
Kampeni ya mwaka jana ya mabao 30 ndiyo iliyomletea mafanikio zaidi, ikifuatiwa na mabao manane pekee msimu huu.
Ana kasi na nguvu ya kumaliza ambayo hutishia mabeki wa timu pinzani. Lakini mara nyingi kiwango chake cha uchezaji hushuka.
Kama mmoja wa wachezaji wanaopata pesa nyingi zaidi United, kiuhalisia soko la Rashford ni dogo. Inaonekana kuna uwezekano mkubwa atabaki Old Trafford.
Evan Ferguson
Evan Ferguson, 19, mchezaji wa mbele wa Brighton. Alitia saini mkataba mpya mwaka jana ambao utakamilika 2029. Thamani yake sokoni inakadiriwa kuwa ni pauni milioni 68. Anahusishwa na Arsenal na Chelsea.
Evan Ferguson alivutia vilabu vingi vilivyoongoza msimu uliopita, alipoteuliwa kuwania tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa PFA.
Ulikuwa msimu wa mafanikio kwa mchezaji wa kimataifa wa Jamhuri ya Ireland huku Brighton ikifuzu kucheza kombea la Ulaya kwa mara ya kwanza.
Amefunga mabao sita pekee msimu huu, matatu kati ya hayo aliifunga Newcastle 2 Septemba na safari yake imesita kwa jeraha la kifundo cha mguu.
Hata hivyo, bado anavutia na klabu zote zinazoongoza zinatafuta washambuliaji. Swali kubwa ni, Brighton itakuwa tayari kumuuza ikiwa ada itakuwa nzuri?
Kiernan Dewsbury-Hall
Kiernan Dewsbury-Hall, 25, kiungo wa kati wa Leicester. Ana mkataba hadi 2027. Thamani yake inakadiriwa kuwa pauni milioni 35 sokoni. Anahusishwa kuhamia Brentford, Brighton na Fulham.
Brighton walihusishwa pakubwa kutaka kumnunua Kiernan Dewsbury-Hall mwezi Januari lakini Leicester walishikilia msimamo na kukataa kumuuza walipokuwa wakitafuta kurejea Ligi Kuu.
Uhamisho wa Alex Scott wa pauni milioni 25 kwenda Bournemouth kutoka Bristol City mwaka 2023 na uhamisho wa Adam Wharton wa pauni milioni 22 kutoka Blackburn hadi Crystal Palace mwezi Januari huenda ukawa ndio viwango vya chini zaidi - lakini kwa kuwa Dewsbury-Hall ana uzoefu wa Ligi Kuu ya Uingereza, Leicester huenda ikahitaji pesa zaidi.
Amefunga mabao 12 katika mechi 44 na kuisaidia Foxes kushinda taji la Ubingwa na kurudi mara moja kwenye ligi kuu.
Klabu hiyo ilirekodi hasara ya pauni milioni 89 mwaka 2022-23 na tayari imeshtakiwa kwa ukiukaji wa kanuni za faida na uendelevu.
Watahitaji kuwauza wachezaji kabla ya tarehe 30 Juni ili kujaribu kuzuia kutozwa faini mara ya pili 2023-2024 na Dewsbury-Hall ndiyo atatoa faida nyingi zaidi.
Kuhusu mchezaji bora wa mwaka katika tuzo za Leicester za mwisho wa msimu siku ya Jumanne, Dewsbury-Hall alisema: "Nimekuwa katika klabu hii tangu nikiwa na umri wa miaka minane. Sina nia ya kuondoka."
Jarrad Branthwaite
Jarrad Branthwaite, 21, mlinzi wa Everton. Alisaini mkataba mpya mwezi Oktoba hadi 2027. Thamani yake sokoni inakadiriwa kuwa pauni milioni 43. Anahusishwa kuhamia Manchester United.
Jarrad Branthwaite alikuwa akiichezea Carlisle United katika Ligi ya Pili akiwa na umri wa miaka 17, kabla ya Everton kulipa pauni milioni 1 na kuanza kumkuza katika kikosi chao cha chini ya miaka 23.
Amekuwa muhimu katika katika msimu mwingine wenye misukosuko kwa Everton kwa kuonyesha utulivu kwenye safu ya ulinzi na kumfanya kuitwa katika kikosi cha England mara kwa mara.
Beki huyo wa kati mwenye kasi na mahiri ameunda ushirikiano mzuri na nahodha James Tarkowski katika kikosi ambacho kimecheza mechi 12 bila kufungwa msimu huu.
Kwa uchezaji wake wa kuvutia kufikia sasa, Branthwaite atalenga kuwa katika kikosi cha wachezaji 26 cha Gareth Southgate na atakuwa katika nafasi ya kuwania mchezaji bora wa Everton.
Jacob Ramsey
Jacob Ramsey, 22, kiungo wa kati wa Aston Villa. Ana mkataba hadi 2027. Thamani yake sokoni inakadiriwa kuwa pauni milioni 34. Anahusishwa kuhamia Newcastle, Bayern Munich au Tottenham.
Jacob Ramsey alishinda tuzo ya akademi ya Ligi ya Kuu ya Uingereza, msimu uliopita baada ya kufunga mabao sita katika michezo 38, na kuisaidia Villa kurejea katika ligi ya Ulaya.
Lakini alivunjika uti wa mgongo, jeraha ambalo limemzuia kurudi Ligi Kuu. Villa wamesisitiza hauzwi huku meneja Unai Emery akiweka wazi msimamo wake mwezi Januari.
Emery alisema: "Katika sehemu ya pili ya msimu atakuwa muhimu sana kwetu. Uwezo wake ni wa juu sana, na kiwango cha juu zaidi kuliko matarajio yangu."
Hata hivyo, kumuuza mchezaji huyo kungesaidia klabu katika juhudi zao za kufuata faida baada ya kupoteza pauni milioni 119.6 mwaka unaoishia Mei 31, 2023.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah