Mambo matano yatakayoathiri vita vya Ukraine 2024

    • Author, Halyna Korba & Kateryna Khinkulova
    • Nafasi, BBC World Service

Baada ya kutawala vichwa vya habari kimataifa kwa karibu miaka miwili, vita nchini Ukraine vitaendelea mwaka 2024. Lakini kuna uwezekano vitaendelea kwa namna tofauti.

Hapa kuna mambo matano ambayo yataathiri vita hivi 2024.

Fedha

Uwezo wa Ukraine wa kupinga uvamizi wa Urusi mwanzoni mwa mwezi Februari 2022 uliwashangaza wengi, kwa sababu washirika wa kimataifa wa nchi hiyo walitoa silaha nyingi.

2024 hili linaweza kubadilika, kwani baadhi ya misaada imesitishwa.

Misaada ya Marekani kwa Ukraine inahitaji kupigiwa kura katika Bunge la Congress na huhusisha mijadala mikali kati ya Republican na Democrats. Msaada wa kijeshi wenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 61 utapitiwa tena mwanzoni mwa Januari.

Katika Umoja wa Ulaya, msaada wa kifedha wenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 55 pia umeingia katika mvutano kati ya mmoja wa wanachama wa EU, Hungary, na muungano huo.

Hungary inaegemea upande wa Urusi, tofauti na mataifa mengine ya EU, na inataka msaada kwa Ukraine usitishwe kabisa.

Pia Unaweza Kusoma

Silaha

Kucheleweshwa kwa utoaji wa misaada kunapunguza kasi ya Ukraine ya kusambaza silaha kwa jeshi lake, na kusababisha wasiwasi mkubwa kwa Kyiv na Moscow inazidi kujiamini.

Katika mkutano wake wa mwisho wa mwaka na waandishi wa habari, Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema jeshi la nchi yake linazidi kuimarika na kile alichokitaja kama silaha za bure kwa Kyiv kutoka nchi za Magharibi zinaelekea kuisha hivi karibuni.

Katika mazungumzo yake ya mwisho wa mwaka na vyombo vya habari, Rais Volodymyr Zelensky alikiri hali ni ngumu lakini akaeleza matumaini yake kwamba suala la msaada wa kijeshi litatatuliwa hivi karibuni na Ukraine itaweza kuongeza uzalishaji wake wa ndege zisizo na rubani, jambo ambalo limeonekana kuwa muhimu katika vita hivi.

Mwezi Novemba, EU iliripoti kwamba haitafikia lengo lake la kusambaza makombora milioni 155 kwa Ukraine ifikapo Machi 2024. Rais Zelensky alisema moja ya sababu za mashambulio ya Ukraine kutoanza mapema ni ukosefu wa silaha.

Katika mahojiano ya hivi karibuni na BBC, wanajeshi wa Ukraine walisema wanalazimika kupunguza matumizi ya makombora. Kuwa na silaha kidogo itamaanisha kuwa Ukraine italazimika kuondoka katika maeneo na ardhi zao. Hivi sasa Urusi inadhibiti karibu 17% ya eneo la Ukraine.

Ukraine inakadiria kuwa vita hivyo vimeugharimu uchumi wake dola bilioni 150. 2024 inapanga kutumia dola bilioni 43.2 kwa jeshi. Bajeti ya kijeshi ya Urusi inakadiriwa itapanda hadi dola bilioni 112.

Pia Unaweza Kusoma

Watu

Kuwa na askari wa kutosha itakuwa changamoto kwa pande zote mbili. Kabla ya Februari 2022, idadi ya watu wa Ukraine ilikuwa watu milioni 44.

Raia milioni sita wa Ukraine wanakadiriwa kukimbia nchini hiyo – ingawa wengi wanaaminika kurejea. Maelfu ya wengine wamelazimika kuyahama makazi yao ndani kutokana na uvamizi wa Urusi na mashambulizi ya mara kwa mara. Na Maelfu ya raia wengine wameuawa.

Kuleta na kufundisha vikosi vipya itakuwa changamoto. Chini ya sheria ya kijeshi, Ukraine imepiga marufuku wanaume wenye umri wa miaka 18 hadi 60 kuondoka nchini humo.

Hivi karibuni, Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Rustem Umerov alisema Kyiv itahitaji kuwaomba wanaume wa Ukraine wanaoishi nje kurudi kujiunga na jeshi.

Maelfu ya wanaume wa Ukraine walio katika umri wa kupigana wanaaminika kuishi nje ya nchi. Estonia tayari imesema itasaidia Kyiv katika kuandaa raia wa Ukraine wanaofaa kwa jeshi, ambao kwa sasa wanaishi Estonia.

Wakati Urusi ina jeshi kubwa zaidi na idadi kubwa ya watu karibu watu milioni 144. Nayo imepata hasara kubwa katika miaka miwili ya vita. Wanajeshi wake wengi waliopata mafunzo bora wameuawa. Pia askari wa miavuli na wahudumu wa jeshi la anga, mafunzo yao ni ya gharama kubwa na huchukua miaka mingi.

Takribani Warusi milioni moja wanakadiriwa kuondoka nchini humo kufuatia uvamizi wa Ukraine na tangazo la kutaka raia wajiunge na jeshi. Urusi vilevile iliamua kuajiri wafungwa na wahamiaji wasio na hati ili kujaza jeshi lake.

Hasara za kijeshi hazijafichuliwa kikamilifu na pande zote mbili lakini inakadiriwa kuwa maelfu ya wanajeshi wameuawa kwa upande wa Ukraine.

Kwa upande wa Urusi, BBC ilikusanya orodha ya wanajeshi waliothibitishwa kuuawa, hadi mwishoni mwa Disemba 2023 – idadi ilikuwa zaidi ya 40,000.

Ujasusi wa Marekani hivi karibuni ulifichua ripoti inayoeleza kwamba hasara ya Urusi, kwa waliouawa au kujeruhiwa, inafikia 315,000.

Kuichoka Ukraine

Kinachosumbua zaidi Kyiv ni kile kinachojulikana kama "kuichoka Ukraine" - kupungua huruma na kuungwa mkono kutoka kwa umma katika nchi washirika.

Chaguzi za hivi karibuni nchini Uholanzi na Slovakia tayari zimesababisha kupungua kwa uungwaji mkono. Slovakia imesimamisha msaada mkubwa kwa Ukraine, wakati Uholanzi huenda isitume ndege za F-16 zilizoahidiwa kwa muda mrefu.

Uchaguzi wa Novemba 2024 nchini Marekani; ikiwa Donald Trump atarejea Ikulu kunaweza kutokea mabadiliko makubwa ya sera kuelekea Ukraine na Urusi.

Kura za maoni nchini Marekani zinaonyesha idadi ya wanaoamini kuwa Washington inaisaidia Ukraine kupita kiasi imeongezeka kutoka 21% hadi 41%. EU, katika nchi nane kati ya 27, watu wengi wanapinga kutoa msaada kwa Ukraine.

Ukraine na Urusi zitaendelea kutafuta uungwaji mkono Kusini mwa Ulimwengu mwaka mpya ujao. Nchi nyingi za Mashariki ya Kati, Amerika ya Kusini na Afrika zina urafiki na Moscow, katika upinzani dhidi ya Marekani. Tangu kuanza kwa uvamizi, Urusi ilijaribu kuimarisha uhusiano wake, wakati Ukraine ilifanya kazi ya kutafuta uungwaji mkono.

Katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov alikwenda Afrika mara nne, akizuru nchi 14. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba alitembelea nchi tisa katika ziara mbili barani Afrika katika muda huo huo.

Ukraine itajitahidi kukabiliana na ushawishi wa Urusi barani Afrika ambapo propaganda za Moscow katika baadhi ya nchi na kundi la mamluki la Wagner zimekuwa na manufaa katika kuimarisha ushawishi wa Urusi.

Mwisho wa Vita

"Vita hivi vitaisha vipi?" ndilo swali ambalo wanasiasa na wataalamu wengi wamekuwa wakijaribu kulijibu.

Ukraine inasema; ukombozi kamili kutokana na uvamizi wa Urusi na kurejea kwenye mipaka inayotambulika kimataifa ndiyo utakaomaliza mzozo huu.

Urusi inasema iko katika mzozo mkubwa na nchi za Magharibi na itapigana kwa muda mrefu iwezekanavyo.

Huenda 2024 ukawa sio mwisho wa vita hivi. Yumkini kutaendelea kuwepo - hasara zaidi, vifo vya kila siku na uharibifu nchini Ukraine. Na Urusi itazidi kutengwa na nchi za Magharibi na kuathirika zaidi kiuchumi.

Pia Unaweza Kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Lizzy Masinga