Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: Hakuna matokeo ya haraka katika mashambulizi, anasema Jenerali Syrskyi
"Tungependa kupata matokeo ya haraka sana, lakini kwa kweli haiwezekani," anasema mwanamume anayesimamia mashambulizi mapya ya Ukraine katika mashariki.
Tunakutana na Jenerali Oleksandr Syrskyi mahali pa siri kando ya gari analotumia kuwatembelea wanajeshi wake na kufuatilia vita. Juu ya gari kuna ni bunduki kubwa. Ndani ya gari, televisheni kubwa inayoonesha maeneo ya vita kutoka katika ndege zisizo na rubani.
Mtafute Jenerali Syrskyi mtandaoni na utamwona akielezwa kama "jenerali aliyefanikiwa zaidi hadi sasa kwa Karne ya 21."
Aliongoza ulinzi wa Kyiv mwanzoni mwa uvamizi wa Urusi mwaka jana. Alikuwa mpangaji mkuu wa mashambulio ya kushtukiza ya Ukraine na kufanikiwa kujibu mapigo huko Kharkiv wakati wa kipindi cha majira ya joto. Sasa, yeye ndiye mkuu wa operesheni za kijeshi mashariki mwa Ukraine.
Tunatazama mashamba yenye makovu mengi ya vita katika mji wa Bakhmut, ambapo baadhi ya wanajeshi wake wanajaribu kuyachukua tena maeneo. Namuuliza ikwa lengo lake ni kuuteka tena mji? Anatabasamu na kusema: "Ndiyo, bila shaka. Ninajaribu kufanya hivyo."
Lakini hata yeye anakiri kwamba, zaidi ya mwezi mmoja tangu kuanza, mashambulizi ya Ukraine yaliyosubiriwa kwa muda mrefu yanakwenda polepole kuliko wengi walivyotarajia.
Anasema mashariki, sawa na kusini, eneo hilo limejaa mabomu ya ardhini na vizuizi vya ulinzi. Anasema, Warusi wana ngome nyingi: "Kwa hivyo, maendeleo yetu hayaendi haraka kama tunavyotamani."
Lakini Jenerali Syrskyi anaamini Ukraine bado ina faida moja ya kipekee.
"Ninaamini umoja katika uongozi wetu wa kijeshi na kuaminiana kwa askari wetu ni faida muhimu kwa jeshi letu."
Hiyo ni kinyume kabisa na uongozi wa kijeshi wa Urusi, ambao unaonekana kukumbwa na malumbano, huku maafisa wakuu wakiondolewa kwenye uongozi.
Jenerali Syrskyi anapendwa na wale walio karibu naye, ambao wanapenda kujitolea kwake, uamuzi wake na ujanja. Analala kwa saa nne na nusu tu usiku.
Kusini na kaskazini mwa Bakhmut, Ukraine inasema imechukua tena karibu kilomita za mraba 30 (kama maili za mraba 12) kutoka kwa Warusi.
Kwake kuikamata tena Bakhmut ni "jambo la heshima." "Tulipoteza ndugu zetu wengi, wanajeshi wetu, tulipokuwa tukiitetea Bakhmut, kwa hiyo inatubidi tu kuirejesha."
Naibu waziri wa ulinzi wa Ukraine, Hanna Maliar, alituambia - majeshi ya Urusi katika mji huo watazingizrwa hivi karibuni. Lakini mizinga bado ilikuwa ikinyesha kwenye eneo la Ukraine tuliyotembelea kilomita 3 tu kutoka jijini.
Alex, mmoja wa askari kutoka Brigedi ya 57 ya Ukraine, anaelezea hali ni mbaya. Anaonyesha shimo kubwa iliyoundwa na kombora la kivita la Urusi lililopiga mapema asubuhi hiyo. Ilitua mita chache tu kutoka kwenye mtaro wake. Muda mfupi baadaye, sisi pia tulilazimika kukimbilia mahali pa kujificha.
Mbali na mashambulizi ya makombora, makamanda katika chumba kirefu cha chini ya ardhi wanaratibu juhudi za kuikamata tena Bakhmut. Miezi miwili iliyopita, nilipokuwa hapa mara ya mwisho, wanajeshi wa Ukraine walikuwa wakipoteza mwelekeo na walikuwa hatarini kuzingirwa. Sasa, meza zimegeuka.
Kanali Oleksandr Bakulin, kamanda wa Brigedi ya 57, ananiambia sasa ni Warusi ambao wako taabani.
Anasema hamdharau adui yake, lakini wanajeshi wa kawaida wa Urusi anaokabiliana nao sasa si kama mamluki wa Wagner wa Yevgeny Prigozhin ambao waliuteka mji huo mapema mwaka huu.
Wagner, anasema, "walikuwa maadui hatari, walikuwa wakiua kwa ajili ya kuua".
"Ikiwa tutaweka juhudi kidogo, Bakhmut inaweza kuzingirwa," Kanali Bakulin anasema. Pia anasema waathiriwa katika vita hivyo ni wachache kuliko wakati ule wa kuutetea mji. Kusonga mbele, ingawa ni polepole, kumeongeza ari.
Kwa mara ya kwanza upande wa mashariki, idadi ya wanajeshi wa Ukraine sasa inalingana na ile ya wanajeshi wa Urusi - karibu 160,000. Walakini, Ukraine bado inazidiwa na mizinga ya Kirusi.
Je, mienendo inaweza kubadilika kwa kuwasili silaha zinazotolewa na Marekani, ambazo zina mabomu yanayoweza kushambulia katika eneo kubwa zaidi? Zaidi ya nchi mia moja zimepiga marufuku mabomu hayo.
Kanali Bakulin anasema wanahitajika "kuleta uharibifu mkubwa kwa wanajeshi wa ardhini wa Urusi". "Kadiri askari wa miguu wanavyokufa, ndivyo jamaa zao huko Urusi wanavyoiuliza serikali yao 'kwanini?'
Lakini, anaongeza: "Siwezi kusema mabomu hayo yatatatua matatizo yetu yote kwenye uwanja wa vita."
Pia anakubali silaha hizo zina utata: "Ikiwa Warusi hawakuzitumia, labda sisi tutazitumia."
Jenerali Syrskyi alithibitisha kuwa mabomu ya vishada ya Marekani sasa yamewasili Ukraine na yatakuwa tayari kutumika ndani ya siku chache. Tuliona jinsi ndege za M777 zinazotolewa na Marekani, ambazo zitarusha makombora, zikiwa tayari karibu na Bakhmut.
Jenerali huyo anasema kukamatwa tena kwa jiji hilo kutakuwa na thamani kubwa. Anasema Bakhmut. Pia, jiji hilo lina umuhimu wa kimkakati - kama lango la miji mingine muhimu katika kanda.
Lakini, anasema: "Watu wetu wanasubiri ushindi. Wanahitaji ushindi."