Wagner kusitisha kuajiri wapiganaji wapya ikijielekeza zaidi Afrika na Belarusi - Prigozhin

Mkuu wa kundi la mamluki la Wagner la Urusi, anasema kundi hilo litaendelea na shughuli zake barani Afrika na nchini Belarus, n kwa kwa sasa halitaajiri wapiganaji wapya.

Yevgeny Prigozhin, alikuwa akizungumzia mustakabali na malengo yajayo ya kundi hilo, katika ujumbe wa sauti uliochapishwa kwenye akaunti ya Telegram yenye mahusiano na Wagner.

Wapiganaji wa Wagner wamekuwa na jukumu muhimu wakati wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Mnamo Juni, maelfu kadhaa kati ya wapiganaji hao walishiriki katika maasi ya muda mfupi ya kujaribu kupindua uongozi wa kijeshi wa Urusi.

Katika ujumbe wake wa sauti, Bw Prigozhin alisema wapiganaji wengi wa Wagner kwa sasa wako likizo, kwa sababu "kabla ya hapo kulikuwa na kipindi kirefu cha kazi ngumu sana".

Alisema kundi hilo limeshafanya maamuzi ya shughuli zake za siku zijazo, ambazo "zitatekelezwa kwa ajili ya Urusi".

Kundi hilo litaendelea "kufanya kazi barani Afrika na katika vituo vya mafunzo huko Belarus", aliongeza katika ujumbe wake - ambao ulichapishwa kwenye akaunti ya Gray Zone.

Hakutoa maelezo zaidi, ingawa Wagner inajulikana kuwa inaendelea kuwajibika katika sehemu nyingi za Afrika. Wapiganaji wake pia wamekuwa Belarus kufundisha vikosi vya ulinzi wa eneo hilo.

"Ingawa hatuna upungufu wowote wa wafanyakazi, hatuna mpango wa kuajiri wapya," Bw Prigozhin alisema. "Hata hivyo, tutashukuru sana ikiwa utaendelea kuwasiliana nasi, na mara tu nchi yetu mama (Urusi) itakapohitaji kikundi kipya ambacho kitaweza kulinda masilahi ya nchi yetu, hakika tutaanza kuajiri."

Aliongeza kuwa hakuna vikwazo vilivyowekwa kwa wapiganaji wake kuhamia kwenye "majeshi mengine" ya Urusi, na "kwa bahati mbaya, wengine" walikubali kufanya hivyo.

Baada ya kushindwa kwa uasi wa Wagner tarehe 24 Juni, Rais Vladimir Putin aliwaalika wapiganaji kutoka kundi hilo ambao hawakushiriki katika uasi huo kutia saini mikataba ya kazi na wizara ya ulinzi ya Urusi.

Katika matukio mengine, angalau mtu mmoja aliuawa Jumatatu katika mji wa Kryvyi Rih nchini Ukraine baada ya makombora ya Urusi kushambulia eneo hilo, kwa mujibu wa Wizara ya mambo ya ndani.

Wakati huo huo, shambulio la ndege zisizo na rubani limeripotiwa katika eneo la mpakani la Urusi la Bryansk - huku Gavana Alexander Bogomaz akisema kituo cha polisi kilishambuliwa.

Siku ya Jumamosi, maafisa wa Urusi walisema ndege tatu zisizo na rubani za Ukraine zilidunguliwa mjini Moscow - ikiwa ni shambulizi la hivi karibuni zaidi katika mfululizo wa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye mji mkuu wa Urusi.

Meya wa Moscow Sergei Sobyanin aliilaumu Ukraine kwa shambulio hilo, ambapo majengo kadhaa ya ofisi yaliharibiwa, ingawa hakukuwa na majeruhi.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alionya kwamba vita vinakuja tena nchini Urusi, na kwamba katika eneo la Urusi ni "mchakato usioepukika, wa asili na haki kabisa" wa vita kati ya nchi hizo mbili.