Kumalizika kwa vita Ukraine: Jinsi vita vinavyoweza kufikia mwisho 2025

Muda wa kusoma: Dakika 8

"Lazima niseme kwamba hali inabadilika sana," rais wa Urusi, Vladimir Putin, alisema katika mkutano wake wa mwisho wa mwaka akizungumza na wanahabari mwezi Desemba. "Kuna harakati katika mstari mzima wa mbele Kila siku."

Katika eneo la mashariki mwa Ukraine, wapiganaji wa Moscow wanasonga mbele polepole maili kwa maili kupitia uwanja wazi wa Donbas, wakipita vijiji na miji mingi.

Baadhi ya raia wanakimbia kabla ya vita kuwafikia. Wengine husubiri hadi makombora yaanze kulipuka pande zote kabla ya kufunga vitu wanavyoweza kubeba na kupanda treni na mabasi kuelekea mahali salama zaidi huko magharibi.

Urusi inaimarika kwa haraka zaidi kuliko wakati wowote tangu ilipoanzisha uvamizi wake kamili mnamo Februari 2022, licha ya rekodi ya kuvutia ya Kyiv ya mashambulizi yaliyotangazwa vyema dhidi ya jirani yake mwenye nguvu.

'Kukwama kwa Mazungumzo ya amani'

Ahadi ya Trump ya kumaliza mzozo ndani ya saa 24 baada ya kuingia madarakani ni majigambo makubwa, lakini inatoka kwa mtu ambaye hana ustahimilivu kuhusu vita na namna inavyolitia gharama kubwa taifa la Marekani.

"Idadi ya askari vijana waliokufa vitani kila mahali inashangaza," amesema. "Ni mambo yanayofanyika."

Lakini utawala unaokuja wa Marekani unakabiliwa na changamoto mbili, kulingana na Michael Kofman,Kiongozi katika Wakfu wa kimataifa wa amani Carnegie.

"Kwanza, watarithi vita kwa njia mbaya sana, huku kukikosekana wakati wa kuleta utulivu," alisema mwezi Desemba. "Pili, watarithi bila nadharia wazi ya mafanikio."

Rais huyo mteule alitoa vidokezo wakati wa mahojiano ya hivi karibuni kuhusu jinsi anavyokusudia kukabiliana na vita.

Aliliambia Jarida la Time kuwa hakubaliani "vikali" na uamuzi wa serikali ya Biden, mwezi Novemba, kuruhusu Ukraine kurusha makombora ya masafa marefu yaliyotolewa na Marekani kulenga nchini Urusi.

"Tunazidisha vita hivi na kufanya hali kuwa mbaya zaidi," alisema.

Mnamo tarehe 8 Desemba, aliulizwa na NBC News kama Ukraine inapaswa kujiandaa kwa msaada kidogo.

"Inawezekana," alijibu. "Pengine, hakika."

Lakini kwa wale wanaoogopa, kama ambavyo wengi huogopa, kwamba kiongozi mpya wa Marekani ana mwelekeo wa kuondoka Ukraine, alitoa hakikisho. "Huwezi kufikia makubaliano ikiwa utaacha majadiliano, kwa maoni yangu," amesema.

Ukweli ni kwamba: Nia ya Trump iko mbali sana.

Na kwa sasa mamlaka ya Ukraine inakataa aina yoyote ya mazungumzo ya shinikizo, au kwamba ujio wa Trump kumaanisha kuwa mazungumzo ya amani yanakaribia.

"Kuna kauli nyingi kuhusu mazungumzo, lakini ni mazungumzo hewa," anasema Mykhailo dolyak, mshauri wa mkuu wa ofisi ya Rais Zelensky.

"Hakuna mchakato wa mazungumzo unaoweza kufanyika kwa sababu Urusi haijalipa gharama ya kutosha kwa vita.

Zoezi la mkakati mahiri la Zelensky

Pamoja na mashaka yote ya Kyiv kuhusu kufanya mazungumzo huku majeshi ya Urusi yakiendelea na harakati zao zisizoweza kuepukika mashariki, ni wazi kwamba Rais Zelensky ana wasiwasi kujiweka kama mtu ambaye Trump anaweza kufanya shughuli naye.

Kiongozi huyo wa Ukraine aliharakisha kumpongeza Trump kwa ushindi wake wa baada ya uchaguzi na kuchelewa kutuma maafisa wake wakuu kukutana na timu ya rais huyo mteule.

Kwa msaada wa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Zelensky pia alikutana na Trump wakati wawili hao walipotembelea Paris kwa ajili ya kufungua tena kanisa kuu la Notre Dame.

"Tunachokiona sasa ni mkakati mzuri sana wa Rais Zelensky," waziri wake wa zamani wa mambo ya nje Dmytro Kuleba aliliambia Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Marekani mwezi Desemba.

Zelensky, alisema, ilikuwa "ikiashiria utayari wa kushirikiana na Rais Trump."

Kwa ishara kidogo kwamba Kremlin inafanya ishara kama hizo, serikali ya Kyiv inajaribu waziwazi kufanya mbinu ya kutangulia mbele zaidi.

"Kwa sababu Trump hajaeleza kikamilifu jinsi atakavyoshughulikia, raia wa Ukraine wanajaribu kumpa mawazo ambayo anaweza kuyawasilisha kama yake," anasema Orysia Lutsevych, mkuu wa Jukwaa la Ukraine katika Chatham House.

"Wanajua jinsi ya kufanya kazi nae"

Unaweza pia kusoma

Mkakati wa Ushindi: mwisho unaowezekana

Hata kabla ya uchaguzi wa Marekani, kulikuwa na dalili kwamba Zelensky alikuwa akitafuta njia za kuimarisha mpango wa Ukraine kama mshirika wa baadaye wa rais mteule Trump ambaye kwa kawaida anaonekana anasitasita kuendelea kuhakikisha usalama zaidi wa Ulaya.

Kama sehemu ya "Mpango wake wa Ushindi", uliozinduliwa mnamo Oktoba, Zelensky alipendekeza kwamba wanajeshi wa Ukraine walioko vitani wanaweza kuchukua nafasi ya vikosi vya Marekani huko Ulaya baada ya vita na Urusi kumalizika.

Na alitoa matarajio ya uwekezaji wa pamoja wa kutumia maliasili ya Ukraine, ikiwa ni pamoja na madini ya uranium, grafiti na lithiamu.

Rasilimali hizo za kimkakati, Zelensky alionya, "zitaimarisha Urusi au Ukraine na ulimwengu wa kidemokrasia".

Lakini vipengele vingine vya Mkakati wa Ushindi wa kiongozi huyo wa Ukraine - ni suala la uanachama wa Nato na wito wake wa "hatua za kuzuia mkakati wa nyuklia" - inaonekana kupokelewa kwa mwitikio wa wastani miongoni mwa washirika wa Kyiv.

Uanachama wa Nato haswa unasalia kuwa hoja nyeti, kama ilivyokuwa tangu kabla ya uvamizi kamili wa Urusi.

Kwa Kyiv, ndiyo njia pekee ya kuhakikisha mustakabali wa nchi hiyo, dhidi ya adui yake Urusi iliyedhamiria kuitiisha Ukraine.

Lakini licha ya kutangaza Julai iliyopita kwamba Ukraine ilikuwa kwenye "njia isiyoweza kuenguliwa kwa ushirikiano kamili wa Euro-Atlantic, ikiwa ni pamoja na uanachama wa Nato" muungano umegawanyika, na Marekani na Ujerumani bado hazijaunga mkono kutoa mwaliko huo.

Rais Zelensky amedokeza kwamba ikiwa mualiko wa uanachama utatolewa kwa nchi nzima, ndani ya mipaka ya Ukraine inayotambulika kimataifa, atakuwa tayari kukubali,kwanza kwa eneo lililo chini ya udhibiti wa Kyiv pekee.

Hii, aliiambia Sky News mwezi Novemba, inaweza kumaliza "vita kali'', kuruhusu mchakato wa kidiplomasia kushughulikia suala la mipaka ya mwisho ya Ukraine.

Lakini, alisema, hakuna hatua kama hiyo bado iliyotolewa.

Hali ya kutetereka kwa Kyiv

Ikiwa sio NATO, basi nini? Huku uwezekano wa mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Trump yakikaribia na Ukraine kupoteza nafasi katika uwanja wa vita, mjadala wa kimataifa ni kuhusu kuimarisha msimamo wa Kyiv unaoyumba.

"Ni muhimu kuwa na dhamana kali, kisheria na kiutendaji," Andriy Yermak, mkuu wa ofisi ya Rais Zelensky, aliliambia shirika la utangazaji la serikali ya Ukraine tarehe 12 Desemba.

Maisha ya hivi karibuni ya Ukraine, alisema, yameacha historia chungu. "Kwa bahati mbaya, kutokana na uzoefu wetu, dhamana zote tuliokuwa nazo hapo awali hazikutuhakikishia usalama."

Bila mbinu madhubuti sawa na aina ya dhana ya ulinzi wa pamoja iliyojumuishwa na Kifungu cha 5 cha mkataba wa mwanzilishi wa Nato, waangalizi wanahofia hakutakuwa na chochote cha kuzuia shambulio lingine la Urusi.

"Zelensky anaelewa kuwa hawezi tu kuwa na usitishaji mapigano rahisi," Orysia Lutsevych anasema.

"Lazima iwe zaidi ya usitishwaji mapigano. Itakuwa kujiua kwa Zelensky kukubali tu usitishaji mapigano na pasipo kuwa na mkakati wa namna gani Ukraine itahakikishiwa ulinzi."

Katika vikao vya sera za Ulaya, wataalam wamekuwa wakiangalia njia ambazo Ulaya inaweza kusaidia kubeba jukumu hili zito.

Mawazo hayo yamejumuisha kupelekwa kwa askari wa kulinda amani nchini Ukraine (pendekezo lilitolewa kwa mara ya kwanza Februari mwaka jana na Macron), au kuhusika kwa Kikosi cha Pamoja cha Usafiri kinachoongozwa na Uingereza, ambacho huunganisha pamoja vikosi kutoka nchi nane za Nordic na Baltic, pamoja na Uholanzi.

Lakini Kofman ana shaka. "Uhakikisho wa usalama ambao hauhusiki na Marekani kwa kuwa mmoja wa wadhamini ni jambo lisilowezekana kufanikiwa.

Ni mtazamo ulioungwa mkono huko Kyiv.

"Ni mbadala gani unaweza kuwa? Hakuna njia mbadala leo," anasema Bw Podolyak.

Vipande vya karatasi, kama vile Mkataba wa Budapest wa 1994 (kuhusu mipaka ya baada ya Soviet Union) au makubaliano ya Minsk ya 2014-15 (ambayo yalitaka kumaliza Vita vya Donbas) havina nguvu, anasema, bila hatua za ziada za kuzuia uvamizi wa kijeshi.

"Urusi lazima ielewe kwamba punde tu watakapoanza uchokozi, watajibiwa kwa kushuhudia idadi kubwa ya mashambulizi," anasema.

Uingereza, Biden na jukumu la mataifa ya Magharibi

Kwa kukosekana kwa makubaliano juu ya mustakabali wa muda mrefu wa Ukraine, washirika wake wanafanya wawezavyo kuimarisha ulinzi wake.

Mnamo Desemba, Katibu Mkuu wa Nato, Mark Rutte, alisema "kila kitu" kilikuwa kikiangaliwa, ikiwa ni pamoja na usambazaji wa mifumo ya ziada ya ulinzi wa anga, kwa sehemu ya kulinda miundombinu ya nishati iliyoharibiwa nchini humo kutokana na wimbi jipya la mashambulizi ya makombora ya ndege zisizokuwa na rubani za Urusi.

Huku Ukraine ikiendelea kukumbwa na uhaba mkubwa wa wafanyakazi, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza John Healey alisema serikali inaweza kuwa tayari kutuma wanajeshi wa Uingereza nchini Ukraine kutoa msaada wa mafunzo.

Kwa upande wake, utawala unaomaliza muda wake wa Joe Biden unaonekana kudhamiria kutoa usaidizi wa kijeshi ulioidhinishwa na bunge kadri uwezavyo kwa Ukraine kabla ya kuondoka madarakani, ingawa ripoti zinaonyesha kuwa huenda ukakosa muda wa kutuma kila kitu.

Mnamo tarehe 21 Disemba iliripotiwa kuwa Trump ataendelea kupeleka msaada wa kijeshi kwa Ukraine, lakini angetaka wanachama wa NATO kuongeza bajeti ya ulinzi.

Washirika wa Kyiv pia wameendelea kuweka vikwazo dhidi ya Moscow, kwa matumaini kwamba uchumi wa Urusi wa wakati wa vita, ambao umeonekana kustahimili, unaweza hatimaye kuzorota.

"Kumekuwa na kufadhaika sana kwamba vikwazo havijafanikiwa kuathiri vikali uchumi wa Urusi ," chanzo cha bunge la Marekani kilisema, kwa sharti la kutokujulikana.

Baada ya awamu nyingi za vikwazo (kumi na tano kutoka EU pekee), maafisa wa serikali wamekua na wasiwasi wa kubashiri mafanikio.

Lakini viashiria vya hivi karibuni vinazidi kuwa tishio kwa Kremlin. Huku viwango vya riba vikiwa 23%, mfumuko wa bei ukiwa juu ya 9%, kuporomoka kwa sarafu yake na ongezeko la uchumi linatarajiwa kushuka sana mnamo 2025, matatizo ya uchumi wa Urusi hayajaonekana kuwa makubwa zaidi.

Putin anaweka uso wa ujasiri. "Vikwazo vina athari," alisema wakati wa mkutano wake wa mwisho wa mwaka, "lakini sio muhimu sana."

Pamoja na hasara kubwa ya Urusi kwenye uwanja wa vita - maafisa wa magharibi wanakadiria kuwa Moscow inapoteza wastani wa watu 1,500, kuuawa na kujeruhiwa, kila siku - gharama ya vita hivi bado inaweza kumfanya Putin kushiriki katika meza ya mazungumzo.

Lakini ni eneo gani zaidi Ukraine itakuwa imepoteza - na ni watu wangapi zaidi watakuwa wameuawa - wakati hatua hiyo inafikiwa?

Imetafsiriwa na Martha Saranga