Ukraine inaweza ‘kupoteza’ vita katika mstari wa mbele huku Urusi ikiongeza kasi ya mashambulizi, wataalam waonya

Muda wa kusoma: Dakika 7

Na Matt Murphy, Paul Brown, Olga Robinson, Thomas Spencer & Alex Murray

BBC Verify

Uamuzi wa Rais Biden wa kutoa mabomu ya kutegwa ardhini kwa Ukraine, na kuruhusu matumizi ya makombora ya masafa marefu katika ardhi ya Urusi unakuja wakati jeshi la Urusi likiongeza kasi ya mafanikio yake katika mstari wa mbele wa mapigano.

Takwimu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Vita (ISW) inaonyesha kuwa Urusi imepata karibu mara sita ya eneo kubwa katika mwaka 2024 kama ilivyokuwa katika mwaka 2023, na inaendelea kuelekea vituo muhimu vya vifaa vya Kiukreni katika mkoa wa mashariki mwa Donbas.

Wakati huo huo, uvamizi wa kushangaza wa Ukraine katika mkoa wa Kursk wa Urusi unapungua.

Wanajeshi wa Urusi wamepunguza mashambulizi ya Kyiv.

Wataalamu wamehoji mafanikio ya mashambulizi hayo, huku mmoja akiyaita "janga la kimkakati" kutokana na uhaba wa wapiganaji unaoikabili Ukraine.

Hatua hizi zinakuja wakati ambapo kuna hali ya sintofahamu huku utawala wa pili wa Donald Trump ukikaribia kuingia madarakani.

Rais mteule wa Marekani ameapa kumaliza vita hivyo atakapoingia madarakani mwezi Januari, huku baadhi wakihofia kuwa huenda akapunguza msaada wa kijeshi kwa Ukraine.

Unaweza pia kusoma:

Urusi imepiga hatua mashariki mwa Ukraine

Katika miezi michache ya kwanza ya vita mstari wa mbele wa vita ulipanuka haraka, na Urusi ikapata ardhi haraka kabla ya kusukumwa nyuma na vikosi vya Ukraine. Lakini mwaka 2023 hakuna upande uliopata mafanikio makubwa - huku mzozo huo ukiingia katika mkwamo.

Lakini takwimu mpya za ISW zinaonyesha hadithi hiyo mnamo 2024 ni nzuri zaidi kwa Urusi. ISW inaangazia uchambuzi wake juu ya picha za mitandao ya kijamii zilizothibitishwa na ripoti za harakati za wanajeshi.

Takwimu za ISW zinaonyesha kuwa vikosi vya Moscow vimeliteka karibu kilomita za mraba 2,700 za eneo la Ukraine hadi sasa mwaka huu, ikilinganishwa na kilomita za mraba 465 tu katika mzima wa 2023, likiwa ni ongezeko la karibu mara sita.

Mtafiti wa masuala ya ulinzi katika chuo cha Kings College London, Dkt Marina Miron, aliieleza BBC kwamba kuna uwezekano wa upande wa mashariki wa Ukraine "kuanguka" mikononi mwa urusi, ikiwa Urusi itaendelea kusonga mbele kwa kasi.

Zaidi ya kilomita 1000 za mraba zilichukuliwa kati ya Septemba 1 na Novemba 3, na kusema kuwa msukumo huo uliongezeka katika miezi ya hivi karibuni.

Maeneo haya mawili ni Kupiansk katika mkoa wa Kharkiv, na Kurakhove, eneo muhimu la kuingia katika eneo Pokrovsk katika mkoa wa usambazaji wa vifaa vya kijeshi wa Donetsk.

Kupiansk na maeneo ya mashariki mwa mto Oskil yalikombolewa katika mashambulizi ya Kharkiv ya 2022, lakini Urusi imechukua tena eneo la mwisho.

Katika taarifa ya hivi karibuni ya kijasusi, wizara ya ulinzi ya Uingereza ilisema vikosi vya Urusi vinajaribu kuingia katika viunga vya kaskazini mashariki mwa mji huo.

Picha za video zilizochapishwa tarehe 13 Novemba na kuthibitishwa na BBC zinaendana na uchambuzi huu. Video hiyo inaonyesha msafara wa silaha za Urusi ukiondolewa baada ya kufika ndani ya kilomita 4 za daraja muhimu katika eneo la Kupiansk, barabara kuu ya mwisho katika eneo hilo.

Wakati ripoti hizi si lazima kutafsiri kwa udhibiti wa eneo, ni dalili ya jinsi mstari wa ulinzi wa Ukraine ulivyopanuka.

Kwingineko, tangu kuuteka tena mji wa Vuhledar mnamo Oktoba – ni eneo lenye muinuko lililo juu ya mistari muhimu ya usambazaji ambalo Moscow ililitumia miaka miwili kupigana.

Vikosi vya Ukraine vinavyoulinda mji huo hadi sasa vimerudisha nyuma mashambulizi kusini na mashariki. Lakini mstari wa mbele unakaribia, huku Urusi pia ikitishia kuyalinda maeneo yenye ulinzi mkali ya kaskazini na magharibi.

Mkuu wa zamani wa mawasiliano ya kimkakati na wafanyakazi wa Ukraine Kanali Yevgeny Sasyko, alisema Urusi inaweka "silaha zenye nguvu."

Picha za video kutoka mji huo zilizothibitishwa na BBC zilionyesha uharibifu mkubwa, huku majengo ya makazi yakiharibiwa vibaya.

ISW inahitimisha kuwa Moscow sasa ina jumla ya kilomita za mraba 110,649 nchini Ukraine. Kwa kulinganisha, vikosi vya Ukraine viliteka zaidi ya kilomita za mraba 1,171 katika mwezi wa kwanza wa uvamizi wake huko Kursk - ingawa vikosi vya Urusi sasa vimechukua karibu nusu ya eneo hilo.

Licha ya mafanikio yake ya eneo, ushindi wa Urusi umekuja kwa gharama kubwa.

Uchambuzi uliofanywa na BBC Idhaa ya Kirusi umethibitisha kuwa takriban wanajeshi 78,329 wameuawa tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake kamili mwezi Februari 2022, huku Urusi ikipoteza maeneo kuanzia Septemba hadi Novemba mwaka huu, ikiwa ni zaidi ya mara moja na nusu zaidi ya kipindi kama hicho mwaka 2023.

Hasara hiyo imechangiwa na mbinu ya “meat grinder” inayosemekana kupendelewa na makamanda wa Urusi - ikielezea kupelekwa kwa wimbi la wanajeshi wanaopelekwa kuelekea maeneo ya Ukraine katika juhudi za kuwamaliza wanajeshi.

Licha ya maendeleo ya Urusi, baadhi ya wataalamu wamebaini kuwa kasi halisi ya mashambulizi bado ni ya kusuasua.

Mchambuzi wa masuala ya kijeshi, David Handelman, amedokeza kuwa wanajeshi wa Ukraine mashariki wanaondoka taratibu ili kuhifadhi nguvu kazi na rasilimali, badala ya kuteseka kutokana na kuangukia mikononi mwa urusi kwa eneo hilo

Mahesabu ya kuiteka Kursk

Ukraine ilizindua mashambulizi yake ya kushtukiza katika mkoa wa Kursk nchini Urusi mwezi Agosti. Haijulikani ni kwa nini Urusi ilichukua muda mrefu kujibu operesheni hiyo, ambayo ilipelekea vikosi vya Kyiv kupata udhibiti wa haraka wa jamii kadhaa za mipakani.

Dr Miron alisema kwamba wakati Kremlin ingepata gharama za kisiasa za ndani kwa muda mrefu kama uvamizi huo ungeendelea, mdhamiri mkuu wa jeshi la Urusi alikuwa na nia ya kuweka vikosi vya Ukraine vilivyotekwa huko Kursk wakati vikosi vyake vilipoteka mahali pengine kwenye mstari wa mbele.

Lakini Moscow sasa ina nia ya wazi ya kurejesha eneo lililopotea kwenye ardhi yake. Takriban wanajeshi 50,000 wamepelekwa katika eneo hilo.

Video zilizothibitishwa kutoka eneo la Kursk zinaonyesha mapigano makali yanafanyika - na kwamba Urusi inakabiliwa na hasara kubwa katika suala la nguvu kazi na vifaa. Lakini takwimu zinaonyesha wazi kuwa udhibiti wa Ukraine katika eneo hilo unapungua.

Tangu mwanzoni mwa mwezi wa Oktoba, mashambulizi ya Urusi yamerejesha eneo la kilomita za mraba 593 katika eneo la mpakani, takwimu za ISW zilionyesha.

Uvamizi wa Kursk hapo awali ulikuwa ni pigo kubwa kwa Ukraine kwa suala la maadili wakati wa vikwazo vikubwa, na ujasiri wa operesheni hiyo ulikuwa ukumbusho wa uwezo wake wa kushangaza na kumdhuru adui yake.

Lakini Dkt Miron alisema wakati uvamizi wa Kursk ulikuwa wakati wa "mzuri" pia umekuwa "janga la kimkakati" kwa Ukraine.

"Wazo zima lilikuwa ni kupata nguvu za kisiasa katika mazungumzo, lakini pia kijeshi kuviteka vikosi vya Urusi vilivyo mbali na Donbas ili kuikomboa Kursk. Na kile tunachoona badala yake ni kwamba vitengo wanajeshi wa Ukraine wamefungiwa huko."

Baadhi ya vitengo vya kijeshi vya Kyiv vyenye uzoefu na ufanisi vinajulikana kuwa vinapigana huko Kursk. Vitengo vya mitambo vilivyo na silaha za hali ya juu za Magharibi pia vinashiriki katika mashambulizi.

Viongozi wa Ukraine walikuwa wamedokeza kwamba walitarajia uvamizi huo utailazimisha Moscow kuelekeza baadhi ya vikosi vyake kutoka mashariki mwa Ukraine, na kupunguza kasi ya Urusi kuingia huko. Badala yake, wataalamu wanasema vikosi vingi vilihamishwa hadi Kursk kutoka sehemu za Ukraine ambako mapigano sio makali.

"Kulingana na wanajeshi wa Ukraine kutoka sehemu tofauti za mstari wa mbele wa mapigano, wanajeshi wa Urusi wanaoimarisha udhibiti wa Kursk waliondolewa kutoka Kherson na Zaporizhzhia," Yurri Clavilier, mchambuzi wa masuala ya ardhi katika taasisi ya kimataifa ya mafunzo ya kimkakati, aliiambia BBC.

"Mapambano ya hapa sio makali kama ilivyo katika eneo la Mashariki. Baadhi ya vitengo vya Urusi vilivyoshambulia Kharkiv pia vilielekezwa Kursk wakati Ukraine ilipofanikiwa kuzuia mashambulizi ya Urusi huko," aliongeza.

Umuhimu wa eneo kwa pande zote mbili ni nguvu inayotoa nafasi yao katika mazungumzo yoyote yanayoweza kutokea. Ingawa hakuna mazungumzo ya amani yaliyojadiliwa, Rais mteule wa Marekani Trump amedai kuwa anaweza kumaliza vita ndani ya saa 24, bila kusema ni kwa namna gani.

Hofu inaendelea nchini Ukraine kwamba Trump anaweza kupunguza msaada wa kijeshi kama njia ya kuilazimisha Kyiv kukaa katika meza ya mazungumzo. Rais Volodymyr Zelensky aliliambia shirika la habari la Fox News siku ya Jumanne "Nadhani tutapoteza [vita]" ikiwa kupunguzwa kwa muda kutalazimishwa.

"Tuna uzalishaji wetu, lakini haitoshi kushinda na nadhani si wa kudumu," alisema.

Siku ya Jumanne, Ukraine ilirusha makombora ya masafa marefu yaliyorushwa na Marekani nchini Urusi kwa mara ya kwanza - siku moja baada ya Washington kutoa ruhusa ya kufanya hivyo. Inafikiriwa kuwa uamuzi huo ulifanywa kwa sehemu kuisaidia Ukraine kushikilia sehemu ya mkoa wa Kursk, kusaidia kuutumia kama mbinu ya mazungumzo ya baadaye.

Dkt Miron ameiambia BBC kuwa hatua ya Urusi imewapa nafasi kubwa ya majadiliano wakati timu mpya ya sera za kigeni ya Trump ikijiandaa kuingia madarakani.

"Kile wanachokidhibiti kwa sasa, kinawapa faida fulani," alisema. "Kama ni suala la mazungumzo, nina uhakika kwamba kama upande wa Urusi imekuwa ikisisitiza, 'tutafanya hivyo kwa kuzingatia hali katika uwanja wa vita'.

"Kwa mtazamo wa Urusi, wana kadi bora zaidi kuliko Waukraine."

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi