Kipi kifuatacho kwa Iran baada ya mhimili wake wa upinzani kukongolewa?

rff

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Caroline Hawley
    • Nafasi, BBC News World
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Picha ya Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei iko chini imepasuliwa kwenye sakafu ya ubalozi wa Iran mjini Damascus. Kuna picha zilizochanwa pia za kiongozi wa zamani wa vuguvugu la Hezbollah nchini Lebanon, Hassan Nasrallah, ambaye aliuawa katika shambulio la anga la Israel huko Beirut mwezi Septemba.

Picha nyingine iliyoharibiwa ni ya kamanda wa zamani wa Walinzi wa Mapinduzi ya Iran Qasem Soleimani - aliyeuawa kwa amri ya Donald Trump wakati wa urais wake. Mfululizo wa hasara ambayo Iran imekumbana nayo, ilifikia kilele Jumapili kwa kuanguka mshirika wake mkuu, rais wa Syria Bashar. al-Assad.

Wakati Jamhuri ya Kiislamu ikilamba majeraha yake, na kujiandaa kwa urais wa Donald Trump. Je, itaamua kuja na mitazamo mikali zaidi - au itaanzisha upya mazungumzo na nchi za Magharibi? Na utawala huo upo imara kiasi gani?

Khamenei mwenye umri wa miaka 85, anakabiliwa na changamoto juu ya mrithi wake, yuko madarakani nchini Iran tangu 1989. "Iran ina nguvu na itakuwa na nguvu zaidi," alisema katika hotuba yake ya kwanza tangu kupinduliwa Asaad.

Alisisitiza kuwa muungano unaoongozwa na Iran, Mashariki ya Kati, unaojumuisha Hamas, Hezbollah, Houthis wa Yemen na wanamgambo wa Shia wa Iraqi dhidi ya Israel - utaimarika pia. "Kadiri unavyozidisha shinikizo, ndivyo upinzani unavyozidi kuwa na nguvu."

"Makundi yote yanaanguka," anasema James Jeffrey, mwanadiplomasia wa zamani wa Marekani na naibu mshauri wa usalama wa taifa, ambaye sasa anafanya kazi katika kituo cha fikra cha Wilson Center kisichoegemea upande wowote.

"Mhimili wa Iran wa Upinzani umevunjwa na Israel, na sasa umelipuliwa na matukio nchini Syria. Iran imesalia bila wakala mwenye nguvu katika eneo hilo zaidi ya Wahouthi nchini Yemen."

Iran bado inaunga mkono wanamgambo wenye nguvu katika nchi jirani ya Iraq. Lakini kulingana na Jeffrey: "Hili ni anguko ambalo halijawahi kushuhudiwa kabisa katika kanda hiyo."

Mara ya mwisho kuonekana hadharani kwa Assad ilikuwa katika mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, tarehe 1 Disemba, alipoapa "kuwaponda" waasi wanaosonga mbele katika mji mkuu wa Syria. Ikulu ya Kremlin imesema sasa yuko nchini Urusi baada ya kuikimbia nchi hiyo

Pia unaweza kusoma

Iran ilivyojenga mtandao wake

rfd

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Picha iliyochanika ya aliyekuwa kiongozi wa Hezbollah, Sheikh Hassan Nasrallah (kushoto) na Jenerali wa Iran, Marehemu Qassem Soleimani.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Iran imetumia miongo kadhaa kujenga mtandao wake wa wanamgambo ili kudumisha ushawishi katika eneo hilo, pamoja na kuzuia mashambulizi ya Israel.

Katika vita vya Iran na Iraq, babake Bashar al-Assad, Hafez, aliiunga mkono Iran.

Muungano kati ya viongozi wa Kishia nchini Iran na Assad ulisaidia kuimarisha ngome ya Iran Mashariki ya Kati yenye Wasunni wengi. Syria pia ilikuwa njia muhimu ya Iran ya kupeleka silaha kwa mshirika wake huko Lebanon, Hezbollah, na makundi mengine ya kikanda yenye silaha.

Iran iliwahi kumsaidia Assad hapo awali. Alipoonekana kuwa hatarini baada ya ghasia za mwaka 2011 kubadilika na kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, Tehran ilitoa wapiganaji, mafuta na silaha. Zaidi ya wanajeshi na majenerali 2,000 wa Iran waliuawa.

"Njia ambayo Iran itajaribu, katika siku zijazo, kuitumia kusambaza silaha tena kwa Hezbollah nchini Lebanon - na makundi mengine - imekatwa," anasema Dk Sanam Vakil, mkurugenzi wa mpango wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika taasisi ya Chatham House.

"Mhimili wa Upinzani ulikuwa mtandao uliobuniwa na Iran kimkakati na kuilinda Iran dhidi ya mashambulizi ya moja kwa moja," anasema Vakil. "Mkakati huu umeshindwa kabisa."

Mahesabu ya Iran ya nini cha kufanya baadaye yataathiriwa sio tu na kuangamia kwa Assad lakini pia na ukweli kwamba jeshi lake lilipata pigo kutoka Israel katika makabiliano ya kwanza ya moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili mapema mwaka huu.

Makombora mengi ya balistiki ambayo Iran ilirusha kwenda Israel mwezi Oktoba yalinaswa, ingawa baadhi yalisababisha uharibifu katika kambi kadhaa za anga. Mashambulizi ya Israel yalisababisha uharibifu mkubwa kwa ulinzi wa anga na uwezo wa Iran w kutengeneza makombora. "Tishio la makombora makubwa limethibitishwa kuwa ni simba wa karatasi," asema Jeffrey.

Mauaji ya kiongozi wa zamani wa Hamas, Ismail Haniyeh, mwezi Julai pia yalikuwa ni aibu kubwa kwa Iran.

"Mwelekeo wa baadaye wa Jamhuri ya Kiislamu kuanzia hapa na kuendelea ni uhai wake yenyewe. Itataka kujiimarisha na kile kilichosalia katika mhimili wa upinzani, na kuwekeza tena katika uhusiano wa kikanda ili kustahimili shinikizo ambalo Trump anaweza kulileta," anasema Dk Vakil.

Iran imedhoofika sana kimataifa - huku Donald Trump ambaye hatabiriki anakaribia kutwaa urais nchini Marekani, na Israel imedhihirisha uwezo wake wa kuwaondoa maadui zake.

Uwezo wa nyuklia

Iran inasisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa amani. Lakini imeendeleo ya mpango huo tangu Donald Trump alipoachana na makubaliano ya 2015, ambayo yalipunguza shughuli za Iran za nyuklia kwa malipo ya kuondolewa kwa baadhi ya vikwazo vya kiuchumi.

Chini ya makubaliano hayo, Iran iliruhusiwa kurutubisha uranium hadi asilimia 3.67%. Uranium inayorutubishwa kwa kiwango cha chini inaweza kutumika kuzalisha mafuta kwa ajili ya mitambo ya kibiashara ya nyuklia. Lakini Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, linasema Iran sasa imeongeza kwa kiasi kikubwa kiwango ambacho inaweza kuzalisha cha uranium iliyorutubishwa hadi 60%.

Iran inasema inafanya hivyo ili kulipiza kisasi vikwazo ambavyo Trump alivirejesha na ambavyo vilisalia baada ya utawala wa Biden ulijaribu na kushindwa kufufua mpango huo.

Uranium ya kiwango cha silaha, ambayo inahitajika kwa bomu la nyuklia, inarutubishwa kwa 90% au zaidi.

Imekadiriwa kuwa Iran sasa inaweza kurutubisha uranium ya kutosha kwa silaha ndani ya takriban wiki moja, ikiwa itaamua kufanya hivyo, ingawa itahitaji kujenga mfumo ambao wataalamu wanasema utachukua miezi au mwaka.

Nchi za Magharibi zina wasiwasi

re

Chanzo cha picha, getty

Maelezo ya picha, Bashar al-Assad alidumisha uhusiano wa karibu na Ali Khamenei

"Ni wazi kwamba Trump atajaribu kurudisha tena mkakati wake wa 'shinikizo dhidi ya Iran," anasema Dk Raz Zimmt, mtafiti mkuu katika Taasisi ya Mafunzo ya Usalama wa Taifa ya Chuo Kikuu cha Tel Aviv, Israel.

"Lakini nadhani pia atajaribu kuihusisha Iran katika mazungumzo mapya akijaribu kuishawishi kurudisha nyuma uwezo wake wa nyuklia."

Licha ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kutangaza kutaka mabadiliko ya utawala huko Iran, Dk Zimmt anaamini nchi hiyo itachukua muda wake, ikisubiri kuona Donald Trump atafanya nini na jinsi Iran itakavyojibu.

"Iran haitaki kuzusha mzozo kamili. Nadhani Donald Trump - kama mfanyabiashara - atajaribu kushirikisha Iran na kuunda makubaliano," anasema Nasser Hadian, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Tehran.

"Iwapo hilo halitafanyika, ataweka shinikizo kubwa ili kuileta mezani."

Anaamini makubaliano yanawezekana zaidi kuliko migogoro, lakini anaongeza: "Kuna uwezekano kwamba, ikiwa atatumia shinikizo kubwa, mambo yataharibika na tutapata vita ambavyo hakuna upande unavitaka."

Hasira nchini Iran

fgc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Huko Aleppo mpiganaji wa waasi alibomoa picha ya Bashar al-Assad

Jamhuri ya Kiislamu pia inakabiliwa na changamoto nyingi za ndani, wakati inapojiandaa kwa ajili ya urithi wa Kiongozi Muadhamu.

"Khamenei analala akiwa na wasiwasi juu ya historia na mabadiliko na anatazamia kuiacha Iran katika sehemu tulivu," kulingana na Dk Vakil.

Utawala wake ulitikiswa vibaya na maandamano ya nchi nzima ya 2022 yaliyofuatia kifo cha msichana, Mahsa Jina Amini, ambaye alituhumiwa kutovaa hijabu ipasavyo.

Maandamano hayo yalipinga uhalali wa kuanzishwa kwa polisi wa maadili na ulikandamizaji wa kikatili.

Bado kuna ghadhabu kubwa dhidi ya utawala ambao umemwaga rasilimali katika migogoro nje ya nchi wakati Wairani wengi wanakabiliwa na ukosefu wa ajira na mfumuko mkubwa wa bei.

Na kizazi cha vijana wa Iran, kinazidi kujitenga na Mapinduzi ya Kiislamu, huku wengi wakikerwa na vikwazo vya kijamii vilivyowekwa na utawala huo. Kila siku, wanawake bado wanakaidi amri za utawala, wakihatarisha kukamatwa kwa kwenda nje bila ya kufunika nywele zao.

Hata hivyo, hiyo haimaanishi kwamba kutakuwa na anguko la utawala huo sawa na lile la Syria, wanasema wafuatiliaji wa Iran. Hawaamini kuwa serikali kwa sasa iko hatarini.

Mamilioni ya Wairani hawaiungi mkono, lakini mamilioni bado wanaiunga mkono serikali hiyo. Na serikali haionekani kama iko katika hatari ya kuanguka hivi karibuni.

Lakini inapozidi kukabiliwa na hasira nyumbani, kupoteza mbabe wake nchini Syria - na mashambulizi mengine mengi dhidi makundi yake ya kikanda - kumeifanya kazi ya watawala wa Iran kuwa ngumu zaidi.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah