Ushindi wa Trump una maana gani kwa Iran?

Katika mojawapo ya nafasi chache za maafisa wakuu wa Iran, msemaji wa serikali alipuuza athari za matokeo ya uchaguzi wa Marekani kwa Iran.
Fatemeh Mohajerani alieleza kwamba haijalishi nani atakuwa rais wa Marekani. Mpango wetu tayari umefanikiwa.
Bi Mohajerani alisema kwamba Iran imedhoofishwa kufuatia vikwazo vya muda mrefu. Alisisitiza kwamba ‘’hatuogopi kuchaguliwa tena kwa Trump na wala hatuoni tofauti kati ya wawili hawa.
Nchini Iran kwa mabadiliko ya rais sera zote kwa ujumla kuhusu Marekani hazitabadilika sana, lakini nchini Marekani kubadilika kwa rais huenda kukabadilisha sera zake na hata sera kuhusu washirika wake.
Leo rais wa Ufaransa na kansela wa Ujerumani wamezungumza kwa njia ya simu kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Marekani. Mataifa haya mawili ya Ulaya yana wasiwasi kuhusu athari za sera za Donald Trump kwa Umoja wa Ulaya.
Lakini mamlaka za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimejaribu kupunguza athari za matokeo ya uchaguzi wa Marekani kwa Iran. Fatemeh Mohajerani, msemaji wa serikali, anasema sera za jumla za Marekani na Jamhuri ya Kiislamu zimewekwa sawa na hazitabadilika kutokana na mabadiliko ya aliyeko madarakani.
Nchini Marekani, rais huamua sera za miaka minne ijayo na kwa kubadilisha rais, sera za nchi hiyo kuhusu Iran huenda zikabadilika. Lakini nchini Iran ni kura ya Ayatollah Ali Khamenei, kiongozi mkuu wa serikali huamua sera kuu za nchi na sio kura za watu.
Moja ya mifano ya mabadiliko ya sera za Marekani ni makubaliano ya nyuklia ya Iran na mataifa ya Magharibi, yanayojulikana kama JCPOA, wakati wa uongozi wa Barack Obama mwaka 2015.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini baada ya Donald Trump kuingia madarakani, aliiondoa nchi yake katika mkataba wa JCPOA mwaka 2018 na akaiwekea Iran vikwazo vikali zaidi, vikwazo ambavyo vilikuwa na athari zenye shaka kwa uchumi na maisha ya wananchi wa Iran.
Ilikuwa chini ya amri ya Bwana Trump ambapo Qasem Soleimani, kamanda wa Kikosi cha IRGC Quds, aliuawa huko Baghdad mnamo 2020.
Sasa ushindi wa Donald Trump bila shaka utaathiri sera za Marekani kuhusu Iran. Hasa wakati huu Iran inahusika katika makabiliano ya kijeshi na Israel.
Katika miaka ya hivi karibuni, Waziri Mkuu wa Israel na wafuasi wanaounga mkono Israel nchini Marekani wamekuwa karibu na Warepublican kuliko Wanademocrats.
Bwana Trump ndiye aliyeitambua Jerusalem kuwa mji mkuu badala ya Tel Aviv kwa Waisraeli na wakati huohuo akafanya juhudi kubwa za kurekebisha uhusiano kati ya nchi za Kiarabu na Israel.
Wakati wa kampeni za uchaguzi, Bw. Trump ametoa ujumbe wenye pande mbili kuhusu Iran.
Mnamo Julai mwaka huu, baada ya ripoti kuhusu njama ya serikali ya Iran ya kutaka kumuua, Bw. Trump alisema kuhusu jaribio la kumuua: "Ninatumai Marekani itaiangamiza Iran na kuifutilia mbali katika uso wa dunia." Ikiwa halitafanyika, viongozi wa Marekani watafahamika kwa waoga wasio na huruma."
Lakini wiki mbili zilizopita, katika mahojiano na Patrick Bett David, alisema kwamba anataka Iran ifanikiwe na hataki kujihusisha na masuala ya ndani ya Iran. Wakati huo huo, alisema kuwa Iran inakaribia kuunda silaha ya nyuklia na hataruhusu Iran kupata silaha hizo.
Katika mahojiano haya, Bw.Trump alizungumzia uwezekano wa vikwazo vikali dhidi ya Iran na wale wanaonunua mafuta kutoka Iran.
Akikumbuka vikwazo dhidi ya Iran wakati wa uongozi wake, alisema wakati huo aliionya China kwamba ikiwa itanunua mafuta kutoka Iran, China haitaweza tena kufanya biashara na Marekani.
Sera za Bwana Trump kuhusu Iran haziwezi kutabiriwa mapema, kwa sababu amethibitisha huko nyuma kwamba anaweza kufanya maamuzi yasiyotarajiwa;
Hali hii isiyotarajiwa ya kiongozi ajaye wa Ikulu ya White House itawatia wasiwasi viongozi wa serikali ya Tehran.
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Seif Abdalla












