Harufu za ajabu za anga za juu zinazowashangaza wanasayansi

Chanzo cha picha, NASA
- Author, Katherine Latham
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Wanasayansi wanachunguza harufu za anga za juu - karibu na Dunia, hadi sayari zilizo umbali wa mamia ya miaka ya mwanga - ili kujifunza kuhusu muundo wa Ulimwengu.
Marina Barcenilla, anasema “sayari ya Jupiter inanuka kama bomu." Ndio sayari kubwa zaidi katika mfumo wa jua.
"Safu ya juu ya wingu katika Jupiter, tunaamini, imetengenezwa kwa barafu ya amonia," anasema Barcenilla, akifananisha harufu ya safu hiyo na mkojo wa paka. "Kisha, unaposhuka zaidi, unakutana na sulfidi ya amonia, hapo utakuta uvundo wa mayai yanayooza."
Barcenilla ni mwanasayansi wa anga, mtaalamu wa harufu na mwanafunzi wa PhD ya anga za juu katika Chuo Kikuu cha Westminster, London.
Pamoja na kazi yake ya kitaaluma ya kutafuta dalili za maisha kwenye sayari ya Mihiri - Barcenilla ana kazi ya kutambua na kuunda harufu zilizopo angani katika Makumbusho ya Historia ya Asili ya London.
Kuna harufu ya uvundo wa mayai yaliyooza hadi harufu nzuri ya mlozi, angani ni sehemu yenye harufu za kushangaza, anasema. Nyota, sayari, miezi na mawingu ya gesi kila moja ina harufu yake ya kipekee ikiwa tunaweza kunusa kwa pua zetu.
Uwezo wa kunusa

Chanzo cha picha, Marina Barcenilla
Uwezo wa kunusa ni matokeo ya uwezo wa kugundua kemikali katika mazingira yanayotuzunguka. Pua zetu zina neva zinazojumuisha mamilioni ya niuroni maalum ambazo zimejaa molekuli zinazojulikana kama chemoreceptors. Molekuli hizo zinapokutana na kemikali, hutuma ishara kwenye ubongo wetu na ubongo hutafsiri harufu hiyo.
Hisia hii ya harufu inamaanisha kuwa tuna uwezo wa kugundua kemikali zinazotuzunguka. Kwa wanadamu, harufu haitusaidii tu kutambua vyakula au kutuonya kuhusu hatari za kimazingira, lakini pia huibua kumbukumbu muhimu katika maisha yetu. Uwezo wa kunusa unahusishwa na afya bora ya kihisia.
Wanaanga wameelezea uwepo wa harufu ya nyama iliyoungua, baruti au nyaya za umeme zilizoungua huko angani. Pia angani kuna harufu ya nyota zilizokufa, ambazo hutoa kiasi kikubwa cha nishati. Nyota hizi huzalisha hidrokaboni zenye kunukia. Nyota zinapokufa, hutengeneza molekuli kisha huelea angani milele.
Nyingi ya kemikali hizi hutengeneza harufu kama nondo, wakati wengine kama kuchoma plastiki au lami.
Harufu hutokea wapi?

Chanzo cha picha, NASA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Darubini ya Anga ya Nasa ya James Webb (JWST) ilinasa mlipuko wa kwanza wa kaboni dioksidi (CO2) katika angahewa wakati mlipuko wa sayari iliyo nje ya mfumo wetu wa jua ulipotokea.
JWST haikunusa CO2 kwa maana ya kuivuta puani, lakini iligundua uwepo wake kwa kufuatilia jinsi ya angahewa ya sayari hiyo ilivyobadilisha mwanga mbele ya jua lake. Kwa kuchanganua mabadiliko madogo madogo katika mwanga, JWST inaweza kutambua kemikali mbalimbali za angani.
“Anga ni kubwa,” anasema Barcenilla. Imejaa harufu nyingi na tofauti. Uchambuzi wa kemikali katika angahewa kwenye Titan, mwezi mkubwa zaidi wa Zohali, unapendekeza kuwa kuna harufu ya lozi, petroli na samaki wanaooza.
Wakati huo huo, harufu ya mayai yaliyooza utayapata ukitembelea sayari ya HD 189733 b, iliyoumbali wa takriban miaka 64 ya mwanga kutoka duniani.
"Na kunusa kemikali za ulimwengu hakuwezi tu kutupa maelezo muhimu kuhusu muundo wa Ulimwengu, pia kunaweza kutupa fununu kuhusu mahali pa kutafuta uhai," anasema Barcenilla.
Kwa hivyo safari ya kwenda angani inaweza isiwe ya lazima kwa kila. Nyingi za harufu za angani tunazifahamu na zinapatikana hapa Duniani - na watu wachache wamejaribu kuunda upya harufu za angani, ikiwa ni pamoja na Barcenilla.















