Wanaanga wafichua jinsi maisha yalivyo katika kituo cha anga za juu cha ISS

k

Chanzo cha picha, NASA

Maelezo ya picha, Kazi ya kujenga Kituo cha Anga cha Kimataifa ilianza 1998
    • Author, Georgina Rannard
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Mwezi Juni ya mwaka huu wanaanga wawili wa Marekani, Suni Williams na Butch Wilmore waliondoka duniani wakitarajia kutumia siku nane kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu (ISS).

Lakini baada ya hofu kwamba chombo chao cha usafiri cha anga za juu cha Boeing Starliner hakikuwa salama kuruka tena kurudi duniani, Nasa, shirika la anga za juu la Marekani, likaamua kuchelewesha kurejea kwao hadi 2025.

Sasa wanaishi katika kituo cha ISS, chenye ukubwa wa nyumba sita vya kulala na wanaanga wengine tisa. Bi Williams anasema ni "mahali pa furaha" na Wilmore anasema "anashukuru" kuwa hapo.

Ni umbali wa kilomita 400 juu ya dunia. Je, wanafanyaje mazoezi? Je, wanafuaje nguo zao? Wanakula nini? Na, muhimu zaidi, kuna harufu gani katika anga za juu?

Wakizungumza na BBC News, wanaanga watatu wa zamani wanafichua siri ya maisha katika kituo hicho.

Pia unaweza kusoma

Maisha ya ISS

j

Chanzo cha picha, NASA

Maelezo ya picha, Mwanaanga wa Canada, Chris Hadfield alikuwa kamanda wa ISS mwaka 2012-13.

Wanaanga wanaamka mapema, takribani saa 12:30 asubuhi, huibuka kutoka sehemu zao za kulala zenye ukubwa wa kibanda cha simu.

"Ni sehemu nzuri ya kulala," anasema Nicole Stott, mwanaanga wa Marekani, kutoka Nasa ambaye alitumia siku 104 angani katika misheni mbili mwaka 2009 na 2011.

Vyumba hivyo vina kompyuta ndogo ili wafanyakazi waweze kuwasiliana na familia na kuna mahali pa kuhifadhi vitu vyao binafsi kama vile picha au vitabu.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wanaanga wanaweza kutumia bafuni, chumba kidogo chenye mfumo wa kufyonza. Kwa kawaida jasho na mkojo hugeuzwa kuwa maji ya kunywa, lakini hitilafu iliyotokea katika kituo cha ISS inamaanisha kuwa wanalazimika kuhifadhi mkojo kwa sasa.

Kisha wanaanga wanaanza kufanya kazi. Matengenezo au majaribio ya kisayansi, ndio kazi kuu kwenye ISS, kituo chenye ukubwa sawa na kasri la Buckingham - au uwanja wa soka wa Marekani.

"Ndani ni kama mabasi mengi yameunganishwa. Inaweza kupita nusu siku na usimuone mtu mwingine,” anaeleza mwanaanga wa Canada, Chris Hadfield, kiongozi wa misheni ya Expedition 35 mwaka 2012-13.

“Kituo ni kikubwa,” anasema.

ISS ina maabara sita kwa ajili ya majaribio, na wanaanga huvaa vifaa vya kuchunguza moyo, ubongo au damu ili kufuatilia hali ya mwili katika mazingira hayo magumu.

Bi Stott, anasema "anga za juu huifanya mifupa na misuli yako kuingia katika mchakato wa kuzeeka polepole zaidi, na wanasayansi wanajua hilo."

Wanaanga wachache wamebahatika kufanya matembezi ya anga nje ya ISS. Hadfield amefanya matembezi ya aina hiyo mara mbili.

"Duniani kuna harufu nyingi tofauti, kama vile harufu ya mashine ya kufulia nguo au hewa safi. Lakini angani kuna harufu moja tu, nasi tunaizoea haraka,” anasema Helen Sharman, mwanaanga wa kwanza Mwingereza, ambaye alitumia siku nane kwenye kituo cha anga za juu cha Soviet, Mir mwaka 1991.

Vitu unavyokwenda navyo, kama suti au vifaa vya kisayansi, huathiriwa na mionzi mikali ya angani. Mionzi huunda molekuli ambazo zikikutana na oksijeni ndani ya kituo cha anga, hunda harufu ya metali," anasema.

"Hakuna hali ya hewa ya duniani kule - hakuna mvua inayokupiga au upepo unaovuma kwenye nywele zako,” anasema, miaka 33 baadaye.

Wanaanga wanaokaa kwa muda mrefu lazima wafanye mazoezi ya saa mbili kila siku. Mashine tatu tofauti huwasaidia kukabiliana na athari za kuishi eneo lisilo na graviti, ambapo uzito wa mifupa hupungua.

'Suruali moja kwa miezi mitatu'

J

Chanzo cha picha, NASA

Maelezo ya picha, Nicole Stott alikuwa kwenye ISS kwa siku 104

“Ukifanya mazoezi, jasho jingi hutoka,” anasema Bi Stott. Sasa suala la kuosha ndio huibuka.

"Hatuoshi nguvo. Nguo zinapokuwa chafu sana, huchomwa moto. Lakini nguo za kawaida, zisizo za mazoezi, huwa safi,” anasema.

"Katika anga kusiko na graviti, nguo huelea juu ya mwili, mafuta ya mwili na vitu vingine, haviathiri. Nilivaa suruali moja kwa miezi mitatu,” anasema.

“Wakati fulani chombo kingine kinaweza kuja, kuleta wafanyakazi wapya au vifaa ama chakula, nguo, na vifaa, kutoka duniani,” anasema Hadfield.

Baada ya kazi ngumu ya siku, ni wakati wa chakula cha jioni. Chakula huwa katika pakiti, hugawanywa katika sehemu tofauti kulingana na nchi.

Anasema: “Nilipenda sana chakula cha Kijapani, au nafaka na supu za Kirusi. Familia huwatumia wapendwa wao vifurushi vya ziada vya chakula. Wafanyakazi hula pamoja mara nyingi.”

“Wanaanga huchaguliwa mapema kutokana na sifa kadhaa - uvumilivu, upole, utulivu - na hufunzwa kufanya kazi kama timu. Hiyo inapunguza uwezekano wa mzozo,” anasema Bi Sharman.

"Sio tu ya kuvumilia tabia mbaya ya mtu, lakini pia kutoitangaza. Na kila mara tunasifiana ili kusaidiana,” anasema.

Wanaanga hutamani kubaki

K

Chanzo cha picha, Ria Novosti/Science Photo Library

Maelezo ya picha, Helen Sharman ndiye mwanaanga wa kwanza wa Uingereza

Na siku ikiisha, tunarudi tena kitandani, ni wakati wa kupumzika baada ya siku katika mazingira yenye kelele. Mafeni yanazunguka, kutawanya kaboni dioksidi ili wanaanga waweze kupumua, na maisha yanakuwa kama kama ofisi yenye kelele nyingi.

"Tunaweza kuwa na saa nane za kulala - lakini watu wengi hubaki kwenye dirisha wakitazama dunia," anasema Stott.

Wanaanga wote watatu walizungumza kuhusu athari za kisaikolojia za kuona sayari yao ya nyumbani kutoka kilomita 400 katika obiti.

"Nilijihisi mtu duni sana katika eneo hilo kubwa la anga," anasema Sharman. "Kuona dunia kwa uwazi, mawingu na bahari, kulinifanya nifikirie juu ya mipaka ya kijiografia tunayounda na ukweli kwamba dunia imeungana kabisa."

Stott anasema alifurahia kuishi na watu sita kutoka nchi mbalimbali, wakifanya kazi pamoja kwa niaba ya viumbe vyote duniani, kutafuta jinsi ya kukabiliana na matatizo.

"Kwa nini hilo haliwezi kutokea kwenye sayari yetu?" anauliza.

Hatimaye wanaanga wote lazima waondoke ISS. Hawaelewi ni kwa nini watu wanafikiri wanaanga wa Nasa, Suni Williams na Butch Wilmore "wamekwama."

"Tulifanya kazi na kujifunza katika maisha yetu yote, ili tukae kwa muda mrefu angani," anasema Hadfield. "Zawadi kubwa unayoweza kumpa mwanaanga, ni kuwaacha akae kwa muda mrefu huko."

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah