Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini baadhi ya watu wanajitolea kuambukizwa magonjwa?
- Author, Luke Mintz
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Kujaribu matibabu mapya au chanjo mpya kunaweza kuchukua miaka mingi, ikiwa sio miongo kukusanya taarifa za kutosha, kwa hivyo wanasayansi wanageukia njia yenye utata ambayo inahusisha kuwaambukiza makusudi virusi hatari, vimelea na bakteria watu waliojitolea.
Mwaka 2017 kulikuwa na kundi la vijana waliokuwa wakisubiri kushambuliwa na mbu waliobeba vimelea vinavyoua zaidi ya watu 600,000 kila mwaka.
Kundi hilo lilikubali kushiriki majaribio ya matibabu katika Taasisi ya Jenner ya Chuo Kikuu cha Oxford, ili kupima chanjo mpya dhidi ya malaria. Chanjo hiyo - inajulikana kama "R21."
Taasisi hiyo imekuwa ikifanya majaribio ya chanjo ya mbu tangu 2001. Kila mtu aliyejitolea aliingizwa katika maabara. Juu ya meza ndani ya maabara, kulikuwa na bakuli dogo, kama umbo la kikombe cha kahawa, na kifuniko cha kitambaa chembamba juu.
Ndani yake kuna mbu watano waliokuwa wakipiga kelele, kutoka Amerika Kaskazini, ambao walikuwa wameambukizwa vimelea vya malaria. Mtu aliyejitolea anaweka mkono wake juu ya kibakuli ili mbu waweze kumtafuna, wakiuma kupitia kitambaa chembamba na kuingia kwenye ngozi ya mtu aliyejitolea.
Wadudu hao wanapofyonza damu, mate ambayo mbu hutumia ili kuzuia mlo wao kuganda huwa yamebeba vimelea vya malaria na huingia kwa mtu kupita kidonda alichotoboa.
Matumaini ni kwamba chanjo hiyo itatoa ulinzi wa kutosha kuwazuia kuugua malaria vijana hao.
Inaweza kuonekana ni kama mbinu hatari, kumuambukiza mtu maambukizi ambayo yanaweza kumfanya awe mgonjwa. Lakini ni mbinu hiyo imekuwa maarufu katika miongo ya hivi karibuni katika tafiti za matibabu. Na ni mbinu yenye matokeo mazuri, na ni ushindi fulani wa matibabu.
Mbinu yenye ufanisi
Chanjo ya R21 baadaye ilithibitishwa kuwa na ufanisi wa hadi 80% katika kuzuia malaria, na imekuwa chanjo ya pili ya malaria katika historia kupendekezwa kutumiwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).
Hivi karibuni, dozi za kwanza za chanjo hiyo zilitolewa kwa watoto wa Ivory Coast na Sudan Kusini – nchi zote mbili hupoteza maelfu ya watu kila mwaka kutokana na malaria. Na wanasayansi wanasema, ilifanikiwa kwa sababu ya watu waliojitolea.
Sasa, wanasayansi wanatazamia kuwaambukiza watu waliojitolea magonjwa mengi zaidi - kwa matumaini ya kutengeneza chanjo na matibabu bora zaidi. Vimelea vya magonjwa kama Zika, homa ya matumbo, na kipindupindu tayari vimetumika katika majaribio. Virusi vingine kama vile vya homa ya ini navyo vitatumika katika siku zijazo.
Watetezi wanaamini manufaa ya tafiti hizi yanazidi hatari zake, ikiwa yatafanywa chini ya mipangilio sahihi. Lakini baadhi ya majaribio yamezusha mjadala juu ya mipaka ya kimaadili kwa matibabu. Na wanasayansi wachache tayari wana wasiwasi kuhusu kasi ambayo majaribio ya aina hii yanavyotekelezwa.
Majaribio mabaya ya kimatibabu
Majaribio yaliyofanywa na wanasayansi wa Nazi, ambapo wafungwa wa kambi ya mateso waliambukizwa kwa lazima kifua kikuu na vimelea vingine vya magonjwa.
Majaribio mengine yasiyojulikana sana ni matendo ya madaktari wa Marekani huko Guatemala, ambao katikati ya miaka ya 1940 waliwaambukiza kimakusudi watu 1,308 kaswende na magonjwa mengine ya zinaa.
Mapema miaka ya 1970, madaktari katika Shule ya Jimbo la Willowbrook katika Jiji la New York, waliwaambukiza zaidi ya watoto 50 walemavu, homa ya ini katika miaka ya 1950 na 1960, kwa lengo la kuunda chanjo.
Kwa baadhi ya watafiti wa kimatibabu, "Willowbrook" umekuwa mfano mbaya wa upotofu wa maadili katika utafiti. Lakini majaribio hayo pia yalichangia ugunduzi wa kujua kuwa kuna zaidi ya vijidudu vya aina moja vinavyohusika na homa ya ini.
“Mifano hii yote ilichangia upinzani dhidi ya wazo la kuwaambukiza watu vimelea kwa makusudi,” anasema Daniel Sulmasy, mkurugenzi wa Taasisi ya Maadili ya Matibabu ya Kennedy, katika Chuo Kikuu cha Georgetown, ambaye alikuwa sehemu ya tume ya rais wa Marekani iliyochunguza majaribio ya kaswende ya Guatemala.
Mwishoni mwa miaka ya 1960 na 1970, wanasayansi katika nchi zenye kipato cha juu walitayarisha miongozo ya majaribio ya matibabu, ambayo yaliweka mbele afya ya watu wanaojitolea. Ili kufanya majaribio ya aina hiyo kuwa magumu kufanyika.
Utengenezaji wa chanjo
Chanjo ya kawaida ya magonjwa ya kuambukiza inaweza kuchukua zaidi ya miaka 10 kuitengeneza, na mamilioni ya dola za Marekani zitatumika, wakati mamilioni ya watu wanaendelea kuugua ugonjwa huo.
"Muda ni muhimu - wakati mwingine tunahitaji kufanya majaribio haraka sana," anasema Andrea Cox, profesa wa dawa katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins huko Baltimore, Maryland.
Kwake anaamini majaribio ya kuambukiza watu, yanaokoa muda, pesa, na hatimaye maisha ya binadamu.
“Majaribio hayo ni muhimu ili kushughulika vimelea vya magonjwa adimu kama vile bakteria wa salmonella na shigella wanaosababisha kuhara na kuhara damu, ambapo majaribio ya kawaida yanaweza kuchukua miaka kwani wanasayansi wanapaswa kusubiri watu wa kujitolea watakao ugua ugonjwa huo.”
"Hivyo kungojea hilo litokee, huchukua muda mrefu sana," anasema.
Sean Cousins, msafirishaji wa mizigo mwenye umri wa miaka 33 huko Southampton, Uingereza, alilipwa zaidi ya dola za kimarekani 11,000, kwa kushiriki katika majaribio matatu kati ya 2014 na 2020.
Katika majaribio mawili aliambukizwa na mafua, na jingine virusi vinavyoshambulia mfumo wa upumuaji (RSV). Lakini anasema angejitolea hata bila pesa.
"Lilikuwa jambo jipya kujaribu. Nilitaka kutoa muda wangu kusaidia wanadamu.”
Wanaounga mkono
“Chanjo wakati mwingine huleta matatizo, na ndio maana ni bora kuzifanyia majaribio katika maabara kwanza ambapo kuna matibabu,” anasema Cox.
Mfano chanjo ya dengvaxi, ilitolewa kwa watoto 800,000 nchini Ufilipino kupambana na homa ya dengu. Watafiti waliona tatizo; chanjo hiyo ambayo ilipatikana kwa njia za kawaida, ilifanya kazi vizuri kwa watoto ambao tayari walikuwa wameugua dengu. Lakini ilikuwa hatari kwa watoto ambao hawakuwa wameambukizwa hapo awali.
Mwaka 2017, Shirika la Afya Ulimwenguni lilibadilisha miongozo yake, na kupendekeza Dengvaxia isitumike kwa watu ambao hawajaambukizwa virusi vya dengue.
“Kama Dengvaxia ingejaribiwa kwa mara ya kwanza katika jaribio la maabara kwa binaadamu,” anasema, “watafiti wangeweza kuangalia jinsi chanjo na virusi vinavyoingiliana ndani ya miili ya wagonjwa mbalimbali - ikiwa ni pamoja na wale ambao walikuwa tayari wameambukizwa na dengu, na wale ambao hawakuwa wameambukizwa.”
"Kujifunza kwamba chanjo husababisha matatizo katika mazingira ambapo kuna uchunguzi mzuri na huduma ya matibabu inapatikana ni bora kuliko kujifunza hilo katika eneo la ambalo kuna rasilimali chache," anasema Cox.
Arthur Caplan, profesa wa maadili ya matibabu katika Chuo Kikuu cha New York cha Grossman School of Medicine, anasema majaribio haya kufanywa tu kwa magonjwa yanayotibika ni kuchanganya maadili.
"Kujitolea na kujaribu kusaidia wengine ni sababu halali ya kutaka kushiriki katika utafiti," anasema. Anatoa mfano majaribio yaliyofanywa kusaidia uchunguzi wa anga.
Katika majaribio haya, watu waliojitolea waliombwa kulala kwenye kitanda cha nyuma kinachoteleza ambacho husababisha damu kuelekea kwenye ubongo wao, ili kuiga athari ya angani.
“Mara nyingi, watu wa kujitolea hawanufaiki sana kwa kushiriki katika majaribio haya, wanafanya hivyo kwa manufaa ya umma,” anasema.
Wenye wasiwasi
Lakini wanasayansi wengine wana wasiwasi kwamba ni hatari kimaadili, kutumia majaribio hayo kwa ugonjwa ambao matibabu yake bado hayapo.
Eleanor Riley, profesa mstaafu wa kinga ya mwili katika Chuo Kikuu cha Edinburgh cha Uingereza, anasema: "Kwa magonjwa ambayo yana uwezo wa kusababisha ugonjwa mbaya sana, na ikiwa hatuna dawa ambayo huzuia ugonjwa huo, hapo tatizo ndio linakuja.”
Wanasayansi wanakubaliana jambo moja; kuna uwezekano wa kuona majaribio mengi ya aina hii katika siku zijazo.
Orodha ya vimelea vinavyotumiwa itaongezeka pia - ikiwa ni pamoja na baadhi ambavyo ni hatari na haviwezi kutibiwa. Hilo linawaacha wanasayansi wengi, kama Sulmasy, na wasiwasi.
Lakini wengine wanaona ni fursa kubwa ya matibabu. Wanasema majaribio haya yanaweza kuleta maendeleo ya haraka na bora ya chanjo kwa magonjwa ambayo yamesumbua binadamu kwa karne nyingi.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah