Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Chanjo ya kuzuia Virusi vya Ukimwi kuanza majaribio Afrika Kusini

Afrika Kusini na Marekani zitaanza majaribio ya chanjo mpya ya kuzuia VVU na zimeanza kuwaandikisha washiriki kushiriki katika majaribio ya kimatibabu.

Moja kwa moja

  1. Watano kushtakiwa nchini Uingereza kwa kuipelelezea Urusi

    Watu watano wanaoshukiwa kufanya ujasusi kwa ajili ya Urusi watafunguliwa mashtaka ya kula njama ya kufanya ujasusi nchini Uingereza.

    Orlin Roussev, Bizer Dzhambazov, Katrin Ivanova, Ivan Stoyanov, na Vanya Gaberova watafikishwa katika Mahakama ya Westminster siku ya Jumanne.

    Raia hao wa Bulgaria wanadaiwa kula njama ya kukusanya taarifa ambazo zingemfaa adui kati ya Agosti 2020 na Februari 2023.

    Ni kufuatia uchunguzi wa Polisi wa Metropolitan - wanashutumiwa kwa kufanya ujasusi nchini Uingereza na Ulaya na kukusanya na kupitisha habari kwa ajili ya Urusi.

    Roussev, 45, anadaiwa kuendesha oparesheni nchini Uingereza na kuwa kiungo wa wale waliopokea taarifa hizo za kijasusi.

    Maafisa waliopekua makaazi ya watuhumiwa watatu Roussev, Dzhambazov, 41, na Bi Ivanova, 31, huko London na Norfolk - walipata hati za kusafiria zinazodaiwa kuwa bandia na hati za utambulisho za Uingereza, Bulgaria, Ufaransa, Italia, Uhispania, Croatia, Slovenia, Ugiriki, na Jamhuri ya Cheki.

    Baadhi ya hati hizo zilikuwa na picha za Roussev na Bw Dzhambazov.

    Kundi hilo pia linashutumiwa kwa kuandaa operesheni ya ujajusi huko Montenegro, Canada iliyohusisha utengenezaji wa vitambulisho ghushi vya wanahabari, kikiwemo kimoja chenye sura ya Ivanova.

  2. Onana: 'Man United ilipoteza kwa Bayern Munich kwasababu yangu'

    Kipa wa Manchester United Andre Onana anasema "ameiangusha timu" na kwamba walishindwa kupata matokeo mazuri dhidi ya Bayern Munich kwa sababu yake.

    Katika mchezo uliokuwa na matukio mengi nchini Ujerumani, makosa ya Onana yaliwapa Bayern bao muhimu na kisha waliongeza mabao.

    Msururu wa mabao ulifuata na United walikuwa wakishambulia kila mara lakini wakakosa, na kupoteza kwa mabao 4-3.

    “Tulianza vizuri sana, baada ya kosa langu tulishindwa kudhibiti mchezo, ni hali ngumu kwetu, hasa kwa sababu mimi ndiye niliyeishusha timu," Onana aliiambia TNT Sports.

    "Tulicheza vizuri sana, hawakutengeneza nafasi yoyote, shuti lao la kwanza lililolenga goli nilifanya makosa. Lilikuwa goli muhimu kwao na timu ilishuka kwa sababu ya kosa hilo. Hatukushinda leo na ni kwa sababu yangu."

    "Lazima nijifunze kwa kosa hili. Mwanzo wangu Manchester haujakuwa mzuri, hivi sivyo ninavyotaka. Huu ulikuwa ni mchezo wangu mbaya zaidi."

  3. Muuaji nchini Rwanda aliyeificha miili jikoni akiri kuwa na hatia

    Mwanaume mmoja raia wa Rwanda amekiri mashtaka mengi yakiwemo ya mauaji ya wanawake 12 na wanaume wawili katika kesi ya hali ya juu iliyoishangaza nchi hiyo.

    Denis Kazungu, 34, anadaiwa kuwazika waathiriwa wake jikoni kwake.

    Polisi waligundua uhalifu huo mapema mwezi huu baada ya kufurushwa kutoka kwenye makao yake ya kukodi huko Kicukiro, kitongoji cha mji mkuu, Kigali.

    Kesi hii iliunguruma ili kubaini iwapo Bw.Kazungu anafaa kusalia kizuizini. Jaji atatoa uamuzi tarehe 26 Septemba.

    Bw.Kazungu, ambaye hakuwa na uwakilishi wa kisheria, alionekana mtulivu na mwenye utulivu wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo na alipoombwa kujibu, alisema kwa sauti thabiti kwamba "ana hatia".

    Alijaribu kuhalalisha uhalifu wake kwa kudai kuwa waathiriwa "walimuambukiza Ukimwi kwa makusudi" lakini hakutoa uthibitisho wowote wa hilo.

    Hali ya afya ya akili ya Bw.Kazungu haieleweki, lakini alionekana mwenye afya njema alipoiomba mahakama kusitisha kesi hiyo, ombi ambalo mahakama ilikataa.

    “Nimefanya uhalifu wa kupindukia na sitaki kuripotiwa kwenye vyombo vya habari,” alisema.

    Bw.Kazungu alikamatwa baada ya mwenye nyumba wake kumripoti kwa polisi kwa kutolipa kodi kwa miezi saba.

    Afisa wa polisi aliliambia gazeti la binafsi la Rwanda, The New Times kwamba alianzisha vita walipomfukuza. "Aliomba msamaha na kulia kupita kiasi, jambo ambalo liliibua mashaka yetu," afisa huyo alisema.

    "Tulimshikilia na mimi binafsi nilimpeleka polisi. Ni katika kituo cha polisi ambako alikiri kuwaua baadhi ya watu, na kusababisha Rib [Ofisi ya Upelelezi ya Rwanda] kuyachunguza makazi yake." Msemaji wa Rib alisema aliwarubuni waathiriwa wake, wengi wao wakiwa wafanyabiashara wa ngono, nyumbani kwake na kisha kuwaibia. Kisha "akawanyonga hadi kufa na kuwazika kwenye shimo lililochimbwa jikoni mwa nyumba yake ya kupanga".

    Wachunguzi bado hawajafichua majina ya washukiwa wote wa Bw Kazungu.

  4. Kenya yasaini makubaliano ya kupeleka msaada wa askari Haiti

    Rais William Ruto na Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry walishuhudia utiaji saini wa mkataba huo katika Misheni ya Kenya mjini New York, Marekani.

    Mkataba huo uliotiwa saini na Waziri Jean Victor Génus na Waziri wa Alfred Mutua utarahisisha ushirikiano katika maeneo yenye maslahi.

    Rais Ruto alitoa wito wa kuangazia masuala kiujumla kisiasa, kiusalama na kimaendeleo ili kushughulikia ipasavyo hali ya Haiti.

    Amesema Kenya itafanya sehemu yake katika kuongoza Misheni ya Usaidizi wa Usalama wa Kimataifa iliyo na rasilimali nyingi na madhubuti nchini.

    "Kama taifa linaloongoza katika ujumbe wa usalama unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini Haiti, tumejitolea kupeleka timu maalumu kutathmini kwa kina hali ilivyo na kuandaa mikakati inayotekelezeka ambayo italeta suluhu ya muda mrefu," alisema.

    Waziri Mkuu Henry alisema Haiti inahitaji usaidizi wote unaohitajika kushughulikia mfumo mkubwa wa changamoto za usalama, kibinadamu, mazingira na kiuchumi.

  5. Kiongozi aliyepinduliwa Niger aomba msaada mahakama ya Ecowas

    Rais wa Niger aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum amekata rufaa katika mahakama ya Umoja wa nchi za Afrika Magharibi ya Ecowas ili aachiliwe, wakili wake amesema.

    Kesi iliwasilishwa kortini Jumatatu ikitaka Bw Bazoum aachiliwe na arejeshwe kama rais baada ya "kukamatwa kwake kiholela" na"kukiuka uhuru wa kutembea" kufuatia mapinduzi ya Julai, wakili wake Seydou Diagne alisema. "Tunaomba... kwa kuzingatia ukiukwaji wa haki za kisiasa, kwamba Niger iamriwe kurejesha mara moja utaratibu wa kikatiba kwa kukabidhi madaraka kwa Rais Bazoum, ambaye lazima aendelee kuyatumia hadi mwisho wa mamlaka yake," alisema.

    Amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema Mkewe na mwanawe, ambao pia wanazuiliwa na jeshi, wametajwa kwenye ombi hilo, shirika la Associated Press linaripoti.

    Ecowas imetishia kuingilia kati kijeshi kumrejesha madarakani Bw Bazoum iwapo juhudi za kidiplomasia zitashindwa.

    Unaweza kusoma;

  6. Chanjo ya kuzuia Virusi vya Ukimwi kuanza majaribio Afrika Kusini

    Afrika Kusini na Marekani zitaanza majaribio ya chanjo mpya ya kuzuia VVU na zimeanza kuwaandikisha washiriki kushiriki katika majaribio ya kimatibabu.

    Kulingana na shirika la utafiti la serikali la Marekani la Taasisi za Kitaifa za Afya (NIH), chanjo hiyo, iitwayo VIR-1388, imeundwa kusaidia seli za T za mwili, zinazosaidia mfumo wa kinga kupambana na vijidudu na kukinga dhidi ya magonjwa.

    Chanjo hiyo inakusudiwa kuelekeza mfumo wa kinga ya mwili kuzalisha T-seli "zinazoweza kutambua VVU na kuashiria mwitikio wa kinga ili kuzuia virusi kuanzisha maambukizi ya muda mrefu".

    Jaribio la chanjo hiyo linafadhiliwa na NIH, Wakfu wa Bill na Melinda Gates na kampuni ya Marekani ya Vir Biotechnology.

    Utafiti huo utaandikisha washiriki 95 wasio na VVU katika maeneo manne nchini Afrika Kusini na maeneo sita nchini Marekani.

    Matokeo ya awali ya jaribio la chanjo yatatangazwa mwishoni mwa 2024, lakini baadhi ya washiriki wataendelea na majaribio kwa miaka mitatu.

    Mnamo mwaka wa 2020, NIH ilisitisha majaribio ya chanjo nyingine ya VVU nchini Afrika Kusini baada ya ukaguzi kugundua kuwa chanjo hiyo haikuwa na ufanisi katika kuzuia maambukizi ya VVU.

  7. Kiongozi wa Ghana adai fidia ya utumwa kwa mataifa ya Afrika

    Rais wa Ghana Akufo-Addo ametaka malipo ya fidia kwa mataifa ya Afrika kutokana na dhuluma za kihistoria za biashara ya utumwa iliyovuka Atlantiki.

    Akizungumza katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano, alisisitiza kuwa huu ndio wakati wa kuweka mada ya ulipaji fidia mbele. Alisema dunia kwa karne nyingi haikuwa tayari na haiwezi kukabiliana na matokeo ya biashara ya utumwa.

    Alisema "fidia lazima zilipwe" , akiongeza kuwa ingawa hakuna fedha zinazoweza kufidia hali ya kutisha ya biashara ya utumwa, ingeleta hoja kwamba mamilioni ya Waafrika "waliozalisha" waliwekwa kazini bila kulipwa fidia.

    Si mara ya kwanza kwa rais wa Ghana kuzungumza kuhusu fidia, mwaka jana alisema muda ulikuwa umechelewa ili kuongeza mijadala kuhusu suala hilo.

    Kisha akatoa wito wa kuomba radhi rasmi kwa mataifa ya Ulaya ambayo yalihusika katika biashara hiyo, na kuutaka Umoja wa Afrika kuwashirikisha diaspora ili kuendeleza kazi ya fidia.

    Biashara ya watumwa iliyovuka Atlantiki, ambayo iliathiri mamilioni ya Waafrika, ilikuwa uhamiaji mkubwa zaidi wa kulazimishwa katika historia na moja ya unyanyasaji wa kibinadamu, kulingana na UN.

    Kuhama kwa Waafrika kulienea katika maeneo mengi ya ulimwengu kwa kipindi cha miaka 400. Ghana ilikuwa mojawapo ya vituo vya kuondoka kwa wengi wa wale waliokuwa watumwa huko Afrika Magharibi.

  8. Katika picha: Kumbukizi ya miaka 10 tangu shambulizi la kigaidi ya Westgate

    Wizara ya Usalama wa Taifa nchini Kenya imezindua rasmi zoezi la kuwaainisha maafisa wa usalama wa kibinafsi katika usalama wa taifa.

    Katika kumbukizi ya miaka 10 tangu shambulizi la kigaidi ya Westgate, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kusimamia Maaskari wa Kibinafsi Fazul Mahamed amesema maafisa hao wa kibinafsi wana sehemu muhimu katika usalama wa taifa.

  9. Kenya yaamuru kurejeshwa kwa dawa maarufu ya homa kwa sababu za kiusalama,

    Mdhibiti wa dawa nchini Kenya ameamuru kurejeshwa kwa dawa ya kumeza inayotumika kupunguza maumivu na homa kwa watoto kutokana na wasiwasi wa usalama.

    Bodi ya Famasia na Sumu (PPB) ilisema kuwa imepokea malalamiko mengi kuhusu ubora wa dawa kadhaa ya paracetamol inayoitwa Tamedol.

    PPB iliwaamuru wafamasia kusitisha uuzaji wa dawa hiyo yenye chapa na kuwataka wananchi kurejesha akiba yoyote walionayo kwenye kituo cha afya kilicho karibu.

    Dawa ya kumeza, iliyotengenezwa na kampuni ya dawa ya Kenya, inakuwa ya tisa katika orodha inayoongezeka ya dawa hadi sasa iliyorejeshwa na mdhibiti mwaka huu pekee.

    Wakati huo huo, PPB imetoa onyo dhidi ya makundi yanayoshukiwa kuwa duni na ya uwongo ya Visipaque, dawa inayotumika kusaidia kutambua matatizo ya viungo vya ndani.

    Mdhibiti huyo anasema dawa zilizoathiriwa, ambazo zilitengenezwa nchini Uchina na Ireland, zilikuwa zimeingia katika soko la nchi hiyo kinyume cha sheria.

  10. Korea Kusini yavamia kambi za kijeshi za Marekani katika msako wa dawa za kulevya

    Polisi wa Korea Kusini wanawachunguza wanajeshi 17 wa Marekani na watu wengine watano wanaodaiwa kusafirisha au kutumia bangi kupitia barua za kijeshi.

    Hii inafuatia uvamizi katika kambi mbili za jeshi la Marekani mwezi Mei, ikiwa ni pamoja na Camp Humphreys, kambi yake kubwa zaidi ya ng'ambo.

    Mfilipino na Mkorea Kusini wamekamatwa, huku waendesha mashtaka wakipitia kesi dhidi ya washukiwa wote 22.

    Kidokezo kutoka kwa kitengo cha utekelezaji cha Jeshi la Marekani kilikuwa kimesababisha uchunguzi wa miezi minne na mamlaka ya Korea.

    Ilikuwa ni moja ya kubwa zaidi katika miaka ya hivi karibuni iliyohusisha askari wa Marekani, vyombo vya habari vya Marekani viliripoti kumnukuu Cha Min-seok, afisa mkuu wa upelelezi nchini Korea Kusini.

    Uvamizi wa pamoja wa polisi wa Korea Kusini na Kitengo cha Upelelezi wa Jinai cha Jeshi la Marekani uligundua gramu 77 ya bangi , aidi ya kilo nne za "miminiko iliyochanganywa" inayotumika kwa kuvuta mvuke na jumla ya dola 12,850 pesa taslimu nyumbani kwa washukiwa 22'.

    Saba kati yao wakiwemo askari watano wanadaiwa kuhusika na uuzaji wa dawa hizo, watumiaji 12 na watatu walikuwa wafanyabiashara wa kati.

    Wanajeshi hao 17 kwa sasa wako katika kambi ya Humphreys, yapata kilomita 48 kusini mwa mji mkuu Seoul, na katika Camp Casey, kituo cha jeshi kilicho karibu kilomita 40 kaskazini mwa Seoul, kulingana na polisi.

    Inadaiwa walisambaza dawa hizo kwenye kambi huku wakiwasiliana kupitia mtandao wa kijamii wa Snapchat.

  11. Indonesia yamfunga mwanamke jela kwa kukufuru kuhusu video ya chakula ya TikTok

    Mahakama ya Indonesia imemfunga jela mwanamke mmoja miaka miwili baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka sheria za kukufuru za nchi hiyo katika video ya chakula ya TikTok aliyochapisha mwezi Machi.

    Video hiyo ilionyesha Lina Lutfiawati akisoma sala ya Waislamu kabla ya kula ngozi ya nyama ya nguruwe iliyokauka na kukusanya mamilioni ya watu waliotazama .

    Nyama ya nguruwe inachukuliwa kuwa 'haram', au hairuhusiwi, chini ya sheria za Kiislamu.

    Siku ya Jumanne, mahakama katika mji wa Palembang nchini Indonesia, sehemu ya kusini ya kisiwa cha Sumatra, ilimpata kijana huyo mwenye umri wa miaka 33 kwa hatia ya "Kueneza habari zilizokusudiwa kuchochea chuki au uadui wa mtu binafsi/kikundi kwa misingi ya dini" na kumuamuru kulipa faini ya rupiah milioni 250 ($16,249.59).

    Indonesia ni taifa kubwa zaidi duniani lenye Waislamu wengi.

    Mahakama ilisema Lutfiawati, ambaye pia anafahamika kwa jina Lina Mukherjee, aliyetambulika kama Muislamu.

    Lutfiawati aliomba radhi kwa umma kwa video hiyo na kueleza kushangazwa na hukumu hiyo.

    "Ninajua kuwa nina makosa, lakini sikutarajia adhabu hii," Lutfiawati alisema kwenye kituo cha habari cha MetroTV.

    Kesi hiyo ni ya hivi punde zaidi kati ya kesi kadhaa za kashfa kote nchini, haswa dhidi ya zile zinazodaiwa kuutusi Uislamu, ambazo wachambuzi wamesema zinadhoofisha sifa ya Indonesia ya kuwa na msimamo wa wastani.

    Mnamo Agosti, mkuu wa shule ya bweni ya Kiislamu ambayo iliruhusu wanaume na wanawake kusali pamoja na wanawake kuwa wahubiri alishtakiwa kwa kukufuru na matamshi ya chuki.

  12. Ethiopia 'yazuia mashambulizi ya wanamgambo 450 wa al-Shabab'

    Ethiopia imepuuzilia mbali video ya mtandaoni iliyotolewa na kundi la al-Shabab ambapo kundi hilo linasema lilishambulia msafara wa Ethiopia nchini Somalia na kuua wanajeshi 167.

    Jeshi la Ethiopia lilitoa taarifa na kusema kuwa limezuia kabisa jaribio la shambulio lililofanywa Jumapili na wanamgambo 450 wa al-Shabab.

    Kanali Feyisa Ayele, kamanda wa kikosi cha Ethiopia nchini Somalia, alisema al-Shabab pia wameacha magari matatu yaliyokuwa na vilipuzi kwenye barabara, ambayo wanajeshi wake waliharibu.

    Hakutaja majeruhi yeyote wa Ethiopia katika taarifa yake.

    Ni nadra kwa jeshi la Ethiopia kujibu ripoti za mashambulizi nchini Somalia, ambapo wanajeshi wake wanaunga mkono serikali katika azma yake ya kuwaangamiza wanamgambo wenye mafungamano na al-Qaeda.

    Wakaazi wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba mapigano hayo yalitokea karibu na mji wa kusini-magharibi wa Rab Dhure, karibu kilomita 20 (maili 12) kutoka mpaka wa Ethiopia.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yaomba kikosi cha Umoja wa Mataifa kuanza kuondoka mwaka huu

    Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Félix Tshisekedi ametoa wito wa kuondolewa kwa haraka kwa kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini mwake kuanza mwaka huu.

    Aliliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jumatano kwamba aliiagiza serikali yake kuanza mazungumzo na Umoja wa Mataifa ili kuleta "mwanzo wa hatua hii ya kujiondoa kutoka Disemba 2024 hadi Disemba 2023".

    Alisema ujumbe huo - unaojulikana kwa kifupi kama Monusco - umeshindwa kuleta amani nchini humo licha ya kuwa huko kwa takriban miaka 25, na kuongeza kuwa ni "udanganyifu na usio na tija kuendelea kung'ang'ania" kikosi hicho ili kudumisha amani.

    "Ni wakati wa nchi yetu kuchukua udhibiti kamili wa hatima yake na kuwa mstari wa mbele katika kuleta utulivu wake," aliuambia mkutano huo New York.

    Monusco - yenye wafanyakazi zaidi ya 16,000 - ni ujumbe wa pili kwa ukubwa wa Umoja wa Mataifa duniani na umezidi kutopendwa katika miaka ya hivi karibuni.

    Umekosolewa kwa kushindwa katika dhamira yake ya kuleta utulivu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na hivyo kuzua maandamano hivi karibuni katika eneo hilo.

    Mwaka jana, mwakilishi maalum wa Monusco wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa aliambia BBC kwamba ujumbe wa kulinda amani utatathminiwa kutokana na maandamano hayo mabaya, ambapo makumi ya watu waliuawa.

    • Shambulizi la Westgate:Ni nini kilitokea Westgate miaka 10 iliyopita?

      Miaka kumi iliyopita, wanachama wa kundi la kigaidi lenye makao yake nchini Somalia la al-Shabab walishambulia jumba la maduka katika mji mkuu wa Kenya Nairobi.

      Shambulizi hilo lilisababisha vifo vya watu 67. Lilidumu kwa muda wa siku nne. Mlipuko mkubwa ndani ya jengo hilo uliashiria mwisho wa shambulio hilo, na kuwaua washambuliaji kwenye vifusi

    • Muswada wa hijab wa Iran: Wanawake wanakabiliwa na kifungo cha miaka 10 jela kwa mavazi 'yasiofaa'

      Bunge la Iran limepitisha muswada wenye utata ambao utaongeza vifungo vya jela na faini kwa wanawake na wasichana wanaokiuka kanuni zake kali za mavazi

      Wale waliovaa "isivyofaa" wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 10 chini ya mswada huo, ambao "kesi" ya miaka mitatu ilikubaliwa.

      Bado inahitaji kuidhinishwa na Baraza la Walinzi ili kuwa sheria.

      Hatua hiyo imekuja mwaka mmoja baada ya kuzuka maandamano ya kupinga kifo cha Mahsa Amini, ambaye alishikiliwa na polisi wa maadili kwa madai ya kuvaa hijabu isiyofaa.

      Wanawake walichoma vitambaa vyao au kuvipeperusha hewani kwenye maandamano ya nchi nzima kupinga utawala wa nchi hiyo ambapo mamia ya watu waliripotiwa kuuawa katika msako mkali wa vikosi vya usalama.

      Idadi inayoongezeka ya wanawake na wasichana wameacha kufunika nywele zao hadharani kabisa huku machafuko yakipungua, licha ya polisi wa maadili kurejea mitaani na kuwekwa kwa kamera za uchunguzi.

    • Venezuela yawatuma wanajeshi 11,000 kuchukua udhibiti wa gereza

      Venezuela imetuma wanajeshi 11,000 kurejesha udhibiti wa moja ya magereza yake makubwa ambayo yalikuwa yamevamiwa na genge lenye nguvu la uhalifu.

      Gereza la Tocoron, kaskazini mwa nchi, lilikuwa chini ya udhibiti wa genge kubwa la Tren de Aragua kwa miaka mingi.

      Wanachama waliweza kutembea kwa uhuru katika gereza hilo, ambalo lilikuwa na vifaa kama hoteli ikiwa ni pamoja na bwawa na kuogolea , klabu ya usiku na bustani ndogo ya wanyama, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

      Maafisa walisema wafungwa hao 6,000 watahamishiwa katika magereza mengine.

      Wakazi wengi huru walikuwa wakiishi ndani ya gereza pamoja na wafungwa waliohukumiwa.Baada ya mamlaka kutangaza kwamba wafungwa wangehamishwa, baadhi ya watu walilia nje, wasijue ni wapi jamaa zao walio ndani ya gereza wangeenda.

      "Nasubiri kusikia wanampeleka wapi mume wangu...nilikuwa nikiishi mle ndani, lakini walitufukuza," Gladys Hernandez aliambia shirika la habari la AFP.

      Iliripoti kuwa waandishi wa habari waliona walinzi wakiwa wamebeba pikipiki, televisheni na microwave kutoka jela.

      Katika taarifa iliyotumwa kwa X, iliyokuwa Twitter, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Venezuela iliwapongeza maafisa kwa kurejesha jela hiyo na kubomoa "kituo cha njama na uhalifu".

    • Magogo ya mbao yenye umri wa miaka nusu milioni yafukuliwa Zambia

      Ugunduzi wa magogo ya kale ya mbao katika kingo za mto nchini Zambia umebadili uelewa wa wanaakiolojia kuhusu maisha ya kale ya binadamu.

      Watafiti walipata ushahidi kwamba mbao zilitumika kujenga muundo karibu miaka nusu milioni iliyopita.

      Matokeo,yaliyochapishwa katika jarida la Nature, yanapendekeza watu wa umri wa mawe walijenga kile ambacho kinaweza kuwa makazi.

      "Ugunduzi huu umebadilisha jinsi ninavyofikiria juu ya mababu zetu wa mapema," mwanaakiolojia Prof Larry Barham alisema.

      Mwanasayansi wa Chuo Kikuu cha Liverpool anaongoza mradi wa utafiti wa Deep Roots of Humanity, ambao ulichimba na kuchambua mbao za zamani.

      Ugunduzi huo unaweza kubadilisha imani ya sasa kwamba wanadamu wa zamani waliishi maisha rahisi, ya kuhamahama.

      "Walitengeneza kitu kipya na kikubwa kutoka kwa mbao," Prof Barham alisema.

      "Walitumia akili, mawazo na ujuzi wao kuunda kitu ambacho hawajawahi kuona hapo awali, kitu ambacho hakijawahi kuwepo hapo awali."

      Watafiti pia waligundua zana za zamani za mbao, pamoja na vijiti vya kuchimba.Lakini kilichowasisimua zaidi ni vipande viwili vya mbao vilivyopatikana kwenye pembe za kulia kwa kila kimoja.

      "Moja imelala juu ya nyingine na vipande vyote viwili vya mbao vimekatwa vipande vipande," mwanaakiolojia wa Chuo Kikuu cha Aberystwyth Prof Geoff Duller alisema.

    • Vita vya Ukraine:Poland kusitisha kusambaza silaha kwa Ukraine

      Mmoja wa washirika wakuu wa Ukraine, Poland, ametangaza kuwa haitasambaza tena silaha kwa nchi hiyo huku mzozo wa kidiplomasia kuhusu nafaka ukiongezeka.

      Waziri mkuu wa taifa hilo alisema badala yake itajikita katika kujizatiti kwa silaha za kisasa zaidi.

      Hatua hiyo inajiri huku mvutano kati ya mataifa hayo mawili ukiongezeka.

      Siku ya Jumanne, Poland ilimwita balozi wa Ukraine kuhusu maoni yaliyotolewa na Rais Volodymyr Zelensky katika Umoja wa Mataifa.

      Alisema baadhi ya mataifa yamejifanya kuwa na mshikamano na Ukraine, ambayo Warsaw ilishutumu kuwa "isiyo na haki kuhusu Poland, ambayo imeunga mkono Ukraine tangu siku za kwanza za vita".

      Waziri Mkuu wa Poland, Mateusz Morawiecki, alitangaza uamuzi wa kutoipatia Ukraine tena silaha katika hotuba ya televisheni siku ya Jumatano baada ya siku ya mvutano unaoongezeka kwa kasi kati ya nchi hizo mbili kuhusu uagizaji wa nafaka kutoka nje.

      Mzozo wa nafaka ulianza baada ya uvamizi kamili wa Urusi dhidi ya Ukraine kufunga njia kuu za meli za Bahari Nyeusi isipokuwa moja na kuilazimu Ukraine kutafuta njia mbadala za kusafiri nafaka yake kupitia nchi kavu .

      Hilo nalo lilisababisha kiasi kikubwa cha nafaka kuishia Ulaya ya kati.

      Kwa hiyo, Umoja wa Ulaya ulipiga marufuku kwa muda uagizaji wa nafaka katika nchi tano; Bulgaria, Hungaria, Poland, Romania na Slovakia kulinda wakulima wa ndani, ambao waliogopa nafaka ya Kiukreni ilikuwa ikipunguza bei ndani ya nchi.

      Unaweza pia kusoma

    • Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja leo Alhamisi tarehe 21 Septemba 2023